MADHEHEBU YA KISHIA

 

UTANGUZI

 

Kabla sijatoa maelezo machache kuhusu Madhehebu za Kishia itakuwa muhimu sana kuzitazama zile tabia za Ushia. Kama anavyosema Mwanachuoni mkuu wa Kishia, Sheikh Al Mufid, kuwa tabia muhimu sana za Ushia ni:

 

(a) Kumfuata Hadhrat Ali bin Abi Talib [a] kumpenda na kumkubali kuwa ni kiongozi wako.

 

(b) Kuamini kuwa yeye ndiye mrithi wa Mtukufu Mtume [s] aliyestahili kushika madaraka mara tu baada ya kufariki kwake; na kuwa wale waliojifanya Makhalifa kabla yake hawakuwa Makhalifa hata kidogo.

 

Kwa vile jina la "At-Tashaiyu" lina maana hiyo iliyota jwa hapo juu, linatumika tu kwa Al-Imamiah na Al- Jarudiyah (kimadhehebu kidogo cha Zaidiyah, ambacho siku hizi kiisha kufa) kuzitofautisha na Madhehebu zote za Ummah wa Kiislamu, kwa sababu ni madhebu hizi mbilitu zitimizazo maa­na hiyo....." Na Mutazilah, Bakriyah, Khawarij na Hasha­wiyah wako nje ya maana hii kwa sababu hawaitimizi maana hii kama tulivyoieleza.

 

Soma kitabu kiitwacho "Awa'il-ul-Maqalat" cha Sheikh Muhammad bin An-Nu’man Al-Mufid, toleo la pili la mwaka 1370 Hijiriyah kilichochapishwa mjini Qum - (Iran), Uk. 4.

 

Sasa hebu yalinganishe maelezo hayo ya neno “Shia” yaliyotolewa na mwanachuoni wa Kishia (aliyeishi katika karne

4 Hijiriya) mwenye sifa kama za Shaikh al-Mufid, na yale yaliyotolewa na adui wao, Ibn Hazm (aliyeishi katika karne ya 5 Hijiriya) yasemayo, “Yule akubalianayena Mashia kuwa 'Ali ni mbora zaidi miongoni mwa watu wote, wa pili kutoka kwa Mtume, na kuwa yeye (Ali) na dhuria wake baada yake ni wenye kuhusika zaidi na Uimamu kuliko ye yote yule, ni Shia” ....(Soma kitabu kiitwacho 'Kitabu al-Milal-wan­-Nihal', cha Ibn Hazm, uk. 32 kamakilivyonakiliwa na Bwana J. N. Hollister katika kitabu chake kiitwacho, "The Shia of India, kilichotolewa na Lucaz & Co., London, Uingereza, 1953, Uk,4).

 

Ibn Hazm hatambui kuwa kwa ufafanuzi wake huo hata Imamu Ahmad bin Hambali angelikuwa Shia, kwa sababu aliuamini ubora wa Hadhrat Ali [a] (kuwa ni wa pili) baada ya Mtukufu Mtume [s],kama asemavyo mwanawe Abdullah:

 

"Nalimuuliza baba yangu kuhusu maoni yake juu ya ubora. Alisema; Abu Bakr na Umar na Uthman. Kisha kwa vile ali­nyamaza, nilimuuliza, Ewe baba, vipi kuhusu Ali bin Abi

Talib? Alijibu:    “Yeye ametokana na Ahlul-Bait. Watu wengine hawawezi kulinganishwanaye.” (Soma kitabu kiitwacho, Yanabi-ul-Mawaddah”, uk. 253, cha Shaikh al-Islam Hafiz Suleiman al-Balakhi al-Qanduzi al-Hanafi).

 

Ukweli ni kuwa, imani ya ubora wa Hadhrat Ali [a] na dhuria wake, na kufikiria kuwa waliustahili Uimamu, hakum­fanyi mtu kuwa Shia, mpaka mtu huyo aamini kuwa walikuwa Maimamu hasa achilia mbali madai ya wadai wengine wa Uimamu.

