Roho ya Matumaini Sayyidina 'Ali bin Abi Talib (a.s.)

Kimetungwa na:
Allama Sayyid 'Ali Naqi Saheb

Kimetafsiriwa na:
Bwana J J Shou

DIBAJI 

Namshukuru Mwenyezi Mungu Mola wa watu wote Rehma na amani zimshukie Hashima yeye na ahli zake.

Utukufu wa Seyyidna Ali mbele ya Mwenyezi Mungu ni jambo lisilo na shaka. Amezaliwa na wazazi watukufu na akalelewa na mtukufu waviumbe ambaye ni mtume Muhammad (S.A.W.). 

Imam Ali bin Abi Talib alikuwa ni mwanafunzi wa kwanza wa Mtume Muhammad (S.A.W.). Na ndiye wa mwanzo kumsadiki kwa kila jambo, hivyo yeye ndiye “SIDDIQUL-AADHAM”. Pamoja nayote hayo Seyyidna Ali cheochake kwa Waislamu ni sawa na uzi unaozidhibiti tasbihi, bila ya uzi huo, tasbihi lazima zitawanyike. 

Kwa maana hii, kusoma na kujua maisha ya Seyyidna Ali ni jambo la wajibu lililo muhimu. 

Namshukuru Maulana Seyyid Naqi Saheeb kwa kututayarishia na kutueleza vema maisha ya Imam Ali, ambaye ni kiungo muhimu katika Uislamu. 

Hawakukosea wale wanaomwita Seyyidna Ali kuwa ni "Imamu-masharik wal-magharib", katika salaa za Ijumaa sifa hiyo ni yake hasa na haimfai yeyote katika saheba za Mtukufu Mtume (s.a.w.). Kitabu hiki kitasaidia vema katika kuwajumlisha Waislamu, maisha sahihi ya Imam Ali (Karamallahu Wajhahu). 

Ni tumainio langu kuwa kitabu hiki mtakipenda.

Ahsanteni Ndugu yenu,

MUHAMMED OMAR ALl,

S.L.P. 45920, 

Dar es Salaam

 

UTANGULIZI

Kila siku binadamu anatafuta mwongozo. Kutafuta huku humfanya binadamu huyu aonane na binadamu wengine wengi, hivyo kwamba tunaweza kukulinganisha huku kujaribu kwake zaidi au kidogo na kuhangaika kwa mtu mwenye kiu katika jangwa lisilo na maji, ambaye anadanganywa na mazigazi, (sarabi) mia moja na moja. 

Tunahitaji mtu asiyefanya dhambi na asiyekosea; mtu ambaye kwamba hata tukichungua kiasi gani utu wake, hatuwezi kuona hata dalili ya hitilafu katika mpango wake, ambao wingi wa tabia zake za maisha hufanya picha tukufu kwa ajili ya macho yetu kutazama na roho zetu kujipatia mwongozo mwema. 

Mtu huyo ni lazima awe katika bali ambayo kila binadamu duniani kote aweze kupata mfano wa kufuata. Tunapolinganisha na kuamua ni yupi kati ya watu mashuhuri duniani, tunaona kwamba uwezo wa uongozi wao unafikia kiwango fulani tu cha kazi zao na nguvu zao za uongozi. Tunaweza tukamtaja Vikramaditya kama mfano wa mfalme mwadilifu lakini mfano wake ni kwa wafalme tu; au tunaweza kumtaja Asoka kama bingwa wa amani walakini anashindwa kutupa matumaini tunapojaribu kumfikiria kama kiongozi mashuhuri wa nchi; na wote hawa wawili waliotajwa hapo juu wanashindwa kutupa mfano kwa raia. Au tunaweza kumtaja Mtakatifu Petro kama roho chamungu lakini atawezaje kutuongoza kama tukikabiliwa na machafuko ya kitaifa? Tunaweza pia kuwataja wapiganaji na watekaji mashuhuri lakini majina yao hayatakuwa na maana kwetu tukihitaji mfano wa mtu mwenye uvumilivu na uwezo wa kuvumilia taabu na mateso. 

Kwa kifupi, tunaweza kupata watu walio nyota zitumulikazo kwa nuru ya sifa za utu moja au zaidi, lakini historia itashindwa kutuonyesha jina linaloweza kuwaongoza, watu wote waishio katika mazingira ya namna mbali mbali isipokuwa Hadhrat Ali bin Abi Talib (Amani ya Mwenyezi Mungu na iwe juu yake) tu.

