rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

1.  KUTOKULIPA ZAKA

Katika Madhambi makuu, dhambi la thelathini na saba ni kule kutokulipa Zaka zilizofaradhishwa na kama vile ilivyoelezwa katika Sahifa ya ‘Abdul ‘Adhim kwamba Maimamu Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s., Imam Musa al-Kadhim a.s. na Al Imam Muhammad at-Taqi a.s. wamesema kuwa hili ni dhambi kubwa kabisa kwani amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Tawbaha,

 Ayah 34 – 35 :

Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahannam , na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, “Haya ndiyo (yale mali) mliojilimbikia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya ) yale mliyokuwa mkikusanya.”

Imeelezwa katika riwaya kuwa neno lililotumika katika Ayah hii (kanz)  inamaanisha mali yoyote ile ambamo Zaka na haki zinginezo zilizofaradhishwa hazijatolewa.

Vile vile Amesema Allah swt katika Qur'an Tukufu, Surah Ali-Imran, 3 , Ayah 180 :

Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allah swt katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao. La ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa za yale waliyoyafanyia ubakhili – Siku ya Qiyamah.

Yaaani wale ambao wanamiliki mali kwa kipindi kifupi tu ambayo hatimaye watakufa na hakuna shaka kuwa hakuna kitakachobakia kingine isipokuwa Ufalme wa Allah swt. Hivyo inatubidi sisi tutumie mali hii vyema iwezekanavyo katika njia ya kutuletea baraka na uokovu Siku ya Qiyamah, kabla mali hii haijatutoka na tukaiacha humu humu duniani. Imeandikwa katika Minhaj-us-Sadiqiin kuwa imeelezwa katika Hadith kuwa :

‘Yeyote yule aliyebarikiwa na Allah swt kwa mali na utajiri, lakini kwa sababu za ubakhili wake hakutoa Zaka na malipo mengine yaliyofaradhishwa kwake, basi Siku ya Qiyamah mali hiyo itatokezea kwake katika sura ya nyoka, ambaye atakuwa mwenye sumu kali kwani hatakuwa na unywele wowote juu ya kichwa chake na atakuwa na alama mbili za rangi nyeusi chini ya macho yake na hii ndiyo dalili ya kutambulisha kuwa nyoka huyo ni mkali sana na hatarikabisa. Basi nyoka huyo atajiviringisha shingoni mwa mtu huyo kama mnyororo na kujivingirisha shingoni mwake. Katika hali ya kumsuta, nyoka huyo atasema: ‘Mimi ni mali yako ile ambayo wewe ulikuwa ukijivuna na kujifakharisha nayo duniani.’

Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Wasail-as-shiah, mlango 3, J.6, Uk. 11:

“Mtu yeyote ambaye hatatoa na kulipa Zaka ya mali yake basiSiku ya Qiyamah Allah swt atamwadhibu kwa miale ya mioto katika sura ya nyoka wakubwa ambao watakuwa wakinyofoa na kula nyama yake hadi hapo hisabu yake itakapokwisha.”

Vile vile Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Tafsir Minhaj as-Sadiqiin kuwa :

“Iwapo mtu aliye na mali na utajiri atakapojiwa na ndugu au jamaa yake kwa ajili ya kuomba msaada kutokea mali na utajiri huo alionao, na yeye kwa sababu ya ubakhili wake akimnyima, basi Allah swt atamtoa nyoka mkubwa kabisa kutokea mioto ya Jahannam ambaye huizungusha ulimi wake mdomoni ili kwamba mtu huyo amjie ili aweze kujiviringa shingoni mwake kama mnyororo mzito.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah, ZAKAT, mlango 3, Hadith 1, J.6, Uk. 11 Kafi :

“Mtu yeyote anayemiliki dhahabu na fedha na asipotoa Zaka yake iliyofaradhishwa (au Khums, kama vile inavyoelezwa katika Tafsir al-Qummi), basi Allah swt atamfunga kifungo katika mahala pa upweke na atamwekea nyoka mkubwa kabisa ambaye atakuwa amedondosha nywele zake kwa sababu ya sumu kali aliyonayo, na wakati nyoka huyo atakapotaka kumshika basi mtu huyo atakuwa akijaribu sana kukikmibia lakini atakaposhindwa hatimaye atakapotambua kuwa hataweza kujiokoa basi atanyooshea mikono nyake mbele ya nyoka huyo. Lakini nyoka huyo ataitafuna mikono hiyo kama vile anavyotafunwa mtoto mdogo wa ngamia na atajiviringisha shingoni mwake kama mnyororo. Na hapo Allah swt anatuambia kuwa ‘Yeyote yule anayemiliki mifugo, ng’ombe na ngamia na asiyetoa Zaka ya mali yake, basi Allah swt Siku ya Qiyamah atamfunga kifungo cha upweke na kila mnyama atamwuma na kila mnyama mwenye meno makali atampasua na yeyote yule ambaye hatoi Zaka kutokea mitende, mizabibu na mazao yake ya kilimo, basi huyo siku ya Qiyamah basi atafungwa shingoni mwake kwa mnyororo wenye urefu wa takriban magorofa saba.”

Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah Mlango 3, J.6, Uk.11 :

 “Allah swt amefaradhisha Zaka pamoja na Sala. Ameamrisha kutekeleza Sala na kutoa Zaka hivyo iwapo mtu atasali bila ya kutoa Zaka, basi atakuwa hakukamilisha Sala .

