rudi maktaba >Maadili >

  Yaliyomo endelea

Mwanamke Mshirika Katika Maisha

Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi..” (49:13)

Je dini zimemdhulumu mwanamke? Wako wasemao hivyo lakini kabla ya kujibu swali hili kwanza ni lazima tufafanue mambo mawili:

Lazima tutofautishe kati ya dini zingine na dini ya Kiislam, kwa sababu katika dini zingine mwanamke huenda akawa na picha mbaya. Nami sina shaka kwamba dini iliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu haiwezi kumdhulumu mwanamke au kumvunjia heshima.

Ama katika dini ya Kiislam, mwanamke ana heshima, na anatukuzwa zaidi ya mwanamume.

Ni lazima tutofautishe kati ya mafunzo ya dini kwa mwanadamu na wanaadamu wenyewe wanaoifuata hiyo dini, kwani huenda ikawa hao wanaofuata dini wanamdhulumu mwanamke katika nyanja fulani, lakini hatuwezi kusema hivyo ndivyo dini inavyotaka, kwa sababu dini yenyewe haitaki uonevu, uwe umefanyiwa mwanamume au mwanamke au hata wanyama na mimea. Kwa hivyo mimi ninapozungumzia haki za mwanamke, sizungumzii msimamo wa wafuasi wa dini, bali nazungumzia msimamo wa dini, basi nasema hivi; dini haiwezekani imdhulumu mwanamke, kwa sababu ndogo tu, nayo ni kwamba dini ni orodha ya maisha iliyoletwa na mwenyewe aliyeumba hayo maisha. Na ikiwa Mwenyezi Mungu alimuumba mwanamke ili amtukuze, basi amemuumba ili amrehemu, ili amuingize peponi, kama alivyomuumba mwanamume kwa hayo; kwa hivyo haiwezekani amdhulumu, kwa sababu huyo mwanamke hakuchagua awe mwanamke au mwanamume.

Mwanamke huzaliwa mke, hana hiyari, na mwanamume pia huzaliwa mume pasi na hiyari. Vipi tena dini imhukumu mwanamke kwa jambo ambalo hakulichagua yeye mwenyewe (la kuwa mwanamke)?

Kwa hakika dini ya Kiislamu yapinga vikali kila aina ya ubaguzi wa jinsi ya mtu alivyozaliwa bila ya kujiamulia mwenyewe. Mathalan ubaguzi wa rangi (mtu hakukhiyari awe mweupe au mweusi), ubaguzi wa lugha, n.k. Dini haibagui mweusi wa Afrika wala mweupe wa Ulaya, wala haibagui kati ya anayezungumza lugha ya Kiingereza au Kijerumani au lugha nyengine. Wala haibagui aliyezaliwa nchi fulani au nyengine, kwa sababu kuchagua rangi, jamii au nchi anayozaliwa mtu hakuko chini ya uwezo wa mtu huyo. Aidha dini haibagui kati ya mume na mke kwa sababu kuchagua jinsi ya kuwa mume au mke hakuko kwenye uwezo wa mwanadamu.

Ama kuhusu kutenda mema dini haibagui katu, hapa yafafanua:

“...Hakika sitapoteza amali ya mtendaji mema miongoni mwenu awe mwanamume au mwanamke.” (3:195)

Aya nyengine yafafanua:

“Na watakaofanya mema wakiwa wanaume au wanawake hali wao ni wenye kuamini basi hao wataingia peponi.”

(4:124)

Vilevile dini yakwambia kwamba, uwezo wa mtu kujichagulia awe mume au mke uko kwa Mwenyezi Mungu.

“Yeye ameumba namna mbili mume na mke.” (53:45)

Na yamkemea vikali anayebagua kati ya mume na mke:

“Na mmoja katika wao anapopewa khabari ya (kuzaliwa kwake) mtoto wa kike uso wake huwa mweusi akajaa sikitiko. Akawa anajificha watu (wasimuone) kwa sababu ya khabari ile mbaya aliyoambiwa! (anawaza) Je akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni (kaburini akiwa hai)? Sikilizeni! Ni mbaya mno hukumu yao hiyo.”

(16:58-59)

(Mambo haya yalikuwa yakifanywa wakati wa ujahiliyya kabla ya Uislamu).

Hii ndiyo picha jumla ya mtazamo wa dini juu ya mwanamke. Na sasa hebu tuangalie kwa ufafanuzi dini isemavyo:

Tukiuliza dini, je una maoni gani au kwa maelezo ya ndani zaidi, nini mtazamo wako juu ya mwanamke? Tunaiona hapa dini ikijibu: Mwanamke yu hali tatu:

Mwanamke anapokuwa mdogo na msimamo wa baba yake kwake.

Mwanamke anapoolewa na msimamo wa mumewe kwake.

Mwanamke anapokuwa mama na msimamo wa wanawe kwake.