Hapa tunatoa kwa ufupi tu maisha ya ajabu ya mtu huyu wa ajabu mwenye uwezo wa kufahamu mambo mengi ambaye walimwengu wanapasika kumjua na kumpendelea.

Nasaba yake: 

Hadhrat Ali (a.s.) alikuwa mwana wa Bwana Abu Talib mwana wa Abdul Muttalib wa ukoo wa Hashim ambao ulikuwa wa kabila la Quraish mtu aliyekuwa na nguvu sana na aliyeheshimiwa, aliyetokana na kizazi cha Nabii Ibrahimu (a.s.). Mama yake Hadhrat Ali (a.s.) ni Bibi Fatimah binti yake Bwana Asad, mwanamke aliyeheshimiwa na aliyekuwa wa ukoo wa Hashim. Hivyo Mtukafu Mtume (s.a.w.) na Hadhrat Ali (a.s.) ukoo mmoja. 

 

 

ABDUL MUTTALIB

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Abdullah

 

Abu Talib

 

 

 

 

 

Mtukufu Mtume Muhammad [s]

 

Ali



 
 

Zaidi ya hayo Bwana Abu Talib ndiye aliyemlea Mtukufu Mtume (s.a.w.) tangu baba yake alipofariki dunia kabla hata ya kuzaliwa kwake Hadhrat Ali (a.s.). 

Kuzaliwa kwake: 

Mtume (s.a.w.) alikuwa na umri wa miaka thelathini alipozaliwa Hadhrat Ali (a.s.) ndani ya Kaaba mnamo tarehe 13 mwezi wa Rajabu mwaka wa 30 Aamul-Fiil (sawa na mwaka 600 Miladiya). Wazazi wake walifurahi sana kuona kuwa mwana wao alikuwa anapendwa sana na mwana wa ndugu yao (yaani Mtukufu Mtume s.a.w.) ambaye alikwishagundua kutokana na uso wa mtoto huyo (Ali a.s.) ushupavu na nguvu vitu ambavyo vitamfanya kuwa msaidizi mkubwa utakapokuja mwito kutoka Mwenyezi Mungu.

Kulelewa kwake. 

Kwa sababu ya matuchumi ya Bwana Abu Talib, Hadhrat Ali (a.s.) alilelewa na Mtukufu Mtume (s.a.w.) ambaye alimpenda na kumtunza vizuri sana kijana huyu aliye binamu yake. Akamwongoza katika fikara zile zile zilizouongoza moyo wake. 

Waujumbe: 

Ilikuwa ni matokeo ya malezi (mema kutoka (wa Mtume s.a.w.) kwamba katika umri wa miaka kumi Hadhrat Ali (a.s.) alisikia Mtukufu Mtume (s.a.w.) akitangaza kuwa amechaguliwa kulichukua Neno Ia Mwenyezi Mungu na kuwataka watu wake waamini na kumuunga mkono. Ilikuwa ni mvulana huyu mwenye umri wa miaka kumi, aliyekuwa na ushupavu wa kusimama tayari kutii na kufuata (utume wa Mtume s.a.w.) na hivyo basi akawa shahidi wake wa kwanza, msaidizi wake na mrithi wake. Sauti ya Hadhrat Ali  (a.s.) ilikuwa (ndio) ile sauti iliyopazwa ili kumpa Mtukufu Mtume (s.a.w.) msaada wake familia yake, kabila lake, jamii yake, jiji lake, na hata watu wote Uarabuni kote walipompinga vikali. 

Nyakati za shida: 