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. Wasa’il as-Shiah, ZAKAT, mlango 3, Hadith 13, J.6, Uk. 11:

amesema kuwa :

“Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. aliingia katika Masjid an-Nabawi, na aliwataja watu watano kwa majina yao na akasema kuwa inukeni na mtoke humu Msikitini na wala msisali kwani nyinyi hamutoi Zaka.

(Wasiolipa Zaka wamefukuzwa kutoka Msikitini !)

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anasema katika Wasa’il as-Shiah, ZAKAT,mlango 3, Hadith 24, J.6, Uk 14 :

“Mtu yeyote asiyelipa Zaka ya mali yake basi yeye wakati wa mauti yake atataka kurudishwa humu duniani ili aweze kutoa na kulipa Zaka, kama vile Allah swt anatuambia: ‘Ewe Allah swt nirudishe tena ili nikafanye mema niliyokuwa nimeyaacha !’ Yaani wakati wa kifo chake atasema kuwa arudishwe humu duniani ili akaitumie mali aliyoilimbikiza katika njia njema, lakini atajibiwa kuwa kamwe haitawezekana hivyo kurudi kwake.”

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameelezea tafsir ya Ayah isemayo kuwa : ‘Allah swt atawaonyesha matendo yao katika hali ya kusikitisha mno kuwa wao hawatatoka nje ya Jahannam’ kama ifuatavyo katika  Wasa’il as-Shiah, mlango 5, Hadith 5, J.6, Uk21 :

“Mtu yule ambaye anakusanya na kulimbikiza mali yake na anafanya ubakhili katika kuitumia katika mambo mema na kwa kutoa zaka n.k., basi anapokufa huku amewaachia mali hiyo wale ambao watatumia mali hiyo katika utiifu wa Allah swt au kwa kutenda madhambi, basi iwapo itatumiwa katika utiifu wa Allah swt basi atakuwa mtu wa kujivuna na iwapo itatumiwa katika maasi na madhambi basi itamdhalilisha.”

Riwaya hii imenakiliwa na ‘Ayyashi, Mufiid, Sadduq na Tabarasi katika vitabu vyao na vile vile wamewanakili Maimamu Al Imam Muhammad al-Baqir a.s. na Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s.

Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema, Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 5, J.6, Uk21 :

“Hakuna kitu kinacho  umaliza uislaam kama ubakhili, na njia ya ubakhili ni njia ya  sisimizi ambayo haionekani na yenyewe ipo kama Shirk ambayo inayo aina nyingi.”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib  a.s. amesema katika Safinat al-Bihar, J.1 Uk. 155 :

 “Watu watakapo kataa kutoa Zaka, basi baraka itakuwa imeondolewa kutoka ardhini kwa kutoa mazao na matunda kutoka mashamba yao,na madini.”

Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. amesema katika Wasa’il as-Shiah,Mlango 1, Hadith  13 :

“Muwatibu wagonjwa wenu kwa kutoa Sadaqah na mutokomeze balaa, maafa kwa Du’a na muhifadhi mali zenu kwa kutoa Zaka.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 10, J.6, Uk23 :

“Allah swt anazo mahala pengi humu ardhini ambazo huitwa ‘kilipiza  kisasi’ hivyo Allah swt anapomjaalia mtu mali na utajiri, na huyo mtu haitumii kwa kutoa malipo aliyofaradhishiwa, basi huwekewa nafasi mahala hapo. Mali ambayo anakusanya kwa mbinu zake zote,inampotoka na anaiacha kwa wengine.”

Na katika riwaya zinginezo imeelezwa kuwa mtu ambaye anafanya ubakhili wa kutumia mali yake katika njia njema basi itatokea kuwa ataitumia katika njia potofu na riwaya ambazo zimeelezwa katika mlango wa Zaka, zipo nyingi, lakini hadi hapa zinatosheleza.

2.  ASIYELIPA ZAKA NI KAFIRI

Kama tulivyokwisha ona hapo awali kuhusu masuala ya zaka na kutokulipa kwake ni dhambi kuu. Iwapo mtu itamlazimu kulipa Zaka na kwa sababu za ubakhili wake, halipi basi atakuwa kafiri na najis kwani Zaka ni sawa na kufaradhishiwa kutimiza jambo muhimu kama Sala, na ni swala moja muhimu katika Dini na kwa kutokutimiza misingi ya dini, basi kunamtoa mtu nje ya dini. Zipo riwaya nyingi ambazo zinazumngumzia kukufurishwa kwa mtu asiyetoa Zaka kwa sababu za ubakhili wake. Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika Wasa’il as-Shiah,mlango 4, Hadith 2, J.6, Uk 18 :

“Bila shaka Allah swt amewawekea hisa mafukara na wenye shida katika mali za matajiri ambayo imefaradhishwa. Faradhi ambayo inapotimizwa inakuwa ni yenye kuwafakharisha matajiri hao na ni kwa sababu ya kutoa huko Zaka kunakoharamisha kumwagwa damu yao na wanaolipa zaka wanaitwa Waislamu.”

Yaani wenye mali iwapo hawatatoa Zaka iliyofaradhishwa kwa kukataa, basi hao si Waislamu na hivyo kumwagwa kwa damu yao haiharamishwi.

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema, Wasa’il as-Shiah,, J.6, Uk18 :

 “Mtu yeyote yule ambaye hatatoa Zaka hata lau kwa kiasi cha Qirat (1.20 Dinar yaani punje nne za Shayiri) basi huyo si Mumin wala si Mwislamu na watu kama hawa ndivyo alivyoelezea Allah swt  kuwa watakuwa wakitaka warudishwe humu duniani ili watekeleze mema. “

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameeleza katika Wasa’il as-Shiah,, J.6, Uk18:

“Mtu yeyote yule ambaye hatatoa Zaka hata kwa kiasi cha Qirat moja (sawa na punje nne za Shayiri) basi huyo atakuwa  bila imani na kifo chake ni sawa na  mauti ya Myahudi au Mnasara.”