Katika hali ya kwanza (anapokuwa mdogo) twaona kwamba Uislamu wamwambia babake kupitia kwa Mtume (saw) akisema: “Mtoto wa kike ni rehma na wa kiume ni neema.” Mtume (saw) pia amesema: “Kumbusu binti yako ni jambo jema.” Amesema pia: “Bora ya watoto wenu ni mabinti.” Amesema pia: “Bora ya watoto ni mabinti wenye kujisitiri.”

Imepokewa Hadith nyingine kwamba: Mtume (saw) alipopewa bishara ya kuzaliwa mtoto wa kike, aliwaangalia maswahaba nyusoni akawaona wamechukizwa, akawaambia: “Mna nini nyinyi? Hilo ni ua la rehani ninalolinusa na aliloniruzuku Mwenyezi Mungu.”

Vile vile twaona katika maisha ya Mtume (saw) kwamba yeye hajawahi kubusu mkono wowote ila mikono ya watu wawili tu:

Mkono wa bintiye Fatima Zahra alipokuwa na miaka tisa, ilikuwa kila aingiapo kwa babake, alikuwa akisimamiwa na babake (Mtume (saw)) kumbusu mkono wake na akimketisha mahali pake; na hilo alilifanya hasa kwa ajili ya kuwazoezesha na kuwafundisha umma wake.

Mkono wa mchapa kazi, aliyekwenda kwa Mtume (saw) akampa mkono, Mtume (saw) akahisi usugu wa mkono wa mtu yule, akamuuliza, “Mbona hivi?” Yule mtu akajibu: “Huu usugu ni kwa sababu ya kuchapa kazi ee Mtume wa Mwenyezi Mungu.”

Mtume (saw) akainama, akambusu mkono wake huo akasema: “Huu ndiyo mkono unaopendwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake!”

Vilevile unahimiza baba anaponunua zawadi za watoto wake, mtoto wa kike apate mbili na wakiume apate moja. Au binti atangulie kupata kabla ya mvulana.

Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibni Abbas; Mtume (saw) amesema: “Atakayekwenda sokoni na kununua zawadi akenda nayo kwa familia yake (nyumbani) huyo ni kama aliyechukua sadaka na kuwapelekea wahitaji, basi na aanze kwa kuwapa watoto wa kike kabla ya watoto wa kiume, kwani atakayemfurahisha binti yake ni kama aliyemwacha huru mmoja miongoni mwa wana wa Ismail (as). Na mwenye kumfurahisha mtoto wa kiume, mtu huyo ni kama anayelia kwa kumcha Mwenyezi Mungu.”

Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi humtanguliza mtoto wa kiume kuliko mtoto wa kike katika maneno na vitendo vinavyohusu mambo yote ya nyumbani. Mtu humnunulia mtoto wake wa kiume akamwacha wa kike au anaposhauri, kuhusu mambo ya ndani ya nyumbani kwake humshauri mtoto wake wa kiume na asimshauri wa kike.

Wazazi wengi wanawapa kipaumbele watoto wa kiume na kuwashughulikia sana kuliko watoto wa kike jambo linalowafanya watoto wa kike wajihisi kuwa wanadharauliwa na hilo huwafanya wakawa na chuki. Kufanya hivi, licha ya kuwa haifai kisheria, vilevile huacha athari mbaya kwenye uhusiano wa wavulana na wasichana na hasa pale kila mmoja wao anapokuwa mwenye familia yake mwenyewe. Jambo hilo twaweza kuligundua tunapochunguza zile familia zenye aidha wasichana tu au wavulana pekee; ambapo utaona watoto wataishi wakiwa wameshikamana, ama wanapokuwa chini ya baba yao, ama kila mmoja anapokuwa tayari ana familia yake, kwa sababu watoto hao hawakubaguliwa kijinsiya. Lakini kinyume nao, wale watoto walioonja ubaguzi wa kijinsiya utawaona hawana mshikamano pale wanapofikia kila mtu wakati wa kujitegemea.

Mtume (saw) asema: “Mtu atakayekuwa na mtoto wa kike na hakumdhalilisha wala hakumtanguliza mwanawe wa kiume zaidi ya huyo wa kike, basi Mwenyezi Mungu atamwingiza peponi.”

Ama hali ya pili: Mwanamke anapokuwa mke wa mtu (rejea nyuma kidogo ili kufahamu zaidi) tutaona kwamba dini ya Kiislamu yamwambia mumewe hivi: “Mcheni Mwenyezi Mungu juu ya wanawake kwani wao ni amana iliyoko kati ya mikono yenu, mmewachukua wao kuwa ni amana ya Mwenyezi Mungu, basi waoneeni huruma na zifurahisheni nyoyo zao mpaka wasimame pamoja nanyi.” Mtume Muhammad (saw).

