rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

[2]Fadak

Fadak kilikuwa ni kijiji kimoja chenye rutuba karibu na Madina huko Arabia na vile vile ilikuwa na ngome iliyokuwa ikiitwa ash-Shumrukh. (Mu'jamal buldan,j.4,uk.238;Mu'jam masta'jam,al-Bakri,j. 3,uk.1015;ar-Rawdhal-mi'tar,al-himyari,uk.437;Wafaa' al-wafaa,j. 4,uk.1280). Fadak ilikuwa ni milki ya Mayahudi katika mwaka wa 7 baada ya Hijri na umilikaji wake ulitoka kwao ukawa chini ya Mtume s.a.w.w. kwa mujibu wa mkataba wa amani.Sababu ya mkataba huu ni kwamba baada ya kuanguka kwa Khaybar,Mayahudi waliitambua nguvu na uwezo halisi wa Waislamu,na ushawishi wao kijeshi ulipungua na walishuhudia kuwa Mtume s.a.w.w. aliwasamehe baadhi ya Mayahudi walipoomba hifadhi,vilevile wao walituma ujumbe wa amani kwa Mtume s.a.w.w. na walionyesha nia yao kuwa Fadak ingeliweza kuchukuliwa kutoka kwao na kwamba eneo lao lisingeligeuzwa kuwa uwanja wa vita.Kwa hivyo,Mtume s.a.w.w. alilikubali ombi lao na kuwapatia amani,na ardhi hiyo ikawa ndiyo milki yake binafsi ambamo hakuna aliyekuwa na hamu na wala kusingaliwezekana kuwa na hamu;kwa sababu Waislamu wanayo haki ya kugawana katika milki zile ambazo wanazoweza kuzipata baada ya kupigana Jihad,ambapo milki inayopatikana bila jihad inaitwa fay' ambayo ndiyo milki ya Mtume s.a.w.w.peke yake na kwamba hakuna mtu mwingine yeyote aliyekuwa na haki humo.

Kwa mujibu wa kesi ya 'dai la Fadak' ni kwamba Bi.Fatimah az-Zahra a.s. alidai kuwa baba yake Mtume Mtukufu Muhammad s.a.w.w. alikuwa amempatia Fadak kama Zawadi (hibah)na alikuwa ni mrithi wa sehemu iliyopatikana ya baba yake ya khums ya khaybar na mali yake huko Madina.Tukio hili limeandikwa kama ifuatavyo katika Sahih Bukhari:

Imeripotiwa na Abdul Aziz bin Abdullah,Ibrahim bin Sa'd , Saleh na Ibn Shihab kuwa  wamepewa habari na Urwah bin Zubayr kuwa  imeripotiwa kutoka  Aisha kuwa baada ya kifo cha Mtume s.a.w.w. Bi.Fatimah a.s. alimwambia Abubakr ampatie ile haki  ya urithi wa Mtume s.a.w.w. ambao umepewa na Mwenyezi Mungu.Hapo Abubakr aliielezea hadith isemayo kuwa 'sisi Mitume hatuachi urithi,na sehemu yetu ni sadaqah' na hapo binti yake Mtume s.a.w.w. alighadhabika mno na tangia hapo aliacha kuzungumza na Abubakr mpaka kufariki kwake,kwani baada ya kifo cha babake,aliishi muda wa miezi sita tu. Aisha anaelezea kuwa Bi.Fatimah a.s. alidai urithi wa Khaybar na kiunga huko Madina,lakini Abubakr alikataa katakata kumpatia. Anaendelea Aisha kusema kuwa Abubakr alisema kuwa yeye hakuwa tayari kamwe kuachia kile alichokuwa Mtume s.a.w.w. akikifanyia kazi,bali nami pia nitaendelea kukifanyia kazi. Mimi ninaogopa katika kutahkiki iwapo nitaliachia katika amri za Mtume s.a.w.w. basi nitatoka katika haki na kuingia katika batili.Lakini ni dhahiri kuwa baada yake Abubakr,urithi wa Madina ulipewa Imam Ali a.s na Abbas. Lakini alibakia na Khaybar na Fadak huku akidai kuwa hivyo vilikuwa ni Sadaqah ya Mtume s.a.w.w. Mambo hayo yalikuwanayo hao wawili kwa mujibu wa matakwa yao."

