SHIA NA QUR'ANI

Majibu Na Maelezo

Abdilahi Nassir

UTANGULIZI

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimshukie bwana wetu na mwombezi wetu, Muhammad b. Abdillahi, na ali zake wema waliotakaswa wakatakasika, na wote wanaofuata nyayo zao.

Hitilafu baina ya Shia na Waislamu wengine wasio Shia haikuanza juzi na jana. llianza karne nyingi zilizopita; mara tu baada ya Mtume Muhammad s.a.w.w. kufariki dunia. Hata hivyo, katika kipindi cha Makhalifa wawili wa kwanza, hitilafu hiyo haikuzusha zogo na fitina kubwa kama lile lililozuka katika kipindi cha Makhalifa wa tatu na wa nne. Na hilo ni kwa sababu ambazo, kwa kuwa ziko nje ya maudhui ya kitabu hiki, sikusudii kuzizungumzia humu. Itoshe tu, kwa hivi sasa, kujua kwamba ni baada ya Khalifa wa tatu (Khalifa Uthman) kuuliwa, na mtu aliyekiitwa Muawiya kuongoza upinzani dhidi ya Khalifa wa nne (Imam Ali), ndipo hitilafu hiyo ilipopaliliwa moto. Na kutokana na upinzani huo ndipo Imam Ali a.s. alipolaaniwa, kwa amri ya Muawiya, katika hotuba zote za Ijumaa, kwa muda usiopungua miaka themanini. Ndipo wote wale waliokimtambua Imam Ali a.s. kuwa ni imamu wa haki (yaani Shia) walipokuwa wakisakwa kama nyoka na kuuawa! Ndipo Imam Hassan a.s., mjukuu wa Mtume s.a.w.w., alipouliwa kwa kutiliwa sumu chakulani mwake! Ndipo Imam Hussein a.s., mjukuu mwingine wa Mtume s.a.w.w., alipouliwa kinyama huko Karbalaa (lraq) kwa kukatwa kichwa chake, Kikatungikwa kwenye mkuki na kuchezewa ngoma, na kuliacha pingiti la mwili wake lishetwe-shetwe na farasi! Ndipo hofu ilipofikia kiwango cha watu, chini ya Ufalme wa Muawiya, kuogopa kuwapa watoto walio wazaa jina la Ali! Ndipo hata mashekhe, kwa kuchelea kuadhibiwa na kuuawa, walipokiogopa kulitaja jina la Imam Ali a.s. katika riwaya za Hadith za Mtume s.a.w.w.; badala yake ikawa husema: 'Amesema Sheikh'!

Hapo ndipo chuki baina ya Shia na wasio Shia ilipozidi na kuendelea kwa miaka mingi - mara inapanda, mara inashuka - hadi hii karne tuliyonayo. Katika karne hii, kiasi cha miaka thelathini hiwi iliyopita, baadhi ya wanazuoni wa Kishia na wasio Shia huko Mashariki ya Kati wakaona la! Hali hii haifai kuachwa ikaendelea. Kwa hivyo wakakutana na kujadiliana jinsi ya kuleta mkuruba na uelewano baina ya madhehebu mbali mbali ya Kiislamu - hasa baina ya Shia na Sunni. Matokeo yake yakawa ni kuundwa chama kilichoitwa Darut Taqrib Baynal Madhahibil Islainiyya na kuweka jukwaa la pamoja la kuwawezesha wanazuoni hao wa madhehebu mbali mbali kueleza imani na misimamo ya madhehebu yao juu ya mada mbali mbali za kidini.

Hatua hii ilisaidia sana kuleta uelewano kiasi cha kwamba, Sheikh Mahmud Shaltut (aliyekuwa Mufti wa AI-Azhar wakati huo) alitoa ile fatwa yake mashuhuri ya kusema kwamba

madhehebu ya Ja'fari (yaani Shia Ithnaashari) ni madhehebu ya Kiislamu yanayojuzu kufuatwa katika kufanyia ibada kama madhehebu mengineo ya Sunni. Na, kwa mara ya kwanza akaruhusu madhehebu hayo yasomeshwe katika Chuo Kikuu hicho cha AI-Azhar huko Misri.

Hata hivyo, baadhi ya masheke wa wakati huo hawakupendezwa na hatua hiyo. Miongoni mwao ni mmoja aliyekiitwa Muhibbudin al-Khatib. Huyu aliandika kitabu kwa lugha ya Kiarabu kiitwacho al-Khututul Aridhwa kuonyesha kwamba ni muhali jaribio hilo la wanazuoni wenzake kufanikiwa - hasa inapokuja kwenye uelewano baina ya Sunni na Shia - na akatoa sababu zake. Sababu hizo ndizo tutakazozijadili katika mfululizo wa vitabu vyangu hivi inshallah, kuanzia ile inayohusu Qur'ani Tukufu.

Japokuwa kitabu hicho kishajibiwa kwa hiyo hiyo lugha ya Kiarabu, inaonekana kwamba wate wasiopendelea umoja baina ya Waislamu hawana habari ya majibu hayo, au labda hawapendi kuwa nayo! Maana kama si hivyo, wasingekuwa wakiendelea kukichapisha kitabu hicho mumo kwa mumo, na kukifasiri kwa lugha nyinginezo, bila ya kusema cho chote juu ya majibu yaliyokwisha kutolewa.

llipofika 1983, miaka minne baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, kitabu hicho kilifasiriwa kwa Kiingereza na kusambazwa ulimwengu mzima. Kwa nini? Kwa sababu ya waandamizi wa marehemu Sheikh M. al-Khatib kuona jinsi juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilivyofanikiwa nje ya Ulimwengu wa Kiarabu, ambako lugha ya Kiingereza hueleweka zaidi, katika kuleta uelewano na umoja baina ya Waislamu.

Huku kwetu Afrika Mashariki, tafsiri hiyo ya Kiingereza ilienezwa zaidi kuliko ile nuskha ya Kiarabu - hasa miongoni mwa wanafunzi wa mashule na vyuo vikuu. Hata hivyo, baada ya kuonekana kwamba athari ya nuskha hiyo ya Kiingereza haikuwa kama ilivyotarajiwa, bali Waislamu wamezidi kuvutiwa na maongozi ya Kiislamu ya Imam Khomeini na kutaka kujua zaidi Ushia, jamaa hao wakaonelea bora itolewe tafsiri ya Kiswahili: hwenda ikaleta athari itakikanayo! Hivyo hivi majuzi (Disemba 1988) kukachapishwa tafsiri ya Kiswahili ya kitabu hicho kwa jina la Misingi Mikubwa lliyojengewa Dini ya Ushia ambapo kitabu hiki inshallah ndiyo mwanzo wa majibu yake.                     

Katika kuandika majibu haya, napenda ieleweke kwamba sikuyaandika kwa hiari; nimelazimika! Sikuyaandika kwa hiari kwa sababu ninaamini kwamba kuna mambo muhimu zaidi, yenye manufaa na Waislamu kwa jumla, ambayo sisi waandishi wa Kiislamu wa leo inatupasa kuyashughulikia. Na nimelazimika kwa kuona hatari ya mfarakano baina ya Waislamu inayoweza kutokea kwa vitabu kama hicho cha Sheikh M. al-Khatib kuachwa bila ya kujibiwa - hasa hivi ambavyo idadi ya Shia wananchi, humu mwetu Afrika Mashariki, inavyozidi kukua, na hasa hivi ambavyo sababu zote alizozitoa shekhe wetu huyo katika kitabu chake hicho hazina mashiko Hivyo nimeyaandika majibu haya ili kuuzuia mfarakano huo unaoweza kutokea; na kwa roho hiyo hiyo nakuomba, ewe ndugu msomaji, uyasome.

Pengine, wakati mwingine, ushahidi utakaotolewa katika mfululizo wa majibu haya utaonekana mkali. Hilo ni kweli! Lakini huo ni ukali usioweza kuepukika! Ni kama daktari mpasuaji kulazimika kukikata kiungo kimoja cha mwili ili kuuhifadhi mwili mzima. Mwili hapa ni umoja wa Waislamu, na kiungo ni Sheikh M. al-Khatib na wale wenye mawazo kama yake.

Nataraji ndugu zangu mtayasoma majibu haya kwa ikhlasi na bila chuki, pamoja na kuyalinganisha na vitabu nilivyovitolea ushahldi, ili mweze kuufikia ukweli. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi.

ABDILAHI NASSIR

Nairobi, Kenya

 Rajab, 1409

 Machi, 1989

SABABU ZAKE

Katika kueleza kwa nini haiwezekani kuwako umoja na uelewano baina ya Sunni na Shia, Sheikh M. al-Khatib ametoa sababu nane kubwa; nazo ni:

(1) Shia wana Our'ani iliyo tofauti na ya Sunni;

(2) misingi ya Hadith inayotegemewa na Shia ni tofauti na ile inayotegemewa na Sunni;

(3) Shia hawawaheshimu sahaba wa Mtume s.a.w.w., bali wanawatukana na kuwalaani;

(4) Shia wanaamini taqiyya ambayo kwayo hujitokeza kwa Sunni 'kwa yasiyokuwa yale wanayoyaficha'. Kwa hivyo huwezi kujua ukweli wao;                 

(5) Shia hawawatambui Makhalifa watatu wa kwanza wanaotambuliwa na Sunni. Wao wanawatambua Maimamu wao kumi na mbili tu;

(6) Imani ya Shia juu ya upweke na ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu aonekana au haonekani, ni tofauti na ile ya Sunni;

(7) misingi ya dini na fiqhi kwa Shia ni tofauti na ile ya kwa Sunni; na

(8) kinyume na Sunni, Shia wanaamini raj'ah; nayo ni imani kwamba mwisho mwisho wa dunia atakuja Mahdi a.s. 'awachinje watesi wake wote wa kisiasa. Na atawarejeshea Mashia haki zao walizonyang'anywa na watu wa madhehebu mengine miaka mingi iliyopita'.