Vile vile amesema (saw): “Mbora wenu, ni yule aliye mbora kwa mke wake, nami ni mbora kwa wake zangu.”

Anaendelea kusema Mtume (saw): “Mja hatazidi kuwa na imani ila atazidi pia na kuwapenda wanawake.”

Katika Hadith nyengine nyingi asema:

“Mtu atakayemuoa mwanamke basi na amheshimu.”

“Dunia ni starehe, na bora ya starehe za dunia ni mke mwema.”

“Mambo matatu mtu akiyapata amefaulu: mke mtiifu, nyumba yenye nafasi na mnyama mwenye kasi.”

Katika Hadith nyingine! “Jibril hakuwacha kuniusia kuhusu wanawake mpaka nikadhani itakuwa haram kuwaacha.”

Imam Ali naye asema: “Ama haki za mkeo, ni wewe ujue ya kwamba Mwenyezi Mungu amemjaalia kuwa ni kitulizo na liwazo kwako, na ujue hiyo ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwako”.

Haki za Ndoa

Kwa mtazamo wa dini, mke ni mshirika katika maisha yeye ndiye anayemkamilisha mume na mume ndiye anayemkamilisha mke. Wewe wamuhitajia, naye pia akuhitajia. Mke si mtumishi, bali ni ‘mke’ kwa hivyo anafaa kutumikiwa.

Ama haki ambazo mwanamke lazima amtekelezee mumewe ni mbili tu. Ya kwanza ni haki ya kitandani (tendo la ndoa), yaani kuonana kimwili(ngono), kumpa mwili wake mumewe anapotaka. Pia Uislamu hapo wasema mtu ajiandae kwa mkewe kama ambavyo mke ajiandae kwa mumewe (kabla ya kuonana). Mume anapoomba hilo na hali zinaruhusu, basi mke ni lazima awe amejiandaa. Sayyidna Ali (k.w.) amesema: “Mke aliye muovu zaidi ni yule amnyimaye mumewe (tendo la ndoa).”

Haki ya pili ni mume kujua mke anapotoka nyumbani, yaani ajue mke anakokwenda. Haifai katika Uislam mke ajiendee tu popote au vyovyote atakavyo huku mumewe hataki. Mtume (saw) amesema: “Mke yeyote atakayetoka nyumbani kwa mumewe bila ya idhini ya mumewe, basi huyo hulaaniwa na kila kitu kinacho chomozewa na jua na mwezi mpaka mumewe amridhie.” Kwa kuwa ajua sababu iliyomfanya atoke ni nzuri hawezi kumficha mumewe. Na ikiwa mume ni mtu muumini haamrishi wala hakatazi ila kwa sababu ya maana. Basi mke anapotoka bila ya idhini yake kila kitu kitamlaani mpaka mume ajue sababu ya kutoka kwake na aridhike. Hizi ndizo haki mbili za mume kwa mkewe.

Ama haki za mke kwa mumewe ni nyingi:

Mume amfurahishe mkewe ki-ngono, na kimapenzi na haifai mume aache kabisa kabisa kounana na mkewe kimwili. Haifai asionekane kwa muda mrefu bila ya udhuru wa maana.

Ni juu ya mume amtimizie mkewe mahitaji ya lazima, nyumba inayofaa, mavazi yafaayo na chakula.

Mke si mali ya mume bali ni mshirika wake katika maisha anaingia mkataba na mume kwa ajili ya kuishi pamoja na kupendana pamoja na kubeba mzigo wa watoto pamoja.

Kwa hivyo, mke si katika majukumu yake kumtumikia mumewe bali kinyume chake. Mume anakalifiwa ki-sheria na kibinaadamu kutosheleza mahitaji yote yanayohitajika.

Ama kupika, kufagia, kufua au kuajiriwa ili kupata pesa, haya yote si wajibu wa mke. Anaweza asipike, asifagie, hata asimnyonyeshe mtoto. Kwani haki yake kwa mtazamo wa dini mume amlipe kwa kuwa maziwa anayompa mtoto ni sehemu ya maisha na mwili wake. Baba ndiye mwenye jukumu la ulezi wa mtoto, kwa hivyo ni haki yake mke alipwe kwa kunyonyesha.

Mke ni “mke” wala si mtumishi, atakapojitolea kufagia, kupika, kunyonyesha na kulea si haki yake bali aweza kujizuia na hayo na haijuzu mume kwa vyovyote kumtenza nguvu apike, afagie afue au aoshe vyombo.

Akijitolea naye mume asimpatilize mathalan kwa kuzidi kutia chumvi kwenye chakula au maji si baridi, nyumba chafu au haikusafishwa vizuri. Kwa sababu hawajibiki na hayo yote, madhali amejitolea basi afanye ni hisani kwa mume. Na kwa sababu hii ndipo tunakuta historia yasema kwamba Mtume (saw) hakulaumu katu mapishi ya chakula katika maisha yake. Alikuwa akishirikiana na wakeze kupika na kufagia na akisema: “Wale wafanyao kazi nyumbani mwao ndio wa kweli katika umma wangu.”

