Bismihi Ta'ala

WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI

UTANGULIZI

Tofauti  kubwa  iliyopo baina ya  Waislamu  wa  Kishia  na Waislamu wa  Kisunni  ni juu  ya imani  ya Ukhalifa  na  Uimamu  baada ya  kuondoka  kwa  Mtukufu Mtume  Mohammad  (SA.W.W). Sisi waislamu  wa  Kishia  tunaamini  kuwa  Imam Ali  bin  Abi Talib (a.s)  ni  khalifa  na Imam  wa  kwanza  baada ya  Mtume (S.A.W.W)  ambapo  ndugu zetu Waislamu wa Kisunni  wanaamini  kwamba  Seyidina  Abubakar ( r.a.) alikuwa  ni khalifa  wa kwanza.

Ingawa  kuna  tofauti  nyingine  ndogo  ndogo  zilizopo  baina  ya  madhehebu  makubwa ya  Kiislamu  (Shia  na Sunni)  kwa  mfano katika  sheria  (Fiqh)  kama  vile  kukunja mikono  wakati  wa kusali  au  kuinyoosha  n.k.  lakini  hizi  ni tofauti  ndogo ndogo  sana  ambazo  zinaweza  hata  kupatikana  ndani ya  madhehebu  manne ya Kisunni (Imam  Shafi,  Maliki,  Hanafi na  Hanbali ).  Masuala haya  tutayajadili hapo  baadaye  InshaAllah.

Mbali  na  tofauti  hiyo  kubwa  kuna  mambo  yanayofanana  katika  imani za Waislamu  wa Shia Ithna Ashariya  na Waislamu wa Kisunni. La  kwanza  ni nguzo tano za Uislamu, yaani :

(a)  Shahada  -  Laa Ilaaha Illallah  -  Mohammadur  Rasuulullah  -  Hakuna mungu  apasaye kuabudiwa kwa  haki  isipokuwa Allah -  na Mohammad  ni Mtume  wa  mwisho wa Allah.

(b)  Sala tano za kila siku

(c)  Kufunga  mwezi  wa Ramadhan

(d)  Kuhiji katika  nyumba  takatifu  ya Kaa'ba

(e)  Zakat  kwa  ajili ya maskini.

Kwa  pamoja  Shia Ithna Asheriyya  na Sunni  wanaamini  juu ya kitabu  cha  mwisho  cha Allah Qur'an  kuwa  bado kipo vile  vile  bila  mapunguzo au maongezo, na wanajaribu kufuata maamrisho yake bila kubakiza.

Kwa  pamoja  Shia  Ithna  Asheriya  na  Sunni  wanaichukulia  Sunnah  na  Siira  ya Mtume  kuwa  ni  muongozo kwa Waislamu  katika  maisha  yao ya kila  siku  na wanajaribu  kuifuata  kwa  uangalifu  mkubwa  ili wapate  kuokoka hapa  duniani  na  Akhera.

Ingawa  wapo watu  waharibifu  katika  jamii  ambao  kwa  makosa  wanatushutumu sisi Shia  Ithna  Asheriya  kwa  madai mbalimbali  ya uongo  kama  vile  kudai  kuwa  Shia  wana Qur'an  yao  au madai  kuwa  eti Shia  wanaamini juu ya Utume wa  Imam  Ali  bin  Abitalib,  n.k.  Wale  wote  wanaoutafuta  ukweli,  wanatakiwa kuyatupilia  mbali madai  (shutuma)  haya  maovu  dhidi yetu  na  tunawaomba watembelee misikiti na  madrassah  zetu  ambazo  mara  zote  zipo  wazi kwa  Mwislamu  yeyote  kuja  kuthibitisha  imani zetu.

Kuna Shia zaidi ya  millioni 250 duniani  kote  ambao  wanaamini  kuwa Mtume  Mohammad  (s.a.w.w)  ni Mtume  wa  mwisho  na  wanafuata  maamrisho  ya Qur'an  na  Sunna  za Mtume  (S.A.W.W)  katika  maisha yao ya kila  siku.  Katika  manispaa  ya  Dodoma  peke yake,  sisi  Shia  tuna  misikiti miwili;  Khoja Shia  Masjid  na  Masjid Imam  Mahdi (A.S)  na tunawaalika waumini  wote  wa  Kiislamu kututembelea  katika  misikiti hii  ili kupata  ushahidi  kwa  macho  yao kuhusiana  na  imani  na  matendo  yetu  kabla  ya  kuangukia  katika  mtego  wa  waharibifu  wanaotuzulia  habari  za uongo.

