RISALATUL HUQUQ (HAKI YA MTU KWA MTU)

Kimeandikwa na: Hadhrat Imamu Ali bin HussainZainul Abidiin (A.S)

Kimetafsiriwa Kwa Lugha ya Kiingereza na: Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

Kwa Lugha ya Kiswahili na: U. M. Kiondo

DIBAJI

Hadhrat Imamu Ali bin Hussain bin Ali bin Abi Talib (A.S) ajulikanaye sana kwa jina lake la cheo la Zainul Abidiin (Kidani cha wenye kufanya Ibada) alieleza haki 50 zinazohusu wajibu zote zinazohusu uhusiano wa wanadamu. kitabu cha haki hizo kinajulikana kwa jina la "Risalatul-Huquq."

Allamah Al-Haj Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Muasisi na Mhubiri mkuu wa Misheni yetu alizitafsiri kwa Kiingereza na kuzitoa kidogo kidogo katika Gazeti la "The Light." Kuanzaia April, 1969 hadi December, 1970. Mwaka 1972 kilichapishwa kitabu kamili kwa jina la Reciprocalj Rights, na kutangazwa na Peermohamed Ebrahim Trust, Karachi Pakistan.

Mwaka wa 1989, Vancour Islamic Education Foundation Canada walichapisha kwa jina la The Charter of Rights na mwaka wa 1991 World Organization For Islamic Service (WOFIS) Tehran Iran, walichapisha kwa jina la Reciprocal Rights Pamoja na Kiarabu chake. Mwaka wa 1998 Bilal Muslim Mission of Tanzania ilichapisha kwa jina la The Charter of Rights.

Mnamo mwaka 1979 Mallim Dhikiri U. M. Kiondo, alikitafsiri kutoka tafsiri hiyo ya Kiingereza na kukitoa kidogo kidogo katika Gazeti la "Sauti Ya Bilal".

Mnamo mwaka 1980 Misheni imeamua kukitoa katika hali ya kitabu kamili, na hadi mwaka 1994 kilichapishwa Toleo Nne. Toleo hili ni la Tano ambalo limepigwa chapa upya na kugawiwa ili kuzidi kuwasaidia. Waislamu.

Insha Allah Taala.

UTANGULIZI

(Kwa maneno ya Mfasiri wa Tafsiri ya Kiingereza)

Hii ni tafsiri ya kijitabu cha Imamu wetu (wa Nne), Zainul Abidiin (a.s), kinachojulikana kwa jina la "Risalatul -Ul-Huquq" (Kitabu cha Haki). Katika Risala hiyo, Imamu (a.s) amezielezea kwa maneno yaliyo wazi wazi wajibu zote (ambazo ni 50) ambazo mtu anategemewa kuzitimiza katika maisha yake.

Nakala ya asili imeandikwa katika kitabu kiitwacho "Tuhaf-Ul-Uquul-an-Adlir-Rasuul" cha Sheik Abu Muhammad Al-Hasan bin Ali bin Al-Husain bin Shubba al-Harrar aliyeishi katika zama zile zile za Sheikh Saduqi (katika karne ya 4 A.H) na ni mmoja wa watu wanaokubaliwa maneno yao wa Madhehebu ya Shia. Kitabu chake hicho kimetukuzwa katika kila karne.

Tafsiri yangu si sahihi hata kidogo, kwa maana sitegemei kupata maneno yenye kuwakilisha maana halisi iliyodhamiriwa katika vifiingu vya maneno vilivyotumiwa. Hata hivyo nategemea kuwa tafsiri itatoa dirisha ambalo kwalo wasomaj i wataweza kupata mtazamo wa mara moja katika Akhlaqi tukufu za Kiislamu.

Nakala ya Hadithi hiyo iliyotolewa na Imamu (a.s) haina vifungu vifungu au vichwa vya habari vidogo vidogo, wala hakuna vituo wala nambari. Mambo hayo yameongezwa katika tafsiri ili kuifanya ieleweke zaidi kwa wasomaji waliozoea kusaidiwa na mambo hayo katika kusoma.

Sayyid SaeedAkhtarRizvi

RISALATUL HUQUQ

Fahamu, Mwenyezi Mungu na akurehemu, kuwa Mwenyezi Mungu anazo haki fulani juu yako. Zenye kukuenea kila uendapo na kila ukaapo, katika kila sehemu uwayo, na katika kila kiungo ukisogezacho, au kila zana unayoitumia. Baadhi ya haki hizi ni kubwa kuliko nyinginezo.

Na iliyo kubwa zaidi kuliko zote ni ile haki aliyonayo Mwenyezi Mungu Mwenyewe juu yako, hiyo ndiyo mzizi wa haki zote, kwa kuwa haki zote zinatokana na haki hiyo. Kisha Ameziweka haki ambazo viungo vyako tofauti tofauti  zinavyo juu yako, kutoka kichwa hadi miguu. Hivyo, aliyapa haki macho yako masikio yako, ulimi wako, mikono yako, miguu yako, tumbo lako, na viungo vyako vya siri. Haki hizi zinahusu karibuni shughuli zako zote maishani mwako.

Kisha Mwenyezi Mungu ameweka haki  ya matendo  juu yako  kuhusu sala yako, funga yako, Zaka yako, sadaka zako, na matendo mengine ya ibada.

Baada ya hapo hufuatia haki walizonazo watu wengine juu yako, ambazo zilizo muhimu zaidi ni haki za mkuu wako, wadogo wako, na ndugu zako. Na hizi aina tatu za haki zimezaa matawi mengi ya haki.

Hivyo, haki za wakuu wako ni za aina tatu. Haki ya mfalme haki ya mwalimu wako na haki ya mkubwa (mwajiri) wako. Na haki ya wanao kutegemea ni za aina tatu. Haki ya raia zako, Haki ya mwanafunzi wako kwa kuwa mwanafunzi yu mwenye kumtegemea mwalimu katika elimu yake na haki za wake zako.

Na haki ya ndugu zako ni nyingi sana kutegemeana  na ukaribu (au umbali) na ndugu hao. Hivyo iliyo muhimu sana kati ya hizo ni  haki  ya  mama yako,  kisha haki  ya  baba yako, kisha ya watoto wako. kisha ndugu zako (wa kiume) kisha ndugu wengineo kufuatana na ubora wa undugu wake nawe  ndugu wa karibuni kwanza, kisha ndugu wa mbali.

Kisha kuna haki ya mkubwa wako (wa kazi), na ya mtumishi wako;  kisha haki ya mfadhili wako, kisha haki  ya  Muadhini, anayekuita kwenye Sala, na haki ya Imamu anayekuongoza  katika sala kisha haki ya mfuasi wako, kisha haki ya jirani yako, kisha haki ya wenzi wako na washirika wako.

Kisha iko haki  iliyonao utajiri wako  juu yako, kisha haki ya mdaiwa wako, kisha haki ya aliyekukopesha, na haki ya rafiki yako, na haki ya mtu anayekulalamikia.

Kisha hufuatia haki ya mtu anaye kutaka ushauri, na mtu anayekushauri, na yule anayetaka mwongozo kutoka kwako na yule anayekuongoza.

Kisha kuna haki ya mtu aliyekuzidi umri, na ya mtu uliyemzidi umri, na ya mtu anayekuuliza jambo na haki ya mtu unayemuuliza jambo.