Amesema vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. katika Wasa’il as-Shiah, ZAKAT, mlango 3, Hadith 1, J.6, Uk. 19 na  Kafi :

“Allah swt ameruhusu kumwagwa damu ya watu wa aina mbili ambapo hukumu hii itatekelezwa pale atakapodhihiri Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, a.s. na hivyo mmoja miongoni mwa watu hao wawili ni yule anayefanya zinaa ilhali anae mke  hivyo atauawa kwa kupigwa mawe hadi kufa kwake na wa pili ni yule asiyetoa Zaka, huyo atakatwa kichwa.”

Vile vile amesema, katika Wasa’il as-Shiah,mlango 5, Hadith 8, J.6, Uk20 :

“Mali haipotei katika majangwa na Baharini ispokuwa ile isiyolipiwa Zaka na atakapodhihiri Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, a.s. basi wale wote wasiolipa Zaka watasakwa na kukamatwa na watakatwa shingo zao.”

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Fussilat, 41, Ayah 6 – 8 :

“Ole wao wanaomshirikisha, ambao hawatoi Zaka na wanaikataa Aakhera.” 

Amesema Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. , katika  Al-mustadrak :

“Kwa kiapo cha Allah swt ambaye anayo roho ya Mtume Wake katika kudura yake, kuwa hakuna mtu anayemfanyia khiana Allah swt isipokuwa Mushrikina kama hawa ambao hawatoi Zaka kutoka mali zao.”

Vile vile Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. alimwambia Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s., katika Al-Khisal, Uk. 450, Mlango Kumi :

“Ya Ali ! Katika Ummah wangu wapo makafiri wa makundi kumi

1.Mfitini na mchonganishi 

2.Mchawi

3.Dayyuth yaani mwanamme yule ambaye anajua kuwa mke wake anazini lakini hajali bali anapuuzia,

4.Mwanamme yule ambaye anauroho wa kiharamu wa kutafuta wanawake mbalimbal kwa kulawiti,

5.Anayewalawiti wanyama 

6.Anayezini pamoja na wale walioharamishwa kwake yaani ambao ni mahram kwake,

7.Anayechochea na kuzidisha moto wa fitina na chuki miongoni mwa watu, 

8.Anayewasaidia makafiri kihali na mali kupigana dhidi ya Waislamu,

9.Asiyetoa Zaka

10.Asiye Hijji ilhali ana uwezo kamili na kutimiza masharti yake na akifa katika hali hiyo.”

Kwa kuzingatia riwaya kama hizi tunaona kuwa kutokusali, kutokutoa Zaka na kutokuhiji wakati hali inaruhusu, kwa misingi ya ujauri wetu wenyewe, basi huyo ni kafiri na atakosa baraka na neema za Aakhera ambayo ni kumwokoa kutoka Jahannam   na vile vile humu duniani hatakuwa toharifu kama Waislamu na hataruhusiwa kurithi, kuoana pamoja na waislamu, n.k., lakini iwapo mtu hatoi Zaka kwa ubakhili wake (Ingawaje hakatai wala kupinga Zaka) basi huyo hawezi kuwa kafiri.  Ingawaje kidhahiri yeye ni Muislamu lakini kiundani mwake anayo sifa mojawapo ya ukafiri na iwapo atakufa , basi atatumbukizwa katika adhabu kali mno, kama vile ilivyoahidiwa.

3.  SABABU ZA KUFARADHISHWA KWA ZAKA

Katika kufaradhisha utoaji wa Zaka na Sadaqah zinginezo zinahekima ndani yake ambazo hazipo dhahiri mbele yetu. Hata hivyo baadhi yao zimeletwa mbele yetu (ambavyo ni kutokea Allah swt ) mtihani kwa wenye mali na utajiri kwa kujiuliza je kwao Allah swt ni mpenzi zaidi kuliko mali zao ambazo zitakwisha siku moja ?  Na je kwa kweli wana imani kamili juu ya Thawabu, Jannat, Jazaa ( malipo ) au hawana imani ? Je kwa kweli wanafanya ibada ya Allah swt kwa moyo mkweli au sivyo ? 

Faida ya pili ni kuwaondolea shida na taabu wale wanaostahiki misaada hiyo ili waweze kuishi vizuri, na kwa hayo Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema katika kuzungumzia faida za utoaji wa Zaka, katika Kafi Wasail, Mlango 1, Hadith 9 :

“Bila shaka Zaka imefaradhishwa kwa ajili ya kuwajaribu (mtihani) matajiri na wenye mali na kuwatimizia mahitaji ya wenye shida na kwa yakini, iwapo watu wangalikuwa wakitoa Zaka ipasavyo, basi kusingalikuwapo na Waislamu masikini na wenye shida na wala kusingalikuwa na mmoja kumtegemea mwingine na wala kusingalikuwapo na wenye kuwa na njaa au wasiokuwa na nguo. Lakini taabu na shida zote walizonazo masikini ni kutokana na wenye mali na utajiri kutotimiza wajibu wao wa kutoa Zaka na Sadaqah. Hivyo Allah swt humtenga mbali na neeema na baraka Zake yule ambaye hatimizi wajibu wake huo. Nami naapa kwa kiapo cha Allah swt ambaye ameumba viumbe vyote na anawapatia riziki zao, kuwa hakuna kinachopotea katika mali katika nchi kavu au majini isipokuwa ile isiyotolewa  Zaka.

