KUSOMA QUR'AN KWA AJILI YA MAITI

Wako baadhi ya Waislamu wanapinga kumsomea Qur'an maiti, wakisema kwamba kufanya hivyo ni bid'a na bid'a mahala pake ni motoni. Katika kupinga jambo hili wanatoa hoja zao kama ifuatavyo:

  1. Imethibiti kuwa: Mtume (s.a.w.) hakumsomea Qur'an maiti yeyote katika uhai wake, kama jambo hilo ni jema Mtume asingeliacha kufanya kheri hiyo. Kwa hiyo, yeyote leo anae soma Qur'an kwa ajili ya mait, akaamini kuwa itamnufaisha, bila shaka mtu huyo anadai kuwa Mtume amefanya khiyana katika umma huu. Na hilo ni kosa kubwa kuamini kuwa Mtume hakufikisha baadhi ya mambo katika umma wake.
  2. Mwenyeezi Mungu anasema: "Na ya kwamba mtu hatapata isipokuwa aliyoyafanyia juhudi" 53:39. Na kwa Aya hii Imam Shafi amesema kuwa: Kisomo (anachosomewa maiti) thawabu za kisomo hicho hazifiki kwa maiti. Kwa sababu hilo haliko katika matendo yake, na kwa sababu hii, Mtume hakuwawekea umma wake, wala hakuhimiza (wafanye) kwa mtu yeyote. Wala hakupendekeza, wala sahaba yeyote hakuna aliyepokea (jambo hili)
  3. Taz: Tafsir ibn Kathir J. 4 Uk. 276

  4. Amesema Mtume (s.a.w.): "Anapokufa mwanadamu, matendo yake humalizika yote isipokuwa mambo matatu: sadaka ya kudumu, au elimu yenye kunufaisha, au mtoto mwema atakaemuombea baada yake". Kwa hiyo, wasomaji wa khitima hupoteza bure muda wao, kwa kufanya jambo haliko katika Uislamu.