Kisha iko haki y a mtu uliye mkosea  kwa maneno au kwa matendo, ambaye bahati yake mbaya amejieleza kwa maneno au kwa matendo katika hali ya kuifurahia kwa kudhamiria au kwa bahati mbaya tu.

kisha iko haki ya Waislamu wenzio, kwa ujumla; na haki ya wale wasio Waislamu ambao wako katika hifadhi ya Waislarnu (yaani Dhimmi); na kisha haki nyinginezo zilizo wajibu katika hali mbali mbali na kwa sababu mbali mbali.

Hivyo basi, aliyebarikiwa ni yule ambaye Mwenyezi Mungu Humsaidia kuzitimiza haki zote zilizo wajibu juu yake.

HAKI YA MUNGU, NAFSI NA VIUNGO VYA MWILI

HAKI YA MWENYEZI MUNGU

Hivyo, ni haki ya Mwenyezi Mungu  kuwa  umuabudu  yeye tu bila ya kumwekea mwenzi au mshirika. Na kama ukiutimiza wajibu huu kwa uaminifu, basi Mwenyezi Mungu ameahidi kukutosheleza katika mambo ya ulimwenguni hapa na Kesho huko Akhera, na kukuwekea kila unacho kipenda katika ulimwengu huu.

NAFSI:

Na ni haki  ya Nafsi  yako  kwako kuwa uitumie kikamilifu kumtii Mwenyezi Mungu, kwa kutoa haki ya ulimi wako, masikio yako, macho yako, mikono yako, miguu yako, tumbo lako, na via vya siri hali ya kuwa unatafuta msaada wa Mwenyezi Mungu katika kuifanikisha kazi hiyo.

3. HAKI YA ULIMI:

Ni haki  ya ulimi  wako kuwa  ni lazima ufikirie kuwa ni jambo lenye heshima sana kuto zungumza mambo machafu; na kuufundisha kuzungumza mambo mazuri na kuutiisha katika tabia njema, na kuuweka kimya ila katika muda ambao unakuwepo ulazima  wa kusema na kwa faidi  ya kiroho au kimwili; na kuuambaza na mambo yasio na faida, kusema Mambo yasio faida (ambayo yanaweza kusababisha madhara zaidi yenye faida kidogo)

Basi ulimi ni ushahidi wa uwezo wi kiakili na kiongozi cha hiyo nguvu ya kiakili; na utiifu wake mzuri humuongoza vozuri mtu kwenye hekima katika hekima zake.

Na hakuna nguvu yeyote ile,  ila Mtukufu tu.

4. HAKI YA MASIKIO:

Ni haki yi kia chako cha kusikiza kuwa usikigeuzie moyoni kwako (usikilize) ila kwa ajili ya mazungumzo bora ambayo yanaweza kutoa (mawazo fulani mazuri) moyoni mwako au ambayo yanaweza kukupatia tabia nzuri; kwa sababu (kusikia) ndio mlango unaoruhusu mazungumzo kuingia moyoni mwako yakiwa yamechukua hizi aina mbali mbali za mawazo; yawe mazuri au maovu.

Na hakuna nguvu yoyote  ile,  ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

5. HAKl YA MACHO:

Na ni haki ya kia chako cha kuonea kukikinga kisiyaone yale mambo ambayo hayaruhusiwi kuyaona na kutokitumia ila tu mahali ambapo utapata funzo ambalo litakuongezea  kuona kwako (kwa kiroho) au patakupatia elimu fulani, kwa sababu kuona ni mlango wa kifikira.

6.HAKI YA MIGUU:

Na ni haki ya miguu yako kuwa usiitumie kwendea kwenye sehemu ulizokatazwa kwenda; na Usiifanye farasi wako wa kupatia njia yenye fedheha, kwa sababu miguu yako ndio njia yako ya kuendea, na ni lazima ikupeleke kwenye njia ya dini na maendeleo tu.

Na hakuna nguvu yoyote ile, ila Mwenmyezi Mungu tu.

7. HAKI YA MKONO:

Na ni haki y a mkono wako kuwa kusiunyooshe kwenye kitu ulicho kikatazwa; au sivyo utapata adhabu ya Mwenyezi Mungu kesho   huko Akhera, na lawama za watu katika ulimwengu huu. Na katu usiuzuie kufanya (matendo) ambayo Mwenyezi Mungu kakuwajibisha kuyafanya.

Na ni lazima uiongoze heshima ya mkono wako kwa yale matendo yaliyo mazuri japo si wajibu juu yiko, kwa kuwa kama matendo ya mikono yako yanategemeana nahekima na utukufu, kwa hakika yatapata thawabu nzuri kesho huko Akhera.

8. HAKI YA TUMBO:

Ni ni haki  ya tumbo lako kuwa usiligeuze kuwa mtungi wa chakula haramu; (kiwe kichache au  kingi) na kuwa usile hadi ukavimbiwa kwa sababu kufanya hivyo kutakugeuza kula huko kuwa ulafi na kutokuwa na aibu badala ya kukupa nguvu; na ni lazima ulitawale tumbo lako unapokuwa na njaa au kiu kwa sababu kula kupita kiasi (ambako wakati mwingine huleta ugonjwa wa kuhara damu)  huleta uvivu,   hukuzuia kufanya kazi na humwondoa mtu kutoka katika kila lililo zuri na utukufu, na kunywa kupita kiasi (ambako pengine huleta ulevi) humfanya mtu aonekane kwamba yu juha, njinga na aliyekwezwa.

9. HAKI YA VIA VYA SIRI:

Na ni haki ya via vyako vya uzazi kwamba uvilinde kutokana na matumizi yaliy o haramu, na kujisaidia katika kazi hii kwa kuyaangusha macho yako, kwa sababu (kuangusha macho yako) ndio msaidizi mkubwa na kwa kukikumbuka kifo na kujionya dhidi ya (hasira za) Mwenyezi Mungu na Adhabu Yake (kwa wafisadi).

Na kwa Mwenyezi Mungu kuna usalama na msaada; na hakuna nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

HAKI ZA MATENDO

Kisha hufuatia Haki za Matendo

10. HAKI YA SALA:

Na ni haki ya sala kuwa ni lazima utambue kuwa ni baraza la Mwenyezi Mungu, na kuwa wakati wa sala unasimama mbele ya Mwenyezi Mungu. Utakapotambua hivyo, kusimama kwako kutakuwa kule kwa mja wa Mwenyezi Mungu aliye mnyenyekevu, ukiwa una hamu kubwa (ya rehema za Mwenyezi Mungu), akiogopa (adhabu Yake, Mwenyezi Mungu), akihofia ghadhabu Yake (Mwenyezi Mungu),ukitegemea (kupata rehema Zake), ukiwa mkata, ukiomba (Huruma Zake), ukimheshimu yule ambaye uko mbele yake kwa utulivu na ukimya, ukionyesha heshima katika viungo, ukitoa roho yako kwake (yeye Mwenyezi Mungu), ukimwambia siri za moyoni mwako, kwa njia nzuri, ukimwomba akuache huru kutokana na dhambi zilizokufanya mtumwa na makosa yaliyo kuangamiza.