Ama hali ya tatu ya mwanamke ni pale anapokuwa mama, uislamu unawalazimisha watoto kumheshimu, inasema Qur’an.

“Wala usiwaambie Ah!…” (17:23)

Kijana mmoja alikwenda kwa Mtume (saw) akasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni yupi aliye bora zaidi kwangu nimtendee mama?” Mtume akamjibu: “mamako.” Yule kijana akauliza “kisha nani?” Mtume akajibu: “kisha mamako.” Akuliza tena: “Kisha nani?” Akajibu: “Kisha mamako” akauliza (mara ya nne): “Kisha nani?” Akamjibu: ”Kisha babako”.

Yaani hii ni kuonyesha kwamba haki za mama ni nyingi zaidi kuliko za baba mara tatu zaidi.

Alikwenda kijana mwingine kwa Imam Sadiq (A.S) akasema: “Ee mjukuu wa Mtume, mimi nilimbeba mama yangu mgongoni kwangu na kuhiji naye mara nyingi akiwa mgongoni kutoka Madina hadi Makka, je nimetekeleza haki zake?” Akatabasamu Imam Sadiq akamjibu: “Wallahi bado hujatekeleza haki yake hata ya usiku mmoja alipoamka akakuwekea titi lake mdomoni ukanyonya.”

Hivi ndivyo ilivyo, utaona kwamba Uislamu unaangalia mwanamke kama mwanaadamu aliyeumbwa na Mungu kwa matakwa haswa ya muumba, kama alivyoumba mwanamume kwa kutoka kwake yeye muumba na ndio maana akaamrisha mwanamke ahishimiwe.

Anapokuwa msichana, dini yakwambia mheshimu. Anapoolewa, dini yakwambia mheshimu, na anapokuwa mama, dini yakwambia mheshimu.

Dini inawatahadharisha wale wanaowapiga wake zao, inasema: “Mwenye kunyoosha mkono wake ili amzabe kofi mwanamke huyo ni kama aliyeunyoosha mkono wake motoni.”

Pili inasema: “Mkeo asiwe ni mtu umchukiaye, kwa kuwa mwanamke ni ua la mrehani si mtumishi. Na jiepusheni na wivu pasipo mahali pake, kwani kufanya hivyo humfanya yule mzima akapata maradhi, na asiye na hatia kumtia kwenye shaka.”

Masuala ya upande wa kike

Baadhi ya watu hujiuliza kuhusu Hijab, kwa nini dini ikawajibisha? Wengine huuliza: Je inafaa mwanamke afanye biashara, au ukulima?

Wengine wanataka kujua je mahari ni thamani (bei) ya mwanamke? Na wengine wanauliza kama inafaa mwanamke mmoja aolewe na waume wengi!

Ama kuhusu Hijab, kwa hakika mtazamo wa dini kwa mwanamke ni mtazamo wa kijumla, yaani ujumla mwanamke ni binaadamu na siyo wa kujistarehesha naye tu.

Kwa hivyo inatubidi tumuangalie ki-upande huo, lakini kwa kuwa yeye ni kivutio kwa sababu ana maumbile mazuri ya kike yanayomvutia mwanamume, ndipo dini ikafaradhisha Hijab ili kuzuia mwanamke asigeuzwe njia ya kujistarehesha, na haifai tumtazame mwanamke kama bidhaa ya kuuzwa au chombo cha starehe kama yanavyofanya maendeleo ya ki-magharibi ambayo yamemvua ubinadamu wake na kumbakishia uanamke wake ndipo akafanywa ni kitu cha matangazo ya biashara ili kumvutia mteja. Mwanamke anatumika kwenye biashara kiasi kwamba wanapotaka kuuza gari humsimamisha msichana mzuri kando ya gari hilo wakampiga picha nalo ili lipate kuuzwa.

Isitoshe hata wanapotaka kuuza farasi maalum, watamsimamisha msichana mrembo kando ya ranchi ya farasi ili awavutie wanunuzi wamnunue farasi huyo. Hata kwenye matangazo ya bustani ya kufugwa wanyama mwanamke amekuwa akitumika! Hivi ndivyo mwanamke anavyotumika kwa faida ya kibinadamu naye huhitajiwa tu pale anapokuwa mrembo wa kumezewa mate; ama akiwa mbaya au ameumbwa na uzuri wa kawaida tu, huwa hana thamani kwa sababu huyo hawezi kuvutia wanaume.