Mara tu baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) kutangazia Ujumbe wake upinzani ulianza pande zote. Watu ambao mpaka jana yake, kabla ya kuutangaza Ujumbe huo walimheshimu kwa sababu ya ukweli na uaminifu wake, sasa walianza kumwita mnafiki, kichaa, mchawi na kwa nini wasimuite hivyo? Walianza kuweka miiba katika njia yake, walimpiga mawe na hata kumtupia taka taka kichwani kwake. Katika dhidi yote hii kijana mwenye umri wa miaka kumi ndiye sahaba peke yake aliyelichukua Neno la Mwenyezi Mungu. Hadhrat Ali (a.s.) katu hakukata tamaa na kila mara alikuwa karibu zaidi na Mtume (s.a.w.). Hatimaye, wakati ulifika ambapo watu wa Maka waliamua kumgomea Mtume (s.a.w.) na familia yake. Bwana Abu Talib alimchukua Mtume (s.a.w.) na watu wake na kuwapeleka kwenye bonde (Iiitwalo (Shaab Abi Talib) lililokuwa jirani na jiji la Maka na kuishi huko kwa muda wa miaka mitatu wakiwa wametengwa kahisa na watu wengine. Waliishi katika hatari ya kila mara ya kushambuliwa na maadui wao wakati wa usiku. Hivyo, ili kumkinga Mtume (s.a.w.) na dhara lo lote lile liwezalo kutokea, Bwana Abu Talib alikuwa akichukua hadhari ya kumhamisha Mtume (s.a.w) kutoka kitanda kimoja hadi kingine kila usiku na kitandani pake Mtume (s.a.w.) alikuwa akimlaza mmoja wa wanawe. Kutokana na hayo, Hadhrat Ali (a.s.) alijifunza jambo ambalo alikuwa akilikariri kila mara katika maisha yake.

Hijrah 

Baada ya kifo cha ami yake mpenzi Bwana Abu Talib, Mtume (s.a.w.), ilimbidi kukutana na dhiki na matatizo makubwa na maadui zake wakawa wakatili zaidi. Siku moja maadui wa Mtume (s.a.w.) waliamuwa kuizunguka nyumba yake na kumuua akiwa usingizini. Mtume (s.a.w.) alipopata hatari hizi alimwita Hadhrat Ali (a.s.) na akamwambia aIale kitandani pake badala yake yeye Mtume (s.a.w.) aondoke kimya kimya kwenda Madina. Hadhrat Ali (a.s.) alimuuliza Mtume (s.a.w.), "Je, Mpango huu utayaponyesha maisha yako, ewe Mtume wa Mungu? Alipopata jibu la kumthibitishia kuwa Mtume (s.a.w.) atasalimika, Hadhrat Ali (a.s.) alilala usingizi mzito (wa furaha kitandani pa Mtume (s.a.w.). 

Usika wote ule Machifu wa Makuraishi waliokuwa na hamu ya kumwaga damu, walingojea mpaka kuche na waingie ndani na kumuua Muhammad (s.a.w.) Lakini  asubuhi yake wale maadui waliona kuwa yule waliyekuwa wakimngojea alikwishaondoka na badala yake walimkuta Hadhat Ali ambaye walimdhania kuwa ni yeye Mtume (s.a.w.). Maadui hao walimwuliza Hadhrat Ali (a.s.) alikokwenda Mtume (s.a.w.). Hadhrat Ali (a.s.) aliwauliza maadui hao swali badala ya kuwapa jibu la swali lao akiwauliza kama walimuweka kuwa mchunga wa Muhammad. Hivyo maadui hao walirudi makwao huku wakiwa wamejaa hasira na wasi wasi. Mtume (s.a.w.) alifaulu kwenda mwendo mrefu bila ya matatizo yo yote. Hadhrat Ali (a.s.) alibaki mjini Maka kwa muda wa siku tatu zaidi na aliutumia muda huo kuwarudishia wenyewe vitu vilivyowekwa amana kwa Mtume (s.a.w.). Baada ya hapo Hadhrat Ali (a.s.) aliondoka kwenda Madina kwa miguu akiongoza msafara wa ngamia waliowabeba wanawake wa nyumba yake. Alipofika Madina miguu yake ilikuwa inatoka damu na nyayo zake zilikuwa zikitoka malengelenge. Hii inaonyesha imani Mtume (s.a.w.) aliyokuwa nayo juu ya Hadhrat Ali (a.s.) na nguvu na ujasiri vita ambavyo Hadhrat Ali (a.s.) alivithibitishia imani yake hiyo.  

