UTHMAN BIN AFFAN

Mara alipochaguliwa Uthman, Abu Sufiyan alikwenda kumpongeza Uthman. Katika baadhi ya risala yake alisema hivi "Sasa (utawala) umekufikia baada ya kushikiliwa na Bani Taymi, basi zungusha kama mpira (wanavyopasiana) na weka viongozi wake wakuu Bani Umayya. Kwa sababu huu sasa ni ufalme, wala sina habari kama kuna pepo wala moto".

Taz: Al-Istiia'b J.2 Uk. 690

Abdullahi bin Saad bin Abi Sarhi, huyu ni ndugu ya Uthman wa kunyonya. Alisilimu kabla ya Fat'hu Makka, akawa pamoja na Mtume katika vikao mbalimbali, kisha baadae Alirtaddi (alitoka katika Uislamu) akawa pamoja na Makuraishi akiwaambia: "Nilikuwa nikimkejeli Muhammad namna nipendavyo".

Ilipokuwa siku ya Fat'hu Makka Mtukufu Mtume alitoa agizo ya kwamba:- Abdullah bin Saad bin Abi Sarhi auliwe po pote atakapokuwa japokuwa awe katika pazia la Kaaba". Wanafiki wakamjulisha habari hii Abdullah bin Saad bin Abi Sarhi, naye akakimbilia kwa Uthman bin Affan. Uthman akamficha, mpaka bali ilipotulia, Uthman akaenda naye kwa Mtume kumuombea msamaha. Mtume akakaa kimya kwa muda mrefu kisha akajibu, "Ndiyo" Alipoondoka Uthman na mtu wake, Mtume (s.a.w.) akawauliza waliokuwapo hapo:

"Sikunyamaza kitambo chote kile ila nilingoja miongoni mwenu asimame amkate kichwa chake" Mtu mmoja katika Ansar akamwambia Mtume: Mbona hukunikonyeza ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtume (s.a.w.)? Akajibu, "Kukonyeza si tabia ya Mtume".

Taz: Usudul Ghaba J.3 Uk. 173

Mali yote iliyopatikana baada ya kufutuhiwa Afrika mpaka Tanjat, Uthman akampa Abdullah bin Saad bin Abi Sarhi. Baadae Uthman katika mwaka wa ishirini na tano alimtawalisha Abdullah kuwa Gavana wake katika nchi ya Misri baada ya kumuuzulu A'mri. Abdullah bin Abi Sarhi akakaa miaka mingi akiwa mtawala wa Misri, watu wa Misri wakapeleka malalamiko yao kwa Uthman dhidi ya utawala wa Ibni Abi Sarhi. Uthman akaandika barua ya kumkanya Ibnu Abi Sarhi lakini hakusikia. Hapo Waislamu hawakuvumilia tena vitendo viovu aliivyokuwa akiwafanyia na kuamua kwenda kuonana na Uthman.

Walipofika kwake na kumueleza yote, Uthman akawaambia: "Chagueni mtu mmoja atakaekuongozeni mahala pa Ibni Abi Sarhi. Watu wote wakamchagua Muhammad bin Abi Bakr. Uthman akampa Muhammad makaratasi ya kumtambulisha kuwa yeye ni gavana wake katika nchi ya Misri. Watu wote katika Muhajir na Ansar wakatoka kushuhudia tukio hilo, na Muhammad bin Abi Bakr gavana mteule akiwa na ujumbe wake wakaondoka kwenda Misri. Walipokuwa njiani mara aliwatokea kijana mmoja aliyekuwa na ngamia wake mwenye mbio za ajabu. Walipomuuliza anakwenda wapi na kuna nini alisema, yeye ametumwa na Uthman kwenda kwa kiongozi wa Misri. Jamaa wakamwambia Kiongozi wa Misri ni huyu (Muhammad bin Abi Bakr) kijana akajibu: "Huyu siye niliyetumwa kwake." Alipoulizwa kuwa anayo barua? Akajibu, "Sina". Wakampekuwa wakamkuta nayo barua aliyoificha, walipoifungua kuisoma ilikuwa hivi: Atakapokufikia Muhammad bin Abi Bakr na wenziwe, fanya kila njia uwauwe na upuuze barua yao, na wewe uendelee kukalia kiti chako".

Walipoisoma barua hiyo, Muhammad na ujumbe wake, walifadhaika sana na wakaamua kurudi Madina. Walipofika huko wakakusanyika: Talha, Zubeir, Ali, Saad, na Masahaba wengine wengi, ikasomwa barua hiyo mbele yao na wote wakahuzunika mno.