Ama Uislamu haukubali mwanamke atupwe kwenye matamanio, kama alivyosema Imam Ali: “Mwanamke ni rehani na si mtumishi.” Mrehani lazima uhifadhiwe. Na mwanamke ni almasi lazima athaminiwe. Tunaposema almasi lazima ifichwe ili isiibiwe, je huko utasema ni kuivunjia heshima almasi au kuichunga? Basi vivyo hivyo mwanamke na Hijab!

Hapana. Hijab si kumtweza mwanamke bali ni kumchunga kutokana na wizi wa ngono. Na maadam mwanamke anatakiwa na mwanamume kwa matamanio basi yampasa ajihifadhi maumbile yake ya kike kwa njia ifaayo, nayo ni kuficha vivutio vyake. Mwanamke mzuri ni yule anayejistiri mwili wake na waume wengine na kujionyesha kwa mumewe tu. Mtume (saw) asema: “Bora ya wanawake zenu ni yule mzazi, mwenye mapenzi, mwenye kujisitiri, mwenye kumtii mumewe, mwenye kujichunga na mwengine, anayemsikiza na kumtii amri zake na wanapokuwa faragha, humpa akitakacho.”

Amesema pia: “Mbora wa wanawake wenu ni yule anapokuwa faragha na mumewe huvua vazi la kuona haya.”

Ama kuhusu wanaume ambao hawamtaki ila kwa ajili ya kufaidi tu, Uislamu umemzuia na hilo. Kwa sababu kijana anayemchukulia msichana kama mpita njia tu kwa ukweli huwa hana haja naye ila hutaka kutimiza haja za matamanio yake tu wala hana penzi. Kwa hivyo anachotaka ni kukidhi haja zake tu wala hajali mabaya wala mazuri ya mwanamke huyo.

Mara ngapi tumeona matukio kadha wa kadha katika nchi mbalimbali ambapo msichana amechukuliwa na kijana akatembea naye kisha akamwacha abebe mateso yake.

Kuhusu kufanya kazi, Uislamu haumkatazi mwanamke kufanya kazi yoyote. Uislamu hausemi kwamba ni haramu kwa mwamanke awe mfanyi kazi au mkulima au mfanyi biashara, bali ni haki ya mwanamke afanye kama afanyavyo mwanamume katika kufanya kazi, kulima, biashara n.k. kwa sharti tu awe na “heshima” na kuulinda utu wake.

Uislamu unakataza kwenda tupu na mwanamke kujionyesha sehemu za mwili wake, haukatazi kufanya kazi.

Sote tunajua ya kwamba Bi Khadija bint Khuwailid (r.a.) alikuwa tajiri na mfanyi biashara mkubwa na alijuana na Mtume (saw) kupitia biashara zake ambapo Mtume (saw) alikuwa akifanya kazi kwake.

Mwanamke anaweza kufanya kazi ikiwa atahifadhi Hijab yake kazini, au asichanganyike na wanaume wawezao kumuoa. Kwa sababu bila ya kufanya hivyo atageuka kuwa ni burudani kwa wanaume.

Ama kuhusu mahari, kwa mtazamo wa uislamu, ni alama ya kuonyesha kuwa msichana huyu anatakiwa namvulana huyu. Hutolewa mahari ili mwanamke ajihisi kuwa anahitajiwa na mwanamume na si yeye anayemtaka mume, jambo linalo mtosheleza haya zake alizoumbwa nazo na heshima zake ambazo bila shaka zitavunjika pale yeye atakapomtaka mwanamume.

Mahari si thamani ya bei anayolipa mume kuununua mwili wa mwanamke, na ndipo ukaona uislamu haukupanga kiwango cha mahari na kitu chochote chaweza kuwa mahari (k.v. vyombo n.k.) hata kumfundisha hesabu au sura ya Qur’an kunaweza kuwa mahari, au chochote hata kiwe kidogo namna gani.

Isitoshe, uislamu unapenda mahari yawe kidogo. Mtume (saw) anasema: “Bora ya wanawake wa umma wangu ni wale wazuri wa uso wenye kutolewa mahari kidogo.” Na kila mahari yanapokuwa kidogo, inaamanisha kwamba huyo msichana (kwani ndiye anayetaja mahari) anamtaka huyo mume mwenyewe na si mali yake, na huyo mume anamtaka mke mwenyewe si kwa sababu amemnunua.

Kuhusu suala la mke na waume wengi, dini imekataza hilo kwa sababu hizi:

Mwanamke hafai kushea ikiwa wewe hufai kushea hata kalamu yako, utaridhika kushirikana mkeo?

Suala la kuona ni utangulizi wa kupata watoto, na kuwa na waume wengi ni kuchanganya watoto.

Mwanamke ana hisia za ‘ulinzi’ yeye vyoyote ilivyo anatafuta mtu wa kumlinda. Hebu uliza nchi gani inayotawaliwa na maraisi wawili? Au dola gani ya ndoa inayotawaliwa na waume wawili?