Ndoa yake: 

Mtume (s.a.w.) alipofika Madina, kitu cha kwanza kumuoza binti yake Bibi Fatimah (a.s.) kwa Hadhrat Ali (a.s.). Mtume (s.a.w.) alimpenda sana binti yake na kila mahali alipomjia, Mtume (s.a.w.) alisimama ili kuonyesha heshima yake kwake. Kwa hiyo, kila mmoja alitazamia kumuoa Bibi Fatimah (a.s.) na wengine waliwahi hata kupeleka posa zao kutaka kumuoa binti wake Mtume (s.a.w.). Lakini Mtume (s.a.w.) alimwambia kwamba binti yake hawezi kuolewa bila ya ruhusa ya Mwenyezi Mungu. Ilikuwa katika mwaka wa kwanza wa Hijira Hadhrat Ali (a.s.) alipochaguliwa kutunukiwa heshima hii ya kumuoa binti yake Mtume (s.a.w.) na harusi ilifanyika katika njia rahisi sana. Binti yake Mtume (s.a.w.) hakufungashiwa hata vyombo vya nyumbani na baba yake, bali vile vyombo vya nyumbani alivyovipata vilinunuliwa kutokana tu na fedha aliyoitoa Hadhrat Ali (a.s.) kwa ajili ya "Mahari". Vyombo hivyo ni pamoja na vyungu vya udongo wa mfinyanzi vichache, mito michache ya majani ya mtende, kitanda cha ngozi, gurudumu Ia kusokotea nyuzi za sufi, kijaa na kiriba. Na Hadhrat Ali (a.s.) aliuza deraja yake ili kupata fedha ya kulipia mahari. Kwa hiyo, ulikuwa mfano kwa Waislamu wote ili kutumia akili katika matumizi yao na kuepuka kutumia pesa zao holela wakati wa sherehe za harusi.  

Maisha ya familia: 

Hadhrat Ali (a.s.) na Bibi Fatimah walionyesha mfano mzuri wa maisha ya wanyumba. Wametuonyesha jinsi mwanaume na mwanamke wanavyoweza kushirikiana katika maisha kila mmoja wao akifanya kazi katika eneo lake Ia kazi alilowekewa na Mwenyezi Mungu na kuwa njia hii ilithibitika kuwa ni yenye kumsaidia kila mnyumba. Mbali na anasa za maisha na kupenda sana raha za dunia, maisha yao yalikuwa mfano mzuri wa amani ya fikara, ushirikiano na uaminifu wa kinyumba na kuelewana. 

Hadhrat Ali (a.s.) alikuwa akifanya kazi ya kumwagilia maji bustani za Wayahudi na alipata ujira ambao aliutimia bra kununua shayiri ambayo mke wake aliisaga kwenye kijaa, alioka mikate na kufagia nyumba. Licha ya kuikidhi familia yake kwa mambo ya maakuli na mavazi ya watoto wake, vile vile Bibi Fathimah (a.s.) alisokota nyuzi za sufu kwa kulipwa na hivyo ujira wake uliongeza kipato cha familia yao

Jihad: 

Mtume (s.a.w.) alitaabishwa na maadui zake huko Maka. Maadui hao walikuwa na kawaida ya kuwatesa sana Waislamu. Waliwaua wengine, na wengine waliwafunga na kuwapiga. Waliwahi kukusanya silaha na kuushambulia mji wa Madina ambako Mtume (s.a.w.) alikuwa akiishi wakati huo. Mtume (s.a.w.) hakupendelea kuishi mjini Madina kwani kufanya hivyo kungehatarisha amani ya wenyeji wa mji huo. Kwa hiyo, Mtume (s.a.w.) aliamua kuwakabili maadui zake nje ya mji wa Madina. Alichukua wanaume mia tatu na kumi na watatu na silaha chache na akaenda kukutana na maadui hao katika uwanja wa "Badr". Mtume (s.a.w.) aliwaweka ndugu zake kabisa katika sehemu zilizokuwa za hatari sana na binamu yake Bwana Ubaida-bin Harithi-bin Abdul Muttalib alikufa kishahidi katika vita hii. Hadhrat Ali (a.s.) alipata fursa ya kushiriki katika vita kwa mara yake ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka ishirini na mitano, na nusu ya maadui waliouawa na Waislamu waliuawa na Hadhrat Ali (a.s.) peke yake. Baada ya vita hii, ilifuata vita ya Uhud, Khandaq na Hunain ambazo Hadhrat Ali (a.s.) alionyesha ushujaa wake na karibu katika kila vita alikuwa mshika bendera wa Mtume (s.a.w.). Katika vita ya Khandaq alipomshinda nguvu askari mkuu wa wakati ule aliyeitwa Amir-ibin-Abd-i-Wadd na kumuangusha chini na kumkalia kifuani karibuni sana kumkata kichwa, huyu mtu mwenye kukata tamaa alimtemea mate usoni Hadhrat Ali. Hadhrat Ali (a.s.) alipandishwa hasira kali na jambo hili, hivyo alishuka toka kifuani mwa Abd-i-Wadd, ili asimuuwe kwa sababu ya hiyo hasira yake jambo ambalo lingeliharibu dhamira yake ambayo ni lazima kila mara ibakie kuwa kwa ajili ya penzi la Mwenyezi Mungu tu wala si kwa ajili ya kitu kama vile hasira yake. Hata maadui zake Hadhrat Ali (a.s.) waliukiri ushujaa, juhudi na ubora wa roho yake. Hasira yake ilipomwishia, Hadhrat Ali (a.s.) alimkata kichwa Amr kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hadhrat Ali (a.s.) hakuichukua ile deraja aliyoivaa yule adui aliyechinjwa ingawa ilikuwa na faida kwake na ilikuwa tabia ya Waarabu kufanya hivyo. Hivyo umbu lake 'Amr alipokuja kuitazama maiti alisema, “Naona mtu aliyemuua umbu langu alikuwa na moyo mzuri kwa sababu hakutaka kuitukanisha maiti ya adui yake.” Hadhrat Ali (a.s.) hakuwahi maishani mwake kumuudhi mwanamke ye yote au mtoto au kuzijali nyara za vita japo kidogo tu. 