Hizo, kwa jumla, ndizo sababu kubwa zllizompelekea Sheikh M. al-Khatib kuandika kitabu chake hicho ili kuwaonya Sunni hatari ya kuitikia mwito wowote wa kuleta umoja na uelewano baina yao na ndugu zao wa Kishia. Na bila shaka ndizo sababu pia za waandamizi wake kuitoa tafsiri yake kwa Kiswahiii.

Zaidi ya hayo, kuna tuhuma nyingine ndogo ndogo zilizopachikwa pachikwa na kurudiwa rudiwa hapa na pale katika kitabu hicho. Ni nia yangu inshallah kuzijibu na kuzieleza zote hizo kadiri nitakavyoweza. Na kuwafikiwa ni kwa Mwenyezi Mungu.

Katika majibu yangu haya nitajaribu inshallah kuonyesha kwamba:

(i) baadhi ya mambo yaliyosemwa na Sheikh M. at-Khatib ni kinyume na Ushia ulivyo;

(ii) imani yoyote ya kidini ambayo Shia wanayo, ina mategemeo yake katika Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume Muhammad s.a.w.w.;

(iii) karibu katika kila tuhuma ambayo Sheikh M. al-Khatih amewafanyia Shia, tuhuma kama hiyo inaweza kufanyiwa Sunni kutokana na yaliyomo katika vitabu vya Kisunni na mila zao; na kwa hivyo

(iv) hitilafu zilizoko baina ya Sunni na Shia si kubwa hivyo hata zizuie umoja na uelewano baina yao.

Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada.

     Ewe Mola! Tuonyeshe Haki kuwa ni Haki, uturuzuku kuifuata. Utuonyeshe batili kuwa ni batili, uturuzuku kuiepuka.

SUNNI NI NANI

Kwa kuwa kitabu cha Sheikh M. al-Khatib kimeandikiwa Sunni kuwatahadharisha na hatari ya Ushia, nimeona kwamba itakuwa vizuri Sunni ajijue yeye mwenyewe kabla ya kumzungumza Shia. Maana ionekanavyo, Sunni wengi sana hawajijui wao ni nani; na kama wakijijua, hujijua kimakosa!

Kwa mfano, baadhi ya wale waliosoma miongoni mwa Sunni hudhania kwamba wameitwa hivyo kwa sababu wao tu ndio wanaoiamini na kuifuata sunna ya Mtume Muhammad s.a.w.w.

- kama kwamba madhehebu mengine ya Kiislamu (k.v.Shla Ithnaashari, Zaydiyya au Ibadhi) hayafuati! Wengine hudhani wameitwa hivyo kwa kuwa madhehebu yao yalikuwako tangu zama za Mtume s.a.w.w.! Kumbe zote fikira mbili hizo ni kinyume na mambo yalivyo.

Ukweli ni kwamba Sunni ni wale ambao, katika mambo ya sheria, hufuata maoni ya mmojawapo wa maimamu wanne (Abu Hanifa, Malik, Shafi au Hanbali) au wanafunzi wao; na katika mambo ya akida (imani), hufuata maoni ya Abul Hassan al-Ash'ah. Bila ya kufanya hivyo- kwa mfano, kama mtu atafuata maoni ya wasiokuwa hao katika sheria na /au katika imani -hawi ni Sunni.

Kwa hivyo, ili mtu aelewe n lini hasa ulipoanza Usunni, itambidi ajue (japo kidogo) historia ya maimamu hao. Nayo ni kama ifuatavyo:

Abu Hanifa ndiye wa kwanza. Yeye alizaliwa Kofa mwaka 80H na kufariki Baghdad mwaka 150H. Miongoni mwa walimu aliosoma kwao ni Imam Ja'far as-Sadiq a.s. (aliyekuwa Imam wa Sita wa Shia Ithnaashah) hata akasema kwamba, kama si miaka miwili aliyojifunza kwake, basi angeangamia.

Malik ndiye wa pili. Yeye alizaliwa Madina mwaka 93H na kufariki huko huko Madina mwaka 179H. Yeye pia, kama Abu Hanifa, alisoma kwa Imam Ja'far as-Sadiq a.s. miongoni mwa walimu wengine.

Wa tatu ni Imam Shafi. Yeye alizaliwa Gaza mwaka 150H na kufariki Misri mwaka 204H.

Na wa mwisho ni Imam Hanbali aliyezaliwa Baghdad mwaka 164H na kufariki huko huko Baghdad mwaka 241 H.

Hao ni wa upande wa sheria. Kwa upande wa akida (imani), Sunni humfuata Abul Hassan al-Ash'arl ambaye alizaliwa Basra mwaka 260H na kufariki Baghdad mwaka 333H.

Sasa, unapotazama tarehe za maimamu hao utaona kwamba wa kwanza kabisa ni Abu Hanifa aliyezaliwa mwaka 80H. Hii ina maana kwamba yeye alikuja duniani miaka sabini hivi

baada ya kufa Mtume Muhammad s.a.w.w.(ambaye alifariki dunia mwaka 10H). Jee basi, kama ni hivyo, wale Waislamu walioishi baina ya kufa Mtume s.a.w.w. na yeye kuwa Imamu (kipindi cha zaidi ya miaka 70) walikuwa wakimfuata nani? Hawakuwa Waislamu? Jee, wale walimu waliomsomesha yeye hawakuwa na wafuasi? Wafuasi hao walitowekea wapi? Jee, anayefuata maoni ya walimu hao hawi Mwislamu hali anayefuata maoni ya wanafunzi wao huwa? Kama hawi Mwislamu, basi ni kwa hoja gani? Kama huwa, basi kwa nini Sunni wa kawaida kupawa fikira kwamba wao tu ndio Waislamu wa haki?

Japokuwa hayo ni maswali ambayo majibu yake yangehitajia kitabu chake peke yake, maana ni hadithi ndefu yenye undani mwingi, ningependelea ewe ndugu msomaji ujiulize au umuulize anayejua zaidi yako, na uyazingatie majibu yake kwa makini. Maana, kwa kupata majibu ya kuridhisha ya maswali hayo, ndipo utakapoweza kutatukiwa na kitendawili hiki cha mfarakano na kutoelewana baina ya Waislamu.

Tukija upande wa akida (imani), itaonekana kwamba Sunni hufuata mawazo ya mtu aliyekuja duniani miaka 19 baada ya imamu wa mwisho wa Kisunni kufariki, yaani Imam Hanbali! Maana yeye alifarikl mwaka 241 H hali Abul Hassan al-Ash'ari alizaliwa mwaka 260H! Kwa hivyo al-Asha'ri hakukutana na yeyote kati ya maimamu wa Kisunni wa sheria! Kama ni hivyo basi, hao maimamu wanne, kabla ya kufariki kwao, walikifuata imani gani? Ya al-Ash'ari, ambaye alikuwa bado hajazaliwa, au imani nyingine iliyokuwako kabla ya kuzaliwa al-Ash'ari? Kama ni nyingine, ni ipi? Na jee, walikuwa ni Waislamu kwa kuamini hivyo? Kama walikuwa ni Waislamu - na sidhani kuwa yuko yeyote anayeweza kujasiri kusema kuwa maimamu hao walikuwa makafiri - basi kwa nini iwe ni wao tu? Kwa nini mtu mwingine, anapofuata maoni ya asiyekuwa al-Ash'ari, awe si Mwislamu? Kwani yeye al'Ash'ari alipozaliwa, alizaliwa na hayo maoni yake? Jee hakuwa akifuata maoni ya wataalamu aliowakuta kabla ya yeye kuzuka na maoni yake? Kama alikifuata mawazo ya wengine - na ukweli ni kwamba alikifuata - jee, wakati huo yeye alikuwa si Mwislamu? Kama alikuwa ni Mwislamu, pamoja na kwamba alikifuata maoni yasiyokuwa yake, kwa nini leo mtu mwingine awe si Mwislamu kwa kufanya vivyo hivyo?

Hayo nayo pia ni maswali ambayo, ewe ndugu msomaji, inataka ujiulize (au umuulize anayekuzidi elimu) na uyazingatie majibu yake kwa makini. Maana majibu sahihi utakayoyapata ndiyo yatakayokusaidia kuelewa kiini cha mzozo huu tunaoujadili katika mfululizo wa vitabu hivi.

Kutokana na maelezo mafupi haya, na majibu sahihi utakayoweza kuyapata ya maswali machache tuliyoyauliza, nataraji inshallah kila aliye Sunni ataweza kujijua yeye ni nani. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada.

QUR'ANI TUKUFU

Mwenyezi Mungu s.w.t. amesema:

(i) Hakika Sisi ndisi tuliouteremsha Ukumbusho (huu), na hakika Sisi ndio Wenye kuulinda. (Sura 15:9)

(ii)... Bila shaka hicho ni Kitabu Kitukufu. Hakitajiliwa na batili mbele yake wala nyuma yake;

ni wahyi utokao kwa Mwenye hekima, Asifiwaye. (Sura 41:41-42)

Hayo ni maneno ya Mwenyezi Mungu yanayotuthibitishia kwamba Qur'ani ni kitabu kilichohifadhiwa na kila aina ya nyongeza, upungufu au mabadiliko. Waislamu wote - wa zama zote na nchi zote - wanaamini kwamba hii Qu'rani tuliyonayo leo ndiyo ile ile iliyokuwako zama za Mtume s.a.w.w., chapa kwa ya pili, na ndiyo hii hii itakayokuwako mpaka Siku ya Kiyama, Kwa hivyo, mtu ye yote atakaye amini kinyume cha hivyo, huyo si Mwislamu.