Na hakuna nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

11.HAKIYA FUNGA:

Na ni haki y a funga yako kuwa ni lazima uitambue kuwa i- pazia la Mwneyezi  Mungu aliloliweka katika ulimi wako, masikio yako, macho yako, via vyako vya siri na tumbo lako kukulinda kutokana na Moto wa (Jahanam); na imepokewa katika Hadithi (ya Mtukufu Mtume s.a.w) kuwa "Funga ni ngao ya kujikinga na Moto" Hivyo basi, kama ukivituliza viungo (vya mwili wako) na kuviweka kabisa katika pazia hili, unaweza kutegemea viungo hivyo kudumu katika hilo pazia; na kama ukiviruhusu viwe vinatokatoka katika pazia hili na kujaribu kuibua makona y a pazia  hili, ili viweze kujua kilichokuwa halali kwao kwa tazamo linalosababisha tamaa na nguvu kubwa iliyo nje ya mipaka ya Taqwa (kumwogopa) ya Mwenyezi Mungu, huwezi kuwa na uhakika kuwa haitapasua lile pazia na kwenda nje.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

12. HAKI YA ZAKA:

Na ni haki ya zaka kuwa ni akiba yako kwa Mola wako, na dhamana isiyohitajika shahidi yeyote yule. Utakapoitambua hivyo, utakuwa na matumaini katika akiba hiyo uliyoihifadhi kwa siri (yaani zaka uliyoitoa kisirisiri) kuliko ile uliyoitao hadharani; na inakufanya kuziweka siri zako kwa Mwenyezi Mungu kwa cho chote kile utakachokipendelea kukidhihirisha; na siri hii ni lazima kila mara ibakie baina yako na Yeye, na usijaribu kumfanya (mtu fulani kuwa) shahidi (ili) aone au kusikia (habari za) zaka hii. Au sivyo, itakuwa ishara ya kuwa unalo tegemeo zaidi kwa shahidi (huy o) kuliko kwa Mola wako, kuhusu malipo

ya dhamana hii kwako.

Zaidi ya hapo, usimfanye mtu yeyote kuhisi kuwa yua wajibikiwa kwako (kukutendea kitu fulaii kwa sababu umempa zaka) kwa sababu zaka hii ni kwa faida yako wewe mwenyewe. Hivyo, kama ukimfanya kuwa yua wajibikiwa kwako vipi utakuwa na uhakika kuwa wewe mwenyewe hutakuwa katika daraja lake (hapo baadaye), kwa sababu matendo yako yataonyesha kuwa hukuiweka zaka hiyo kwa ajili ya faida yako wewe mwenyewe. Kama ungelihisi hivyo kuwa zaka ile ni kwa faida yako wewe mwenye usingeliweza  kuwadai watu wengine wajibu fulani fulani.

Na hakuna nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

13. HAKI YA MNYAMA WA KAFARA:

Na ni haki ya Mnyama wa kafara kuwa atolewe kafara kwa nia safi, kwa ajili ya Mola wako, ukitafuta Msamaha Wake, na kibali chake; na sio kwa ajili ya (kuonwa na) macho yawatazamaji. Utakapotoa kafara yako kwa mujibu huu, hutakuwa onyesho na mtu mwenye kuonyesha watu, bali utakuwa mwenye kutafuta tu (radhi ya) Mwenyezi Mungu.

Na tambua kuwa Mwenyezi Mungu anatafutwa  kwa  kile unacho kiweza (wewe kukifanya) sio kwa (tafrija) ngumu; kwa maana Yeye Mwenyewe amezifanya Sheria kuwa rahisi kwa viumbe vyake, na hataki kuwaweka viumbe wake katika  magumu, na pia unyenyekevu ni bora kwako kuliko majivuno; kwa sababu majivuno na ubadhilifu ni mafungu ya wenye kujikweza. Na pia kwa unyenyekevu na haya

hakutakuwepo na makuu na uharibifu kwa sababu ni vitu vya asili navyo vinapatikana katika tabia thabiti za mwanadamu.

Na hakuna nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

HAKI ZA WAKUU

14. HAKI TAWALA

Na ni haki ya mtawala wako kuwa ni lazima utambue kuwa u jaribio kwake na kuwa yu katika kujaribiwa kwa sababu ya madaraka aliyonayo juu yako; na kuwa usimuasi kwa sababu mikono yake ni yenye nguvu juu yako na (kwa kuasi kwako), utakuwa chanzo cha maangamizi yako wewe mwenyewe na yake (kwa sababu kwa kukomesha au kukuuwa atalaaniwa na Mwenyezi Mungu).

Na itafute radhi yake kwa unyenyekevu na heshima kwa kiasi ambacho kitatosha kukuondolea madhara na ambacho hakiingilii dini yako; na omba msaada wa Mwenyezi Mungu katika kufanya hivyo.

Na usijiingize katika kumpinga au kumchukia kwa sababu kama ukifanya hivyo, hutakuwa mwenye kushukuru (kwa sababu umej ifanya kuwa dango kwa kufanyia udhalimu wake), na hivyo hunabudi kuhesabiwa kuwa u msaidizi wake dhidi yako (wewe mwenyewe) na mshirika wake katika kila anachokitenda dhidi yako.

Na hakuna nguvu yo yote ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

15. HAKI YA MWALIMU:

Na ni haki ya mwalimu wako kumheshimu na kuiheshimu heshima ya wasikizi wake na kumsikiliza kwa makini ukimwelekea na kumsaidia akufundishe elimu (ambayo huwezi kukaa bila ya kuwa nayo) kwa kumpa akili zako, na kuwepo kwa fikara zako na usafi wa moyo wako, na usafi wa kuona kwako, kwa kutojitia katika starehe na kwa kuwa na tamaa chache.

Na ni lazima utambue kuwa u mjumbe wake (katika kila anachokufundisha) kwa watu wale wasiojua ambao wanaweza kukujia (ili wajifunze elimu hiyo). Hivyo basi, ni lazima kwako kuutoa ujumbe wake (kuitoa elimu hiyo) na kuwapa (watu hao) kwa njia nzuri, na bila ya kuvunja uaminifu wakati unapoutoa ujumbe wake, na kutimiza wajibu wako kwa niaba yake unapotukia kuchukua wajibu huo.

Na hakuna uwezo au nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

16. HAKI YA TAJIRI WAKO:

Haki ya tajiri wako ni kama ile ya mtawala wako, ila tu kwamba tajiri wako anayo madaraka zaidi juu yako kuliko mtawala  wako. Ni lazima umtii katika mambo yote makubwa na madogo, ila tu inapotukia kuwa kumtii kwako kunakuwa kinyume na kumtii Mwenyezi Mungu na kunazuia kutimiza wajibu wako kwa Mwenyezi Mungu na viumbe wake. (Inapokuwa hivyo, usimtii na ni lazima utimize huo mujibu tulio utaja). Lakini baada ya kutimiza wajibu huo, ni lazima utimize wajibu wako kwake (huyo tajiri wako); na jishughulishe na wajibu huo.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

HAKI YA WENYE KUKUTEGEMEA

Kisha hufuatia haki za wenye kumtegemea mtu.