Utumishi wake: 

Licha ya kupigana vita na maadui wa Uislamu, Hadhrat Ali (a.s.) alikuwa tayari kufanya kila kitu ili kuutumikia Uislamu na Mtume (s.a.w.). Hadhrat Ali (a.s.) aliandika barua za Mtume (s.a.w.), alitengeneza mikataba na aliweka kumbukumbu za aya za Qur'ani Tukufu zilizokwisha funuliwa. Alipelekwa Yemen kwenda kueneza Uislamu na aliifanya kazi hiyo kwa uaminifu sana kiasi ambacho baada ya muda mrefu Yemen yote ilikuwa imeelekea kwenye Uislamu. Hadhrat Ali (a.s.) alitumwa na Mtume (s.a.w.), kufuatana na amri ya Mwenyezi Mungu, kuwapelekea na kuwasomea makafiri Sura muhimu ya Al-Bara’at (Sura ya tisa ya Qur'ani Tukufu). Siku zote Hadhrat Ali (a.s.) alikuwa tayari kufanya lo lote lile kwa ajili ya Mtume (s.a.w.) na kila mara alikuwa akionekana na viatu vya Mtume (s.a.w.) akivishona na kuvitengeneza. 

Heshima yake mbele ya Mtukufu Mtume (S.A.W.): 

Kwa ajili ya sifa hizi za Hadhrat Ali (a.s.) Mtume (s.a.w.) alikuwa akimheshimu sana na alionyesha heshima hii katika vitendo na hotuba zake. Wakati mwingine Mtume (s.a.w.) alikuwa akisema "Mimi ni jiji Ia elimu na Ali ni lango lake", wakati mwingine alisema "Ali anatokana na Mimi na Mimi ninatokana na Ali", wakati mwingine alisema "Uhusiano wa Ali na Mimi ni sawasawa na ule wa Harun kwa Musa", wakati mwingine alisema "Uhusiano wa Ali na Mimi ni kama ule wa roho na mwili, au "kichwa na kiwiliwili.” Pia alisema "Anayeheshimiwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni Ali". Mtume (s.a.w.) alichukua familia yake kwenda nayo kwa Wakristo wa Najran ili kufanya nao Mashindano (yajulikanayo katika historia kwa jina la Mubahila) ya kuomba laana ya Mwenyezi Mungu iwaangukie wasemao uongo, Hadhrat Ali (a.s.) aliitwa Nafsi ya Mtume (s.a.w.). 