Kisha wakaafikiana kwenda kumuona na kumuuliza Uthman juu ya barua hiyo. Walipofika kwake, wakiwa pamoja na barua hiyo na kijana aliyepewa barua, Imam Ali akamuuliza: "Huyu ni kijana wako? Uthman akajibu: "Ndiyo" Ali akasema: "Ngamia huyu ni wako?" Uthman akajibu "Ni wangu" Ali akauliza: "Wewe ndiye uliyeandika barua hii? (akaonyeshwa) Uthman akajibu: "Hapana" Akaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye hakuandika barua hiyo wala hakuagiza iandikwe. Ali akamuuliza: "Huu muhuri ni wako?" Uthman akajibu: "Ni wangu" Imam Ali akamuuliza: "Itawezekanaje kijana wako amchukue ngamia wako na barua iliyo na muhuri wako na wewe usiwe na habari yo yote?"

Taz: Tarikhul Khulafai Uk. 156-160

Uthman alimuuzulu Saad bin Abi Waqqas katika mkoa wa Kuufa na mahala pake akamtawalisha Al'Walid bin Uqba ndugu yake kwa upande wa mama.

Saad alipoona hivyo alishangaa na kuuliza: "Hivi wewe umekuwa mwema baada ya kuondoka mimi huko Madina, au mimi nimekuwa mjinga sikujui?" Al'walid akajibu: "Yote hayo hayakutokea (mimi si mwema na wewe si mjinga) huu ni ufalme asubuhi huliwa na hawa na jioni ukaliwa na wengine".

Taz: Tarikh Ibn Athir J.3 Uk. 42

Waislamu yalipowachosha matendo ya Uthman ya kuwatawalisha Bani Ummayya na kuwauzulu Masahaba wakubwa, walimfuata Abdur Rahmani bin Awf wakamwambia: "Hii ndiyo kazi yako na uchaguzi wako kwa Umat Muhammad."

Uthman akaanza kusambaza misaada kwa Bani Umayya akichota katika Baitilmal. Akampa Marwan bin Al'hakam aliyompa, akampa Harith bin Al'hakam bin Abil'As dirham laki tatu, akampa Zaid bin Thabit Al'ansary dirham laki moja.

Hapo Abudharril Ghifar akawa anawakumbusha Waislamu Maneno ya Mwenyezi Mungu. "Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Mwenyezi Mungu basi wape habari za adhabu iumizayo. Siku itakapotiwa joto (mali yao) katika moto wa Jahanamu na kwa moto huo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao. Haya ndiyo mliyoyakusanyia nafsi. zenu, basi onjeni (adhabu) ya yale milyokuwa mkikusanya" 9:34-35

Uthman akamfukuza Abudharri akaamuru apelekwe Rabadha (mji mdogo ulio karibu na Makka) akaagiza Mar'wan bin Al'hakam ndiye atakaempeleka huko. Na hakuna ruhusa kwa mtu ye yote kutoka kumuaga wala kumsalimia Abudharri, na watu wote wakajifungia majumbani isipokuwa Imam Ali na nduguye Aqil na Hassan na Husein na Ammar, wao walitoka kumsindikiza.

Taz: AI'Ansab J.5 Uk. 52 - 54
Tabaqatul Kubra J.4 Uk. 168

Uthman alimrejesha Madina ammi yake Al'hakam bin Abil'As ambaye Mtume (s.a.w.) alimfukuza Madina akampeleka Taif.

Taz: Usudul Ghaba J.2 Uk. 34
Al'bidayatu Wannihaya J.8 Uk. 262

Uthman alimpa Abu Sufiyan dirham laki mbili katika Baitulmal, akampa Abdullah Ibn Abi Sarhi dirham laki moja.

Uthman alimgawia dirhamu milioni mbili na laki mbili Talha bin Ubeidillah, na Zubeir akampa dirhamu hamsini na tisa milioni na laki nane. Alhakamu bin Abil'As ammi yake Uthman ambaye alifukuzwa na Mtume yeye alipomrudisha Madina akampa dirhamu laki tatu. Na familia ya Alhakamu akaipa dirhamu milioni mbili na ishirini elfu, na wengine wengi katika Bani Umayya.

Ukijumlisha matukio haya yote utaona kuwa mauwaji aliyofanyiwa Uthman, ilikuwa ni matokeo ya hali ya hewa katika kipindi hicho.