 

Al-Imamiyah:

 

Neno “Al-Imamiyah” lina maana ya kile kikundi cha Mashia ambao vile vile huamini kuwa ni lazima na ni wajibu kuwepo imamu kila wakati; na kuwa imefahamika kutokana na “Nass” (tangazo la Mtume au Imamu aliyetangulia kuhusu mrithi wake) iliyo wazi kabisa; na ambao huiamini 'Ismat’ (utakatifu) wa Maimamu na kuwa kila Imamu alikuwa mbora katika matendo yote mema; na ambao huamini kuwa baada ya Imamu Husain [a] Uimamu uliendelea, katika kizazi Chake….. (Soma kitabu cha Shaikh Al-Mufid tulichokitaja hapo juu, uk. 7).

MAADHEHEBU ZA KISHlA

 

Kama ilivyoelezwa hapo juu, Mashia wamegawanyika mafungu mawili, Imamiyah na Jarudiyah, kwa sababu wote wanaamini kuwa Hadhrat Ali [a] ndiye Khalifa wa kwanza, na mrithi wa Mtukufu Mtume [s] kufuatana na Nass yake. Kabla sijatoa maelezo zaidi kuhusu madhehebu hizi, itamsaidia msomaji kuzitazama baadhi ya madhehebu za zamani ambazo sasa zimekufa:­

 

1). Kaisaniya:

 

Hawa waliamini kuwa Bwana Muhammad bin Ali (anayefahamika sana kwa jina la lbnul Hanafiya) alikuwa Imamu wa Nne baada ya nduguye Husain, Shahidi wa Karbala. Waliamini kuwa Ibn-ul-Hanafiya alikuwa hai, na yeye ndiye Mahdi aliye tabiriwa na Mtukufu Mtume [s] na atadhihirika tena karibu na Siku ya Kiyama.

 

Kundi hili lilikufa baada ya kufariki kwake Abu Hashim (mwanawe Ibnul Hanafiya) aliyeuwawa kwa sumu na Hisham bin Abdul Malik, mfalme wa ukoo wa Bani Umayyah.

 

Haifahamiki kama waliwahi kuandika kitabu cho chote kuhusu imani yao ya kimadhehebu. Hakuna maandishi yo yote yaliyoonekana katika Mashariki ya kati yanayohusu mafundisho yao. Sasa, miaka 1300 baada ya kusahauliwa kwao, mwandishi ataona shairi la Kiswahili hapa katika Pwani ya Afrika ya Mashariki lithibitishalo kuwa Makaisaniya waliamini kile kidaiwacho na wanachuoni wa Kisunni na Kishia kuwa walikiamini. (Soma kitabu kiitwacho “Uteuzi Wa Sayyidina Husain bin Ali". Maelezo kuhusu Uteuzi huo yalichapishwa (kwa Kiingereza) katika gazeti letu 'The Light' Vol. VI, No. 1, na mwandishi wa Makkah Makala iitwayo “Some Evidences of Shi'ite Connection with with Early History of East Africa.” Maelezo yake machache yamechapishwa (kwa Kiingereza) kama “Nyongeza” katika kitabu kiitwacho “Ibn Battuta in Black Africa”, kilichoandikwa na Bwana Said Hamdun na Professor Noel King, na kutolewa na Rex Collings, London, Uingereza mnamo mwaka 1975).

 

2). An-Nawusiya:

 

Hawa waliamini kuwa Imamu wa sita Jaafar Sadiq alikuwa Mahdi na Imamu wa Mwisho. Madhehebu hii ilipewa jina la muanzilishi wake Bwana Abdallah bin Nawus. Ilikufa mara tu baada ya kuanzishwa kwake.

 

3). Al-Fathiya:

 

Hawa waliamini kuwa Imam wa baad ya lmamu wa sita ni mwanawe mkubwa Bwana Abdullah Al-Aftah, cheo kilichoi­pa jina Madhehebu hiyo.  Hawa nao walipotea mara moja.

 

4) Al-Waqifiya:

 

Waliamini kuwa Imamu wa saba, Musa Al-Kadhim aliku­wa Imamu wa Mwisho na ndiye Mahdi. Hawa nao, hadi katika zama za Imamu wa tisa Muhammad Taqi [a] walikuwa

Weshamalizika.

 

Pia yalikuweko makundi mengine machache yaliyozuka na kufa mara moja bila ya kuacha kumbukumbu zo zote zile. Makundi haya hayakuwa na uhusiano wo wote na dini wala historia.

 

Sasa twazijia zile Madhehebu za Kishia zilizoko siku hizi.