Kwa kuwa Sheikh M. al-Khatib, katika kitabu chake hicho (uk. 4), amedai kuwa Shia hawaamini hivyo, nimeona ni bora nianze majibu yangu haya kwa madondoo ya wanazuoni mbalimbali wa Kishia, wa nyakati mbalimbali, yanayo batilisha madai yake hayo. Baada ya hapo ndipo niendelee na madai yake mengine:

(1) al-Fadhl b. Shaadhaan: Huyu ni kati ya wanazuoni wakubwa wa Kishia aliyeishi katika karne ya tatu ya Hijria. Katika kitabu chake kiitwacho al-lidhaah, katika kukataa baadhi ya maoni ya wanazuoni wa Kisunni wa zama zake kwamba Qur'ani Tukufu imepotolewa, amesema:

Lakini wale ambao, kwa kutaja Hadith kama hizo, wadhania kwamba nassi ya Qur'ani imepotolewa, bila shaka wanakosea.

(2) Abu Ja'far Muhammad b. Ali b. Baabawayh al-Qummi: Mwanachuoni huyu ni maarufu zaidi kwa jina la al-Shaykh as-Saduq na alifariki dunia katika mwaka 381 H. Yeye amesema hivi katika kitabu chake kiitwacho al-l'tiqaadaat:

lmani yetu ni kwamba Qur'ani ambayo Mwenyezi Mungu s.w.t. amemteremshia Mtume Wake Muhammad s.a.w.w, ni hii hii iliyo baina ya majalada mawili na iliyomo mikononi mwa watu; si zaidi ya hiyo... Na yeyote anayetusingizia kwamba twasema zaidi ya hivyo, basi huyo ni mwongo.

(3) Sayyid al-Murtadhaa Ali b. al-Husayn al-Muusawi al-Alawi: Huyu ni mwanachuoni mwingine mkubwa wa Kishia aliyefariki dunia katika mwaka 436H. Yeye, katika kujibu maswali ya Taraabulusiyyaat, amesema:

Ujuzi wa kwamba mapokezi ya Qur'ani ni sahihi ni kama ujuzi wa nchi na miji, matukio makubwa makubwa ya kihistoria, vitabu mashuhuri, na mashairi yaliyoandikwa na Waarabu. Hili ni kwa sababu hamu na sababu za kuinakili na kuihifadhi Qur'ani zilishitadi na kufikia kiwango ambacho hakikufikiwa na hayo mengine tuliyoyataja.... katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w. Qu'rani ilikuwa ni mkusanyo uliotungamanishwa

kama ulivyo hivi sasa. Mtume s.a.w.w. alikuwa hata ameteua masahaba wa kuihifadhi kwa moyo na kuilinda. Pia ilikuwa ni desturi (ya baadhi ya masahaba) kuisoma mbele zake ili kuhakikisha kuwa ndivyo. Kikundi cha masahaba, kama vile Abdullah b. Mas'ud, Ubayy b. Ka'b, na wengineo walikiihitimisha Qur'ani mbele za Mtume s.a.w.w. hitima kadha wa kadha. Na yote haya yaonyesha, hata kwa taamuli ndogo, kwamba Qur'ani ilikuwa ni mkusanyo uliopangwa; haukukatika kipande wala haukutawanyika.... Na kwamba yeyote katika Imamiyya (Shia Ithnaashari) au Hashwiyya (wasiokuwa Shia), anaye amini kinyume cha hivyo, basi kinyume hicho chatokana na watu wa Hadith walionakili Hadith dhaifu wakidhania ni sahihi; hali Hadith dhaifu kama hizo haziwezi kulirudi jambo ambalo usahihi wake unajulikana kwa njia isiyo na shaka.

Maneno hayo unaweza kuyaona katika Majma'ul Bayaan, Juzuu ya Kwanza, uk. 15.

(4) Shaykh at-Taifah AbuJa'far Muhammadb. al-Hasan at-Tusi: Huyu alifariki katika mwaka 461 H. Yeye amesema, kama ilivyo katika uk. 48-49 wa Juzuu ya Kwanza ya Tafsirus Swaafi:

Ama neno la kwamba (Qur'ani) imezidi au imepungua; hilo si jambo lililo laiki yake. Maana (kusema) kuwa imezidi, kuna kongamano (la wanazuoni kwamba fikira hiyo) ni batili. Ama kuwa imepungua, lililo dhahiri vile vile katika madhehebu yote ya Kiislamu ni kinyume chake. Na ndilo lililo sahihi katika madhehebu yetu. Na hii ndiyo (imani) iliyoungwa mkono na Sayyid al-Murtadhaa r.a., na ndiyo iliyo dhahiri katika riwaya mbalimbali. Hata hivyo, kuna riwaya nyingi za kwa upande wa Shia na Sunni kuhusu kupungua kwa aya nyingi za Qur'ani, na kuhusu baadhi ya aya kuwa mahali pa aya nyingine. Lakini riwaya zote hizo ni za aahaad (si mutawaatirl zisizo na yakini. Kwa hivyo lililo bora ni kujiepusha na riwaya kama hizo na kutoshughulika nazo. Maana yamkinika kuziawili (riwaya kama) hizo. Na lau kama riwaya hizo zingalikuwa sahihi zisingaliweza kuyatia doa yale yaliyomo baina ya majalada mawili (ya Qur'ani) kwa kuwa yajulikana kuwa yote ni sahihi isiyopingwa wala kukataliwa na yeyote katika umma wa Kiislamu...

(5) Abu Ali at-Tabarsi: Huyu alifariki katika mwaka 548H. Yeye amesema katika Juzuu ya Kwanza ya tafsiri yake iitwayo Majma'ul Bayaan: (uk 15).

Kuna kongamano la Waislamu kwamba hakuna kilichozidi katika Qur'ani. Ama kuwa imepungua; baadhi ya watu wetu na baadhi ya Hashwiyya (yaani Sunni) wamesema kuwa kuna mabadiliko na upungufu katika Qur'ani. Lakini lililo sahihi katika madhehebu ya watu wetu ni kinyume chake...

(6) Sayyid Ibn Twaawus: Huyu alifariki katika mwaka 664H. Yeye amesema:

Maoni ya Imamiyya ni kwamba Qur'ani haikupotolewa.

Kisha akaendelea kusema, katika kuwarudl Sunni:

Mimi nawastaajabia wale ambao hutoa ushahidi kwamba Qur'ani imehifadhiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w., na kwamba yeye mwenyewe ndiye aliyeikusanya, kisha wakataja hitilafu iliyoko baina ya watu wa Makka na Madina, na watu wa Kofa na Basra. Na wakaamini kwamba Bisinillahir Rahmanir Rahim si sehemu ya sura! Bali lililo la ajabu zaidi ni kule kutoa hoja kwao kwamba lau ingelikuwa ni sehemu ya sura, basi pangelitajwa kifunguzi chengine kabla yake. Ajabu iliyoje! Kama Qur'ani imehifadhiwa na ziada na upungufu wowote, kama inavyokubaliwa na akili na sheria, basi vipi itawezekana kuwa na aya kabla yake ambayo haimo ndani yake? Vipi itawezekana hivyo?

Hayo ndiyo maneno ya mwanachuoni huyo yaliyomo katika uk. 144-145 na 192-193 wa kitabu chake kiitwacho Sa'dus Su'ud.

Kwa kuwa hatukusudii kuyafanya mambo marefu katika majibu haya (ingawa tutakuwa tayari kufanya hivyo iwapo dharura), hatuna haja ya kuendelea kuyadondoa yote yaliyosemwa na wanazuoni wa Kishia juu ya jambo hili. Twadhani hayo tuliyoyataja yatatosha kwa sasa. Lakini, kwa faida ya wasomaji wetu, tunawatajia hapa chini baadhi ya majina ya wanazuoni wengine wa Kishia (sio wote) waliosema kuwa Qur'ani Tukufu iliyokuwako zama za Mtume s.a.w.w. ndiyo hii hii waliyonayo Waislamu leo; haikuzidi, haikupungua:

(1) Mulla Fathullah al-Kashani (aliyefariki mwaka 988H) katika tafsiri yake Manhajus Sadiqin.

(2) al-Muhaqqiq Zaynuddin al-Bayadhi (aliyefariki mwaka 877H) katika kitabu chake as-Swiratum Mustaqini.

(3) Muhammad Bahauddin al-Amili, maarufu Shaykh al-Bahai (aliyefariki mwaka 1031H), Kama alivyonakiliwa katika Tafsiri ya Aalaair Rahman.

(4) Mulla Muhsin, maarufu kwa jina la al-Faydhul Kashani (aliyefariki mwaka 1091H) katika tafsiri yake iitwayo Tafsirus Swafi.

(5) Muhammad b. al-Hasan al-Hurrul Amili (aliyefariki mwaka 1104H) katika risala yake kwa Kifursi Risala Fi Ithbati Adamit Tahrif.

(6) al-dadhi Sayyid Nurullah as-Shustari (aliyefariki 1091H) kama alivyonakiliwa katika Aalair Rahman.

(7) Sayyid Muhammad Mahdi b.Sayyid Murtadha at-Tabatabai, ajulikanaye kama Bahrul Ulum (aliyefariki 1212H) katika kitabu chake kiitwacho Fawaidul Usul.

(8) Ja'far b. Shaykh Khidhr aj-Janahi an-Najafi, ajulikanaye kama Kashiful Ghitaa (aliyefariki 1228H) katika kitabu chake kiitwacho Kashful Ghitaa An Mubhamatis Shariatil Gharraa.

(9) Muhammad Hassan b. al-Mawla Abdullah al-Mamaqani (aliyefariki 1323H) katika kitabu chake kiitwacho Tanqihul Maqal.

(10) Muhammad Jawad al-Balaghi (aliyefariki 1352H) katika tafsiri yake iitwayo Aalair Rahman.

(11) Ayatullah Sayyid Husayn Kuhkamah (aliyefariki 1299H), kama ilivyoelezwa na mwanafunzi wake katika Bushral Wasul lla llmil Usul.

(12) Mirza Hassan al-Ashtiyani (aliyefariki 1319H) katika kitabu chake kiitwacho Bahrul Fawaid.

(13) Sayyid Abdul Husayn Sharafuddin al-Musawi al-Amili (aliyefariki 1377H) katika kitabu chake kiitwacho Ajwibatu Masaili Musa Jarullah.