17. HAKI YA RAIA:

Na ni haki ya raia wako kuwa ni lazima ukumbuke kuwa umewashinda ikiwa ni matokeo ya nguvu yako nani raia wako kwa sababu ya unyonge na unyenyekevu wao. Hivyo, jinsi gani ahitajivyo huruma, ulinzi, na uvumilivu mtu yule ambaye kwa unyonge wake na unyenyekevu wake ameifanyakazi yako kwa ajili yako katika kumfanya kwako kuwa raia wako na kumlazimisha sana azitii amri zako (ulizoziweka) juu yake; kiasi ambacho sasa hana msaada wala nguvu yoyote ile dhidi yako na hawezi kupata msaidizi yeyote yule (kama ukimtia matatani) ila Mwenyezi Mungu tu. Na jinsi gani unavyohitaji kumshukuru Mwenyezi Mungu unapozifurahia Neema zake Mwenyezi Mungu kwa kukupa nguvu yake na uwezo. Na yule mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu huzizidisha baraka Zake kwake.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

18. HAKI YA MWANAFUNZI:

Na ni haki ya wenye kukutegemea katika elimu kuwa ni lazima utambue kuwa Mwenyezi Mungu kakufanya kuwa bwana wao kwa kukupa elimu na kukupa hazina ya hekima. Hivyo kama u mkarimu katika huu ujumbe aliokupa Mwenyezi Mungu, na ukiwa mdhamini mkarimu mwenye kumtakia mema bwana wake katika kuwatunza vizuri waja wake (na ambaye yu) mvumilivu na mwenye kuangalia vya

kutosha katika kuleta utajiri wa mkono wake (hazina ya elimu) kila unapomwona mwenye kuhitaji (elimu hiyo) utakuwa mtu mwema na utakuwa na tegemeo na imani ya kweli. Au siyo utakuwa mkosefu wa wizi (wa Elimu uliyopewa dhamana na) Mwenyezi Mungu, na mdhalimu kwa viumbe Vyake; na utastahili kunyang'anywa (elimu hii) na heshima (pia).

19. HAKI YA MKE:

Ni haki ya mkeo kuwa ni lazima utambue kuwa Mwenyezi Mungu amemfanya kuwa utulivu na starehe kwako (katika hofu) na rafiki na ngao (dhidi ya dhambi).

Na, hivyo hivyo, ni wajibu kwenu ninyi wote wawili (mume na mke) kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mkeo au mumeo kutambua kuwa yu Neema ya Mwenyezi Mungu juu yako.

Na ni wajibu wako kuwa na ushirikiano mzuri na hii Neema ya Mwenyezi Mungu (yaani mke) na kumheshimu na kumhurumia (japo kuwa haki zako za kuwa mumewe kwake) ni kubwa na utii wake kwako humalizikia kwenye matakwa yako na unayoyachukia (yaani afanye upendavyo na asitende uchukiavyo) iwapo si dhambi. Hivyo astahili mapenzi na ushirikiano; na mahali pa kupumzikia (yaani nyumba) ili kuwa tamaa za kiasili ziweze kutimizika na huo wenyewe ni wajibu mkubwa.

Na hakuna uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

20. HAKI YA MTUMISHI:

Na ni haki ya yule unayemtegemea kiutumishi kumtambua kuwa yu kiumbe wa Mola wako na kuwa yu pande la Mwili wako na damu yako, ingawa u bwana wake.

Sio kuwa umemuumba wala hukuyatengeneza masikio yake au macho yake wala hukumpa wewe riziki zake. Bali ni Mwenyezi Mungu aliyemfanyia yote hayo na kisha akamfanya kuwa mwenye kukutegemea naye akiwa dhamana kwako: ili kuwa uiangalie dhamana ya Mwenyezi Mungu kwa niaba yake na mtendee sawa na yale Mwenyezi Mungu awatendeavyo viumbe wake (yaani kwa mapenzi na uangalifu.

Hivyo umlishe kwa kile unachokila; na kumvisha kile unachokivaa; na usimtake asichoweza kukutendea. Na kama humpendi, jitoe katika kutimiza wajibu wako kwake (ulio uwekewa na Mwenyezi Mungu) kwa kumbadilisha na mwingine lakini usikiadhibu kiumbe cha Mwenyezi Mungu.

HAKI ZA NDUGU

21. HAKl YA MAMA:

Tukizijia haki za ndugu, ni haki y a mama yako kuwa ni lazima utambue vyema kuwa alikuchukua kwa kiasi ambacho hakuna mtu y e yote yule awezaye kumchukua mwingine zaidi ya hapo(yaani katika tumbo lake la uzazi), na kukulisha matunda ya moyo wake ambayo hakuna mtu yeyote yule mwingine amlishaye mwingine kwayo na akakuhifadhi (wakati wa ujauzito) kwa masikio yake, macho yake, mikono yake, miguu yake, nywele zake, viungo vyake, (kifupi ni kuwa alikulinda) kwa uwezo wake wote tena kwa furaha, kwa moyo mkunjufu na kwa uangalifu; akizivumilia hofu zote. maumivu yote, shida zote na huzuni zote za (ujauzito), mpaka mkono wa Mwenyezi Mungu ulipo kuondoa katika mwili wake, na kukuleta katika ulimwengu huu. Hapo alifurahi sana akikulisha wewe (na kuisahau njaa yake), akikuvika (japo kuwa yeye mwenyewe hakuwa na nguo), akikunyonyesha maziwa na maji (bila ya kujali kiu yake yeye mwenyewe). akikuweka kivulini, (japo kuwa ilimbidi yeye mwenyewe kutaabika kwa joto la jua), akikupa kila faraja kwa taabu zake yeye mwenyewe, akikuweka ulale na yeye mwenyewe akibakia kuwa macho.

Na (kumbuka kuwa) tumbo lake la uzazi lilikuwa maskani yako, na mapaja yake yalikuwa makimbilio yako, na matiti yake yalikuwa chombo cha kukulishia na uzima wake wote ni hifadhi yako; ndiye yeye, wala si wewe, aliyekuwa na moyo wa ushujaa katika kuupoza huu ulimwengu ili kupata usalama.

Hivyo basi, ni lazima ubakie kuwa mwenye shukrani kwake kwa ajili hiyo na huwezi kumshukuru ila kwa msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

22. HAKI YA BABA:

Na ni haki ya baba yako kutambua kuwa  yu  mzizi wako na wewe  u matawi y ake; na kuwa ulikuwa kitu kisichokuwepo (ila kwa ajili yake umekuwepo). Hivyo basi, kila unapoona kitu kinachokupendeza, kumbuka kuwa baba yako ndiye chanzo cha zawadi hii (ya Mwenyezi Mungu kwako), Na kuwa mwenye shukrani kwa Mwenyezi Mungu na mwenye shukrani kwa baba yako kwa ajili hiyo,

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

23. HAKI YA MTOTO:

Na ni haki ya mtoto wako kutambua kuwa anatokana nawe, na kuwa, kwa matendo yake mazuri au mabaya anahusika nawe katika ulimwengu huu; na kuwa wewe unapaswa kumfundisha tabia nzuri, kumuongoza kuelekea kwa Mola wake, umsaidie katika kuzifuata amri Zake (Mwenyezi Mungu) zinazohusu wewe au yeye; na utapata thawabu au utaadhiiwa (kutegemeana na kufaulu kwako au kushindwa kwako katika uongozi huu).