 

1). Ithna-ashariya:

 

Wao ni, na wamekuwa wakibakia kuwa kikundi kikubwa cha Kishia ulimwenguni. Katika Mashariki ya Kati na Asia ya Kusini Mashariki, kila jina 'Shia' linapotumika huwana maana ya kundi hili tu. Inabidi Makundi mengine yajitambulishe kwa majina mengine. Ithna-asharia wanawaamini Maimamu Kumi na Wawili wakianzia na Ali na kumalizia na Muhammad Al-Mahdi ambaye wanamwamini kuwa yu hai na atadhihiri tena kabla ya Siku ya Kiyama. Orodha ya Maimamu wote ku­mi na wawili imetolewa hapa chini ili kumpasha habari mso­maji:

 

1.       Ali bin Abi Talib (Al-Murtada [a])

2.       Hasan bin Ali (Al-Mujtaba [a])

3.       Husain bin Ali (Sayyidus-Shuhada [a])

4.       Ali bin Husain (Zainul Abidiin [a])

5.       Muhammad bin Ali (Al-Baqir [a])

6.       Jaafar bin Muhammad (Al-Sadiq [a])

7.       Musa bin Jaafar (AI-Kadhim [a])

8.       Ali bin Musa (Ar-Ridha [a])

9.       Muhammad bin Ali (At-Taqi [a])

10.   Ali bin Muhammad (An-Naqi [a])

11.   Hasan bin Ali (Al-Askari [a])

12.   Muhammad bin Hasan (Al-Mahdi [a])

 

Wafuasi wa Kikundi hiki wanapatikana Iran, Iraq, Pakistani, Uhindi, Bangladesh, Shamu, Lebanon, Kuwait, Muungano wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Uarabuni ya Saudia, Burma, Thailand, Indonesia, Urusi, Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Zaire, Malagasy, Ungazija, Uingereza, Kanada, Umarikani (U.S.A.) n.k.

 

Pia wanaitwa Imamiya na Jaafariya. Wakati mwingine maadui zao huwaita "Rafidhi".

 

2).        Ismailiya:

 

Wanaamini kuwa Uimamu baada ya Imamu Jaafar Sadiq ulichukuliwa na mwanawe Ismail. Maismailiya Wamegawa­nyika tena katika Madhehebu ndogo mbili:­

 

(a)        Maagha Khani:

 

Hawa hufahamika zaidi kwa jina la Maismailiya hapa Afrika ya Mashariki na sehemu nyinginezo, ingawa vitabu vya kidini huwaita Nazariya.  Wanamwamini Mtukufu Karim Aga Khan IV kuwa ni Imamu wao wa 49.

 

(b)        Mabohora:

 

Katika elimu ya kidini wanaitwa Mustalawiya.  Wanaamini kuwa Imamu wa 21 yu katika Ghaib (haonekani) na yu hai. Kwa wakati huu kiongozi wa jamii yao anaitwa "Dai Mutlaq". Dai-Mutlaq wa sasa (wa 52) ni Mtakatifu Burhanuddin wa Bombay, Uhindi.

 

Sasa twawajia Jarudiya. Wao ni Madhehebu ndogo ya Zaidiya.

 

"Zaidiya wamegawanyika makundi matatu:

 

(a)        Al-Jarudiya:

 

Hawa ni wafuasi wa Bwana Abul-Jarud. Wanaamini kuwa Mtume [s] alimteua Ali bin Abi Talib kuwa Mrithi wake, lakini sio kwa kumtaja jina. Kufuatana na imani yao, Mtume [s] alizitaja tu zile sifa njema (za lazi­ma kwa Khalifa kuwa nazo) ambazo hazikupatikana kwa mtu ye yote yule mwingine ila Hadhrat Ali [a]. Baada ya Hadhrat Ali [a], Hadhrat Hasan [a] na Hadhrat Husain [a] ni Maimamu wao. Baada ya Hadhrat Husain [a], Waislamu wamepewa uhuru wa kuchagua wenyewe Imamu wao chini ya masharti ya kuwa Ukhalifa usitoke mikononi mwa dhuria wa Bibi Fatima [a].

 

(b)        Sulaimaniya:

 

Hawa ni wafuasi wa Bwana Suleiman bin Jarir. Wanasema kuwa Mtume [s] hakumchagua mtu ye yote kuwa Khalifa wake, si kwa jina wala kwa sifa njema. Kufuatana na imani yao, Abu Bakr (r.a.) na Umar (r.a.) walikuwa Makhalifa wa haki. Lakini Ukhalifa wa Bwana Uthman (r.a.) haukusihi.