Wakati milango yote ya nyumba za Waislamu iliyoelekea kwenye kiwanja cha msikiti wa Mtume (s.a.w.) ilipofungwa, ule wa Hadhrat Ali (a.s.) ulibakishwa kuwa wazi. Na Waislamu walipopangwa wawili wawili katika udugu wa kidini, Hadhrat Ali (a.s.) aliachwa kwanza mpaka mwishoni, Mtume (s.a.w.) alimtangaza kuwa atakuwa ndugu yake hapa duniani na Kesho huko Akhera pia. Na mwisho wa yote, wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwa anarudi kutoka kwenye Hija yake ya mwisho, alisimama mahali paitwapo "Ghadir-i-Khum" aliwaita Waislamu wote, akatengeneza mimbari ya matandiko ya ngamia, akasimama juu yake akamshika Hadhrat Ali (a.s.) makwapani na kumwinua juu sana na akawatangazia Waislamu akisema "Kama vile nilivyo mwenye mamlaka na Bwana wa Waislamu, na Ali atakuwa vivyo hivyo". Waislamu wote walimpongeza Ali (a.s.) kwa kuteuliwa kwake kuwa Khalifa wa Mtume (s.a.w.). 

Kifo cha Mtume (SA.W.): 

Mtume baada ya kwa miaka kumi ya kuishi mjini Madina ambapo Mtume (s.a.w.) aliugua kwa mara ya mwisho. Huu ulikuwa ni muda mbaya sana kwa familia yake. Hadhrat Ali (a.s.) alikaa karibu na Mtume (s.a.w.) kwa wakati wote wa ugonjwa wake na Mtume (s.a.w.) hakupendelea Hadhrat Ali (a.s.) aachane naye hata kwa muda mfupi tu. Hatimaye, Mtume (s.a.w.) aliaga dunia na kurudi kwa Bwana Wake. Kabla hajafa Mtume (s.a.w.) alimtaka Hadhrat Ali (a.s.) asogee karibu naye, akamkumbatia na akazungumza naye kwa muda mrefu akiwa na madhumuni ya kumpa maagizo ya mwisho. Hata baada ya Mtume (s.a.w.) kumaliza mazungumzo yake na Hadhrat Ali (a.s.) hakumwachilia aende, bali aliendelea kumshika mkono na kuuweka kifuani pake na roho ya Mtume (s.a.w.) ilipotoka mkono wa Hadhrat Ali (a.s.) ulikuwa bado upo kifuani pake. 

Baada ya Kifo cha Mtume (SA.W.): 

Vipi Hadhrat Ali (a.s.) angeliweza kuuacha mwili wa Mtukufu Mtume (s.a.w.), baada ya kushirikiana naye kwa muda mrefu? 

Hivyo ibada za maziko ya Mtume (s a w) ziliendeshwa na Hadhrat Ali (a.s.) ambaye pia aliongoza na kushiriki katika kuteremsha maiti ya Mtume (s.a.w) kaburini. Na Ali (a.s) alipoinua kichwa chake alikuta swali la kushika nafasi ya Mtume (s.a.w.). Ukhalifa limekwisha kuamuliwa mara moja kwa watu wote, na wale ambao kwao swali hili lilikuwa swali muhimu sana baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.). Lakini kwa Hadhrat Ali (a.s.) kuendelea kuueneza Uislamu ndilo jambo muhimu zaidi. 

Baada ya kifo cha Mtume (s.a.w.) Hadhrat Ali (a.s.) alijitenga akawa kimya kimya anaendelea kueneza Ujumbe, kwani alijua kuwa ilikuwa ni kazi yake ambayo aliifurahia kuifanya, na kila siku alikuwa tayari kutatua matatizo ya Waislamu waliyomletea kuyatatua.  

Hadhrat Ali (a.s.) alitayarisha toleo la Qur'ani Tukufu na kuzipanga Aya zake kwa utaratibu wa kufunuliwa kwao, pamoja na maelezo ya aya zilizochukua mahali pa aya nyingine (Nasikh), zile zilizochukuliwa mahali pao (Mansuukh), zile aya zisizo eleweka vizuri (Mutashaabi haat) na zile zilizo wazi wazi kabisa. Hadhrat Ali (a.s.) alianzisha ari ya utafiti na uandishi katika tabaka Ia Waislamu wasomi. Na yeye mwenyewe aliacha zana muhimu sana kwa ufafanuzi wa Qur’ani, lugha, fiqah na mambo mengine ya kidini. Aliwatayarisha wanavyuoni ili waweze kuiendeleza kazi ya kuwaelimisha Waislamu baada ya kufa kwake. Alizipanga vizuri kanuni za sarufi ya Kiarabu na elimu ya ufasaha wa kusema. Hivyo Hadhrat Ali (a.s.) alitoa mafunzo kwamba wakati uwapo mbaya na ubora wa mtu hautambuliwi, basi mtu anaweza kubakia nyumbani mwake na anaweza kuwatumikia watu wake na aangalie mawazo yake yasimpoteze kutoka katika misingi ya utu. 