(14) Ayatullahil Udhmaa Sayyid Abul Qasim al-Khui (ambaye bado yu hai) katika tafsiri yake iitwayo al-Bayan.

(15) al-lmam al-Khumayni katika kitabu chake kiitwacho Kashful Asrar.

(16) Muhammad an-Nahawandi katika tafsiri yake iitwayo Nafahatur Rahman.

(17) Sayyid Ali Naqi al-Hindi katika utangulizi wa kitabu chake kiitwacho Tafsirul qur'an.

Hayo basi ndiyo maneno ya baadhi ya wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kishia - kuanzia karne ya tatu hadi hii tuliyonayo! Unapoyasoma maneno yao unaona wazi kwamba imani ya Shia kuhusu Qur'ani Tukufu ni kama ile ya Waislamu wote - kwamba tangu ilipoteremshwa hadi leo haijabadilika hata kitone. Lakini, kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, Shelkh M. al-Khatib hakupendelea kujulisha Waislamu maneno hayo. Badala yake amependelea kuwambia yafuatayo; kwamba:

(i) misingi ya dini kwa Shia Imesimama 'juu ya kutaawili aya kuyapindua maana yake zifahamike kinyume na walivyozifahamu maswahaba kutoka kwa Mtume s.a.w.w. na kinyume na walivyozifahamu wale watu wa mwanzo ambao qur'ani iliteremka kwao! (tazama uk. 4 wa kitabu chake hicho).

(ii) 'Qur'ani imezidishwa na imepunguzwa', na kwamba ushahidi wa hilo umo katika kitabu kiitwacho Fasl ul-Khitab Fi Ithbati Tahrifi Kitabi Rabbil Arbab cha Haji Mirza Husayn at-Twabarsy. (uk. 4)

(iii) Miongoni mwa ushahidi kwamba Qur'ani imepungua ni Surat al-Wilaya ambayo ati Shia wanadai kwamba imetolewa katika misahafu tuliyo nayo; na kwamba sura hiyo imethibitishwa katika hicho kitabu cha at-Twabarsy tulichokitaja hapo (ii) juu. (uk. 5)

(iv) 'Sura hiyo vile vile ilo kwenye kitabu chao (Dabistan Madhhabi kwa lugha ya Kifursi kilichoandikwa na Muhsin Faniy al-Kashmiri.' (uk. 6)

(v) Hali kadhalika, kama alivyotoa ushahidi kwa Surat al-Wilaya kuthibitisha kwamba qur'ani imebadilishwa, at-Twabarsy ametoa ushahidi 'kwa yaliyo kwenye ukurasa wa 289 wa kitabu cha (al-Kafi} chapa ya mwaka wa 1278H, Iran.' Kitabu hicho kwa Shia, anavyodai Sheikh M. al-Khatib, 'ni Swahihi ya Bukhari kwa Waislamu.' (uk. 6)

(vi) 'Miongoni mwa aya wanazozidai Mashia kuwa zimeondolewa kwenye qur'ani' ni ile aya isemayo: Waja'alnaa Aliyyan swihraka, yaani: 'Na tukamfanya Ali kuwa ni mkwe wako.' (uk. 7).

(vii) Shia wana Mswahafu wa Fatima ambao 'ndani yake kuna kama qur'ani yenu hii mara tatu. Hakuna ndani yake herufi moja ya qur'ani yenu!' (uk. 9)

Kwa hivyo, hebu tuyachambue na kuyajibu madai hayo moja baada ya moja:

Kuawili aya

Hilo ndilo dai la kwanza la Sheikh M. al-Khatib kwamba Shia,Wanapoifasiri Qur'ani, huziawili aya na kuzipindua maana yake ili 'zifahamike kinyume na walivyozifahamu masahaba kutoka kwa Mtume (s.a.w.w.), na kinyume na walivyozifahamu wale watu wa mwanzo ambao Qur'ani iliteremka kwao.' (taz. uk. 4).

Hapa, jambo la kushangaza ni kwamba shekhe wetu huyo hakutupa angalau mfano wa aya mbili tatu tu zllizoawillwa hivyo ili kuthibitisha dai lake hilo. Pengine wale walioko hai sasa, waliomshikia kazi yake, watatufanyia wema wa hilo pindi itakapowapendeza kutujibu.

Kwa hivi sasa ningependa wasomaji wetu watukufu waelewe kwamba baadhi ya tafsiri za qur'ani za Shia, kama zilivyo zile za Waislamu wa madhehebu mengine, zimekusanya riwaya zilizo sahihi na zisizo sahihi. Na mtu anaposoma vitabu vya wafasiri na wahadithi wa Kishia ataona jinsi mabingwa hao walivyozichambua - ama kwa kuzikubali au kuzikataa - riwaya kama hizo. Na hivi hivi ndivyo ilivyo kwa Sunni.

Lakini kama Sheikh M. al-Khatib ana lazima Shia wote wawe makosani kwa sababu tu baadhi ya mashekhe wao wameziawili baadhi ya aya - hata kama taawili hizo si zenye kukubaliwa na Shia wote - jee na Shia nao wasemeje kuhusu taawili kama hizo kwa upande wa Sunni? Au shekhe wetu huyo, na wengine wenye fikira kama zake, hawazijui taawili zilizomo katika vitabu vya Kisunni vya tafsiri - kama vile ad-Dwrul Manthuir ya Suyuti, Gharaibul Qur'an ya An-nishaburi, Tafsirul Qur'anil Adhim ya at-Tustari, Araisul Bayan ya as-Shirazi, Tafsir ya Ibn Arabi, na nyinginezo? Au akataa kwamba hao wote ni Sunni, si Shia?

Kwa hivyo, ndugu yangu, hiyo ya taawili ya aya si hoja ya kuzuia Sunni na Shia kukurubiana na kushirikiana kwa maslaha ya Uislamu. Maana lidaiwalo liko kwa Shia, na kwa Sunni nako liko!

Daila pili la shekhe wetu M. al-Khatib ni la kitabu kiitwacho Faslul Khitab Fi Ithbati Tahrifi Kitabi Rabbil Arbab cha Haji Mirza Husein at-Twabarsy.

Katika uk. 4 wa kitabu chake, Sheikh M. al-Khatib amesema kwamba ndani ya kitabu hicho cha Faslul Khitab mna ushahidi kwamba, kwa imani ya Kishia, 'qur'ani imezidishwa na imepunguzwa.'

Kuhusu dai hilo, tazama uk. 9-11 wa kitabu hiki uone jinsi wanazuoni mbalimbali wa Kishia walivyokanusha jambo hilo. Pia tazama uk. 19-22 uone kwamba fikra hiyo ya qur'ani kuzidishwa na kupunguzwa iko hata kwa Sunni - tena katika vitabu vyao vikubwakubwa vinavyotegemewa kuwa ndivyo 'sahihi mno baada ya Qur'ani'! Sasa basi, kama mambo ni hivyo, kwa nini zani iwashukie Shia peke yao?

Tukija kwenye hicho kitabu chenyewe, Faslul Khitab; ni kweli, kama alivyosema Sheikh M. al-Khatib, kilichapishwa Iran katika 1298. Lakini si kweli kwamba kimekusanya ushahidi wa wanavyuoni wa Kishia na wana ijitihadi wao' peke yao! Bali ukweli ni kwamba kitabu hicho kimekusanya ushahidi wa hata Sunni - tena kwa wingi zaidi!

Hata hivyo, lililo muhimu hapa ni kujua kwamba, baada ya kitabu hicho kuchapishwa, palitokea wanazuoni wa Kishia walioandika vitabu kukirudi. Nao ni Sayyid Muhammad Husein Shahristani kwa kitabu chake: Risalatu Hifdhil Kitabis Sharifi An Shubhatil Qawli Bit Tahrif na Sheikh Mahmud at-Tahrani kwa kitabu chake: Kashful Irtiyabi. Jee, shekhe wetu huyo hakuyajua hayo?

Juu ya yote hayo, ieleweke kwamba mwandishi huyo wa Faslul Khitab, kabla ya kufariki dunia, alikiri kosa lake la kukiita kitabu hicho hivyo alivyokiita. Bali akasema kwamba lililokuwa bora ni kukiita kitabu hicho Faslul Khitab Fi Adami Tahrifil Kitab maana katika kitabu chake hicho amethibitisha kwamba sura na aya zote za qur'ani Tukufu, iliyomo baina ya majalada mawili na kuenea pande (zote) za ulimwengu, 'ni wahyi wa Mwenyezi Mungu ambao haukuingiliwa na mageuzo wala mabadiliko, ziada wala upungufu - tangu ilipokusanywa hadi leo....'

Lakini hata kama tutakubali kuwa yote yaliyomo katika Faslul Khitab yatoka katika riwaya za Kishia, na hata kama tutakataa ripoti ya Sheikh at-Twabarsy kukiri kosa lake, Sheikh M. al-Khatib atatwambiaje kuhusu baadhi ya zile riwaya zilizomo katika Juzuu ya Pili ya Al-ltqan ya Suyuti ambazo ni sawa na zile zilizomo katika hiyo Faslul Khitab? Jee kwa hilo, yeye au wale wenye fikira kama zake, yu tayari kuwahukumu Sunni kama alivyowahukumu Shia kwa Faslul Khitab? Kama hawatakuwa tayari, basi wasomaji wetu watukufu watakuwa na haki ya kutaka kujua kwa nini.

Surat al-Wilaya

Hii ndiyo sura inayochezewa mno ngoma na wapinzani wa Shia.

Kwa mujibu wa Sheikh M. al-Khatib (uk. 5) sura hiyo imetajwa katika uk. 180 wa Faslul Khitab. Hali kadhalika, mwanachuoni mmoja 'mwenye kuaminika' aitwaye Muhammad Ali

Saudiy na aliyekuwa mshauri mkubwa wa Wizara ya Sheria ya Misri, aliuona msahafu wa Kiirani kwa al-Mustashriq Brown akaweza kuinakili sura hiyo kwa picha!