Katika Sahih Bukhari kisa hiki kimeripotiwa mahala pengi (1) Kitabul Khums,mlango faradh khums, (2)Kitabul Fadhail As-habin Nabii katika  mazungumzo ya Abbas bin Abdul Muttalib (3) Kitabul Maghazi,mlango  wa Ghazwah Khaybar, (4) Kitabul Maghazi,mlango Hadith Bani Nadhiir, (5) Kitabul Faraidh,mlango Qaul Nabii  s.a.w.w.: hakirithiwi tunachokiacha Sadaqah. (6) Kitab al-I'tisaam bil kitaan wa Sunnatah.

Katika Bukhari,sehemu moja baada ya kuelezea kisa hiki cha dai la Fadak,imeelezwa hivi:

"Bi.Fatimah az-Zahra a.s. alikasirishwa mno na alimghadhabikia mno Abu Bakr kwa kumkatalia urithi wake,na kamwe hakuongea naye mpaka alipofariki,baada ya miezi sita tangu baba yake kufariki.Baada ya kifo chake,bwana wake Imam Ali a.s. alimzika wakati wa usiku na Abubakr hakuruhusiwa kushiriki katika mazishi na alimsalia mwenyewe.Watu walikuwa wakimstahi Imam Ali a.s katika uhai wa Bi Fatimah a.s. lakini baada ya kifo chake,watu walimgeuka Imam Ali a.s. na kwa sababu hiyo Imam Ali a.s alifanya Bay'a ya Abubakr baada ya miezi sita" (Sahih Bukhari:Kitabul Maghazi,mlango gazwa Khaybar)

Vivi hivi,kisa hiki kimeelezwa katika Sahih Muslim.Angalia Kitabul Jihad wal Siira,mlango kauli Nabii s.a.w.w.:La nurith maa tarakna fahuwa sadaqah yaani haturithiwi kile tulichokiacha,illa ni Sadaqah.

Kwa kuwa kisa hiki  kinapatikana katika 'sahihain" (vitabu viwili sahihi:Muslim na Bukhari) basi wanahadith wanaafikiana na kukubalia.Sasa nitapenda mutafakari juu ya kisa hicho hicho katika kitabu mojawapo maarufu  'tabaqaatil Kubra' kama vilivyo maarufu Sahih Muslim na Bukhari.

"Abubakr hakumpatia chochote Bi.Fatemah a.s. kutoka kile alichokuwa ameacha Mtume s.a.w.w. na kwa sababu hiyo Bi.Fatimah a.s. alimghadhabikia mno Abubakr na kamwe hakuzungumza naye hadi kufariki kwake.Bi Fatimah a.s. aliishi kwa muda wa miezi sita baada ya kifo cha Mtume s.a.w.w. Jaafer anaripoti kuwa Bi.Fatimah a.s. alimwijia Abubakr na kudai haki za urithi kutokana alivyoviacha Mtume s.a.w.w. na vile vile alikuja Abbas kuja kudai urithi wake. Imam Ali a.s. alikuwa nao.Hapo Abubakr aliwajibu kuwa Mtume s.a.w.w. alisema kuwa 'sisi mitume haturithiwi kwa kile tunachokiacha,huwa Sadaqah' na mimi ninafanya kile alichokifanya Mtume s.a.w.w.. Hapo Imam Ali a.s. alimjibu kuwa katika Quran Tukufu imeandikwa kuwa urithi wa Mtume Daud a.s. ulichukuliwa na Mtume Suleyman a.s. na Mtume Zakariyyahh a.s. aliomba dua ajaaliwe mtoto wa kiume ili aweze kuwa mrithi wake na wa Ale Yaaqub. Abubakr alimjibu kuwa ndivyo vivyo hivyo unavyotamka wewe lakini wewe unajua kile nikijuacho mimi. Imam Ali a.s. alimwambia kuwa hiki ni Kitabu cha Allah  kinachosema katika haqi yetu.Lakini Abubakr alikataa katakata na hapo wote watatu waliondoka kwa ukimya." (Tabaqaat Ibn Sa'ad,j.2,uk.86)

