TUKIO LA SHURA

Imepokewa kwa Qatada kuwa: Umar alipozidiwa karibu atakufa, aliwaita Waislamu mbele yake akasema: "Laiti Abu Ubaida bin Jarrahi angelikuwa hai ningelimchagua kuwa khalifa wenu, na laiti Salim mtumwa wa Hudhaifa angekuwa hai ningemchagua kuwa Khalifa wenu".

Siku ya pili Umar akamwita Ali bin Abi Talib, Uthman bin Affan, Saad bin Abi Waqas, Zuberi bin Awwam, Abdur Rahman bin Awf, akawaambia: "Nimefanya uchunguzi kutafuta atakaeshika mahala pangu, sikuona mwingine isipokuwa nyinyi. Shaurianeni kwa muda wa siku tatu mchague mmoja atakaekuwa Khalifa wenu, Katika siku tatu hizo za mashauriano atakusalisheni Suhaibu, na Talha bin Ubeidillahi. Mchague mmoja atakaekuwa Khalifa wenu. Katika siku tatu ni mwenzenu katika mashauri haya, akirudi katika siku tatu hizi mtieni katika wagombea. Na asipowahi basi chagueni na yeye yuko pamoja nanyi, mwanangu Abdillahi atahudhuria kikao chenu kama mashauri tu.

Watano kati yenu wakimchagua mmoja, na mmoja akipinga, basi kateni kichwa chake. Wanne wakichagua mmoja, na wawili wakikataa, basi wauweni. Ikiwa watatu wakikubaliana mmoja wao, na watatu wakikataa, elekezeni shauri hili kwa mwanangu Abdillahi. Kama atakataa, basi angalieni upande aliosimama Abdur Rahmani bin Awf, ndio ulio na haki na watatu waliobaki wauliwe".

Waislamu wakamuomba ajaribu kumpendekeza anayemuona anafaa kushika mahala pake. Umar akawaambia: "Wallahi hainizi wilii kukupa Ukhalifa ewe Saadi isipokuwa ukatili ulio nao na kwamba ni mpiganaji. Na haikuniziwia kukupa wewe Abdur Rahmani ila ni kwa sababu wewe ni firauni wa umma huu. Na haikuniziwia kukupa wewe Zuberi isipokuwa tabia uliyonayo, unapofurahi huwa muumini kweli kweli na uanapoghadhibika huwa kafiri hasa. Siku moja unakuwa shetani, siku nyingine unakuwa binadamu. Unaonaje siku unayokuwa shetani nani atashika Ukhalifa siku hiyo? Na sitaki kumpa Talha kwa sababu ya majivuno yake, na kama atashika Ukhalifa akili yake yote itafikiria wanawake. Na sitaki kumpa Uthmani kwa sababu uongozi atawaachia Bani Umayya. Na haikuniziwilia kukupa wewe Ali isipokuwa pupa uliyo nayo, na wewe ndiye bora ya watu wote, ikiwa utashika Ukhalifa bila shaka utasimamia sheria za Mwenyezi Mungu".

Baada ya kufa Umar, ile kamati ikakutana, Talha akajitoa katika wagombea, na haki yake akamwachia Uthman bin Affan.

Zubeir naye akajitoa na haki yake akaiacha kwa Ali.

Saad yeye naye akaacha haki yake kwa Abdur Rahman. Kwa hiyo wagombea wakabaki watatu: Ali, Uthman, na Abdur Rahman.

Walipokaa kikao, Abdur Rahman aliuliza: "Nani kati yenu atajitoa katika kugombea ili awe na haki ya kuchagua mwingine"? Jamaa wakakaa kimya. Abdur Rahman akawaambia Nimefanya utafiti kujua nani mnampendelea kuwa Khalifa wenu, nimegundua ama Ali au Uthman. Kisha baada ya majadiliano marefu siku ya tatu, Abdur Rahman akamwita Ali akamshika mkono na kumwambia:- "Toa ahadi kuwa utaongoza kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake na utafuata mwenendo wa Abubakr na Umar". Ali akajibu: "Hapana, isipokuwa nitafuata Quran na Sunna za Mtume" (s.a.w.) Abdur Rahman akamwachia mkono kisha akamwita Uthman naye akamshika mkono na kumwambia: "Toa ahadi kuwa utaongoza kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake na utafuata mwenendo wa Abubakr na wa Umar?" Uthman akakubali; "Ndio" Abdur Rahman akasema, "Ee Mola! Sikia na ushuhudie, mimi nampa dhamana hii Uthman".

Ali bin Abi Talib akatoka nje huku akisema: "Ipo siku itafikia"

Taz: Tarikhut Tabari J.3 Uk. 301
Tarikh Ibn Athir J.3 Uk. 34
Kanzul Ummal J.5 Uk. 741