Ukhalifa: 

Baada ya muda mrefu upatao miaka 25, mnamo mwaka wa 35 Hijirya, Waislamu walimwomba Hadhrat Ali (a.s.) akubali kuwa Khalifa, lakini kwa masharti kwamba atatawala kufuatana na Qur'ani Tukufu na Sunnat za Mtume (s.a.w.). Waislamu waliyakubali masharti haya lakini wakati ulikwisha badilika, hivyo Waislamu wengi hawakuweza kuona haki ikifuatwa na wakakaa kimya. Ukoo wa Bani Umayyah waliiona hatari kwa faida zao katika utawala wake wa kidini. Hadhrat Ali (a.s.) aliona kuwa ni wajibu wake kuyapiga vita mawazo haya na vita vya "Jamal", "Siffin", na Nahrawan", vilishuhudia kuwa mishipa ya Hadhrat Ali (a.s.) ilikuwa na damu ya aina ile ile iliyofanya kazi kishujaa chini ya uongozi wa Mtume (s.a.w.) katikati ya safu za askari maadui katika vita vya “Badr", "Uhud”, "Khandaq" "Khaibar". Vipingamizi vya Bani Umayyah havikumruhusu kutawala na kuwarekebisha watu wake. Lakini hata hivyo, kwa muda mfupi wa maisha yake aliobakia kuendelezea Uislamu, aliifufua misingi ya Uislamu ambayo ni usawa maisha rahisi na kuishi kiaminifu. Akiwa na madaraka ya juu kabisa katika Uislamu, alikuwa na kawaida ya kukaa kando ya barabara akiuza tende, na rafiki yake Bwana Misam aliondoka kwenda kufanya kazi nyingine. Kila mara Hadhrat Ali (a.s.) alivaa nguo za zamani na zenye viraka na alikuwa na mazoea ya kukaa chini na kula chakula pamoja na maskini. Kila mara aIigawanya pesa za 'Baitul-Mal' (Hazina ya Serikali) sawa sawa kati ya wale waliostahili. Siku moja ndugu yake aitwaye Aqil aliomba apewe pesa kidogo zaidi ya wengine. Hadhrat Ali (a.s.) alikataa na akamwambia "Ingekuwa hivyo kama zingelikuwa pesa zangu. Lakini hii ni Mali ya Waislamu wote, hivyo huwezi kupendelewa zaidi kuliko wengine".

Wakati fulani alipokuwa akikagua mahesabu ya pesa za 'Baitul-Mal' mtu mmoja kila mara alimjia kwa mazungumzo ya kibinafsi Hadhrat Ali (a.s.) alikuwa kila mara akizima taa na kusema, "Taa ya 'Baitul-Mal' lazima itumike kwa kazi iwahusuyo Waislamu wote, siyo shughuli zingine". 

Kila wakati Hadhrat Ali (a.s.) alijaribu kugawa pesa za 'Baitul Mal' kwa wale wanaostahili haraka iwezekanavyo. Hakupenda kuiacha kwanza. 

Shahaadah yake: 

Lakini ole wao wale wabaya wa ulimwengu ambao hawakuweza kuyavumilia maisha ya Mchamungu huyu na kuwa bingwa wa amani, usawa, udugu na ubinadamu, Hadhrat Ali (a.s.) alipata pigo la bapa lenye sumu la upanga uliolaaniwa na Abdul Rahman lbn Muljim. Ilikuwa mnamo tarehe ya Mwezi wa Ramadhani wa mwaka wa 40 Hijiriya, kuwa Hadhrat Ali (a.s.) alipata pigo hili kali sana alipokuwa akisali sala ya Alfajiri katika Msikiti wa mji wa Kufa (nchini Iraq). Muuaji huyo alipoletwa mbele yake, huruma za sahaba huyu wa Mtume (s.a.w.) zilimjia na akawaambia wanawe, "Huyu ni mateka wenu. Wala msimtaabishe. Mpeni chakula kile kile mnachokula ninyi wenyewe. Nikipona nitaweza kumuadhibu au kumsamehe lakini kama nikifa, na ikiwa mnataka kumwadhibu basi mpigeni dharuba moja tu kwa sababu yeye alinipa dharuba moja tu. Msimkatekate viungo vyake kwani kufanya hivyo ni kinyume na mafundisho ya Uislamu.