Vile vile Imam Tabari ameelezea kwa mapana zaidi katika historia yake.Rejea Tarikh al-Umam wal Muluuk,j.3,uk.202. Allamah Baladhuri ameongezea mwangaza zaidi katika swala hili:                     

"Abdullah ibn Maimun al-Maktub,Fasiil bin 'Iyaar na malik bin Jawza wamenakiliwa wakiripoti kutoka kwa baba yao kuwa Bi.Fatimah az-Zahra a.s. alimwambia Abubakr kuwa Mtume s.a.w.w. alimpatia zawadi na hivyo amrejeshee.Na katika kuthibitisha hivyo,Imam Ali a.s. alitoa uthibitisho wake na hapo ndipo Abubakr alitaka kuletwa mashahidi wengineo.Ummi Aiman alitoa shahada katika dai la Bi.Fatimah a.s. Hapo Abubakr alimwambia Bi.Fatimah a.s. kuwa "unaelewa vyema kuwa ushahidi haukubaliki hadi kuwepo na ushahidi wa wanamme wawili au mwanamme mmoja na wanawake wawili." Hapo Bi.Fatimah a.s. alirudi na kunijulisha hayo. Ruh al-Karabisi amenakili kwa mlolongo wa walioripoti kutoka  kwa Jaafer ibn Muhammad kuwa amesema kuwa Bib.Fatimah az-Zahra a.s. alimwambia Abubakr amrejeshee Fadak kwani Mtume s.a.w.w. alishamzawadia (hiba)Hapo Abubakr alidai aletewe mashahidi.Hapo Bi.Fatima a.s. aliwaleta Ummi Ayman na Rubah,mtumwa wa Mtume s.a.w.w. kutoa ushahidi nao walitoa ushahidi wa kuthibitisha dai la Bi.Fatimah a.s. Hapo Abubakr alisema kuwa ushahidi huo utakubaliwa pale  atakapo patikana mwanamme mmoja na wanawake wawili."

"Ameelezea Ibn Aisha Maitami kutoka Himad bin Salmah,kutoka Muhammad bin Saib Kalbi ambaye kutoka kwa Abu Salha ambaye ameelezea kutoka kwa Ummi Haani ambaye ameripoti kuwa Bi.Fatimah az-Zhra a.s. bintiye Mtume sa.w.w. alikwenda katika baraza la Abubakr na kumwambia 'utakapokufa wewe urithi wako ataupata nani?' Abubakr alijibu kuwa 'watoto na ahali yangu' Sasa je umekuwaje kuwa umechukua urithi wa Mtume s.a.w.w. na unakatalia kunipatia mimi mustahiki wake? Hapo Abubakr alimjibu kuwa 'mimi sijachukua dhahabu au fedha katika urithi wa baba yako na wala sikuchukua hiki au  wala kile.' Bi.Fatimah az-Zahra a.s. alimwambia'kuna hisa katika Khaybar na Fadak ni zawadi na milki yangu' Hapo Abubakr alimwambia:"Ewe Binti wa Mtume s.a.w.w.!  Mimi nilimsikia Mtume s.a.w.w. akisema kuwa Fadak ni kitu ambacho kinazalisha na kulisha ambapo Allah swt hunipatia humo riziki katika uhai wangu na pale nitakapofariki,itagawiwa Waislamu wote."

(Futuh al-Bayaan.Allamah Abul Hasan Bilazuri,chapa ya Misri,uk.44-45)