 

(c)        Batiriya:

 

Hawa ni wafuasi wa Bwana Batir Ath-Thumi; ambaye imani yake ilikuwa sawa na ile ya Sulaimaniya ila kuwa tu hawakusema cho chote kuhusu kusihi au kutosihi kwa Ukhalifa wa Bwana Uthman (r.a.).

 

Mwanachuoni wa Kisunni, Sharif Jurjani ameandika hivi:

 

"Mazaidiya walio wengi ni Mutazila katika mambo ya Elimu ya Kidini, na wanamfuatia Imamu Abu Hanifa katika Sheria za Kiislamu (soma kitabu kiitwacho “Sharhul-Mawa-qif" cha Sharif Jurjani).

 

Maneno haya yamethibitishwa na mwanachuoni wa Kishia Bwana Khwaja Nasiruddin Tusi ambaye ameendelea kusema:

 

Mazaidiya wanauamini Ukhalifa wa Ali, Hasan na Husain. Lakini hawauamini Uimamu wa Ali bin Husain kwa sababu hakupigana vita. (Kama nilivyoeleza hapo mwanzoni, imani hii si imani ya Mazaidiya wote. Ni wale Mazaidiya walio Jarudiyah tu, wauaminio Uimamu wa Ali, Hasan na Husain). (Badala yake) wanaumini Uimamu wa  mwanawe mwingine, Bwana Zaidi, kwa sababu alipigana dhidi ya Ukhalifa usio sahihi.  Kufuatana na imani yao, “Ukatatifu” sio jambo muhimu kwa Imamu.  Maimamu wawili wanaweza kuchaguliwa kwa wakati mmoja katika sehemu zenye taabu. Ye yote yule mwenye sifa hizi tano anaweza kuwa Imamu:­

 

(1)        Nilazima atokane na dhuria wa Bibi Fatima [a]

(2)        Lazima awe na elimu kubwa ya Sheria za Kiislamu

(3)        Lazima awe Mchamungu

(4)        Lazima awe Shujaa

(5)        Kama mtu mwenye sifa hizo nne zilizotajwa hapo juu akiwaita watu kwenye dini ya Mwenyezi Mu­ngu kwa upanga, basi atakuwa Imamu. (Soma kitabu kiitwacho "Qawaidul- Aqaid" cha Sheikh Khwaja Nasiruddin Tusi.

 

Katika maandishi yangu yaliyotangulia nimeandika kuwa "Mazaidiya si Mashia wala Masunni, bali ni kikundi kilicho baina ya Madhehebu hizo mbili". Maelezo haya ni sahihi ku­fuatana na Mazaidiya wa siku hizi wahusikavyo. Kwa kuwa wao ni Mutazila kiimani na Hanafiya katika Sheria za Kiislamu ni haki wahesabiwe kuwa wao ni Madhehebu pekee.

 

Wasomaji wataona kuwa maelezo hayo hapo juu hayajum­lishi imani ya Madhehebu ya Jarudiya. Lakini Majurudia wa­mepotea miaka mingi iliyopita; na ni jambo la kupendeza kuo­na kwamba Shaikh Mufid nae hawahesabu Mazaidiya wa siku hizi pamoja na Madhehebu za Kishia, kwa sababu hawakubali kuwa Ali ni Khalifa wa Kwanza licha ya madai yote mengi­neyo.

 

Mpaka hapa tumekwishaelezea kuhusu Madhehebu tatu za Kishia zilizopo na tano zilizokufa. Shaikh Mufidi (aliyefariki mnamo mwaka 413 Hijiriya) ameorodhesha idadi ya Madhehebu 14 katika Shia.  Baadaye Madhehebu moja tu zaidi imetokea - yaani baina ya Nazariya na Mustalawiya. Hivyo idadi ya Madhehebu za Kishia imefikia 15, ambazo kati yao, tatu tu ndizo zilizopo siku hizi. Nyinginezo zote zimekufa mara baada ya kuanzishwa kwao. Baadhi yao kama vile Kaisaniya zimekuwepo kwa muda wa miaka 60 hadi 70 kisha zikafa.