Hayo ndiyo anayo twambia shekhe wetu huyo!

Jambo la kushangaza mno kuhusu dai hili ni kwamba kila anayelitolea ushahidi hutoa nakala hiyo hiyo aliyoipata Ustadh Muhammad Ali Saudiy kwa Mr Brown' Kwanini iwe hivyo?Au ndiyo tuseme kuwa ulimwengu mzima hakuna nakala nyingine ya msahafu huo isipokuwa ya Mzungu huyo, Mr Brown? Mzungu huyo aliwezaje kuipata nakala hiyo, shekhe wetu na wenzake wakashindwa kuipata? Na kwa nini Shia waifiche sura hiyo, kama wanaamini ni mojawapo ya sura za Qur'ani, hali inazungumzia wilaya ya Imam Ali a.s. ambayo ni kati ya nguzo kubwa ya imani ya Shia? Kama Shia hutoa ushahidi wa wilaya ya Imam Ali a.s. kwa aya mbalimbali za qur'ani, kwa nini basi waifiche sura hiyo? Na kwa nini tunapotazama tafsiri zote za Shia za qur'ani, za lugha zote, hatuioni sura hiyo? Yote hayo ni maswali ambayo inataka ujiulize, ewe ndugu yangu, ili usizuzuliwe na uzuzi huo.

Hilo la kwamba nakala hiyo ilipatikana kwa mustashriq peke yake ni sababu tosha ya kumfanya Mwislamu yeyote, aliye na insafi na dini yake, kutokubali uzuzi huo. Maana mustashriqn - (au orientalists kwa Kiingereza) ni maadui wakubwa wa Uislamu. Hawa ni wale Wazungu na Mayahudi walioiunda taaluma hii ya istishraq {orientalism) kwa malengo ya kuudhoofisha na kuuvunja umoja wa Waislamu, kuupalilia njia ukoloni uingie katika nchi za Kiislamu, na kuwanyonya Waislamu pamoja na kuwahujumu kwa kuupinga Ukristo katika Zama za Kati. ili kutekeleza malengo yao hayo, walianzisha majarida na vyuo mbalimbali, wakafanya mikutano na kutunga vitabu mbalimbali vya kuhujumu Qur'ani Tukufu, Mtume Muhammad s.a.w.w., na Uislamu kwa jumla - tena kwa njia ya hila sana.

Kama watu hao ni hivyo, vipi basi Sheikh M. al-Khatib atatosheka na ushahidi wa nakala moja tu iliyopatikana kwa watu kama hao? Au kwa nini aone hilo la sura hiyo tu ndilo kubwa? Kwa nini asiyakumbuke na yale yaliyomo katika vitabu vya Kisunni, ya sura zenye aya nyingi zaidi kuliko hizo saba za Surat al-Wilaya, zilizopungua katika Qur'ani?! Hapa chini tutatoa mifano miwili tu; iliyobaki itazame kwenye uk. 19-22 humu:

(i) Katika uk. 152 wa Juzuu ya Saba ya Majma'uz Zawaid imeandikwa 'kwamba Abdulrah-man b. Yazid, yaani an-Nakhai, amesema kwamba Abdallah alikuwa akizifuta muawwidhataini katika misahafu yake, na akisema kwamba hizo si katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu s.w.t. Kisha imeendelea: 'lmepokewa na Abdallah b. Ahmad na Tabrani. Na watu wa Abdallah ni watu sahihi, na watu wa Tabrani ni waaminifu Kwa hivyo, kutokana na Hadith hiyo, sura mbili hizo (Sura 113 na 114) zilizomo katika misahafu tuliyonayo, zimeongezwa! Kama ni hivyo, jee Shia hawatakuwa na haki ya kuwashutumu ndugu zao Sunni kuwa qur'ani yao imeongezwa?

(ii) Ukija kwenye al-ltqan ya Imam Suyuti (Juzuu ya Kwanza, uk. 87), imeandikwa kwamba katika msahafu wa Ibn Abbas na Ubayy b. Ka'b mlikuwa na sura mbili, AI-Khala' na AI-Hafd zisemazo:

اللهم انا نستعينک و نستغفرک ونثنی عليک ولا نکفرک ونخلع ونترک من يفجرک اللهم اياک نعبد ولک نصلی ونسجد واليک نسعی ونحفد نرجو رحمتک ونخشی عذابک ان عذابک بالکافرين ملحق

Jee? Leo ukiuangalia msahafu wako, zimo sura zenye majina hayo? Majibu ni: hamna! Jee, zimo aya kama hizo msahafuni? IVIajibu vile vile ni: hamna! Jee mtu akisema, kwa maneno hayo ya Imam Suyuti, kwamba Qur'ani imepungua sura mbili, atakuwa amekosea? Jee Sheikh M. al-Khatib atazilinganisha vipi sura mbili hizo kwa ile moja ya al-Wilaya?

(iii) Ukija kwenye Sahih Muslim (taz. 'Kitab az-Zakat' Mlango wa 'Law Anna Libni Adama Waadiyayni Labtaghaa Thalithan') twaambiwa kwamba Abu Musa al-Ash'ari amesema kwamba walikisoma sura ambayo urefu wake ulikuwa ni kama wa Sura Bara'ah, lakini sasa ameisahau isipokuwa aya moja tu isemayo:

لوکان لابن آدم واديان من مال لابتغی واديا ثالثا ولا يملا جوف ابن آدم الا التراب

Akasema vile vile kwamba walikiisoma sura waliyokiilinganisha na mojawapo ya musabbi-haat (sura zianzazo kwa sabbaha au yusabbihu) lakini ameisahau isipokuwa aya moja tu aikumbukayo:

يا ايها الذين آمنوا لم تقولون مالا تفعلون، فتکتب شهادة فی اعناقکم فتسألون عنها يوم القيامة

Ewe ndugu yangu! Ukumbuke kwamba Sura Bara'ah ni ile Sura ya 9 katika Juzuu ya 10 ya Qur'ani ambayo vile vile huitwa Sura at-Tawba. Sura hiyo ina jumla ya aya 129. Kwa hivyo;

kutokana na Hadith hiyo tuliyoitaja hapo juu, hii qur'ani tuliyonayo imepungukiwa na sura yenye aya 129. Maana ukiiangalia hata hiyo aya aliyokiikumbuka Abu Musa al-Ash'ari, hivi leo huioni katika misahafu iliyoko! Jee, bado Sheikh M. al-Khatib ataka kuwashutumu Shia kwa kupungukiwa na aya saba za Surat al-Wilaya, lakini Shia wasiwashutumu wao kwa kupungukiwa na aya 129?

Tukiangalia musabbihaat; hizi jumla ni sura sita: Sura ya 57, 59, 61, 62, 64 na 87. Kati ya hizo, iliyo fupi mno ni ile ya 62 (Sura al-Jumu'a) yenye aya kumi na moja. Lakini unapoiangalia sura hiyo, bali na hata hizo nyingine zote, huioni hiyo aya aliyokiikumbuka Abu Musa al-Ash'ari isipokuwa kipande cha kwanza tu ambacho ni aya ya pili ya Sura ya 61 (as-Saff).

Jee, yakifika hapo, tusemeje? Jee, wale waliojitolea kumsaidia Sheikh M. al-Khatib, kwa kukifasiri kitabu chake na kukieneza, watatwambiaje? Bado wataka tukubali kwamba wasemao kuwa qur'ani imepungua ni Shia peke yao?

Kwa wale wenye Sahih Muslim ya Kiingereza, nawaitazame Hadith Na. 2286 iliyo kwenye uk. 500-501 wa Juzuu ya Pili.

Mwisho, amesema shekhe wetu huyo (uk.5) kwamba Sheikh at-Twabarsy ameiandika hiyo Surat al-Wilaya katika uk. 180 wa hicho kitabu chake, Fasul Khitab. Lakini Sheikh Lutful Lahi as-Swafi amelikataa hilo katika uk. 62 wa Ma'al Khatib Fi Khututihil Aridhwa. Akasema:

'Hamna katika Fasilul Khitab - si katika uk. 180 wala mwingineo - tangu mwanzo wa kitabu hadi mwisho wake, mahali palipotajwa sura hiyo (al-Wilaya) ya uwongo . . .!' Jee?

Dabistan Madhhab

Dai la nne la Sheikh M. al-Khatib (uk.6) ni kwamba sura hiyo ya al-Wilaya vile vile iko kwenye

kitabu cha Kishia kiitwacho Dabistan Madhhab kilichoandikwa kwa lugha ya Kifursi na Muhsin Fani al-Kashmiri, na kuchapishwa chapa nyingi huko Iran.

Majibu yetu hapa ni: (i) kitabu hicho si cha Kishia; (ii) hakuna uhakika kwamba mwandishi wake ni huyo aliyetajwa na Sheikh M. al-Khatib; (iii) si kweli kwamba kimechapishwa chapa nyingi huko Iran; na, lililo muhimu sana, (iv) katika kitabu hicho hamkutajwa hiyo Surat al-Wilaya!                                                                    

Hivyo ndivyo asemavyo Sheikh Lutful Lahi as-Swafi, aliyelifanyia utafiti dai hilo na ana yeielewa vizuri lugha ya Kifursi, katika kitabu chake Ma'al Khatib Fi Khututihil Aridhwa (uk.64-66) - maneno ambayo hapa chini twayaeleza kwa muhtasari tu:

Kitabu hicho hakihusu Ushia. Kinahusu mambo ya mila mbali mbali - ya kweli na ya uwongo. Kimejaa visa ambavyo akili haiwezi kukubali kuwa ni vya kweli; na vingi ya visa hivyo vimenakiliwa kwa watu wasiojulikana ingawa, kwa dhahiri ya majina yao, yaonekana ni madarweshi wa Kibaniani

Kitabu chenyewe pia hakina jina la mwandishi wala la madhehebu yake. Bali pana hitilafu juu ya ni nani hasa mwandishi wa kitabu hicho. Wengine wasema ni Muhsin al-Kashmiri. Wengine, ni Dhul Fikar. Wengine, ni Muhammad Fani. Wengine, ni Mobed Shah. Wengine, ni Mobed Afraseyab. Na wengine, ni Kykhosro Ibn Azar Kywan. llmuradi, hakuna uhakika kwamba huyo Muhsin Fani al-Kashmiri ndiye mwandishi wa kitabu hicho.