Hata upande wa mume kuoa wake wengi uliuhusiwa na uislamu kwa sababu ya kutatua matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na idadi ya wanawake kuwa kubwa zaidi ya wanaume. Nchini Merekani pekee, kuna wajane milioni tisa waliofiwa na waume zao, na mamilioni ya washichana ambao hawajaolewa.

Vilevile sababu ya kuwa na wake wengi yaweza kuwa ni kwa ajili ya maslahi ya mwanamke kwa mfano; hebu tuchukulie mke ni tasa, hazai na mumewe anataka watoto na kisha mume tumzuie asiwe na wake wawili (asioe), hii ina maana kwamba tutamruhusu amuache yule mkewe ili aoe wa pili. Hii kwa kweli itakuwa si kwa maslahi ya yule mkewe.

Hili ndilo suala la mwanamke, ambaye ana heshima yake katika uislamu, kwa sababu yeye ni kiumbe cha Mungu, na amejaaliwa hivyo na Mungu muumba kwa ajili ya kujuana kama isemavyo Qur’an:

“Enyi watu! Hakika tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekufanyeni mataifa na makabila (mbali mbali) ili mjuane. Hakika ahishimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi..” (49:13)

Ama maendeleo ya kimagharibi (Ulaya) heshima ya mwanamke imevunjwa, amekuwa ni thamani tu ya kibiashara au burudani ya ki-ngono mambo yanayoutweza utu wake na hili sisi hatuliridhii wala hatutaki limpate mwanamke.

Wanamuua mwanamke siyo!

Siku moja Mtume (saw) alikuwa ameketi na baadhi ya maswahaba zake kwenye changarawe akachora kwa kidole chake ardhini mstari ulionyooka, kisha kando ya msitari huo akachora msitari ya mshazari, mmoja upande wa kulia na mmoja wa kushoto, akaashiria kwenye ule msitari wa kwanza ulionyooka akasema: “Hii ni njia ya Mwenyezi Mungu, kisha akaashiria kwenye ile mistari mingine akisema: “Na hizi ni njia zingine ambazo juu ya kila njia pana shetani anayewaita watu waifuate. Kisha akafumba macho kwa muda mfupi kidogo, kisha akasema: “Kwa hakika hii ndiyo njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Wala msifuate njia zingine mtafarikiana na njia ya Mwenyezi Mungu.”

Kwa hivyo hapa Mtume ameeleza upotofu wa kila njia isiyolingana na njia ya Mungu kama vile alivyoonyesha jinsi njia ya Mungu inavyojitenga kimsingi na njia za shetani. Sasa basi, tunapotaka kuigundua njia ya Mungu kuhusu masuala ya mwanamke tusiwaulize mashetani, na maana ya mashetani hapa ni wote walioanguka chini ya matamanio. Yatupasa tuangalie kwenye maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume, kwa sababu mapenzi ya nafsi daima hufikiria lile jambo ilitakalo na hayafikiri ukweli ulivyo.

Mtu akisema ‘Hijab hakuna katika uislamu’ wakati yeye anasoma jinsi Qur’an inavyosema: “…na mnapowauliza kitu basi waulizeni nyuma ya pazia (hijab), mtu huyo hakusudii hijab kama ilivyo kwenye uislamu ila ni kwa kuwa hijab haikuridhisha matakwa yake, ya kimwili ndiyo maana akasema hakuna hijab.

Hivyo ndivyo ilivyo, na kwa hakika uislamu ndio unaopanga njia ya Mwenyezi Mungu na si watu wengine, na ndipo hapa tunakuta kwamba Mwenyezi Mungu anaweka orodha ndefu kuhusiana na maswala ya mwanamke:

Maisha ya mwanamke ya kipekee

Masuala ya mwanamke ya kijamii

Masuala ya mwanamke ya kifamilia

Masuala ya mwanamke ya ki-jinsiya.

Ufafanuzi wa masuala haya ni kama ifuatavyo:

Kuhusu masuala ya muhusuyo ni kwamba yeye anapaswa kutenda yale yapasayo mwanamume kuyatenda kama kufanya ibada, kuwa na tabia nzuri n.k.

Mwanamke ana haki zote za kijamii na anaweza kufanya biashara kulima na kufanya kazi mradi tu ahifadhi heshima yake ya kike.

kifamilia, mwanamke ni msimamizi wa utekelezaji ndani ya nyumba ambapo mume anakuwa ni kiongozi wa taasisi ya familia. Aya isemayo: “Wanaume ni wasimamizi wa wanawake” haimaanishi mwanamume atumie mabavu, na kulazimisha mambo; uislamu haumuangalii mwanamke kama mtumishi au si bandia wa anayefaa atishwe mizigo ili mwanamume ajinufaishe.

Mwanamke ni mshirika wa wanaume, si mtumishi kwa hivyo yampasa mume kwa sababu mke ni bibi wa familia amuandalie mshirika wake huyo maisha mema ya ki-binaadamu.