Hivyo basi, ni lazima ujitahidi katika kumuelimisha kama vile afanyavyo mtu ambaye atarembeshwa kwa athari zake (kwa mwanawe) katika ulimwengu huu (na anayetaka) kuthibitisha mbele ya Mola wake kuhusu madaraka yake kwa mtoto (wake), kwa ulezi wake mzuri na kwa kuzichukua haki za Mwenyezi Mungu kutoka kwa mtoto huyo.

Na hakuna uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

24. HAKI YA AKHI:

Na ni haki ya akhi (ndugu mume) wako kutambua kuwa yu mkono wako unaonyoosha, na (mwega wa) mgongo wako unaoutegemea, na uwezo wako unaoutegemea, na nguvu yako ambayo kwayo unashambulia (adui wako). Hivyo basi, usimfanye kuwa zana ya kufanyia dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu wala njia ya kuzivunjia haki Zake (Mwenyezi Mungu); na usijitoe katika kumsaidia dhidi ya nafsi yake (yaani katika kumuonya ayatambue maovu) na kumsaidia dhidi ya adui zake na kumhifadhi na Shaitani, na kumshauri kwa uaminifu na kumwendea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Kisha kama akimtiii Mola wake na akiuitika barabara wito wa Mwenyezi Mungu (itakuwa bora kwenu nyote); au sivyo; (mchague) Mwenyezi Mungu, badala ya akhi wako, kuwa chaguo lako la heshima yako (yaani, kama akhi wako akienda kinyume na Sheria na akakataa kuyasikiliza mashauri yako na nasaha zako, ni lazima usiwe na uhusiano wowote naye).

25. HAKI YA ALIYE KUHURlSHA:

Na ni haki ya mtu yule aliye kuhurisha  kutambua kuwa alitumia mali yake kwa ajili yako na kisha akakutoa katika fedheha na ukiwa wa utumwa na kukuweka  katika heshima na furaha ya uhuru; na amekuhurisha kutokana na kifungo cha utumwa, na kufanya manukato ya heshima yawe yenye kupatikana kwako na kukutoa katika jela ya udhalimu na kuondoa shida, ameufungua ulimi wake wa haki kwa faida yako, na amekufungulia ulimwengu  mzima; na amekufanya kuwa bwana juu yako wewe mwenyewe, na kuzifungua nyororo zako, na amekupa nafasi ya kumuabudu na kumtii Mola wako peke yake (bila ya haja yoyote ya kutumia sehemu ya muda wako katika kumtumikia bwana wako); na kwa kukuhurisha amepata hasara ya pesa zake.

Hivyo basi, ni lazima utambua kuwa, baada ya ndugu zake, yeye (mtu huyu aliyekuhusisha) yu (mbora kwako) zaidi ya mtumwingine ye yote yule, anazo haki kwako, katika uhai wako na katika kifo chako, na yu mtu astahiliye zaidi msaada wako, kwa ajili ya (kutafuta radhi ya) Mwenyezi Mungu. hivyo basi, kama akihitaji chochote kutoka kwako, usikione kuwa ni bora kuliko yeye.

26. HAKI YA HURIA:

Na ni haki ya huria (wako) kutambua kuwa Mwenyezi Mungu amekufanya  kuwa hifadhi yake, ngao yake, msaada wake na kimbilio lake; na (Mwenyezi Mungu) amemfanya (huyo huria) kuwa msuluhishi kati yako na Mwenyezi Mungu

Hivyo basi, ni haki kwamba,Yeye (yaani Mwenyezi Mnngu) akuhifadhi kutokana na moto (yaani kwa kumhurisha yule mtu, unajipatia uthibitisho dhidi ya moto wa Jahannam).

Hivyo, huku kumhurisha kutaleta thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, katika maisha ya Akhera; na katika ulimwengu huu, Mwenyezi Mungu amekupa urithi wake (mtu huyu uliyemhurisha) kama hana ndugu kabisa. Udugu huuu katika kuufikiria utajiri ulio utumia kwa ajili yake na katika kukufikiria kule kumpa (kwako) haki zake, (kwa kumhurisha) japo kwa kupoteza kitu muhimu.

Kwa upande mwingine, kama humjali, inahofiwa kuwa urithi wake hautaonekana kuwa ni wenye kupasika nawe.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

27. HAKI YA MFADHILI:

Na ni haki ya Mfadhili wako kuwa umshukuru na kuzikumbuka fadhili zake (alizokutendea) na mtangaze (mfadhili wako huyo) kwa maneno mazuri  na muombee kwa uaminifu kati  yako na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu,  kama ukifanya hivyo utakuwa umeshukuru kwa uaminifu dhahiri kabisa. Baada ya hapo,kama inawezekana kumlipa fadhili zake kwa matendo yako basi fanya hivyo, au sivyo, basi jaribu kutafuta nafasi ya uwezekano wa kufanya hivyo (Kumlipa fadhili zake) kwa moyo wako wote.

28. HAKIYA MUADHINI:

Na ni haki ya Muadhini kukumbuka kuwa anakukumbusha Mola wako na anakuita kupata fungu lako (katika Rehema za Mwenyezi Mungu) na kuwa  yu  msaidizi wako mkuu katika kutimiza wajibu wako ulio wekewa na Mwenyezi Mungu. Hivyo, ni lazima umshukuru kwa ajili hiyo, kama vile unavyomshukuru mtu aliyekufanyia huruma; na hata kama uko nyumbani mwako, na unamdhania (mabaya) usimtweze kwa kazi yake (anayoifanya) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; na fahamu kuwa bila ya shaka yoyote ile, yeye yu Rehema za Mwenyezi Mungu kwako. Hivyo basi, ni lazima uwe mwenye huruma na mwenye adabu kwake, ukimshukuru Mwenyezi Mungu kwa Rehema hizi vyo vyote vile iwavyo.

Na hakuna nguvu  yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

29. HAKI YA "IMAMU"

Na ni haki ya Imamu wa sala yako kuwa ni lazima utambue kuwa amechukua jukumu la kuwa balozi wako mbele ya Mungu na mjumbe wako kwa Mola wako; amezungumza kwa niaba yako lakini wewe hukuzungumza kwa niaba yake; hukumsalia lakini yeye kakusalia; na kakuombea (kwa Mwenyezi Mungu) lakini wewe hukumuombea; amekuokoa kutoka katika" fadhaa ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu  na  kumuomba wewe mwenyewe, lakini wewe hukumuokoa kutokana na fadhaa hii. Hivyo kama upo upungufu wowote ule katika tendo lolote lile kati y a mtendo hayo yaliyotajwa hapo juu, ni yeye wala si wewe atakaye ulizwa kuhusu kosa hilo; kama alifanya kosa, wewe hutashirikiana naye katika kosa hilo (ingawa wewe hu mbora kuliko yeye). Hivyo, ameiokoa nafsi yako kwa nafsi yake na ameiokoa sala yako kwa sala yake; hivyo ni  lazima uwe  mwenye kushukuru kwa haya aliyokutendea.

Na hakuna nguvu wala uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu.

30. HAKI YA MWENZI:

Na ni haki ya mwenzi  wako kuwa uwe mpole (kwake) na mwenye kupatana naye, na kumtendea haki katika mazungumzo, na unapomtazama usitoe macho yako kutoka kwake mara moja na unapozungumza shabaha yako ieleweke kabisa.