Faida ya tatu, Nafsi yetu inatoharishwa kwa udhalilisho wa ugonjwa sugu wa ubakhili na hivyo inatubidi sisi lazima tuutibu ugonjwa huu unaoangamiza na kutumaliza.

Hivyo Amesema Allah swt katika Quran: Surah al-Tawbah, Ayah 103 :

Chukua sadaqah katika mali yao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaqah zao na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Kwa hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu, na Allah swt ndiye asikiaye na ajuaye.”

Vile vile Amesema Allah swt katika Quran: Surah al – Hashri, 59,  Ayah 9 :

“Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda waliohamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa waliyopewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji.  Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.”

Hivyo tumeona kuwa matibabu ya ugonjwa uitwao ubakhili ni kule kutoa Zaka, misaada na Sadaqah na tuwetukitoa kila mara kiasi kwamba iwe ndiyo tabia yetu na kwa kuzingatia ustaarabu na adabu tukitoa Sadaqah basi tunaweza kuokoka na ugonjwa huu unaotuangamiza.

4.  ZAKA NA SADAQAH HUONGEZA NEEMA

Faida kuu mojawapo ya kutoa Zaka ni kuongezeka kwa neema na baraka ya mali yetu iwapo itatolewa kwa kuzingatia kanuni na ustaarabu wa kutoa, na ni kinyume na mawazo na mipango ya Ki-Shaytani, kwani mabakhili hufikiria daima kuwa kwa kutoa mali yako kwa ajili ya misaada na Sadaqah na Zaka, basi mali yao hupungua na hivyo wanaweza kuwa masikini na kwa hakika hayo ndiyo mawazo na upotofu wa Shaytani.

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Baqarah, Ayah 28 : “Allah swt huongezea katika Sadaqah” yaani huongezea baraka humu duniani na vile vile kutakuwapo na malipo mengine huko Aakhera na amesema Allah swt katika Quran: Surah al – Saba,34, Ayah 39 : ‘Chochote kile mtakachokitoa (katika njia yake), basi Atawalipeni (humu humu duniani) malipo yake, Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.’

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Rum, 30,  Ayah 39 :

‘Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Allah swt . Lakini mnachokitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Allah swt, basi hao ndio watakaozidishiwa.’

Katika Ayah hizo, tumeona kuwa kuongezeka zaidi mno na vile vile Baraka pia itakuwamo, vyote kwa pamoja. Katika kusisitiza hayo, zipo riwaya nyingi mno.

Amesema Bi. Fatimah az-Zahra bintie Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika hotuba aliyoitoa kuzungumzia Fadak katika Bihar al-Anwaar, J.8, Uk 109 :

 “Kwa ajili ya kujitakasa na dhambi la Shirk, Allah swt ametufaradhishia kuikamilisha imani yetu ( yaani mtu yeyote anayetaka kujitakasisha na unajisi basi inambidi kuleta imani kwa moyo wake kamilifu), na Sala inamwepusha na magonjwa ya kiburi na kujifakharisha, na Zaka inamwepusha mtu kwa magonjwa ya ubahili ili mwanadamu awe mkarimu na mpenda kutoa kwa ajili ya mema ili atakasike) na hii pia ndiyo sababu kuu katika kujiongezea riziki .”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib  a.s. ameripotiwa akisema katika Al-Kafi:

“Yeyote yule anayetumia kutoka mali yake katika njia ya kheri, basi Allah swt anamlipa mema humu duniani na kumwongezea katika malipo yake.”

Vile vile ameripotiwa akisema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib  a.s.  katika Wasa’il as-Shiah : Mlango Sadaqah, Hadith 19, J.6, Uk. 259 :

“Tafuteni riziki yenu kwa kutoa Sadaqah.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa katika Kitab ‘Uddatud-Da’I kuwa  alimwuliza mtoto wake :”Je nyumbani kuna kiasi gani kwa ajili ya matumizi ?”

Naye alimjibu : “Zipo Dinar arobaini tu.” 

Imam a.s. alimwambia “Dinar zote hizo zigawe Sadaqah.”

Kwa hayo mtoto wake alimwambia Imam a.s. “Ewe Baba ! Mbali na Dinar hizi arobaini, hatutabakia na akiba yoyote.”

Imam a.s. alimwambia : “Nakuambia kuwa zitoe Dinar zote Sadaqah kwani ni Allah swt tu ndiye atakayetuongezea kwa hayo. Je wewe hauelewi kuwa kila kitu kina ufunguo wake ? Na ufunguo wa riziki ni Sadaqah ( kutolea mema ).”

Kwa hayo, mtoto wake aliyekuwa akiitwa Muhammad, alizitoa Sadaqah Dinar hizo na hazikupita siku kumi, Imam a.s. alitumiwa Dinar elfu nne. Hapo Imam a.s. alimwambia mwanae : “Ewe Mwanangu ! Sisi tulitoa Dinar arobaini tu na Allah swt ametupa Dinar elfu nne badala yake.”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib  a.s. amesema katika Nahjul Balagha kuwa :

“Mtu anapokuwa masikini au mwenye shida basi fanyeni biashara pamoja na Allah swt kwa kutoa Sadaqah.”