Kuhusu dai kwamba kitabu hicho kimechapishwa 'chapa nyingi huko Iran', Sheikh Lutful Lahi as-Swaafi amesema (uk. 66) kwamba, baada ya utafiti mkubwa sana wa maktaba zote kubwar kubwa, ameweza kupata nakala tatu tu za kitabu hicho: kimoja ni chapa ya kwanza iliyochapishwa Bombay, mwaka 1262. Cha pili ni chapa ya pili iliyochapishwa mwaka 1268, lakini haikutajwa mahali ilipochapishwa. Na cha tatu ni chapa ya tatu iliyochapishwa Bombay vile vile katika mwaka 1277. Jee, hizo ndizo 'chapa nyingi'? Na jee, Bombay iko Iran?

al-Kafi si Bukhari

Dai la tano la Sheikh M. al-Khatib (uk.6) ni kwamba at-Twabarsy ametoa ushahidi kuwa qur'ani imebadilishwa 'kwa yaliyo kwenye ukurasa wa 289 wa kitabu cha (al-Kafi)....' na kwamba kitabu hicho kwa Shia 'ni Swahihi ya Bukhari kwa Waislamu!' Kama kwamba Shia si Waislamul!

lli kuweza kulijibu dai hilo, hebu tuangalie wanavyosema Shia juu ya al-Kafi, na wanavyosema Sunni juu ya al-Bukhari; jee vitabu viwili hivyo vinalingana?

Amesema Sayyid Hashim Ma'ruf al-Hasani, katika uk. 132 na 134 wa kitabu chake kiitwacho Diraasaatun Fil Hadith Walmuhaddithin kwamba (wanazuoni) waliotangulia hawaku-kongamana katika kuzitegemea riwaya zake (yaani, za al-Kafi) zote - kwa jumla na kwa tafsili.' Kisha akasema: '(Katika) Hadith za al-Kafi ambazo zimefikia Hadith 16199 (elfu kumi na sita, mia moja na tisini na tisa), Hadith 5072 (elfu tano na sabini na mbili) ndizo sahihi, 144 ni hasan, 1128 ni muwath-thaq, 302 ni qawiy, na 9553 ni dhaif.'

Kutokana na maelezo hayo basi, itaonekana kwamba zaidi ya 50% (asilimia hamsini) ya Hadith za al-Kafi si sahihi!

Hivyoni wasemavyo Shia wao wenyewe juu ya kitabu chao hicho. Sasa tutazame wasemavyo Sunni nao juu ya chao, al-Bukhari.

Amesema Imam Dhahabi kwamba al-Bukhari 'ndicho kitabu kikubwa na bora kuliko vitabu vyote vya Kiislamu baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu s.w.t.' Na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Hadith wamepokea kwamba Imam Bukhari amesema: 'Nimekifanya (kitabu changu hiki) ni hoja baina yangu na Mwenyezi Mungu s.w.t. Na sikuzitia humo isipokuwa (Hadith) sahihi tupu. Na nilizoziacha katika (Hadith) sahihi ni nyingi zaidi ili (kitabu cheke) kisiwe kikubwa mno.' (taz. uk. 379 wa al-Hadith Wal Muhaddithun cha Muhammad Abu Zahra).

Zaidi ya hayo, hivi karibuni (katika Februari 1966) jarida moja lichapishwalo huko Kuwait, na liitwalo Majallatul Arabiy, lilichapisha (katika Toleo lake Na. 87) makala ya Abdul Warith Kabir yenye kichwa cha habari: 'Si Kila Kilichomo Katika Sahih Bukhari ni Sahihi, Bali Yamo ya Uzuzi na Munkar.' Makala hayo yaliudhi mashekhe wengi wa Kisunni wakiwamo, miongoni mwao, Sheikh Muhammad Abu Zahra na Sheikh Yusuf al-Qardhawi. Hata wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Damascus, wapatao 31, wakaandika ardhilhali kali kwa Mfalme wa Kuwait kupinga makala hayo, na kumtaka Mfalme huyo atumie uwezo wake kuzuia uchapishaji wa makala ya aina hiyo. Kwa upande mwingine, chama kimoja cha Kuwait kiitwacho Jumuiyyatul Islahil Ijtimaiy kikakusanya makala mbalimbali, yaliyoandikwa na mashekhe mbalimbali kumtetea Bukhari, na kuyachapishia kijitabu kiitwacho Kullu Maa Fil Bukhari Sahih (Kila Kilichomo Katika Bukhari ni Sahihi). Kwa hivyo, mpaka katika hii karne tuliyonayo, Sunni bado wanaamini kwamba yote yaliyomo katika al-Bukhari ni sahihi!

Sasa basi,ewe ndugu yangu, kama Shia waamini kwamba zaidi ya asilimia hamsini(50)ya Hadith zilizomo katika al-Kafi si sahihi; na kama Sunni waamini kwamba Hadith zote zilizomo katika al-Bukhari ni sahihi, vipi al-Kafi itakuwa ni kama al-Bukhari? Kwa mantiki gani? Pengine wale wanaokubaliana na mawazo ya marehemu Sheikh M. al-Khatib watajaribu kutweleza, itakapowapendeza kutujibu.

Kwa maelezo haya mafupi, itadhihirika kwamba huo ushahidi anaosema Sheikh M. al-Khatib kuwa umo katika uk. 29 wa al-Kafi utakuwa ni wa hizo Hadith zisizo sahihi. Na hilo lishasemwa na wanazuoni wa Kishia wa Hadith katika vitabu vyao mbalimbali - kwa mfano, Rijaalun Najjaashi; Qaamusur Rijaal; Mu'jam Rijaal al-Hadith; Khulaasatur Rijaal; na Diraasaatun Fil Hadith Wal Muhaddithin.

Hayo ndiyo majibu yetu, kwa ufupi, juu ya al-Kafi na yaliyomo humo.

Waja'alnaa Aliyyan Swihraka

Hilo ni dai la sita la shekhe wetu, M. al-Khatib - kuwa maneno hayo ni aya iliyokuwamo katika Qur'ani, lakini sasa Shia wadai imeondolewa!

Majibu:Baada ya kuelewa msimamo wa Shia juu ya qur'ani (kwamba iko vile vile kama alivyoteremshiwa Mtume Muhammad s.a.w.w.), na maneno ya wanazuoni wao wa Hadith juu ya Hadith zinazogusia kupungua au kuzidishwa kwa Qur'ani (kuwa si sahihi), bila shaka hiyo

'aya' iliyotajwa hapo juu itakuwa ni miongoni mwa riwaya hizo hizo zisizo sahihi.

Na kupatikana riwaya kama hizo katika vitabu vya Shia si bina. Maana hata katika vitabu vya Sunni zimo! Kwa mfano, tazama Sahih Bukhari: 'Kitab at-Tafsir," Mlango wa 'Tabbat Yadaa Abi Lahabin Watabba/ utaona kwamba Ibn Abbas amesema: 'lliposhuka:

وأنذر عشيرتک الأقربين «ورهطک منهم المخلصين»

Jee, tusemeje na hiyo ni Sahih Bukhari ambayo usahihi wake tushaona ulivyo tetewa (taz. uk. 17)? Jee hicho kipande cha mwisho kisemacho warah twaka minhumul mukhlaswiin kimo'katika Qur'ani tuliyonayo? Hebu hakikisha kwa kutazama Sura 26:214 ambapo utakiona hicho kipande cha kwanza tu! Jee hicho kipande cha pili cha aya hiyo kimekwendapi?

Kwa wale wenye Sahih Bukhari kwa lugha ya Kiingereza, na watazame Hadith Na. 495 iliyoko kwenye ukurasa 467 wa Juzuu ya Sita, wataliona hilo tunalolisema.

Hata hivyo, inahuzunisha kuona kwamba ingawa Hadith hiyo, katika hiyo nuskha ya Kiingereza, imeandikwa kama tulivyoinukuu hapo juu kwa Kiarabu, kipande cha warahtwaka minhumul mukhlaswiin hakikuandikiwa tafsiri yake kwa Kiingereza! Kwa hivyo yeyote atakayei soma Hadith hiyo kwa Kiingereza, kama hajui Kiarabu, hatajua kwamba pameachwa kitu! Swali hapa ni: jee, tafsiri ya kipande hicho imeachwa kwa mghafala au makusudi?

Msahafu wa Fatima

Hili ni dai la saba la Sheikh M. al-Khatib - kwamba Shia wana msahafu uitwao Msahafu wa Fatima, na ambao ni tofauti na misahafu waliyonayo Waislamu!

Na hilo ni kweli! Lakini neno msahafu hapo halina maana ya qur'ani. Maana humo humo, katika hiyo hiyo al-Kafi aliyoitaja shekhe wetu huyo (taz. uk. 237-242 wa Juzuu ya Kwanza), mna Hadith zinazoeleza kwamba katika msahafu huo hamna chochote cha Qur'ani.

Kwa mfano, hiyo Hadith aliyoitaja yeye ni Hadith Na. 1 katika mlango uitwao Fiihi Dhikrus Swahifa Wal Jafr Wal Jami'a Wamaswhaf Fatimah a.s. Lakini mbona hakuitaja na lle Na. 3 isemayo wazi kwamba huyo huyo Abu Abdillahi aliyetajwa katika Hadith Na. 1, katika hiyo Hadith Na. 3 amesema: 'Sidai kwamba katika (msahafu) huo mna qur'ani'? Au kwa nini hakuitaja na ile Hadith Na. 4 isemayo kuwa lililomo humo ni 'wasia wa Fatima a.s ?