KWA NINI SHIA WANAAMINI KUWA IMAM  ALI (A.S) NI

KHALIFA WA KWANZA BAADA YA MTUME ?

Shia  Ithna  Ashariya  wanaamini kuwa  Imam  Ali bin  Abitalib  ni Khalifa  na Imam wa kwanza  baada ya Mtume  (S.A.W.W) kwa  kuzingatia  sababu  moja  rahisi  sana  na iliyo  wazi.  Sababu  hii ni  kuwa;  "Imam  Ali  bin Abitalib  (.A.S)  aliteuliwa  kwa  amri ya  Mwenyezi Mungu  kuwa  Khalifa  wa  kwanza  wa  Waislamu na  Mtume  mwenyewe  kwa  amri ya  Mwenyezi  Mungu  (s.wt).  Hii  ndio  sababu  na  hakuna  sababu  nyingine.

  Katika Qur'an  tukufu (59: 7)  Mwenyezi  Mungu  anasema: "-----Na  anachokupeni  Mtume  basi  pokeeni  na  anachokukatazeni  jiepusheni  nacho".

  Qur'an (33:36): "Na  haiwi kwa  mwanamune  aliyeamini wala kwa  mwanamke  aliyeamini,  Mwenyezi  Mungu  na Mtume  wake  wanapokata  shauri,  wawe  na  hiari  katika  shauri  lao.  Na  mwenye  kumuasi Mwenyezi Mungu  na Mtume  wake, hakika  amepotea upotevu  ulio  wazi"'.

Shia wanaamini  kwamba  maadamu  Mtume  (S.A.W.W)  mwenyewe  kwa  amri  ya Mwenyezi Mungu  alimteua  Imam Ali (a.s) kuwa  Khalifa, Waislamu  hawana  hiari  yoyote  isipokuwa  kutii amri hii.

MITUME NA  MAIMAMU HUTEULIWA  NA

MWENYEZI MUNGU TU NA SI VINGINEVYO

Shia  wanaamini kuwa  ni  Mwenyezi  Mungu (Allah)  tu  ndiye  anayeweza  kumteua  mrithi  wa Mtume  na Imam wa  Waislamu,  na  kwamba  Ummah  wa Kiislamu hauna  hiari yoyote  katika  jambo hili.

USHAHIDI KUTOKA  KATIKA  QUR'AN

Aya  za  Qur'an  zifuatazo  zina  thibitisha  kuwa   Mitume  wote  na  Maimamu waliteuliwa  na Allah  Mwenyewe.

1)  "Na Mola  wako  huumba  atakavyo  na  huchagua;  Hawana  hiari ya  kuchagua" (Qasas 28:68)

2)  "Mimi nitaleta  khalifa  katika  ardhi".  (Baqara 3:30)

3)  "Ewe  Daud!  Hakika  tumekujaalia kuwa  khalifa  katika  ardhi  ---- ". (Saad  38 :26)

4)  "(Allah)  alisema  kwa  hakika  nitakufanya  wewe  (Ibrahimu  )  kuwa Imam  wa  watu (Ibrahimu); alisema Je na katika kizazi changu pia? Akasema (Ndio lakini) ahadi  yangu haitawafikia waovu (madhalimu)". (Baqara  2:124)

5)  "Na  tukawajaalia  kuwa  Maimamu  wanaoongoza kwa amri Yetu".  (Anbiya 21:73)

6)  "Na Unifanyie Waziri  (msaidizi) katika jamaa zangu ........... ndugu yangu Haruni .......... Mwenyezi Mungu Akasema: Hakika umepewa maombi yako, ewe Musa". (Taha  20: 29 - 36)

7)  "Na  hakika  Mwenyezi Mungu alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha Ibrahimu na kizazi  cha Imrani  juu ya walimwengu wote. Ni  kizazi cha wao kwa wao; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenyekujua". (Al- Imran  3:33 - 34).