Al Imam ‘Ali ar Ridha  a.s. alimwambia mfanyakazi wake : “Je leo umeshagawa chochote katika njia ya Allah swt .”  Mfanyakazi huyo, “La, bado sijagawa.”  Kwa kuyasikia hayo Imam a.s. alimjibu, “ Sasa kama haukufanya hivyo, basi Allah swt atatulipa nini badala ya tendo letu ? Hivyo hatutapata baraka wala neema yoyote kutoka kwa Allah swt . Tukitoa chochote ndipo Allah swt atatulipa kwa wingi badala yake.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameelezea Hadith katika Al-kafi, Kitab ad-Du’a, J. 2, Uk.595  moja kwa kutokea Ayah Fahuwa Yukhlifuhu (yaani chochote kile kinachotolewa katika njia ya Allah swt , basi hulipa malipo yake kwa haraka sana ). Na Hadith yenyewe ni :

“Je utadhaniaje kuwa Allah swt anakiuka ahadi aliyoitoa ?”

Basi mwandishi  akajibu : “La ! Sivyo hivyo.”

Ndipo Imam a.s. alimwuliza : “Sasa je kwanini wewe haupati malipo yako kwa yale unayoyatoa na kugawa ?”

Naye akajibu, “ Kwa hakika mimi sijui sababu zake.”

Imam a.s. alimjibu, “Iwapo miongoni mwenu yeyote atakayekuwa akiipata riziki yake kwa njia zilizo halali, na kama ataitumia hata Dirham moja katika njia zilizo halali, basi lazima mtapata malipo yake na kwa wingi zaidi.  Na iwapo mkiona kuwa hamkupata chochote katika malipo yenu basi mutambue kuwa mali hiyo ilichumwa kwa njia zilizo haramu au ilitolewa na kutumiwa katika njia iliyoharamishwa.”

Kuhusiana na swala hili zipo Ayah na riwaya nyingi mno, lakini tunatua hapa. Marehemu Nouri katika kitabu chake Kalimah at-Tayyibah amezungumzia mengi na kwa mapana na undani zaidi kuhusu kutoa Sadaqah katika njia ya Allah swt  na amedondoa hekaya takriban arobaini ambamo ‘Alim rabbani akhwand Mullah Fath ‘Ali amenakili kisa cha jamaa yake ategemewae ambaye amesema,

“Mwaka mmoja ambapo hali ya ughali ilikuwa imekithiri, nilikuwa na kipande kimoja cha ardhi ambapo nilikuwa nimepanda Shayiri na ikatokea kuwa shamba langu hilo likawa na mavuno mengi mno kuliko mashamba mengineyo. Kwa kuwa hali ilikuwa ni mbaya kwa watu wengineo, hivyo tamaa ya kujitafutia faida zaidi katika mazingara hayo niliyatoa kutoka nafsi yangu. Hivyo mimi nilikwenda moja kwa moja Msikitini na kutangaza kuwa mazao yote yaliyo shambani mwangu nimeyaacha kwa masharti kwamba yeyote mwenye shida tu ndiye aende kuchukua na masikini na mafukara waendekuchukua kwa ajili ya chakula cha familia zao. Wote wachukue kiasi wanachokihitaji. Hivyo masikini na mafukara na wenye shida walikuwa wakichukua mavuno kutoka shambani mwangu huku wakisubiri mavuno yao kukomaa. Kwa hakika nafsi yangu ilikuwa imetulia vyema kabisa kwani sikuwa na wasiwasi kwani nilikuwa nimeshajitenga navyo.

Wakulima wadogowadogo wote walipovuna mazao yao, nami nikavuna kutoka mashamba yangu mengine na nikawaambia wafanyakazi wangu waende katika shamba ambalo nilikuwa nimeligawa kuwasaidia wenye shida wakati huo, wakaangalie kama kumebakia chochote ili waweze kuvuna.

Kwa hakika hao walipokwenda shambani humo walikuta shamba zima limejaa Shayiri kupita kiasi na baada ya kuvuna na kusafisha nilikuta kuwa nimepata mavuno mara dufu kuliko mashamba yangu mengineyo. Ingawaje humo watu wote walikuwa wakivuna kwa ajili ya chakula chao na familia zao, ilitakiwa kuwa tupu kumbe Allah swt amerudishia mavuno tena mara dufu.

Vile vile sisi tulikuwa ukipanda mwaka mmoja na kuipumzisha ardhi mwaka mmoja, lakini shamba hilo halikuhitaji kupumzishwa wala kuwekewa mbolea na badala yake nimekuwa nikilima na kupanda nafaka kila mwaka na nilikuwa nikipata mavuno mara dufu kila msimu.

Mimi kwa hakika nilistaajabishwa mno kuona hayo na nikajiuliza isije hiki kipande cha ardhi kikawa ni kitu kingine na mavuno yanapokuwa tayari, hupata mavuno mengi kabisa kuliko mashamba mengine yangu na ya watu wengineo.

Mbali na hayo, Marehemu amenakiliwa kuwa :

‘Yeye alikuwa na shamba moja la mizabibu kandoni mwa barabara na kwa mara ya kwanza kulipozaa zabibu katika matawi yake, alimwammuru mtunza shamba wake kuwa zabibu zote zilizopo kando ya barabara aziache kwa ajili ya wapitao njia. Hivyo kila mpita njia alichuma na kula zabibu zilizokuwa hapo na wengine hata walichukua pamoja nao. Msimu ulipokwa ukiisha aliwaamuru wafanyakazi wake waende kuangalia kama kulibakia zabibu zilizokuwa zimefichika nyuma ya majani au pembeni. Lakini jambo la kustaajabisha ni kwamba, wafanyakazi waliporudi, walikuwa wamevuna zabibu mara dufu ya mashamba yake mengineyo pamoja na kwamba kila mpita njia alikuwa akichuma zabibu hapo.’