Sumu kali ilifanya kazi yake na mnamo tarehe 21 mwezi wa Ramadhani, Hadhrat Ali (a.s.) alifariki dunia. Wanawe Hasan na Husain (Amani ya Mwenyezi Mungu na iwe juu yao wote) walimfanyia ibada za maziko na lile ua la utu lililazwa kwenye mapumziko yake ya milele katika ardhi ya Najaf, nchini Iraq. 

Baadhi ya Hadithi za Hadhrat Ali (a.s.): 

Hizi zifuatazo hapa chini ni baadhi tu ya Hadithi (Semi) nyingi za Hadhrat Ali bin Abi Talib (a.s.): 

1. Ulimwengu unapomsikiliza mtu, humpa mtu huyo wema wa watu wengine, lakini unapompa mtu huyo kisogo unamwondolea mtu huyo wema wake yeye mwenyewe. 

2. Muadhibu ndugu yako (kwa makosa yake) kwa wema na mlipe madhara yake kwa ukarimu (wako). 

3. Ye yote yule ajiwekaye katika hali ipasiwayo na masengenyo, asimlaumu mtu ye yote ajengaye wazo baya juu yake.

4. Wapende watoto wa watu wengine na utawatengenezea watoto wako maisha yao ya baadaye.

5. Dhambi mbaya sana ni ile inayodharauliwa na mtenda dhambi. 

6. Kuridhika ni hazina isiyofilisika. 

7. Jinsi mtu azidivyo kuwa mwenye hekima, ndio jinsi apunguzavyo mazungumzo yake. 

8. Yule mwenye uwezo mkubwa wa kuadhibu huwa mvumilivu zaidi. 

9. Cho chote kile mtu akifichacho hufichuliwa katika midomo ya ulimi wake na hall ya uso wake.

10. Watu wengi wenye elimu wanapata matatizo kwa ajili ya ujinga wao, na elimu yao hubakia bila faida yo yote. 

11. Kufaulu hakumshindi mwenye subira ingawaje kuje baadaye kabisa. 

12. Ng'oa uovu kutoka katika nyoyo za wengine kwa kuung'oa kutoka katika moyo wako wewe mwenyewe. 

13. Kama mtu ana wazo zuri kuhusu wewe, basi thibitisha kuwa unastahili kufikiriwa hivyo. 

14. Majivuno ni moja ya maadui wa busara. 

15. Siri ya uongozi ni kuwa na huruma sana. 

16. Choyo ni utumwa wa milele. 

17. Kama unaogopa kitu fulani cho chote kile, basi kikabili; kwa maana taabu ya hofu yako ni kubwa kuliko ile ya taabu zenyewe. 

18. Kama kupotea kwa utajiri wako kunakufanya uwe mwenye busara, basi hiyo si hasara. 

19. Thawabu ya kwanza kwa mwenye kuvumilia ni kuwa watu humtetea dhidi ya wakaidi.

MWENYEZI MUNGU ANASEMA:

(Ikumbuke) Siku Tutakapowaita kila watu na Imamu wao …” (Banii-Israil, 17:710.

HADITH THAQALAIN 

MtuIwfu Mtume alihutubia akisema:

"(Enyi Waislamu!) Nimeitwa na Mola wangu na nimeitika

amri yake (Yaani hivi karibuni nitafariki)". 

"Ninakuachieni miongoni mwenu Vitu viwili vyenye thamani zaidi (Thaqalain). Kimoja miongoni mwao ni kikubwa kuliko kingine - (1) Kitabu cha Allah, ambacho ni kamba ya Allah illyotanda kutoka mbinguni hadi nchini, na kingine ni (2) Dhuria wangu, ambao ni Ahlul-Bait wangu. Vitu hivi havitatengana hadi vitakaponijia vyote kwa pamoja kwenye Hodhi ya kawthar (huko Peponi)…

Kisha akamwinua Bwana 'Ali bin Abi Talib (a.s.) na akasema: 

"Ye yote yule ambae mimi ni Bwana wake, basi huyu 'Ali nae yu Bwana wake". 

(Sahih ya Tirmidhii, Khasais cha Imamu Nasai, Kanzul Ummal cha Sheikh Ali Muttaqi n.k.).


 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.


 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.