Yampasa mke aishi vizuri na mumewe na amtosheleze nastarehe za jinsiya inavyotakiwa na kwa ndoa ya kisheria, na uislamu una orodha na miongozo mirefu juu ya suala hili linalofafanua kwa usawa kwa mume na mke njia za kuonana kimwili Nayo ni miongozo iliyofafanuliwa inayoeleza hata namna ya kufanya tendo la ndoa na wakati muwafaka wa hilo.

Kwenye orodha hizi zinazohusu masuala ya mwanamke katika uislamu tunagundua kwamba zinamuangalia mwanamke kuwa ni mwanaadamu, mwenye haki ya kuishi kwa usawa na mwanamume.

Lakini kuna zingine zisizokuwa za kiislamu ambazo zamuangalia mwanamke kama mwanaserere (kijisanamu) wa kujistareheshwa naye tu kamili.

Na kama tulivyoona, ni kwamba Uislamu unafanya juhudi kuona kwamba umedhibiti starehe za kimwili kwenye familia na maisha ya ndoa. Uislamu hauruhusu starehe hizo kutangazwa sokoni, barabarani, mabarazani au kwenye mikusanyiko. Pia hauruhusu kwenda uchi, kujionyesha mapambo, au kuchanganyika kuovu kwa wake na waume na kukaa faragha. Hayo yote yanaambatanishwa na adabu, desturi na hukmu maalum.

Hivi ndivyo Uislamu unavyolipa suala la mwanamke la jinsiya picha yake halisi na kulipa umuhimu kama yalivyo masuala mengine yawe ya kijamii au ya kifamilia. Hivyo ndipo uzani wa usawa unapohifadhika na kuzuia mwanamke asitumiwe kama chombo cha madhambi au kisanamu cha kuchezewa.

Ama mifano mingine (isiyo ya Kiislamu) yenye misingi na hukmu ambayo inaendelea hivi leo chini ya kivuli cha ‘maendeleo’(kompyuta na electroniki) inafanya juhudi za kufanya mwanamke awe ni ‘jinsi nyingine’. Asipotimiza wayatakayo basi hapana haja aweko. Kwa msingi hii haya yote yamepangwa juu ya desturi za mambo hayo, ambapo baadaye hakuna kizuizi kwa mwanamke kuyafuata kama; kusambaratika kwa familia, kuzaa nje ya ndoa, kuenea zinaa n.k.

Kwa hivyo mwanaadamu leo yampasa achague moja kati ya njia mbili. Ama njia ya kujizuia, (maisha ya ki-familia ya ndoa) au njia ya zinaa (kuharibika kwa familia).

Njia ya kwanza ni ya Mungu na ya pili ni ya shetani. Wale wanaochagua njia ya pili, yawapasa wafahamu kwamba jambo haliishi kwa wao kuifuata kando kando (bora wasifuate kabisa). Ama kujaribu kuchanganya baina ya njia mbili hakufai ila ufuate njia ya Mungu tu. Kwa sababu njia ya shetani ni njia ya matamanio nayo hayana mwisho mwema. Kila mwanaadamu anapotopea humo, matamanio nayo humwambia; vipi nyongeza!

Suala: Je! yapasa kumpendelea mwanamume zaidi ya mwanamke kiasi cha kumnyima mwanamke haki nyingi za kisiasa na kijamii?

Jibu: Lau kama mwanamke hatofautiana na mwanamume upande wa maumbile yake ya kimwili, kiakili na kifikra, hapa suala la kupendelewa lingeingia mahali pake. Lakini kwa kuwa mwanamke kimsingi anatofautiana na mwanamume hapa suala si ‘kupendelewa’ bali suala ni ‘kuhusishwa’ na kuweka kila jambo pale panapofaa. Hivi hasa ndivyo inavyoafikiana na maoni na mfumo wa Uislamu. Mwanamke kwenye Uislamu ana nafasi zake maalum, kwa sababu sehemu hizo zahitaji ahusishwe nazo yeye hasa.

Mathalan; kama ambavyo si sahihi daktari asomeshe mambo ya uhandisi (uinjinia), au kipofu achukuliwe kuwa muongozaji rada! Basi vile vile si sahihi mwanamke abebeshwe majukumu asiyoweza kuyabeba. Hata sayansi inatuonyesha kimsingi jinsi mwanamke alivyo tofauti na mwanamume.