Vile vile imenakiliwa kuwa :

‘Kila msimu alipokuwa akivuna ngano na kuzisafisha, alikuwa akizileta nyumbani kwake na hapo ndipo alipokuwa akitoa Zaka yake. Lakini safari moja alipovuna na kusafisha, akiwa akielekea nyumbani kwake aliwaza kuwa inambidi alipe Zaka haraka iwezekanavyo, kwani si vyema kuchelewesha ulipaji wa Zaka. Ni ukweli kwamba ngano ipo tayari na mafukaraa na masikini pia wapo. Hivyo aliwajulisha mara moja mafukaraa na masikini waje kuchukua ngano, na hivyo akapiga mahisabu yake na kuwagawia sehemu yao na hivyo sehemu iliyobakia aliileta nyumbani kwake na kujaza madebe makubwa makubwa na alikuwa akijua ujazo wao. Lakini alikuja kuangalia hapo baadaye akakuta kuwa idadi ya ngano imeongezeka mara dufu pamoja na kwamba alikuwa amepunguza kwa ajili ya kuwagawia mafukaraa na masikini.Na hivyo alikuta idadi ya ngano ipo pale pale kabla ya kutoa Zaka.’

Katika kitabu kilichotajwa, Alhaj Mahdi Sultan Abadi amenakili kuwa :

‘Mwaka mmoja mimi nilipovuna mavuno, nilipima uzito wa ngano na nikatoa na kuigawa Zaka yake. Na nafaka hizo zilibakia mahala hapo hapo kwa muda wa mwezi mmoja ambapo wanyama pamoja na mapanya walikuwa wakila humo. Na nilipokuja kurudia kupima uzito wake nikakuta kuwa uzito wa ngano ulikuwa vile vile kama siku ya kwanza yaani kiasi nilichokitoa Zaka na kilicholiwa na wanyama na mapanya hakikupungua hata chembe kidogo.’

5.  AINA ZA ZAKA NA VIWANGO VYAKE

Zaka imegawanywa katika makundi mawili

 Zaka  iliyofaradhishwa

 Zaka iliyo Sunnah

Na Zaka iliyofaradhishwa pia imegawanywa katika makundi mawili :

1.  Zaka ya mali

2.  Zaka ya Mwili  ( Zakati Fitrah )

Zaka iliyofaradhishwa inayo aina tisa za mali na aina nne za nafaka ( ngano, Shayiri, tende na zabibu ), aina tatu za wanyama (kondoo au mbuzi, ng’ombe na ngamia ) na aina mbili za madini (dhahabu na fedha ).

Mahisabu ya aina nne za nafaka :

1. Ngano, Shayiri, tende na zabibu zitastahiki kutolewa Zaka iwapo zitafikia kiwango maalum ambavyo ni Saa 300 au mann 280 Tabrizi na ni pungufu kwa mithqal 45 ambayo ni sawa na takriban Kilogramu 847 .

2. Na iwapo ( ngano, Shayiri, tende na zabibu )  zinalimwa kwa umwagiliaji wa maji ya mvua au mito au kwa urutubisho wa ardhi (kama yalivyo baadhi ya mazao huko Misri ) basi Zaka yake itakuwa ni asilimia 10  ( 10 % )

3. Na iwapo inamwagiwa kwa maji ya kisima basi Zaka yake itakuwa asilimia 5. ( 5% )

1.  zaka ya mali

(A).  ZAKA KATIKA WANYAMA

(i) VIWANGO  VITANO VYA KONDOO NA MBUZI

1. Idadi yao iwapo ni arobaini (40 ) basi Zaka yake ni kondoo au mbuzi mmoja ( 1 ) na iwapo hawatafika arobaini basi hakuna Zaka.

2. Idadi yao iwapo ni mia moja na ishirini na moja ( 121 ) basi Zaka yake itakuwa ni kondoo au mbuzi wawili ( 2 )

3. Iwapo idadi yao ni mia mbili na moja ( 201 ) basi Zaka yao itakuwa ni kondoo au mbuzi watatu ( 3 ).

4. Iwapo idadi yao ni mia tatu na moja ( 301 ) basi Zaka yao itakuwa ni kondoo au mbuzi wanne ( 4 ).

5. Iwapo idadi yao ni mia nne ( 400 ) au zaidi basi Zaka yao itakuwa ni kondoo au mbuzi mmoja kwa kila kondoo au mbuzi mia moja  ( 1 ).

(ii) VIWANGO  VIWILI  VYA NG’OMBE  1.Kiwango cha kwanza ni ng’ombe 30. Iwapo mtu atakuwa na ng’ombe 30 basi itambidi alipe Zaka ambayo ni ndama dume mmoja wa ng’ombe ambaye ameingia katika umri wa mwaka wa pili. Na iwapo watapungua ng’ombe chini ya 30, basi hawatakiwi kulipa Zaka.

2.Kiango cha pili ni ng’ombe 40 na Zaka yake ni ndama jike wa ng’ombe ambaye ameshaingia katika mwaka wa tatu .

·· Iwapo mtu atakuwa na ng’ombe kati ya 30 na 40  ( mfano ng’ombe 39 ) basi anatakiwa alipe Zaka za ng’ombe 30 tu.

·· Na iwapo anao ng’ombe 60 basi atalipa Zaka ya  ndama 2 ambao wameingia katika mwaka wa pili.