Na kama umekwenda kukaa (kuzungumza) naye  uko huru kuondoka (wakati wowote ule); lakini kama yeye amekuja kukaa pamoja (kuzungumza) nawe, anao uhuru wa kuchagua (kubakia hapo au kwenda) na (katika hali hii) usiamke kutoka katika kikao hicho bila ya ruhusa yake.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

31. HAKI YA JIRANI:

Na ni haki ya jirani yako kuyalinda (mambo yake) wakati awapo hayupo, na kumheshimu uwapo mbele yake, na kumsaidia awapo au asipokuwepo. Usizichunguze aibu zake (zilizo jificha) na usiyajasusi  mambo yake ili kuzijua fedheha zake. Na kama ukitukia kuzigundua kwa bahati mbaya bila ya kuzijasusi, uwe ngome isiyo penyeka (ili kuyaficha) yale uliyo yajua na uwe kizibo kizito (kwa ajili ya kuzificha siri hizo) kiasi ambacho kama mikuki ikiuchoma moyo wako ili kuyapeleleza mambo hayo, haiwezi kuifikia siri hiyo (kwa sababu umeihifaki barabara). Usimpeleleze anapokuwa mzembe. Usimuache katika matatizo na usimuonee kijicho (awapo) katika raha, Msamehe makosa yake na yabeue maneno yake. Na karna anakufedhehesha hapo usiusahau uvumilivu wako, bali zungumza naye kwa amani. Uwe  ngao yake dhidi ya ulimi wa matusi, na hifadhi yake kutokana na udanganyifu wa watu wale wajifanyao kuwa ni waaminifu (lakini kwa hakika wao si waaminifu kwake). na aishi naye maishamazuri.

Na hakuna nguvu yo yote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

32. HAKI YA RAFIKI:

Na ni haki ya rafiki yako kuisihi naye vizuri kwa kadri iwezekanavyo na kama haiwezekani, basi ishi naye kwa uadilifu; na kuwa umheshimu kama anavyokuheshimu, na mhifadhi kama anavyo kuhifadhi; na jaribu kwa kadri y a uwezo wako kwamba asikuzidi katika tendo zuri lolote lile kati yako na yeye; na kama anakupita ni lazima ulipize (kwa tendo zuri); na usimpe mapenzi kidogo kuliko yale anayostahili kuyapata kutoka kwako. Kila mara hakikisha kuwa unabakia kuwa mwaminifu kwake, unamhifadhi unamsimamia katika kumtii Mola wake, na kumsaidia katika mambo yake ya kibinafsi yasiyo kinyume na amri za Mola wake. Na, mwisho kabisa, ni lazima uwe rehema kwake badala ya kuwa kitisho kwake.

33. HAKI YA MWENZI:

Na ni haki ya mwenzi wako kuwa ni lazima ulichukue jukumu lake wewe mwenyewe awapo hayupo, na kufanya kazi sawa na vile afanyavyo awapo yupo. Na usiamue jambo lolote bila ya idhini yake na usitoe mawazo yako bila ya kupata mawazo yake kabla; na muokolee utajiri wake; na zile fedha zake dhidi ya wizi (ni mamoja kama wizi huo ni mkubwa au mdogo), kwa sababu (desturi hii imetufikia kutoka kwa wahenga wetu); "Hakika Mkono wa Mwenyezi Mungu (yaani Baraka zake) uko juu ya washiriki kwa kadiri waabakiavyo katika kutodanganyana.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

34, HAKI YA UTAJIRI:

Na ni haki ya utajiri kuwa huupati ila kwa kutumia njia halali na usiutumie (yaani usiutumie kwa matumizi yaliyoharimishwa); na usiuondoe kutoka kwenye ukweli (yaani usidanganye katika hesabu na usiutumie kiharamu), Na. utajiri unapotokana na Mwenyezi Mungu (kama vile ulivyo kila utajiri) usiutumie ila kwa (kumfikia) Mwenyezi Mungu na ufanye (utajiri huo) kuwa njia ya kufikia kwa Mwenyezi Mungu.

Na usiufanyie ubahili kwa kuishi maisha magumu, na kutolipa wajibu wa kidini, kuuhifadhi kwa ajili ya mtu (yaani mrithi wako), ambaye inawezekana kuwa atakataa hata kukushukuru kwa utajiri huo. Pengine hatakuwa mrithi mwema kwa urithi wako, na hatautumia katika njia ya Mola wako. Hivyo utakuwa msaidizi wake katika hayo madhambi na maasi. Na kama katika kuutumia utajiri huo ambao mwanzoni ulikuwa wako, akayajali matamanio yake (wenyewe), katika kumtii Mola wake, basi atachukua faida zote (za kiroho) na wewe (huko Akhera) utauchukua uzito wote wa dhambi; huzuni, na aibu zaidi ya yale matokeo yake kwa sababu umeufanyia ubahili kinyume na hukumu za sheria (za dini),

Na hakuna nguvu  yoyote  ila kwa Mwenyezi Mungu.

35. HAKI YA MWIA:

Na ni haki ya mwia wako anayetaka umlipe deni ambalo, kama ukimlipa kwa ukamilifu na ukampa kile anachostahili kupewa na ukamfanya kuwa asiye kutegemea; na usimfanye kukimbia katika  mzunguko (kati ya nyumba yake  na  y ako kudai hilo deni lake) na usichelewe (kulipa), kwa sababu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu (s.a.w) amesema, "Kuchelewa kwa tajiri (katika kulipa madeni) ni udhalimu.

Na kama una matatizo basi ni lazima umridhishe (ili akupe muda zaidi) kwa maneno ya upole na umuombe kwa upole akuongezee muda na arudi kwa ukarimu; na usimfanye ataabike kwa sababu yako zaidi ya kule kupoteza pesa kwa sababu (kufanya hivyo) ni choyo.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

36. HAKI YA MSHIRIKA:

Na unawiwa na Mshirika wako kuwa usimdanganye au kumpunja, wala usiseme uongo kwake, usimlaghai, au kumfanya asiyejali. Usijifanye Kwake (kwa nia ya kutaka kumvunja nguvu) kama vile afanyavyo adui asiyekuwa na huruma. Na kama akikuamini jaribu kwauwezo wako wote kumthibitishia (kuukubali kwako) mwamana wake na utambue kuwa kuvunja mwamana ni riba.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

37. HAKI YA MDAI (HAKI):

Na ni haki ya mdai (haki) dhidi yako kuwa kama dai lake dhidi yako ni la haki usijaribu kuzivunja hoja zake na usijaribu kulikanusha dai lake kwa juhudi nyingi, Badala yake, ni lazima ujipinge mwenyewe kwa ajili yake, na uwe hakimu dhidi yako wewe mwenyewe, nauwe shahidi wake kwa ajili ya dai lake bila ya haja yoyote ile ya kuwepo shahidi mwingine kwa kuwa ni wajibu uliowekwa na Mwenyezi Mungu.