 

Katika msingi huu, tunastaajabu sana tunapoona katika vitabu vya Mabwana Sharistani na Maqrizi Madhehebu za Kishia ambazo hazikuwepo ila kwa kubuniwa tu katika fikara za waandishi hao. Jambo linaloumiza zaidi ni kule kuyakubali tu maandishi ya hayo bila ya kufikiria, kulikofanywa na waandishi wote waliotokea baadaye. Sisi mashia pia tunahusika katika hali hii, kwa kadri waandishi wa Kizungu wahusikavyo kwa sababu vitabu vyetu havikuwa vikipatikana kwa urahisi katika lugha za Kiulaya. Lakini ni udhuru gani uwezao kutolewa na waandishi hao ambao lugha yao ilikuwa, au ni Kiarabu, Kiajemi, au Kiurdu. Vitabu vyetu inauzwa kwa wingi sana katika maduka ya vitabu katika nchi za Mashariki ya Kati, Uhindi na Pakistan. Hakuna kilicho siri katika Madhehebu yetu. Kila kitu kimeelezwa wazi wazi kabisa. Lakini labda waandishi hao wafikiria kuwa njia mzuri ya kujifunzia imani ya kikundi fulani ni kwa kutovitazama kabisa vitabu vya kikundi hicho, na badala yake, kuendelea kunakilitena na tena kile kilichoandikwa na adui wa zamani kuhusu kikundi hicho - japo iwe adui huyo yeye mwenyewe hakukijua kile alichokuwa akikiandika.

 

Nikitoa mifano fulani fulani:

 

Bwana Maqrizi amesema katika kitabu chake kiitwacho "Al-Khutat": Makundi ya Marafidhi (Mashia) ni karibuni 300 ambayo kati ya hayo 20 yanafahamika sana (kama ifahamikavyo siku hizi, hata hayo 20 ni udanganyifu mtupu. Hata Shah Abdul-Aziz Dehlawa naye katika kitabu chake kiitwacho “Tuhfa-I-Ithna-ashariya" ameifanya dhama yake  kupotea. Amedai kuwa zilikuwepo Madhehebu 67 za Kishia, na alipo­ziorodhesha alitoa 61 tu. Kisha alipokuwa akizitaja hizo Madhehebu 20 za kubunia anasema: Zurariya, ambao ni wafuasi wa Zurarah bin A'yun, walisema kuwa Imamu, baada ya Imamu Jaafar Sadiq, ni mwanawe Abdallah ........ na baadaye walimkataa Abdallah na wakasema kuwa Imamu, baada ya Imamu Jaafar ni Musa bin Jaafar.

 

Kisha anaendelea kuhesabu: Madhehebu ya kumi ni Zura­riyah wafuasi wa Zurarah bin Ayun. Yeye aliamini kuwa Mwenyezi Mungu hapo mwanzoni hakuwa Mjuzi wa yote wala Muweza wa yote, na baadaye Alijipatia sifa hizi.

 

Lakini Bwana Zurarah ni sahaba maarufu sana wa Imamu wa Tano na wa Sita. Alifariki mjini Kufa (Iraq) mnamo mwaka 150 Hijiriya muda kidogo baada ya kusikia habari za kifo cha Imamu wa sita, Jaafar Saadiq [a]. Alimtuma mwanawe aitwaye Ubaid kwenda Madina kwenda kuchunguza ni nani aliyemrithi wa Imamu wa Sita. Lakini ugonjwa wake uliendelea hivyo akaichukua Qur'ani mikononi mwake na akasema, "Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika Imamu wangu ni yule mwana wa Jaafar bin Muhammad ambaye Uimamu wake unathibitishwa na hii Qur'ani. Kisha Bwana huyu akafariki. Soma vitabu hivi: (1) Kamaluddin-wa-Tamamun Ni’mah cha Shaikh As Saduq (2) "Al-Fihrist” cha Shaikh At-Tusi nakala ya mwaka 1961 Miladiya, kilichochapishiwa mjini Najaf, Iraq, Uk. 100 (mwishoni mwa ukurasa huo) (3) Tafsir ya Aiyyashi Juzuu ya Kwanza Uk. 27).