·· Na iwapo anao ng’ombe 70 basi atalipa Zaka ya  ndama 1 ambaye ameingia katika mwaka wa pili na ndama jike mmoja ambaye ameingia katika mwaka wa tatu.

·· Kwa kila idadi itakavyoongezeka basi itabidi kupigia hisabu kwa 30 au 40 na Zaka itatolewa hivyo.

(i)

 (iii) VIWANGO  12  VYA NGAMIA

1. Iwapo mtu atakuwa na ngamia 5 basi Zaka yake ni mbuzi au kondoo mmoja. Iwapo idadi ya ngamia 5 haitafika basi hatatakiwa kulipa Zaka.

2. Ngamia 10 na Zaka yake ni mbuzi au kondoo 2

3. Ngamia 15 na Zaka yake ni mbuzi au kondoo 3

4. Ngamia 20  Zaka yake ni mbuzi au kondoo 4

5. Ngamia 25  Zaka yake ni mbuzi au kondoo 5

6. Ngamia 26  Zaka yake ni ngamia mmoja ambaye ameingia mwaka wa pili

7. Ngamia 36  Zaka yake ni ngamia mmoja ambaye ameingia mwaka wa tatu

8. Ngamia 46  Zaka yake ni ngamia mmoja ambaye ameingia mwaka wa nne

9. Ngamia 61  Zaka yake ni ngamia mmoja ambaye ameingia mwaka wa tano

10. Ngamia 76  Zaka yake ni ngamia wawili ambao wameingia mwaka wa tatu

11. Ngamia 91  Zaka yake ni ngamia wawili ambao wameingia mwaka wa nne

12. Ngamia 121  Zaka yake itahesabiwa ama kwa makundi ya ngami 40, na atatoa Zaka ngamia mmoja aliyeingia mwaka wa tatu na kila kikundi cha ngamia 50 atatoa ngamia mmoja aliyeingia mwaka wa nne.

(B).  VIWANGO 2 VYA DHAHABU NA FEDHA[1]

(1) VIWANGO 2 VYA  FEDHA

1. Kiwango cha kwanza ni Mithqaal  105, sawa na uzito wa Gramu 483.88  na kama fedha hiyo imebadilishwa katika sarafu kwa ajili ya kufanyiwa biashara na zimewekwa mahala kwa muda wa mwaka mmoja basi Zaka yake itakuwa ni asilimia 2.5  (2.5 % ) Na iwapo kiwango hicho kitapungua basi hakuna Zaka itakayolipwa.

2. Kuongezeka kwa Mithqaal 21 katika Mithqaal 105 zikawa jumla ya Mithqaal 126, basi itambidi alipe Zaka ya Mithqaal 126. Na iwapo itakuwa chini ya Mithqaal 126 ( kama haitafikia Mithqaal 21 ) basi itambidi alipie Zaka katika Mithqaal 105. Hivyo itambidi alipe  sehemu 1 / 40 ya jumla. Lakini lazima iwe imefikia Mithqaal 21 na kama itapungua basi kiwango hicho kitabaki kilipofikia. Mfano iwapo mtu atatakiwa kulipia Mithqaal 110 basi yeye atalipia Mithqaal  105 ambayo ni sawa na 2. 5 % ( au 2.625 Mithqaal) na mara nyingine itambidi alipie  Mithqaal 5zilizo zidi ambayo si faradhi.

1) 2)   VIWANGO 2 VYA  DHAHABU

1. Kiwango cha kwanza ni Mithqaal 20 (Shar’ee) katika sura ya sarafu zitumiwazo katika kufanyia biashara na zikakaa kwa muda wa mwaka mmoja mahala moja bila kutumiwa ambapo Mithqaal  1 ni sawa na uzito wa  3.456 gramu na hivyo inapofikia kiwango cha 20 Mithqaal ( ispofikia hivyo, hakuna Zaka )  inambidi mtu alipe Zaka kwa kiwango cha  sehemu  1/40 ambayo ni sawa na uzito wa 1.728 gramu.

2. Kiwango cha pili ni kule kunapoongezeka kwa dhahabu zaidi ya Mithqaal  20 Shar’ee,  iwapo kutaongezeka Mithqaal  4 Shar’ee juu ya Mithqaal  20 Shar’ee basi  inambidi mtu alipe Zaka kwa kiwango chote kwa ujumla kwa kiwango cha  2. 5 %  na iwapo kiwango cha nyongeza kitakuwa ni pungufu ya 4 Mithqaal,  basi Zaka italipwa kwa 20 Shar’ee Mithqaal  tu na haitamlazimu kulipia Mithqaal  iliyozidi ambayo ni pungufu ya 4 Mithqaal .

2.  ZAKAT-ul-FITRAH

Mtu yeyote yule ambaye katika usiku wa kuamkia Idd-ul-Fitr ( usiku wa kuamkia tarehe mosi ya Mwezi mtukufu wa Shawwaal ) baada ya kuzama kwa jua akabalehe, akawa na akili timamu na ghanii ( yaani ambaye anajitimizia mahitaji yake ya dharura ya kila mwezi, huitwa ghanii, yaani si mwenye dhiki ) basi ni faradhi juu yake  kutoa Zakat-i-Fitri yake binafsi na wale wote wanaomtegemea kimaisha na kichakula hata wale watoto wachanga wanaonyonya,  vile vile kama kutatokezea mgeni basi awalipie nao pia. Kiwango cha  Fitrah ni Sa’a imoja ambayo ni sawa na kiasi cha kilogramu 3 za ngano, zabibu, tende, mchele au cho chote kile anachokitumia yeye kama chakula chake cha kila siku na itambidi awape wale wanaostahiki au anaweza kutoa thamani yake kifedha, nayo inafaa.

