MJADALA WA RIWAYA ZA WAHY

Kwa kweli tukitaka kuijadili mada hii kwa undani zaidi, itatulazimu tutumie muda mrefu katika kuchambua kifungu kimoja baada ya kingine. Na hilo litahitaji kuchukua nafasi ya kitabu kizima ili kujaribu kutatua utata huo. Lakini, kama wasemavyo wataalamu: "Maa Laa yudraku kulluhu laa yutraku kulluhu" yaani, "Yasiyowe za kupatikana yote, hayaachwi yote". Kwa hiyo nasi hatutaacha kutaja japo kidogo:

Kutokana na sanad ya Hadithi, ambapo mategemeo yake yamepokelewa katika sahihi mbili (Bukhari na Muslim) na zingine, ambazo zinaonyesha kama:

Imepokewa kutoka kwa Az Zuhry kutoka kwa U'rwa bin Zubeir kutoka kwa Mwana Aisha. Sasa: hapa tutaangalia mambo ya fuatayo:

Az Zuhry na U'rwa hawa walikuwa wapinzani wa Imam Ali (a.s.) na wakimtukana.

Taz: Qamusir Rijal J. 6 Uk. 300

Algharat J. 2 Uk. 558-560

Na Mtume (s.a.w.) amesema juu ya Imam Ali (a.s.) kuwa: "Yeyote mwenye kumtukana Ali basi amenitukana mimi na mwenye kunitukana mimi amemtukana Mwenyezi Mungu".

Taz: Mustadrakul Hakim J. 3 Uk. 121

Musnad Ahmad J. 5 Uk. 30

Alfusulul Muhimma Uk. 111

Tarikh Ibn Asakir J. 2 Uk. 184

Manaqibu Ali Uk. 394

Kwa hiyo, mtu mwenye kumtukana Mtume (s.a.w.) hawezi kuwa mwema hata kidogo, licha ya kupokea mafunzo ya dini kutoka kwake.

Amma kuhusu Mwana Aisha (mkewe Mtume) ambae katika mwaka wa thelathini na sita Hijra, alitoka nyumbani mwake Madina kwenda Basra ili kumpiga Ali bin Abi Talib (a.s.) na akafanya hivyo.

Kitendo cha mke wa Mtume cha kutoka nyumbani mwake kwenda nje, ni jambo lililokatazwa na Mwenyeezi Mungu: "Na kaeni majumbani mwenu" 33:33 Mwana Aisha ameipuuza hukumu hii! Aidha, kitendo cha kumpiga Imam Ali (a.s.) ni jambo linalomuweka mtu mahala pabaya. Imepokewa kutoka kwa A'diyyi bin Thabiti kutoka kwa Zuhry amesema: "Amesema Imam Ali kuwa: "Ninaapa kwa ambaye ameumba mbegu na akaumba upepo, hiyo ni ahadi ya Mtume kwangu mimi kuwa: Hanipendi mimi isipokuwa mu'umin na hanibughudhi (hanichukii) mimi isipokuwa mnafiki".

Taz: Sahihi-Muslim katika kitabul Iman

Sahihit Tirmidhi J. 2 Uk. 301

Musnad Ahmad J. 1 Uk. 84

Tarikh Bughdad J. 2 Uk. 255

Hilyatul Awliyaa J. 4 Uk. 185

Kanzul Ummal J. 6 Uk. 394

Mustadrakul Hakim J. 3 uk 129

Al Istiab J. 2 Uk. 214

Addurrul ManthurAya ya 25 sura 47.

Mwana Aisha ameipuuza hukumu hii! Nanikweli Mwana Aisha hampendi kabisa Imam Ali (a.s.). Hilo linathibitishwa na hali halisi, kwanza, amepigana na Imam Ali (a.s.) na kupiga hakuanzi kabla ya kuchukia. Na alipopata habari Mwana Aisha kuwa Imam Ali ameuliwa, alisujudu kumshukuru Mwenyeezi Mungu!!!