Kwa hivyo ni wazi kwamba, kutokana na Hadith hizo zilizomo katika al-Kafi, 'Msahafu wa Fatima' si msahafu wa Qur'ani. Maana hamna aya yoyote humo, wala maneno yoyote, yaliyofanana na aya yoyote ya qur'ani. Neno msahafu hapo limetumiwa tu kwa maana ya 'mkusanyo wa suhuf (kurasa)'; si kwa maana ya qur'ani. Maana si kila msahafu ni Qur'ani kama ambavyo si kila Jami'i ni msikiti.

Kwa majlbu haya mafupi, kuhusu madai muhimu ya Sheikh M. al-Khatib dhidi ya Shia juu ya qur'ani, nataraji nimeweza kuwaondolea ndugu zangu Waislamu tashwishi yoyote ambayo wangekuwa nayo dhidl ya ndugu zao Shia baada ya kusoma madai ya shekhe wetu huyo.

Sasa tuangalie yaliyomo katika vitabu vya Kisunni ya kuonyesha kwamba Qur'ani imepungua, tungojee majibu na maelezo ya wenye mawazo kama ya Sheikh M. al-Khatib maana yeye mwenyewe, kwa bahati mbaya, amefariki.

Hadith za al-Kafi si sahihi!

Hivyo ni wasemavyo Shia wao wenyewe juu ya kitabu chao hicho. Sasa tutazame wasemavyo Sunni nao juu ya chao, al-Buktiari.

Amesema Imam Dhahabi kwamba al-Bukhari 'ndicho kitabu kikubwa na bora kuliko vitabu vyote vya Kiislamu baada ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu s.w.t.' Na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Hadith wamepokea kwamba Imam Bukhari amesema: 'Nimekifanya (kitabu changu hiki) ni hoja baina yangu na Mwenyezi Mungu s.w.t. Na sikuzitia humo isipokuwa (Hadith) sahihi tupu. Na nilizoziacha katika (Hadith) sahihi ni nyingi zaidi ili (kitabuche) kisiwe kikubwa mno.' (taz. uk. 379 wa al-Hadith Wal Muhaddithun cha Muhammad Abu Zahw).

Zaidi ya hayo, hivi karibuni (katika Februarl 1966) jarida moja lichapishwalo huko Kuwait, na liitwalo Majallatul Arabiy, lilichapisha (katika Toleo lake Na. 87) makala ya Abdul Warith Kabir yenye kichwa cha habari: 'Si Kila Kilichomo Katika Sahih Bukhari ni Sahihi, Bali Yamo ya Uzuzi na Munkar.' Makala hayo yaliudhi mashekhe wengi wa Kisunni wakiwamo, miongoni mwao, Sheikh Muhammad Abu Zahra na Sheikh Yusuf al-dardhawi. Hata wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Damascus, wapatao 31, wakaandika ardhilhali kali kwa Mfalme wa Kuwait kupinga makala hayo, na kumtaka Mfalme huyo atumie uwezo wake kuzuia uchapishaji wa makala ya aina hiyo. Kwa upande mwingine, chama kimoja cha Kuwait kiitwacho Jumuiyyatul Islahil Ijtimaiy kikakusanya makala mbalimbali, yaliyoandikwa na mashekhe mbalimbali kumtetea Bukhari, na kuyachapishia kijitabu kiitwacho Kullu Maa Fil Bukhari Sahih (Kila Kilichomo Katika Bukhari ni Sahihi). Kwa hivyo, mpaka katika hii karne tuliyonayo, Sunni bado wanaamini kwamba yote yaliyomo katika al-Bukhari ni sahihi!

Sasa basi,ewe ndugu yangu, kama Shia waamini kwamba zaidi ya asilimia hamsini(50)ya Hadith zilizomo katika al-Kafi si sahihi; na kama Sunni waamini kwamba Hadith zote zilizomo katika al-Bukhari ni sahihi, vipi al-Kafi itakuwa ni kama al-Bukhari? Kwa mantiki gani? Pengine wale wanaokubaliana na mawazo ya marehemu Sheikh M. al-Khatib watajaribu kutweleza, itakapowapendeza kutujibu.

Kwa maelezo haya mafupi, itadhihirika kwamba huo ushahidi anaosema Shetkh M. al-Khatib kuwa umo katika uk. 29 wa a/-kafiy utakuwa ni wa hizo Hadith zisizo sahihi. Na hilo lishasemwa na wanazuoni wa Kishia wa Hadith katika vitabu vyao mbalimbali - kwa mfano, Rijaalun Najjaashi; Qaamusur Rijaal;  Mu'jam Rijaal al-Hadith; Khulaasatur Rijaal; na Diraasaatun Fil Hadith Wal Muhaddithin.

Hayo ndiyo majibu yetu, kwa ufupi, juu ya al-Kafi na yaliyomo humo.

YA MASUNNI

1. Hadith ya kwanza ni ile ya Sahih Bukhari tuliyoitaja uk. 18 humu.

2. Ya pili ni ile ya Sahih Muslim tuliyoitaja uk. 15 humu vile vile.

3. Ya tatu ni ile ya Majma'uz Zawaid tuliyoitaja uk. 14

4. Ya nne ni ile ya al-ltqan, ya sura mbili, tuliyoitaja uk. 14 Zote hizo ni Hadith zinazoonyesha kwamba hii qur'ani tuliyonayo ama imezidi au imepungua! Juu ya hizo, tutazame Hadith zifuatazo:

5. Ukitazama Sahih Bukhari, Mlango wa 'ash-Shahada Takunu Indal  Hakimi Fii Wilayatihi hadhaa/ katika 'Kitabu al-Ahkaami', utaona Hadith isemayo kwamba Umar b. Khattab amesema: 'Lau kwamba si kwa kuogopa watu kusema kuwa Umar amezidisha (kitu) katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ningeliiandika aya ya rajm kwa mikono yangu mwenyewe!'

Na katika Sahih Muslim, 'Kitabu al-Hududi', Mlango wa 'Rajmuth Thayb Fiz Zinaa', imenakiliwa kwamba Umar b. Khattab huyo huyo amesema kwamba hiyo aya ya rajm ilikuwa 'ni miongoni mwa aya alizoteremshiwa (Mtume Muhammad s.a.w.w.)' Kisha akasema: 'Tulikiisoma na kuihifadhi kwa moyo na kuielewa.'

Kwa wale wenye tafsiri za Kiingereza za vitabu viwili hivyo, nawatazame Hadith Na. 21 iliyoko kwenye uk. 212 wa Juzuu ya Tisa ya Sahih Bukhari, na Hadith Na. 4194 iliyoko kwenye uk. 912 wa Juzuu ya Tatu ya Sahih Muslim.

Na kwa wale wasioijua hiyo aya ya rajm kwa Kiarabu, ni hii:

ان الشيخ والشيخة اذا زنيا فارجموهما البتة

ambayo maana yake nl: 'Mzee mwanamume na mzee mwanamke, wanapozini, wapigeni mawe wote.'

Hapa tuna maswali mawili matatu ya kuuliza. Kwanza; hiyo ni aya ya qur'ani au si aya? Kama ni aya, kwa nini Umar b. Khattab aache kuiandika kwa kuogopa watu, asimwogope Mola wake? Kwa nini ikawa haimo katika hii qur'ani tuliyonayo sisi hii leo? Na kama si aya, kwa nini Umar b. Khattab atamani kuiandika lakini aiache kwa kuogopa watu? Kwa nini atamani kuiandika aya katika qur'ani ambayo haikuteremshwa na Mwenyezi Mungu? Na jee, Hadith kama hizo zinakwacha na flkira gani, ewe ndugu yangu?

6. Ukitazama tena Sahih Bukhari, Mlango wa 'Wamaa Khalakadh Dhakara Wal Unthaa' katika 'Kitabut Tafsir' (au, katika tafsiri yake ya Kiingereza, Hadith Na. 468 iiiyoko kwenye ukurasa 441-442 wa Juzuu ya Sita) utaona kwamba Alqama alikiisoma Sura 92:3 sio kama tunavyolsoma sisi leo, wala sio kama ilivyo misahafuni mwetu, bali hivi: Wadh dhakari Wal

Untliaa! Kisha akasema: 'Ninashuhudia kwamba nimemsikia Mtume s.a.w.w. akisoma hivi. Na hawa (yaani baadhi ya masahaba) wananitaka nisome: Wamaa Khalaqadh dhakara wal unthaa. Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Sitawafuata'.

Jee, kwa mujibu wa Hadith hiyo, si wazi kwamba neno wamaa khalaqa, lililomo katika misahafu yetu yote, limeongezwa katika hiyo Sura 92:3? Kisha tazama hapo jinsi Alqama anavyoapa kuwa hivyo ndivyo alivyokimsikia Mtume s.a.w.w. akisoma, na kwamba hatawafuata hao watu wengine waliokimtaka asisome hivyo.

Hapa ni vyema tujue kwamba si Alqama peke yake aliyesema hivyo; bali ukiitazama Hadith nyingine iliyoitangulia hiyo tuliyoitaja hapo juu (Hadith Na. 467) utamwona Abud Dardaa asema kwamba na yeye pia alikimsikia Mtume s.a.w.w. akiisoma aya hiyo kama alivyosikiwa na Alqama. Lakini naye pia akakataliwa!

7. Ukija kwenye al-ltqan Fii Ulumil Our'an ya Imam Suyuti (uk. 33 wa Juzuu ya Pili, chapa ya nne iliyochapishwa 1398H) utaona imeandikwa kwamba Abu Sufyan a!-Kala'i amesema kwamba Muslima b. Mukhallad al-Ansari aliwaambia siku moja: 'Hebu nielezeni habari ya zile aya mbili za Qur'ani ambazo hazikuandikwa msahafuni! Hakuna aliyemweleza japokuwa Abul Kanud Sa'd b. Malik alikuwapo hapo. Basi Ibn Muslima akasoma:

ان الذين آمنوا وهاجروا وجاهدوا فی سبيل الله باموالهم وانفسهم الا أبشروا انتم المفلحون والذين آووهم ونصروهم وجادلوا عنهم قوم الذين غضب الله عليهم اولئک لا تعلم نفس ما اخفی لهم من قرة اعين جزاء بما کانوا يعملون

Jee? Leo waweza kuzipata aya hizo, hivyo zilivyo, katika misahafu tulio nayo? Bila shaka huzipati! Zilizo karibu sana nazo ni Sura 8:72 na 9:20 na 32:17. Hebu zilinganishe uone jinsi zinavyotofautiana!

