HABARI ZA MUAWIA

Jina lake ni: Muawia bin Abi Sufiani bin Harb bin Umayya.

Muawia baada ya kuandikiana mkataba wa amani kati yake na Imam Hasan (a.s.) alikwenda Madina. Alipofika nyumbani kwa Uthman bin Affan akamkuta Aisha bint Uthman, alipomuona tu, Aisha akaangua kilio kumkumbuka baba yake. Muawia akamtuliza akamwambia: "Ewe mtoto wa ndugu yangu! Watu wametutii nasi tumewapa amani, tumeonyesha upole ndani yake kuna chuki na wao wametuonyesha udhalili ndani mna fundo, basi kila mtu ameshika silaha yake na anamwangalia adui yake alipo, tukianza mashambulizi na wao watajibu. Na hatujui tutapigwa au tutawapiga, wewe kuendelea kuwa mtoto wa Amirul Muuminina ni bora kuliko kuwa mateka wa watu."

Taz: Shaikhul Mudhira Uk. 181

Muawia alipompeleka Mughira bin Shuuba kuwa gavana wake katika Mkoa wa Kuufa, mwaka arobaini na moja, alimwita akamwambia:

"Nilitaka kukuusia mambo mengi sana, lakini ninakuachia wewe na akili yako katika yale yatakayo niridhisha na kuinua utawala wangu, na kupatanisha raia. Na sitaacha kukuusia jambo moja, usiache kumtukana Ali na kumkashifu, na kumhurumia Uthman na kumuombea msamaha. Na kuwatia aibu watu wa Ali na kuwatenga mbali, na kuacha kuwasikiliza mahitaji yao".

Taz: Tarikhut Tabari J.4 Uk. 188
Tarikh Ibn Athir J.3 Uk. 234

Muawia aliwaandikia magavana wake katika miji yote kuwa: "Ye yote mtakaemgundua anawaheshimu watu wa nyumba ya Mtume, basi aadhibiwe mara moja".

Muawia aliamuru akamatwe Abdur Rahman bin Hasan Al'a'nz apelekwe kwa Ziyad, kwa sababu Abdur Rahman alikuwa akiwataja kwa wema watu wa nyumba ya Mtume akakamatwa mara moja akapelekwa kwa ziyad naye akamzika akiwa hai!!

Kama ambavyo jeshi la Muawia lilimkamata Muhammad bin Abi Bakr, likamfunga katika kiriba, kisha akawashwa moto mpaka akafa.

Taz: Tarikhut Tabari J.4 Uk. 79
Tarikh Athir J.7 Uk. 313
Annujumuz Zahira J.1 Uk. 110