Taz: Magatilut Talibina Uk. 27

Aljamal Uk. 83-84

Mwenyeezi Mungu anasema: "Haiwi kwa mwanamume aliyeamini, Mwenyeezi Mungu na Mtume wake wanapohukumu jambo wawe na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyeezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotovu ulio wazi" 33:36.

Riwaya za tukio hilo zinagongana kama unavyoziona - kama utarejea kuzisoma utaliona hilo. Lakini, kwanini Jibril amkamate Mtume kisha amkamuekamue mpaka akaribie kuzimia!? Kwanini Mtume akubali kusoma baada ya kukamuliwa kwa nguvu mara ya tatu? Kwanini asikubali tu kusoma mara ya kwanza kabla ya mateso haya? Na, vipi Mtume arudi kwa mkewe akiwa na khofu kubwa kiasi hiki!! Je! Muhammad (s.a.w.) hakuwa na uwezo wa kumpiga kofi malaika huyo?! Kama alivyofanya hivyo Nabii Musa (a.s.) alipoijiwa na Malaika I'zrail ili achukue roho yake, Musa alimpiga kofi moja tu mpaka jicho likang'oka!!

Taz: Sahihi Bukhari J. 1 Uk. 152

Sahihi Muslim J. 7 Uk. 100.

Musnad Ahmad J. 2 Uk. 315

Almuswannaf J. 11 Uk. 274

Sunannun Nasai J. 4 Uk. 118

Albidayatu Wannihaya J. 1 Uk. 317

Tarikhut Tabari J. 1 Uk. 305.

Haiwezekani kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.) alikuwa mwoga hivyo, na Nabii Musa tu peke yake awe shujaa wa kuwang'oa macho malaika!!

Kwamba, Mtume (s.a.w.) aliingiwa khofu kubwa, Khadija na Waraqa walimtuliza mpaka akatulia. Sasa, tuangalie hali hii kama ifuatavyo:

Inawezekana kwa Mwenyeezi Mungu, kumpeleka Mtume ambaye hajui Utume wake yeye mwenyewe! Ila kwa Kuthibitishiwa na mwanamke na mnasara? Vipi jambo nyeti hili agundue mwanamke kuwa huo ni Utume na wala si kichaa (kama alivyodhani Muhammad) pia mnasara ajue yaqini kuwa huo ni Utume?! Hili linatupa kufikiri kuwa hawa (mwanamke na mnasara) ni wajuzi na watukufu zaidi kuliko Muhammad (s.a.w.).

Mwenyeezi Mungu anasema: "Na wakasema waliokufuru: mbona haikuteremshwa kwake Qur'an yote mara moja? Ndivyo ilivyo, ili tukuimarishe kwayo moyo wako na tumeipanga kwa mpango." 25:32

"Waambie (Muhammad) roho takatifu ameiteremsha kutoka kwa Mola wako kwa haki, ili kuwaimarisha wale walio amini, na kuwa muongozo na habari njema kwa waliosilimu." 16:102 katika aya hizi timachunguza ibara isemayo: "ILU TUKUIMARISHE KWAYO MOYO WAKO". Kwa hiyo, moyo wa Muhammad uliimarishwa na Mwenyeezi Mungu sikiliza Mwenyeezi Mungu analifafanua hili:

"Waambie (Muhammad) hakika mimi ninayo dalili ya wazi itokayo kwa Mola wangu" 6: 57

"Waambie (Muhammad) Hii ndiyo njia yangu, ninaita kwa ujuzi hasa, mimi na wanaonifuata." 12:108

Katika Aya hizi tunaangalia maneno: "MIMI NINAYO DALILI YA WAZI ITOKAYO KWA MOLA WANGU" "NINAITA KWA UJUZI HASA" kwahiyo, Mtume Muhammad (s.a.w.) anajua kuwa anayo dalili (ushahidi) ulio wazi, na kwa ajili hiyo, anawaita watu kwa ujuzi kamili. Hii si sawa na kusema: Muhammad (s.a.w.) uliimarishwa moyo wake na mnasara (Waraqa bin Nawfal).