rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

 

UHARAMISHO WA ULEVI

Kimekusanywa na kutarjumiwa na : AMIRALY M. H. DATOO

Katika Islam

UHARAMISHO WA ULEVI

Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari.

Sema: Katika hivyo mna madhara makubwa na (baadhi ya) manufaa kwa (baadhi ya) watu. Lakini madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake.” (Al-Baqarah: 219)

Vile vile twaambiwa katika Ayah nyingine:

“Kwa hakika Shaitani anataka kukutilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na antaka kukuzuilieni dhikri za Allah na kusali. Basi je mtaacha hayo ?

(Al - Maida: 93)

Vile vile kwa ajili ya sala twaambiwa:

Na wala msikaribie sala katika hali ya kulewa.

Ingawaje makala na vitabu vingi mno vimekwisha andikwa juu ya maudhui haya, lakini uovu huu unaonekana bado ukienea kwa kasi kama vile moto unavyoenea porini. Kwa kuwa somo hili ni nyeti sana hivyo nimeona nikitayarishe kijitabu hiki kwa mukhtasari juu ya maovu yatokanayo na ulevi ili tuungane pamoja katika jitihada za kuiokoa jamii zetu zisitumbukie katika balaa hii ya kunywa pombe ambayo inaamgamiza maadili.

Ni jambo la kuvutia kuwa hakuna utofauti wa maoni miongoni mwa wanazuoni katika swala zima la pombe na athari zake mbaya. Sisi tutawaleteeni hoja nyingi kuhusu madhara ya pombe ili kuwathibitishia kuwa pombe ni kitu kibaya kabisa.

Hadi hivi karibuni, majaheli wengi walikuwa wakiamini kuwa iwapo pombe ingekuwa ikinywa kwa kiasi basi haitakuwa na madhara bali kutakuwa na faida ndani mwake. Lakini kutokana na utafiti uliofanywa na Wanasayansi wa Marekani na Ulaya imebainika wazi wazi kuwa pombe kwa kiasi kidogo kabisa pia kinaleta madhara makubwa kwa mnywaji.

Tafadhali zingatia ripoti ifuatayo ambayo imepatikana:

Wakati fulani ambapo mabingwa wa fani ya utibabu walipokusanyika katika kongamano lao la kimataifa huko Washington, Marekani kwa ajili kupiga vita pombe na unywaji wake, nao walitoa kauli moja kuwa pombe ndiye adui no. 1 wa mwanadamu.

Dr. Melvin Kanzeli, ambaye amepitisha miaka mingi katika utafiti juu ya unywaji wa pombe,alisema yafuatayo katika kikao hicho kuwa:

“Unywaji wa pombe unaharibu sana ubongo wa mtu. Wakati mtu ajisikiapo raha na kuburudika kwa kiwango kidogo cha pombe, yeye huwa hana habari kuwa anaziua seli za ubongo wake.”

Dr. Kanzeli ambaye ndiye Mkuu wa taasisi ya utafiti cha Chuo cha Matibabu cha South Carrolina, anaamini kuwa unywaji wa pombe kupita kiasi unasababisha mabadiliko katika damu na mishipa yake kiasi kwamba ubongo unakosa hewa ya oksijeni na hivyo kuharibiwa, au kuharibika kiasi kwamba mtu anatumbukia katika hali ya kuchanganyikiwa akili.

Kuingia kwa pombe katika damu kunaathiri mno mzunguko wa damu, na hivyo mara nyingi husababisha kuganda kwa damu.

Katika hotuba yake ya ufunguzi katika kongamano hilo la kimataifa, Dr. Kanzeli alisema:

“Kwa bahati mbaya, juhudi zilizokwisha fanywa kwa kupiga vita unywaji wa pombe, ambapo wanaoathirika idadi yao huongezeka siku baada ya siku, hazikufanikiwa . Kwa hivi sasa, mamilioni ya watu ulimwenguni kote wapo wametumbukia katika unywaji wa pombe bila ya kutafuta njia ya kujitoa humo.”

Hapa kuna jambo moja ambalo watu wengi mno wanadhani kuwa kunywa pombe kidogo hakuleti madhara yoyote bali ni lazima pia. Baadhi ya watu wanasadiki kuwa iwapo wao watakunywa pombe kiasi kidogo katika hafla zao basi kamwe hawatakuwa na tabia mbaya ya kunywa pombe kupita kiasi. Lakini utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa ulevi wa aina yoyote ile na kwa kiasi chochote kidogo kile lazima kinaathiri kazi sahihi za seli (cells) za ubongo wa mwanadamu.

Dr. Raymond Penington, naye pia katika ripoti yake ya kurasa 4 aliyoiwasilisha katika kongamano hilo, alisema:

“Hakuna shaka kuwa pombe ndiye adui hatari mkubwa sana wa mwanadamu, na wale wote wanaojitamba kuwa wao wanakunywa kwa nadra sana, nao pia wanajitumbukiza katika matokeo maovu kabisa ya adui huyu.