8)  "Mwenyezi  Mungu  amemchagua (Taluti) juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na kiwiliwili, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua". (Baqara  2:247)

9)  "Akasema (Allah) : Ewe Musa! Mimi  nimekuchagua juu ya  watu wote kwa ujumbe wangu na kwa kusema   nawe kwangu, basi pokea haya niliyokupa na uwe miongoni mwa wanao shukuru". (A'raaf 7:144)

10)  "Na  tukawafanya  miongoni  mwao Maimamu  wanaoongoza  kwa  amri yetu, waliposubiri na walikuwa wakiyakinisha  aya zetu". (Sajdah  32: 24).

  Aya  zote za  Qur'an  zilizotajwa  hapo  juu na  nyingine  nyingi  ambazo  hatukuzitaja zinathibitisha  kwamba  Mitume wote  na warithi wao  waliteuliwa  moja  kwa  moja  na Mwenyezi  Mungu  bila  hiari ya  Ummah.

USHAHIDI  /  UTHIBITISHO WA  KIAKILI NA  KIHISTORIA

1)  ADA  YA MITUME  WALIOTANGULIA: Ada ya Mitume wote ilikuwa  ni  kuteua  warithi wao kwa  amri ya Allah  bila kuingiliwa  na  Ummah. Historia  ya Mitume  hawa  haitoi  mfano  hata  mmoja  wa mrithi  wa  Mitume  aliyechaguliwa kwa  kura  za  wafuasi  wake. Hakuna  sababu kwa nini  linapokuja  suala  la mrithi  wa Mtume  wa Mwisho, Mohammad  (s.a.w.w)  sheria  na kanuni  hii ya  Mwenyezi  Mungu  ibadilishwe.

Mwenyezi Mungu  anasema: "Wala  hutapata mabadiliko katika  kawaida ya Mwenyezi Mungu  (Mwendo Wake na sunna yake)".  (Ahzab  33: 62)

2)  MIFANO YA  WARITHI  WA  MITUME  WALIOPITA: Baadhi  ya  mifano ya warithi  wa mitume  walioteuliwa na Mitume  waliopita kwa  amri ya Mwenyezi  Mungu (s.w).

aNabii  Adamu  alimteua  Shiith

  b)  Nabii  Ibrahim  alimteua Ismail

  c)  Nabii Ya'qub  alimteua  Yusuf

  d)  Nabii  Musa alimteua  Yusho'  bin Nuun

  e)  Nabii  Issa alimteua Sham'uun

  f)  Nabii  Mohammad ( S.A.W.W)  alimteua Imam  Ali  Ibn Abi  Talib

  Qur'an  inasema:  "Na  wakumbuke  waja  wetu  Ibrahim  na  Is-haq na  Yaqkub  waliokuwa wenye nguvu na busara. Hakika sisi  tuliwachagua  kwa lile jambo zuri  kabisa  la kuikumbuka  Akhera. Na bila  shaka walikuwa  mbele  yetu  ni  miongoni wa watu bora waliochaguliwa. Na  mkumbuke Ismaili na Alyasaa na Dhulkifli; na hao wote walikwa miongoni mwa watu bora". (Saad 38:45 - 48).

Qur'an inasema: "Na hizi  ndizo  hoja  zetu tulizompa Ibrahim juu ya watu wake. Tunamnyanyua  katika vyeo yule tumtakaye. Hakika mola wako  ndiyeMwenye hikima na  ndiye ajuaye, Na  tukampa (Ibrahim) Is-haq na Ya'quub, wote tukawaongoa. Na  Nuhu tulimwongoa zamani. Na katika kizazi chake Daudi na Suleimani na Ayyub na Yusuf  na  Musa na Haruni. Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na  tukamwongoza  Zakaria  na Yahya  na Issa na Ilyasi wote (walikuwa) miongoni mwa watu wema. Na (tukamwongoza) Ismail na Al-Yasaa (Ilisha) na Yunusi  na  Luti. Na wote  tukawafadhilisha juu  ya walimwengu. Na (tukawaongoa) baadhi ya baba zao na vizazi vyao  na  ndugu zao. Na tukawachagua  na kuwaongoza  katika njia  iliyonyooka. Huu ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kwa huo humwongoza amtakaye katika watu wake". (An-aam  6:83 - 88).

