MWANZO WA WAHY

Amesema Bukhari na Muslim na wengineo kuwa: Imepokewa kutoka kwa Azzuhry naye amepokea kwa U'rwa bin Zubeir naye amepokea kwa Mwana Aisha (mkewe Mtume) kwamba: Malaika Jibril (a.s) alikuja kwa Mtume (s.a.w.) naye akiwa katika pango la Hiraa akamwambia: Soma, Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Mtume anasema: Malaika akanikaba kwa nguvu mpaka nikazidiwa kisha akaniambia: Soma, Mtume akajibu: Mimi sijui kusoma. Kisha ndipo Malaika alipomsisitiza kwa nguvu akisema:

"Soma kwa jina la Mola wako, ambaye ameumba. Amemuumba mwanadamu kutokana na damu iliyoganda. Soma na Mola wako ni Mtukufu kuliko wote". Qur'an, 96:1-3

Baada ya hapo, Mtume (s.a.w.) alirudi kwa mkewe mwana Khadija (a.s.) akiwa amejawa khofu kubwa. Alipoingia ndani alijitupa chini na huku akilalamika: "Nifunikeni, nifunikeni!!" Alipotulia akasema: "Ninaogopa sijui kitanipata nini?!" Khadija akamtuliza: "Sivyo! Wallahi Mwenyeezi Mungu hatakuangamiza abadani, wewe unaunga udugu, unavumilia matatizo, unasaidia wanyonge, unasaidia kuleta haki." Hapo Khadija akamchukua Mtume akampeleka kwa Ibnu ammi yake Waraqa bin Nawfal (alikuwa mnasara, mwandishi wa Injili kwa lugha ya kiibrania).

Walipofika kwa Waraqa, Khadija akamwambia: "Ewe Ibnu ammi! Msikilize Muhammad aliyo nayo." Waraqa akamuuliza, "una nini?" Muhammad akamwelezea yote kama aliyoyaona, Waraqa akamwambia: "Huyu ni Malaika ambaye amepata kumteremkia vilevile Nabii Musa (a.s.) Ee!!!" Natamani kama nitakuwa hai wakati watakapokufukuza watu wako!!! Muhammad (s.a.w) akashituka: "Watanifukuza??" Waraqa akajibu: "Ndiyo, hakuna mtu yeyote anayeleta jambo kama hili uliloleta wewe isipokuwa atapigwa vita na watu wake".

Taz: Sahihi Bukhari J.I uk, 5-6

Sahihi Muslim J. I uk, 97

Almuswannaf J. 5 uk, 322

Tarikhut Tabari J. 2 uk, 47

Madda hii (mwanzo wa Wahy) waandishi wameieleza kwa njia nyingi tofauti zenye kugongana. Hapa tutajaribu kuzitaja chache tu:

  1. Khadija na Abubakr walimpeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa bin Nawfal baada ya kuelezwa Waraqa kuwa Muhammad amepata matatizo, Waraqa akamuuliza Muhammad ana nini? Muhammad (s.a.w.) akamwambia:
  2. "Ninasikia ninaitwa nyuma yangu, ewe Muhammad ewe Muhammad, nikisikia hivyo mimi hukimbia ovyo." Waraqa akamkataza asiwe anakimbia bali akaze roho ili ayasikie anayoambiwa..." Muhammad alishika maelekezo hayo, mara aliposikia akiitwa: Ewe Muhammad! Sema, Bismillahir Rahmanir Rahim, Alhamdulillahi rabbil a'lamina.... mpaka mwisho wa suratul Fatiha. Akaambiwa: Sema: "Laa ilaha illallahu" Muhammad (s.a.w.) baada ya hapo alikwenda kwa Waraqa bin Nawfal, akamjulisha hali hiyo. Waraqa akambashiria habari njema yakuwa: "Hali kama hiyo alipewa pia Nabii Isa bin Maryam".

    Taz; Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 9

    Assiratun Nabawiyya J. 1 uk 83

    Assiratul Halabiyya J. 1 uk 250

    Siiratu Mughlataya uk, 15

  3. Khadija alipompeleka Muhammad (s.a.w.) kwa Waraqa na akamweleza yaliyomtokea. Waraqa alisema: "Huyu ni Nabii wa Umma huu, mwambie atulize moyo."
  4. Taz: Albidayatu Wannihaya J.3 uk, 12

    Siiratu Ibn Hisham J. 1 uk, 238

    Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 239.

  5. Khadija alimwambia Muhammad (s.a.w.) atakapokufikia huyo anayekusomesha, unambie, Mtume (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo akamjulisha mkewe. Khadija akampakata katika mapaja yake, kisha akavua shungi yake, mara Mtume (s.a.w.) akaona yule aliyemjia anaondoka haraka. Mtume akamjulisha mkewe hilo, Khadija akasema, "Huyo ni Malaika, na wala siyo shetani, basi kaza roho na furahi".
  6. Taz: Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 252.

  7. Waraqa bin Nawfal alimwambia Khadija: "Muulize Muhammad (s.a.w.) nani anaemjia! Ikiwa ni Malaika Mikaeli basi amemletea amani. Na ikiwa ni Malaika Jibril basi amemletea vita na mateka. Khadija Alipomuuliza Mtume (s.a.w.) akajibu: "Ni Jibril". Khadija akapiga uso wake.
  8. Taz: Tarikhul Yaa'quby J. 2 Uk. 23.

  9. Khadija alipewa kipande cha karatasi na mganga mmoja ili ampe Muhammad (s.a.w.) kama hali hii (iliyomfikia Muhammad) inasababishwa na ugonjwa wa kichaa, basi atapona... Khadija aliporudi kwa mumewe akamkuta anasoma Qur'an, Khadija akamchukua akaenda naye kwa yule mganga, walipofika kwa mganga, akafunua mgongo wa Mtume akaona muhuri wa Utume uko kati ya mabega mawili!!!
  10. Taz: Tarikhul Khamisi J. 1 Uk. 284

    Assiratul Halabiyya J. 1 Uk. 243

    Assiratun Nabawiyya J. 1. Uk. 83

  11. Muhammad (s.a.w.) alipofikiwa na hali hiyo (ya kujiwa na Malaika) alikuwa akipanda katika kilele cha mlima mrefu na akitaka kujitupa chini (ili afe).
  12. Taz: Almuswannaf J. 5 Uk. 323

  13. Muhammad (s.a.w.) alirudi kwa mkewe (kutoka katika pango) akiwa nafuraha kubwa akamwambia mkewe: "Nataka kukueleza habari njema, mimi nimeona katika ndoto kuwa Jibril amenijulisha kwamba ametumwa na Mola wangu aje kwangu... Khadija akamwambia: "Furahi, wallahi Mwenyeezi Mungu hatakufanyia lolote ila lililokuwa la kheri... kisha Khadija akaenda kwa mganga wa kinasara, kuuliza uwezekano wa kumuona Jibril. Mganga alishangaa sana kusikia jina la Jibril katika nchi hiyo, kisha akasema kuwa: "Huyo ni Mjumbe wa Mwenyeezi Mungu..."

Taz: Albidayatu Wannihaya J. 3 Uk. 13.