Na kama dai lake si la haki, basi zungumza naye kwa wema na iweke hofu (ya Mweny ezi Mungu) moyoni mwake na mpe kiapo kwa jina la dini yake na mpunguze makali yake dhidi yako kwa kumkumbusha Mwenyezi Mungu; na epuka maneno yasiyo na maana, kwa kuwa maneno kama hayo hayawezi kuondoa uadui kwa mpinzani wako na (zaidi yake) utakuwa umefanya dhambi (ya kutumia lugha isiyokuwa nzuri); ukinzani wako utaongezeka, kwa sababu ya maneno hayo ukali wa upanga wa uadui wake dhidi yako utaongezeka kama vile maneno maovu hujenga uovu, na maneno ya heshima huung'oa uovu.

Na hakuna uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

38. HAKI YA MWENYE KUKUTEGEMEA:

Na ni haki ya mtu ambaye umempelekea dai lako, kuwa  iwapo dai lako ni la haki uzungumze naye kwa ukarimu kwa kulielezea wazi wazi lile dai lako kwa sababu mlio wa dai peke yake ni mkali mno (hivyo usiongezee juu yake ufedhuli wa lugha yako tena); na zielezee hoja zako kwa uzuri; mpe muda, mazungumzo yako yafanye kuwa yaliyo wazi wazi, na kuwa mwenye huruma kwake.

Na usitoke katika uthibitisho wako (wa ukweli wa dai lako) kwa kugombana kwa maneno yasiyo ya lazima, kwa maana unaweza kupoteza njia ya haja yako bila ya kupata faida yoyote ile.

Na hakuna uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

39. HAKI YA MWENYE KUTAKA USHAURI:

Na ni haki ya mtu anayetaka ushauri wako kuwa, kama unao ushauri wowote kwake, basi uwe mwaminifu kwake na mpe ushauri ambao, kama ungelikuwa wewe (unayetafuta ushauri huo) ungeliufuata; na (ushauri) ni lazima utolewe kwa adabu na kwa upole, kwa maana upole hukugeuza kutozoeana kuwa urafiki na ufedhuli huwafanya marafiki kutozoeana.

Na kama hufikirii ushauri wowote ule kwake lakini unamfahamu mtu fulani ambaye uamuzi wake unauamini (na ambaye unaweza kumtaka ushauri kwa furaha kuu kama jambo hilo ukiliachiwa), ni lazima umuongoze huyo anayetaka ushauri wako kwa mtu huyo. Kwa kufanya hivyo utakuwa huzitengi huruma zako kutoka kwake, na kuuficha utu wema wako kutokwa kwake.

Na hakuna uwezo au nguvu yoyote ile ila Mwenyezi Mungu tu.

40. HAKI YA MSHAURI:

Na ni haki ya mshauri wako kuwa kama ushauri wake hauafikiani na maoni yako wewe mwenyewe, na huuhisi uaminifu wake wowote ndani yake, kwa sababu ni kumtaka ushauri tu na watu hutofautiana mmoja hadi mwingine kuhusu jambo hilo. Hivyo kama huafikiani naye, basi una uhuru kabisa wa kufuatia maoni yako mwenyewe; lakini si vizuri kwako kumdhania mabaya ambapo ulimfikiria  kuwa anafaa kumtaka ushauri. Na usisahau kumshukuru maana kwa wema wake anakupa maoni yake na ushauri wake mzuri mno.

Na kama ushauri wake unaafikiana na maoni yako wewe mwenyewe, basi mshukuru Mwenyezi Mungu na upokee kutoka kwa ndugu yako, yaani huyo mshauri kwa shukrani.

Na kama wakati fulani (baadaye mtu huyo) atahitaji ushauri wako, mshauri kwa uaminifu kama alivyokufanyia.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu.

41. HAKI YAMHUBIRIWA:

Na ni haki ya mtu anayekuomba uongozi (wa kidini) kuwa, ni lazima umhubirie kufuatana na mahitaji yake na uwezo wake katika njia yenye kuafikiana na usikivu wake (yaani katika lugha ya kuvutia), na zungumza naye kwa njia ikubalianayo na akili (za binadamu), kwa kuwa kila mwenye elimu huyatambua na kuyakubali mazungumzo yanayo Ungana na elimu yake. Na njia yako (yakumhuburia) iwe katika ukarimu.

Na hakuna uwezo wowote ila kwa Mwenyezi Mungu.

42. HAKI YA MHUBIRI:

Na ni haki ya mtu anayekushauri kuwa ubakie kuwa mnyenyekevu kwake, na uweke moyo wako katika mazungumzo yake na kufungua masikio yako kueleke mwito wake, ili uweze kuyaelewa mazungumzo yake.

Kisha yatazame mazungumzo hayo kwa uangalifu. Kama yu sahihi, Mshukuru Mwenyezi Mungu, na ukubali ushauri wake na mheshimu mtu huyo kwa ajili ya ushauri wake huo. Na kama hukuweza kuuona ukweli, kuwa na huruma juu yake na usimlaumu. Ni lazima ukubali kuwa hakukunyima ushauri wake ingawa mawazo yake yamekosewa. Kama unajua kuwa mtu huyo si mwaminifu kwako basi hapo itakuwa tofauti na hayo, lakini kwa sababu hiyo, usimsikilize kwa vyovyote vile.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

43. HAKIYA MTU ALIYE KUZIDI UMRl:

Na ni haki ya mtu aliyekuzidi umri kuwa ni lazima umstahili kwa sababu ya umri wake, na umheshimu kwa sababu ya Uislamu wake (kama anayo Fadhila yoyote upendeleo wa Uislamu) kwa kumuweka mbele kila mara na usibishane naye katika mazungumzo na usijaribu kutaka kumpita uwapo naye katika matembezi na usimtangulie utembeapo naye njiani; na usiwe mfidhuli na mvumilie awapo mfidhuli kwako na endelea kumstahi kwa sababu umri wake ni mkubwa katika Uislamu (kwa sababu thamani ya umri ni kwa mujibu wa thamani ya Uislamu),

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

44. HAKI YA ULIYEMZIDI  UMRI:

Na ni haki ya mdogo wako kwa umri kuwa umpende kwa kumlea na kumuelimisha vizuri; na kumsamehe na kumfichia makosa yake; kuwa mpole kwake na yafiche makosa ayatendayo kwa sababu  ya  umri  wake  mdogo (kwa sababu  upendo kwake na upole ndio njia yake ya kutubia) na mvumilie na usimshawishi (katika kutenda makosa kwa sababu kufanya hivyo kuwa karibu mno na mwongozo wake).

45. HAKl YA MTU ANAYE OMBA:

Na ni haki ya mtu anayeomba (msaada) kuwa, (kama unauamini ukweli wake na unao uwezo wa kumtimizia haja yake) ni lazima umpe (huo, msaada aliouomba) na mwombee ili matatizo yake yamalizike; na msaidie kufuatana na ombi lake.

Na kama unashaka kuhusu ukweli wake na, kwa sababu ya alivyokutendea kabla humwamini (lakini huna uhakika kuwa anakudanganya wakati huu nao),basi jihadhari; pengine hii shaka yako ni mtego wa shetani anayetaka kukutenga mbali na sehemu yako (ya Thawabu) na anataka kuja katikati yako na heshima yako mbele ya Mwenyezi Mungu. Vivyo, kama ukiamua kutomsaidia basi mwache (bila ya kumwaibisha) na mwache aende kwa ukarimu, Na kama ukibadili shaka ya moyo wako juu yake na kumpa chochote kile uonacho kama chamfaa, basi hiyo ni amali njema.