3)MTUME  HAKUFARIKI KABLA YA KUMTEUA MRITHI WAKE (WASII WAKE):  

4)

5) Mitume  wote waliopita  pamoja  na Mtume  Mohammad (s.a.w.w) hawakupata kuziacha Ummah zao japo kwa muda mfupi  bila  kuacha  watu  watakaoshika  mahala pao (warithi). Hata  walipokuwa  wanatoka kwa  safari fupi  walikuwa  wanaacha  watu wa  kushika  mahala pao (warithi). Je  inawezekana  kwa  Mtume  Muhammad (s.a.w.w)  kuondoka  na  kuuacha Ummah wake bila Wasiy  (Mrithi). 

  Mtume  Muhammad  alikuwa  anajua  kuwa muda  wake  wa kuondoka duniani umekaribia, alijua  kuwepo  kwa  wanafiki  katika jamii ya waislam, alijua kuwepo kwa watu walioendekeza  tamaa ya  madaraka katika mioyo yao, hivyo asingeweza  kuuacha Ummah wake bila wasii  (mtu atakayeshika mahala pake). Alimteua Imam  Ali bin Abitalib  kwa  amri ya  Mwenyezi  Mungu  kuwa  mrithi  na  mtu  atakayeshika  mahala  pake baada ya  kuondoka  kwake  hapa  Duniani.

4)  Sababu  zinazofanya  ulazima  wa  Mitume  kuteuliwa na Mwenyezi Mungu  ni hizo  hizo zinazofanya ulazima  wa  Wasii,  Imamu  na  Khalifa kuteuliwa  na Mwenyezi Mungu kwa  sababu  wote  wanateuliwa  kufanya  kazi  za Allah.

5)  Ikiwa  Imam au  Khalifa  atateuliwa  au  kuchaguliwa  na watu, utii wake  wa kwanza  hautakuwa kwa Mwenyezi Mungu  bali  kwa  watu waliomchagua. Kwa  sababu  msingi wa  mamlaka  yake itakuwa  ni watu,  mara  zote  atajaribu  kuwaridhisha  watu,  vinginevyo  ikiwa  watapoteza  imani juu  yake,  atapoteza  nafasi  yake.  Mtu  wa aina  hii hataweza  kutekeleza  majukumu  ya  dini bila woga  au  upendeleo, na  macho  yake  daima  yatakuwa  katika  mtazamo  wa  kisiasa.

6)  Historia  ya  Uislamu  ina mifano tele ya maovu  yaliyofanywa  na  makhalifa  walioteuliwa  na wanadamu.  Mfano  bora kabisa  ni  ule  wa Yazid  bin  Muawiya bin  Abu  Sufiyan  ambaye  waziwazi  kabisa  alizipuuza  sheria,  alikunywa  pombe   kweupe,  alimuua  mjukuu  wa Mtume  Imam Husayn (a.s) na alituma jeshi  Makka ambalo liliichoma  nyumba  tukufu  ya Al- ka'aba  na  kufanya  maovu  mengine  mengi. (Tazama  Taarikhul Khulafaa cha Suyuti).

7)  Pia  ni Mwenyezi  Mungu  tu  ndiye  anayejua  hisia  na  mawazo  ya ndani  ya  wanaadamu, hakuna mwingine anayeweza kujua  undani wa mtu  mwingine.  Wakati fulani anaweza  kujifanya  ni mcha  Mungu  na mwenye  kumuogopa  Mwenyezi  Mungu  ili tu  kuwaonyesha  wenzake  au ili apate  umaarufu  ili achaguliwe  na wenzake kuwa  kiongozi  kwa  manufaa  ya  kiulimwengu.

Mifano ya aina hii si haba  katika  historia.  Tuchukue  mfano  wa  Khalifa  Abdul  Malik  bin Marwan  ambaye  alikuwa  anamaliza  siku  nzima  msikitini  akisali  na kusoma  Qur'an. Siku  moja aliarifiwa juu ya  kifo  cha  baba  yake  na kwamba  watu  walikuwa  wanamsubiri  ili watoe  kiapo  cha utii kwake.  Aliifunika  Qur'an  na kusema :  "Huku  ndio kuachana  kwangu  mimi na  wewe (Qur'an)".  (Yaani  kupata  Ukhalifa  ndio mwisho  wa  kusoma  Qur'an). (Tazama  Taarikhul  Khulafaa ya  Suyuti, Ukurasa  217). Sifa  muhimu  za Imam , ni  Mwenyezi Mungu  tu ndiye anayezijua.