Jee, bado Sheikh M. al-Khatib na wenye fikira kama zake wanashikilia kuwa Shia peke yao ndio wenye Hadith za kuonyesha kuwa Qur'ani imepungua?

Zaidi ya hizo

Mpaka hapa tumetaja Hadith chache tu zinazozungumzia kupungua aya mbili tatu katika Qur'ani. Sasa tuangalie zile zinazozungumzia kupungua sehemu kubwa kubwa:

8. Ukiiangalia al-ltqan, uk. 32 wa hiyo hiyo Juzuu ya Pili, utaona kwamba imepokewa kwa Mwana Aisha kwamba amesema: 'Sura al-Ahzab ilikuwa ikisomwa zama za Mtume s.a.w.w. aya 200 (mia mbili). Lakini Uthman alipoandika misahafu, hatukupata isipokuwa hivi ilivyo sasa!"

Na hivi sasa, ilivyo katika misahafu yote tuliyonayo, ni aya 73 (sabini na tatu). Jee, kama Sheikh M. al-Khatib, au wale wenye fikira kama zake, wataulizwa ziko wapi aya 127 zilizopungua, watajibuje?

9. Isitoshe! Katika hiyo hiyo al-ltqan, ukurasa huo huo wa 32, na mara tu baada ya Hadith tuliyoitaja hapo juu, imeandikwa kwamba Dharr b. Hubaysh aliulizwa na Ubayy b. Ka'b: 'Sura al-Ahzab ina aya ngapi?'

Akajibu: 'Aya sabini na mbili au sabini na tatu.'

Ubayy akasema: 'Japokuwa ilikuwa sawa na Sura al-Baqarah au zaidi yakel'

Haya! Sura al-Baqarah, kama tujuavyo, ina aya 286. Jee tukisha zitoa hizo aya 73 zilizomo misahafuni mwetu, hizo 213 zilizobaki zimepotelea wapi? Jee, utalinganishaje kutokuwamo aya

saba za Sura al-Wilaya katika Qur'ani na hizo 213 za Sura al-Ahzab?

Hadith tuliyoitaja hapo juu vile vile waweza kuipata katika Muntakhab Kanzul Ummal iliyoko pambizoni mwa Musnad Ahmad, Juzuu ya Pili, uk. 1.

10. Tukija kwenye Sura Bara'ah, ambayo ina aya 129 katika misahafu tuliyonayo, twaambiwa la! Ni sawa na Sura al-Baqarah, yenye aya 286! (taz. uk. 80 wa Juzuu ya Kwanza ya al-ltqan). Jee tusemeje? Hizo aya 157 zilizopungua zimekwenda wapi?

11. Bali na zaidi ya hayo! Katika hiyo hiyo al-ltqan, uk. 34 wa Juzuu ya Pili, twaambiwa kwamba imepokewa kwa Hudhayfa (katika al-Mustadrak) kwamba hii Sura Bara'ah tunayoi-soma ni roboo yake!

Kutokana na Hadith hiyo, kwa hivyo, robo tatu hazijulikani ziliko! Na hizo ni aya 387! Jee, Sheikh M. al-Khatib atatwambiaje?

Hadith hiyo vile vile unaweza kuiona katika uk. 31 wa Juzuu ya Saba ya Majmauz Zawaid ambamo imesemwa kwamba wapokezi wake ni thuqaat (wa kutegemeka).

12. Zaidi ya yote hayo; kwa mujibu wa Umar b. Khattab, kama ilivyonakiliwa katika uk. 93 wa Juzuu ya Kwanza ya al-ltqan, Qur'ani ina herufi 1 027 000 (milioni moja na elfu ishirini na saba). Na kama hivyo imeelezwa katika uk. 517 wa Juzuu ya Kwanza ya Kanzui Ummal (Hadith Na. 2308).

Lakini lijulikanalo ni kwamba idadi ya herufi za Qur'ani ni thuluthi (sehemu moja ya tatu) tu ya idadi hiyol Hii, kwa hivyo, ina maana kwamba idadi ya herufi ambayo ni sawa na misahafu miwili kama huu tulionao imepotea; haijulikani ilipo! Kwa maneno mengine, Qur'ani anayokusudia Umar b. Khattab ni mara tatu ya qur'ani tuliyonayo. Kwa hivi sasa sisi tuna thuluthi moja tu!

Tafadhali linganisha msahafu huo na ule wa Mwana Fatima ambao Sheikh M. al-Khatib alitutajia katika uk. 9 wa kitabu chake, na majibu yetu yaliyomo humu ukurasa 18. Jee, wenye qur'ani iliyo mara tatu ya hii tuliyonayo ni Shia au Sunni?

Bali makubwa zaidi

Mpaka hapa tumezitaja Hadith zinazotufahamisha ni aya ngapi zilizopungua, kutokana na vitabu vya Kisunni. Lakini pia kuna zenye habari kubwa zaidi; za kutojulikana ni aya ngapi zilizopotea. Kwa mfano:

13. Ukiangalia al-tqan (Juzuu ya Pili, uk. 32) utaona imeandikwa kwamba imepokewa kwa Nafi' kwamba Ibn Umar amesema: 'Hwenda mmoja wenu akasema kwamba ameichukua qur'ani yote, lakini ni nini kitakachomjulisha hiyo yote ni ipi? (Ukweli ni kwamba) qur'ani nyingi imetoweka. Lakini naseme: Nimechukua ile sehemu iliyodhihiri.'

Ewe ndugu msomaji! Hebu isome tena riwaya hiyo, na uitafakari. Utaona kwamba Ibn Umar alikizuia watu wasiseme kwamba wameichukua Qur'ani yote. Maana hakuna anayeijua Qur'ani yote. Kwa hivyo mtu aseme tu kwamba aliyoichukua yeye ni ile aliyoipata!

Jee, hiyo ambayo haikupatikana ni kadiri gani?

14. Mbali ile sehemu iliyoliwa na mnyama wa kufugwa, na isipatikane! Ukitazama Musnad Ahmad {Juzuu ya Sita, uk. 269) utaona kwamba Mwana Aisha amesema kwamba ukurasa uliokuwa chini ya kitanda chake, uliliwa na mnyama wa kufugwa; na kwamba

kitendo hicho kilitendeka pale alipokufa Mtume s.a.w.w. ambapo kina Mwana Aisha walikuwa wameshughulika na kifo chake.

Kwa hivyo, kutokana na riwaya hiyo, ni wazi kwamba hiyo aya ya rajm, na hiyo ya kumnyonyesha mtu mzima mara kumi, zilikuwamo katika huo ukurasa ulioliwa na mnyama huyo Swali lililopo hapa ni: Sasa aya hizo ziko wapi? Mbona hazimo katika hii misahafu tuliyonayo? Kama Mwana Aisha amesema kwamba aya hizo zilikuwamo katika ukurasa huo hadi Mtume s.a.w.w. alipofariki dunia, ni nani huyo aliyezitoa baada ya Mtume s.a.w.w. kufariki? Kwa idhini ya nani?

15. Mwisho ni swala la misahafu ya masahaba.                    

Katika uk. 9 wa kitabu chake hicho, Sheikh M. al-Khatib ametaja 'msahafu wa Fatima. Lakini hakukumbuka kwamba vile vile kulikuwa na misahafu ya masahaba ambayo, yaliyomo humo, yametajwa katika vitabu kadha wa kadha'vinavyohusika vya Kisunni.

Wakati ambapo yaliyokuwamo katika msahafu wa Fatima, kama tulivyoona katika uk. 18 humu, yalikuwa si aya za qur'ani, yote yaliyomo katika misahafu ya masahaba ni aya za Qur'ani. Na humo twaziona aya ambazo, zilivyoandikwa humo, sivyo zilivyoandikwa katika hii misahafu tuliyo nayo! Jee? Ipi ndiyo sahihi? Misahafu ya hao masahaba, au hii tuliyonayo?

Kwa wale wanaojua Kiarabu, nawatazame kitabu kiitwacho al-Masahif cha Abu Dawud, watayaona hayo tunayoyasema.

Mwisho

Ewe ndugu msomaji! Hizo ni baadhi tu ya Hadith zilizomo katika vitabu vya Kisunni. Zote, kama inavyoonekana, zinaonyesha kwamba qur'ani Tukufu imepungua! Sikuzinakili Hadith hizo kwa kuwa ninazikubali; hasha! Mimi sizikubali, wala Mwislamu yeyote hawezi kuzikubali, kwa sababu zinapingana na Qur'ani (Sura 15:9 na 41:41-42). Nimezinakili tu ili kuonyesha kwamba, kama vile ambavyo katika vitabu vya Kishia hupatikana Hadith ziwezazo kueleweka kwamba Qur'ani imezidi au imepungua, kadhalika Hadith kama hizo hupatikana katika vitabu vya Kisunni. Kwa hivyo, kama Sunni atakuwa na haki ya kumshutumu Shia kwamba ana qur'ani isiyokuwa hii tuliyonayo, Shia naye -kwa hoja hiyo hiyo - atakuwa na haki kama hiyo dhidi ya Sunni.

Kutokana na yote yaliyotangulia, itaonekana kwamba qur'ani inayo aminiwa na Shia ndiyo ile ile inayoaminiwa na Sunni - chapa kwa ya pili. Kwa hivyo, katika hilo, ndugu wawili hao hawana la kugombania.

Inshallah, katika kitabu kijacho, tutatazama msimamo wa Shia juu ya Hadith za Mtume Muhammad s.a.w.w.