 

Bwana Zurarah hakuanzisha Madhehebu yo yote ile, hakuuamini upuuzi uliohusishwa naye kuwa yu mwanzilishi wa Madhehebu ya kubunia ya kumi.  Lakini ilimbidi Maqrizi aonyeshe kuwa zilikuwepo "Madhehebu mashuhuri 20 katika Ushia. hivyo alizibuni Madhehebu na imani zao, lakini kwa bahati mbaya hakuweza kubunia majina mapya na hivyo ilimbidi airudie kuitaja madhehebu ya Zurariyah mara ya pili

 

(Hata kama kwa ajili ya mabishano haya tukichukulia kuwa, kwanza Bwana Zurarah aliuamini Ukhalifa wa Abdallah Al-Aftah na kisha akamrudia Imamu Musa Al-Kadhim [a] itakuwa na maana tu kuwa Bwana huyu alikuwa Fat-hiya ambaye baadaye alikuwa lthna-ashariya. Lakini, vipi imani yake hiyo inaweza kujengwa na kuwa Madhehebu mpya ya Zurariyah? Je, Bwana Marqizi anataka kusema kuwa iliwabidi wafuasi wote wa madhehebu hii ya kubunia kumwamini Abdallah na kisha baadaye katikati ya maisha yao ilibidi wabadili na kumwamini Imamu Musa Al-Kadhim [a]?

 

Vile vile ameibunia Madhehebu ya Hishamiya ambayo ameitumia mara tatu kwa imani tofauti tofauti. Vile vile pamoja na kubunia huku ni Madhehebu ya Yunusia ambayo ameiorodhesha mara mbili. Kisha ameiorodhesha Madhehebu moja iitwayo "Shaitaniya”. Lakini hapa ubuniaji wake umewapanua mawazo baadhi ya watu. Vipi? Baada ya kuihesabu Madhehebu hii ya kubunia miongoni mwa Madhehebu za Kishia, kisha anaihesabu tena miongoni mwa Madhehebu za Mutazila.

 

Na kinachoshangaza zaidi ni kuwa, wale waanzilishi wa kubunia wa Madhehebu zote hizo za kubunia ni watu wale wale waliokuwa na ambao ni miongoni mwa nguzo za imani sahihi ya Kishia. Ni sawa kabisa na kuzihesabu Madhehebu 12 za Wakristo wa Mwanzoni kabisa zilizopewa majina ya wanafunzi 12 wa Yesu na kuzipa Imani nyingine zilizo tofauti na mafundisho ya Yesu.

 

Kwa vile waandishihao wasiokuwa Mashia hawakuzielewa wazi wazi tabia muhimu za Ushia, waliihesabu pamoja na Madhehebu za Kishia hata Ghulat - yaani wale wanaomwamini Ali au Imamu ye yote yule mwingine kuwa ni Mungu au Mdhihiriko wa Mungu. Hawakufahamu kuwa maana ya Ushia ni kuamini kuwa Ali ni Mrithi wa Kwanza wa Mtume wa Mwe­nyezi Mungu - hivyo (Hadhrat Ali [a]) huja baada ya Mwe­nyezi Mungu na Mtume wake, wala sio kuwa yeye (Hadhrat Ali [a]) yu Mungu. Kwa usemi mwingine ni kuwa, tofauti iliyopo kati ya Usunni na Ushia si "dhati ya Ali" bali ni "Cheo cha Ali”, lakini wale waandishi wasiokuwa na ujuzi wa jambo hili walifikiria kuwa ye yote yule aliyelichukulia jina la Ali vyo vyote vile alikuwa Shia - na hiyo ndiyo sababu ya pigo lililoandikwa katika vitabu vyao.

 

Ili kuiweka kumbukumbu hii katika utaratibu mzuri, na nakili kutoka katika vitabu vya Fiqah ya Kishia:

 

­“Hakuna shaka yo yote kuwa "Ghalat” na “Nawasibi” na "Khawarij" ni najisi (sio johara)” (soma kitabu kiitwacho Al-Urwatul-Wuthqa”, cha Sayyid Kadhim Yazdi, kitabu-ut ­Taharat na vitabu vingine vya Fiqah ya Kishia.)

 

"Na kama kitu cha Waqf kinatolewa kwa matumizi ya Mashia, kitatumika kwa Imamiya, na Jurudiya, na Fat-hiya, na Ismailiya, na Nawusiya na Waqifiya na Kaisaniya (soma kitabu kiitwacho Sharaye-ul-Islam" cha Bwana Muhaqqiq, Kitabul-Waqf; na vitabu vingine vyote vya Fiqah ya Kishia].

 

The .HTML version of this book is taken from
www.al-islam.org and ebooked by www.ShiaLibrary.com and www.islamkutuphanesi.com . May Allah be pleased with all.