8)  MAASUM -  Kwa  mujibu  wa  Shia,  Maimamu  na  Makhalifa  lazima  wawe Maasum  -  yaani waliotakasika  kutokana  na madhambi  na uchafu. Hivyo  Maimamu  wote  12 walioteuliwa  na Mtume  Mohammad  (S.A.W.W) walikuwa  Maasum (wasio na madhambi), na  historia ya  Uislamu inashuhudia  umaasumu,  ucha  Mungu, elimu  na tabia  njema  za  Maimamu  12  wa  Shia Ithna  Ashariyah, wa  kwanza  wao akiwa  Imam Ali bin Abitalib (a.s.).  Mada  hii  itajadili zaidi katika  makala  yajayo.

Ismah  (kutakasika kutokana  na  madhambi )  ni  sifa  kutoka  kwa Mungu  ambayo  haiwezi  kupatikana kwa  jitihada  ya mtu  tu bila  ridhaa ya Allah,  hivyo Maimamu  wanatakiwa wateuliwe  na Allah tu.  Sababu  zote zinazothibitisha  kuwa  Mitume lazima  wawe  Maasum pia  hizo hizo  zinathibitisha  kuwa  Maimamu  ni  Maasum.  Maelezo  zaidi yatafuatia.

9)  MIUJIZA - Kwa  mujibu wa Shia,  Maimamu  walioteuliwa  na Allah lazima  wawe  na uwezo   kutoka  kwa Allah  wa  kuonyesha miujiza  kila  itakapohitajika ili kuthibisha Uimamu  wao kama  walivyokuwa wakifanya Mitume. Historia ya Uislamu  inathibitisha  tena  kuwa  Maimamu  12  walioteuliwa  na Allah  walionyesha  miujiza  na  waliwashinda  maadui  zao  katika swala  la  ukweli (haki). Makhalifa  walioteuliwa  na watu huwa  hawana  uwezo  wa  kuonyesha  miujiza, jambo  ambalo  ni muhimu  sana kwa  Mitume  na  Maimamu.

10) UBORA - Shia  wanaamini kuwa,  kama  ilivyo kwa Mtume,  Imamu  lazima  awazidi  wale wote anaowaongoza  katika sifa bora  kama  vile elimu,  Ushujaa, Ujasiri,  Ucha Mungu,  na  Ukarimu. Lazima awe  na elimu  kamili  ya sheria  za Mwenyezi  Mungu. Hapa  pia,  sifa  hizi hazipatikani  kwa  Khalifa yeyote  aliyechaguliwa  au  kuteuliwa  na  watu isipokuwa kwa  Maimamu  12 wa Shia Ithna Ashariya walioteuliwa  na Allah. Soma  makala  yatakayofuata  kwa maelezo zaidi.

Pointi zote  hizi  zinathibitisha  waziwazi  kuwa  warithi,  Makhalifa  na Maimamu  wa  Mitume wote  lazima  wateuliwe na Allah  tu. Maovu yote,  kutokuwepo  kwa  Umoja,  Ujinga , Uvunjaji wa sheria za kiislamu n.k. yote haya  yanatokana  na  makhalifa  waliochaguliwa  na watu  waliopinga  amri  ya Allah  kupitia  kwa  Mitume wake  kuhusiana  na suala la  ukhalifa.

Ili kupata  uokovu, ukweli  na  utukufu  waislamu  wanatakiwa  warudi  na kufuata  amri ya Allah (swt)  kuhusiana na suala  la Imam  baada ya  Mtume,  tunawaita  katika  ukweli  na  haki. Lakini  ni lini Mtume  Mohammad  (S.A.W.W)  alimteua  Imam  Ali bin Abi Talib (a.s) kuwa Khalifa  na  Imam? Je  kuna  ushahidi wowote katika Qur'an  tukufu,  Sunnah  na historia ya Uislamu unaothibitisha uteuzi huu?

Ili kupata  majibu ya maswali haya  soma  makala Na. 2.

Sheikh  Muslim  Bhanji

  TANZANIA ITHNA ASHARIYAH COMMUNITY (T.I.C.)

 Dodoma.

June  2001