SAQIFA

Kwanza; ni vizuri kujua maana ya neno: Saqifa: Ni Klabu au ukumbi.

Amesema Mwana Aisha kuwa: "Zilipotangazwa habari za kifo cha Mtume (s.a.w.) Umar bin Khattab na Mughira bin Shuubam waliingia ndani alikolazwa Mtume (s.a.w.). Umar akasema: Oh msiba mzito kwa kuondokewa na Mtume, kisha walitoka nje, walipokuwa mlangoni Mughira akasema: Ewe Umar! Kwa kweli Mtume amekufa, Umar akajibu: Wewe muongo, Mtume hajafa isipokuwa wewe ni mtu unayesumbuliwa na fitina. Mtume hatakufa mpaka wanafiki wamalizike wote.

Taz: Albidayatu Wannihaya J.5 Uk. 212

Hatimae Umar alikamata upanga akaonya kuwa: Ye yote atakaesema kuwa Mtume amekufa atakata kichwa chake. Alipofika Abubakr, Umar akanyamaza na akaweka upanga wake chini. Kisha Abubakr akatangaza kuwa Mtume amekufa, na hapo ndipo alipoondoka yeye na Umar kwenda mwenye ukumbi wa Bani Saida. Huko walijumuika na Masahaba kutoka Ansar wa Madina tayari kwa uchaguzi. Abubakr alitoa hutuba ndefu katika mkutano huo akiwakumbusha kuwa wao (Muhajir) ndio wenye haki ya kushika uongozi mahala pa Mtume (s.a.w.). Hutuba ambayo ilijibiwa baadae na Hubab bin Mundhir katika Ansar, naye akionyesha kuwa ma-Ansar wanayo haki zaidi yao, kwa sababu kwao (Madina) ndiko kuliko shamiri na kukomaa nguvu za Uislam, na Waislamu kupata Uhuru wa kuabudu. na ikiwa hapana budi basi kwa Muhajir atoke mmoja na kwa Ansar atoke mmoja.

Hapo ndipo Umar aliposimama akasema: "Hilo haliwezekani, panga mbili hazikai katika ala moja, Wallahi Waarabu hawakubali kuwatawalisheni na hali Mtume wao hatokani na nyinyi".

Baada ya mabishano makali na kushutumiana, karibu wauwane, hatimae Abubakr akachaguliwa.

Kama asemavyo Umar: "Kuchaguliwa kwa Abubakr kulitokea ghafla, Mwenyezi Mungu alizuia shari zake, na atakaerejesha kitendo kama hiki auliwe".

Taz. Tarikhul Tabari J.2 Uk. 446/457
Tarikh Ibn Athir J.2 Uk. 223
Sahih Bukhar J.8 Uk. 210
Albidayatu Wannihaya J.5 Uk. 215

Abubakr na Umar hawakuwahi kumzika Mtume (s.a.w.).

Taz: Kanzul Ummal J.5 Uk. 652

Wakati wote huo Imam Ali yuko nyumbani kwa Mtume (s.a.w.) akishughulikia maandalizi ya kumzika Mtume.

Kisha baada ya kumzika Mtume (s.a.w.) Imam Ali alibaki nyumbani kwake yeye na mkewe Mwana Fatima (a.s.) wakawa wanakusanyika hapo Bani Hashim. Abubakr baada ya kutawalishwa alimpeleka Umar bnil Khattab nyumbani kwa Mwana Fatima (a.s.) ili akawatoe wote waje kumbai Abubakr akamwagiza kuwa: Endapo watakataa kutoka kuja kumbai, awauwe. Umar akaenda na kijinga cha moto, Mwana Fatima alipomuona mlangoni na kijinga hicho akamuuliza: Ewe Umar! Umekuja iwasha nyumba yetu? Umar akajibu Ndiyo Wallahi nitakuunguzeni au mtoke kwenda kumbai Abubakr".

Inasemekana kuwa: Umar alipoingia nyumbani kwa Mwana Fatima, alimpiga ngumi ya tumboni, ngumi ambayo iliumiza ujauzito na kuzaliwa mtoto aliyekufa! Na kwa sababu ya kipigo hicho, afya ya Mwana Fatima ilidhoofu sana na baadae kufariki.

Umar alikuwa akiyakumbuka haya, mwenyewe husema "Laiti ningelikuwa kondoo niliyefugwa, nikanenepeshwa kiasi cha kupendeza. Akija mgeni nikatwekatwe sehemu nyama yangu ikaangwe na sehemu ibanikwe, kisha wanile na wanitoe nikiwa mavi nisiwe binadamu".

Taz: Kanzul Ummal J.12 Uk. 619