Dkt. Casius Carel, mshindi wa tuzo la Nobel katika sayansi anasema: “Mambo yanayomtofautisha mwanamume na mwanamke hayaishii kwenye maumbile ya viungo vyao vya uzazi tu, au tofauti katika malezi yao tu, bali kuna mambo mengi. Tofauti hizo zina maumbile ya kimsingi zinazoanzia kwenye mpangilio wa kimwili, mwanamke katika kila kiungo cha mwili wake ana vitu vya maji maji vya kemikali vinavyorutubisha uzao. Wale wanaodai kuwa na malezi sawa, elimu na kazi baina ya wanaume na wanawake hawazijui tofauti hizi kabisa; tofauti za kimsingi. Mwanamke alivyo hasa ana tofauti kubwa na mwanamume kwani kila chembe chembe (cell) katika mwili wake ina umbile la kike, hata mpangilio wa mishipa yake uko tofauti.”

Anaendelea Dkt Carel: “Utaratibu na kazi za vuingo vya mwili una mpangilio maalum kama vile elimu ya nyota na hesabu. Haiwezekani kufanya badiliko lolote kwa kuwa tu mwanaadamu anataka kubadilisha. Kwa hivyo letu sisi ni kukubali kama ilivyo. Na wanawake nao ni lazima wakuze vipawa vyao kulingana na maumbile yao, na waache kuwaiga wanaume kiholela. Nafasi yao katika maendeleo ni kubwa kuliko ya mwanamume na haifai kuiacha.”

Maadam majaribio ya kisayansi yameonyesha tofauti hizo za kimaumbile, basi yapasa kutenganisha suala la mwanamume na la mwanamke. Kila mmoja wao apewe wadhifa ule utakaolingana na sifa zake. Mwanamke ana sifa za huruma basi ni lazima kazi ya kulea watoto aachiwe yeye, kwa sababu kazi hiyo inahitajia huruma. Na mwanamume kwa kuwa ana nguvu za kubeba majukumu mazito, basi hapana budi apewe uongozi wa kusimamia nyumba na nchi.

Isitoshe, inapasa ratiba ya masomo ya mwanamke ibadilishwe ili iambatane na tabia, umbile na akili yake.

Vilevile hapana budi majukumu yake katika maisha ili yalingane na shakhsiya yake ya huruma.

Tutakapomweka mwanamke kwenye nafasi yake ifaayo basi tutaweza kuinua hali ya nchi iliyoporomoka. Kwani kumpa kila mtu nafasi yake anayohusika nayo ndiko kumwezesha kupata fursa kwenye jamii ya kufikia maendeleo.

Jamii ya mwanadamu ina mfumo wa “kutofautiana”. Ama jamii ya wanyama ina mfumo wa “kuwa sawa”. “Kutofautiana” ina maana ni kutofautiana watu na kila aliye na sifa fulani kumfanyia na kumkamilishia mwingine ambapo “kuwa sawa” maana yake ni kuwa sawa bila ya kushughulikiana. Kwa hivyo hapa, utaona kuwa mwanamume anamuhitajia sana mwanamke na mwanamke anamuhitajia sana mwanamume. Lau ingelikuwa mwanamume na mwanamke “wako sawa”, basi mmoja asingelimuhitajia mwengine.

Dkt. Maranon anasema: “Jambo linalothibiti ni kwamba, ukamilifu wa mwanadamu utatimia, na lazima utimie, kwa kuziainisha tofauti zao, yaani mwanamume ajione zaidi ni mwanamume, na mwanamke ajione zaidi kuwa ni mwanamke.”

Kwa hivyo ni upumbavu wanawake wawaige wanaume, na wanaume nao kuwaiga wanawake.

Msichana aliye baleghe hapendezi mbele ya mwanamume pale anapovaa Mini au Kaptula (Short pants) kama vile mwanamume avae gauni, viatu vya mchuchumio (High heels) pochi kwapani na ajitie manukato ya kike ya ki-Faransa!

Takwimu zimeonyesha kwamba wanaume hupendelea sana wanawake wenye kujiheshimu kuliko wenye kujidhihirisha wazi wazi. Ndiyo, ni kweli mvulana (mhuni) mhuni hupata kumchezea msichana anayevaa Mini anapompitia mbele yake barabarani.

Lakini penzi liko mbali na suala la ndoa ya daima, kwani mwanamume katu hawezi kumuoa msichana mwenda-uchi. Anajua wanawe atakaozaa naye wataharibika kwa sababu mama atakayewalea atapenda zaidi kujipamba kwa ajili ya wanaume wengine ili awavutie, kuliko kuwalea wanawe.

Na msichana apendaye kuangaliwa na maelfu ya macho yenye njaa naye hajaolewa, basi hata atakapoolewa atapenda zaidi macho ya watu yamuangalie. Haitaishia hapo, mwisho itafikia kupokea wanaume!

Familia nyingi zimesambaratika kwa sababu mwanamke si mwenye kujistahi. Kwa kweli ni ujinga wa mwisho mwanamke avunje heshima yake kwa sababu tu watu maarufu wa Ujerumani wanafanya hivyo, au vijana wajifanye kama watu washuhuri wa Marekani wafanyavyo.

  Yaliyomo endelea