46. HAKI YA AOMBWAYE:

Na ni haki ya mtu uliyemuomba akusaidie  kuwa, kama akikupa (msaada huo), basi ipokee zawadi yake kwa shukurani ukiufurahia ukarimu wake, na (kama hakukupa), basi zikubali sababu zake za kutoweza kukusaidia na uwe na imani naye.

Na kumbuka kuwa kama akikunyima msaada huo, msaada huo ni mali yake ambao amekunyima na hawezi kulaumiwa kuhusu utajiri wake (kama hakuutoa), Na kama akikunyima utajiri huo kidhalimu, basi unajua kwa "Hakika mwanadamu yu mdhalimu mkubwa, asiyekuwa na shukurani hata kidogo".

47. HAKI YA MTU ALIYE KUFURAHISHA:

Na ni haki ya mtu yule ambaye kupitia kwake, Mwenyezi Mungu amekufurahisha kuwa, (kama mtu huyo alifanya hivyo akiwa yu ajua) ni lazima umshukuru Mwenyezi Mungu kwanza, kisha umshukuru yeye naye kwa kukufanyia wema na jaribu (upatapo nafasi ya kumlipa hisani yake na kumfanyia hata zaidi ya hayo, kwa maana alikuwa na ukarimu wa kuanza  kukufanyia hayo, kwa maana alikuwa na ukarimu wa kuanza kukufanyia hisani (kwa maana hisani zake kwako hazikuwa badala ya hisani zozote zile ulizo mtendea kabla). Na tafuta nafasi fulani ya kumfurahisha.

Na kama mtu yule alikufanyia hisani hizo (zilizokufurahisha) bila kukusudia na bila kujua, ni lazima umshukuru Mwenyezi Mungu na uwe mwenye shukurani kwake (yeye Mwenyezi Mungu), ujue kuwa hisani hizo zimetoka kwa Mwenyezi Mungu aliyezihifadhi kwa ajili yako. Vivyo ni lazima umpende mtu yule (ambaye kwa mkono wake Mwenyezi Mimgu amekutumia furaha ile) kwa sababu alikuwa njia ya kuiletea rehema ya Mwenyezi Mungu kwako na mwombee furaha hata ya huko Akhera kwa sababu chanzo cha baraka za MwenyezLMungu popote pale ilipo, yenyewe ni rehema.

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

48. HAKI YA MTU ALIYE FANYA UDHAUMU:

Na kuhusu mtu aliyekuwa mdhalimu kwako kwa maneno au kwa matendo, kama alifanya hivyo akiwa anajua na kwa kudhamiria basi kumsamehe ni bora zaidi kwako kwa maana kufanya hivyo kutang'oa uadui kati yenu ninyi watu wawili. Na zaidi ya hapo, wako watu wengi hapa duniani na ni bora kuwatendea mambo mema, na Mwenyezi Mungu Anasema:

"Na ajikingaye (katika kulipiza kisasi) baada ya kudhulumiwa, basi hawa ndio (ambao) juu yao hakuna lawama.   !lBasi kwa hakika (lawama) iko juu ya wale wanaodhulumu watu na (ambao) huasi duniani pasipo haki hao ndio watakaopata adhabu iumizayo.

"Na anayesubiri na kusamehe, bila shaka hilo ndilo jambo kubwa (Qur'an 42:41:43)

Na tena Mwenyezi Mungu Anasema:-

"Na kama mkiadhibu, basi adhibuni sawa na vile mlivyoteswa; lakini kama mkisubiri, hakika hiyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri" (Qur'ani 16:126).

Yote hayo yanahusu mtu yule aliyekufanyia udhalimu ule kwa kukusudia, Bali kama haikuwa kwa kukusudia, basi usimtese kwa kulipiza kisasi cha kosa lisilokusudiwa kwa adhabu iliyo kusudiwa.

Kuwa mvumilivu kwake na mwache ajirudi (kutokana na makosa yake) kwa njia ya kikarimu mno.

49. HAKI YA WAISLAMU WENZIO

Na ni haki ya wafuasi wenzio wa dini kuwa na fikara za amani kwao kwa ujumla na kuzitandaza mbawa za rehema juu yao; kuwa mpole kwa wakosefu miongoni mwao na kuwakosoa kwa kuwafanya wakupende; kuwa mwenye kushukuru kwa wale walio wema katika tabia zao au walio wakarimu kwako kwa sababu wema wa tabia zake (bila ya faida maalum yoyote kutoka kwako), wenyewe ni ukarimu kwako kwa maana kufanya hivyo amekuokoa kutokana na utovu wake wa adabu. Na jaribu sana kujiokoa kutokana naye, na jiepushe na matata yake.

Hivyo basi waombee wote wakati wa kusali na uweke tayari tayari msaada wako kwao wote na waheshimu Waislamu wote kufuatana na vyeo vyao maalum. Waweke watu wazima katika cheo cha baba yako, wadogo katika cheo cha mwanao, na wahirimu yako katika cheo cha ndugu yako.

Hivyo, yeyote yule akujiaye muonyeshe ukarikmu na upendo wako; na mpashe habari nduguyo (Mwislamu) kila kilicho wajibu kwa ndugu kuhusu nduguye.

50. HAKI YA WATU WASIO WAISLAMU (DHIMI):

Na ni haki ya watu wasio waislamu (Dhimi -dhimi ni Myahudi Mkristo au Majusi anayeishi katika nchi ya Kiislamu. Makafiri wa aina hii hupewa hifadhi maalum na Waislamu, lakini makafiri wengineo hawapewi hifadhi ya Kiislamu) wanaoishi katika nchi ya Kiislamu kuwa ni lazima ukubali kile ambacho Mwenyezi Mungu amekipokea kutoka kwao na ni lazima utimize wajibu ambao Mwenyezi Mungu amewawekea; na kuhusu (sheria za Mwenyezi Mungu juu ya) wajibu wao; na kama lipo jambo lolote lile kati yao na ninyi, basi liamueni kufuatana na sheria za Mwenyezi Mungu hata kama ni kinyume na faida yenu. Na ni lazima kiwepo kizuizi  kinachokukingieni kuwafanyia udhalimu, kuwanyima hifadhi ya Mwenyezi Mungu, na kudhihirisha kifungo cha Mwenyezi Mungu na MtumeWake (s.a.w) juu yao. Kwa sababu tumeambiwa kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w)) amesema, "Yeyote yule amfanyiaye udhalimu mtu asiye Mwislamu aliyehifadhiwa na Waislamu huwa adui wake (katika siku ya Hukumu).

Hivyo mwogopeni Mwenyezi Mungu (na Wafanyieni uadilifu).

Na hakuna nguvu yoyote ile ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

Hivyo hizi ni Haki Hamsini zilizokuzunguuka, ambazo kwa hali yoyote ile huwezi kuziepuka; ni wajibu wako kujiambatanisha nazo, na kujitahidi mno kuzitoa na tafuta msaada wa Mwenyezi  Mungu (ambaye Umetukuka Utukufu Wake). Na hakuna uwezo wowote ule ila kwa Mwenyezi Mungu tu.

Na Sifa zote na Shukrani Zamstahiki Mwenyezi Mungu tu, Mchunga wa Walimwengu,