Tukumbuke kuwa faida ya papo hapo ya fitrani kule kubakia katika kunusurika na mauti ambazo si za kawaida kama vile ajali n.k. na imeripotiwa na Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. kuwa :

“Alimwambia wakili wake wa matumizi kuwa aende akatoe Zakat-i-Fitrah ya wananyumba yake wote bila hata ya kumsahau mmoja wao kwa sababu iwapo hatatoa Zaka yao basi atakuwa na hofu ya kufa kwao na thawabu zake ni sawa na kukubaliwa kwa saumu za mwezi mzima.

Vile vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. amesema :

“Zakat-i-Fitrah inakamilisha saumu za mwezi Mtukufu wa Ramadhani.”

6.  MATUMIZI YA ZAKA

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al – Tawbah,  9, Ayah 60 :

“Wa kupewa Sadaqah ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allah swt , na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaradhiwa na Allah swt . Na Allah swt ni Mwenye kujua Mwenye hikima.”

Mali ya Zaka inaweza kugawiwa sehemu nane kama ilivyoelezwa katika ayah hii ya Qur'an Tukufu :

1. Fakiri

Ni mtu yule ambaye yeye hana uwezo wa kujilisha yeye pamoja na familia yake kwa muda wa mwaka mzima. Ambaye kwa hakika hana uwezo wa kurejesha sasa hivi au hata hapo mbeleni. Lakini yule mtu ambaye anamiliki majengo, milki au mali haitwi fakiri.

2. Masikini

 Ni yule ambaye hali yake ni ngumu kuliko hata fakiri.

3. Wanaozitumikia

 Ni mtu yule ambaye anakusanya Zaka kwa niaba ya Al-Imam Muhammad Mahdi, sahibuz-zamaan, a.s. na kumfikishia Naibu wa Imam a.s. au wanaostahiki.

4. Wa kutiwa nguvu nyoyo zao

 Ni Waislamu wale ambao imani zao ni dhaifu hivyo kwa kuwasaidia na kuwapa nguvu kimaisha.

5. Kukomboa watumwa

 Kutumia mapato ya Zaka kwa ajili ya kumfanya huru mtumwa ambaye yupo katika hali ya kuteswa mno au kumnunua na kumfanya awe huru

6. Wenye madeni

Kuwasaidia mapato ya Zaka wale wasiojiweza kulipa madeni wanayodaiwa.

7. Njia ya Allah swt

 Mapato ya Zaka yanaweza kutumia katika kila shughuli zenye kuifaidisha Dini mfano ujenzi wa Misikiti au Madrassah ili Waislamu waweze kufaidika kwa kufanyia ‘ibada na vile vile kutolewe mafunzo ya Dini , au kutengeneza madaraja au kusuluhisha makundi mawili au watu wawili waliotafarukiana au kusaidia katika ‘ibada, n.k.

8. Wasafiri :

 Kumsaidia msafiri ambaye amekumbwa na matatizo akiwa safarini ambaye hawezi kuchukua deni au kuuza kitu alichonacho kwa ajili ya kurudi nyumbani kwake hata kama yeye hatakuwa  fakiri nyumbani kwake.

7.  ZAKA ZILIZO SUNNAH

Vitu saba vina Zaka Sunnah :

1. Mali ya biashara au mtaji

Mali ambayo mtu anataka kuitumia katika kufanyia bishara

2. Aina za nafaka :

Mfano mchele, dengu, dengu iliyoparazwa. Lakini mbogamboga kama vile biringanya, matango, matikimaji, maboga hayana Zaka.

3. Farasi jike

4. Vito vya dhahabu na mawe

Vitu vilivyotengezwa vya kuvaa na mawe kama almasi n.k.

5. Mali iliyozikwa au kufichwa

Iwapo mtu atakuwa na mali aliyoizika au aliyoificha ambayo hawezi kuitumia basi kwa misingi ya uwezo inambidi kutoa Zaka ya mwaka mmoja.

6. Kukwepa kutoa Zaka

Iwapo mtu atauza sehemu ya mali kiasi fulani kabla ya kuisha kwa mwaka kwa misingi ya kukwepa kulipa Zaka, basi itambidi uanzapo mwaka mpya, alipie Zaka sehemu hiyo aliyokuwa ameuza kwa ajili ya kukwepa Zaka yake.

7. Mali ya kukodisha

Mtu anayepokea malipo kutokana na kukodisha majumba, maduka, mashamba, mabustani au hamaam (mabafu yanayotoza malipo kwa kutumia ).

8.  KUSALI SALA ZA MAREHEMU NI LAZIMA

Haifai kabisa kufanya uvivu katika Sala zilizofaradhishwa na iwapo kutabakia kwa Sala ambazo zimekuwa Qadhaa za marehemu basi ni wajibu kwake kufanya wasia kuwa sala zake hizo zitimizwe baada  ya kufa kwake. Na marehemu anapofanya wasia kama huo basi ni wajib juu ya muusiwa kutekeleza na kutimiza usia huo kutokea sehemu ya tatu ya mali ya marehemu huyo.


[1] Viwango hivi vimeletwa mbele yenu kwa kimukhtasari tu ili kuweza kuwapa mwanga juu ya masuala haya na hivyo inatubidi sisi turejee vitabu vya Fiq-hi ili tuweze kujua hukumu za Shariah kwa undani zaidi katika masuala haya na mengineyo.