Katika maoni yake, matokeo ya awali ya unywaji wa pombe ni usahaulivu na hatimaye kupoteza kazi aliyokuwa akiifanya mtu. Yeye anasema:

Utafiti wetu umetuonyesha kuwa walevi katika muda mfupi huanza kusahau - sahau na hivyo hujikosesha nafasi ya kujipatia maendeleo. Wao huwa hawana hamu na kazi zao, na hatimaye kupoteza kazi zao jambo ambalo litatumbukiza zaidi katika pombe.”

Kwa bahati mbaya unywaji huu wa pombe umekithiri miongoni mwa tabaka la vijana ambao hujipoteza katika pombe ati kwa kujisahaulisha matatizo ya maisha yao. Katika utafiti wetu, sisi tumefikia uamuzi kuwa zaidi ya asilimia 75 ya vijana wapo wamejielekeza katika unywaji wa pombe, na kiasi cha asilimia 20 - 30 wameshajitosa katika unywaji wa pombe. Kuongezeka daima kwa fujo na ghasia katika mitaa ni uthibitisho wa kuongezeka unywaji wa pombe. Ukipeleleza mafaili ya wahalifu utaona kuwa wahalifu wengi ni wale waliotumbukia katika unywaji wa pombe.”

Dr. Hertbert Moskov, ambaye pia mganga ambaye alishiriki katika kongamano hilo la kupiga vita pombe na ulevi, anasema:

“Pombe hudhoofisha seli za ubongo na kuteketeza nguvu za uwezo wa kukabiliana na matatizo. Lakini tatizo kubwa ni dosari za urithi wa kimwili. Mlevi kwa kawaida huwa amechoka, mvivu na mpumbavu. Yeye huwa hayupo tayari kusoma na daima huwa amelaaniwa.

Hivyo imeonekana mara nyingi kuwa kizazi cha watu kama hao huwa na dosari kuanzia kuzaliwa kwao.”

Uamuzi uliofikiwa kwa kutolewa hoja za wachunguzi wa kisayansi katika kongamano hilo, inaweza kuwaathiri wachache, lakini hii haimaanishi kuwa ndio suluhisho na ufumbuzi wa matibabu. Pombe imeshaota mizizi mirefu katika maisha ya siku hadi siku ya mwanadamu, na iwapo hakutaanzishwa vita dhidi yake, basi mizizi yake itakuwa madhubuti na mipana na kuwatumbukiza watu wengi katika mitego yake.

Kwa hakika utafiti na matokeo ya kazi zao hizo ndizo zinazotuongoza sisi moja kwa moja kupigia magoti Sharia na kanuni za Dini ya Islam - Sharia ambayo miaka 1400 iliyopita, hata kabla ya kuwapo kwa maabara ya uchunguzi na kuwapo kwa vyuo vikuu, iliharamisha unywaji wa pombe hata kwa tone moja.

Katika maisha ya Mwanachuoni mkuuu wa Madhehebu ya Shiah, marehemu Ayatollah Burujerdi, Dr.Arshe Tung, Katibu Mkuu wa Shirika la kupambana na pombe, alitembelea Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran alitamani kupokelewa na kiongozi wa Madhehebu ya Shia’ili aweze kumwuliza baadhi ya maswali.

Mkutano huu uliweza kupangwa na profesa wa Chuo Kikuu cha Teheran na katibu wa jumuiya ya kupambana na pombe. Muhtasari wa mazungumzo ya mkutano huu imetolewa na Profesa pamoja na katibu kama ifuatavyo:

Kwa kuchaguliwa Arshe Tung kuwa Katibu Mkuu wa Shirika la kupambana na pombe, akiambatana nami, tulipokelewa na Ayatollah Burujerdi. Sisi tulivua viatu vyetu mlangoni kabla ya kuingia chumbani mbele ya Mheshimiwa, na tulipoingia chumbani tulikwenda moja kwa moja kwake na kubusu mkono wake kama kutoa heshima zetu. Unyenyekevu na upole wake kwa hakika ulituvutia mno. Uvuto na sura yenye furaha na kutujua hali kwa upole ulitudhihirishia kuwa ametukaribisha vyema. Baada ya mimi kumshukuruu Ayatollah kwa kuturuhusu sisi kumtembelea, mimi nilimtambulisha bwana Arshe Tung kama raia wa Uswisi na Katibu Mkuu wa Shirika la kupambana na pombe, na kuongezea: katika safari zake za Indoneshia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili kuzindua harakati zake hizi, yeye ameonyesha hamu kubwa sana ya kutaka kukutana na Ayatollah, na sasa anaomba kuuliza baadhi ya maswali na kujibiwa.”

Arshe Tung aliuliza:

“ Je ni kwa nini unywaji wa pombe na chochote kile kileweshacho vimeharamishwa katika Islam”

Ayatollah alimjibu:

“ Mwanadamu ni kiumbe bora katika viumbe vyote vya Allah swt kwa sababu ya aql , na madhumuni ya kumwumba ni kumfanya yeye ajiendeleze katika utakatifu na uchaMungu. Yeye amepewa aql na busara, na amepewa baadhi ya maamrisho , vile vile kwa ajili ya kuhifadhi aql na busara. Hivyo kwa kuhusiana nayo, Mtume Muhammad s.a.w.w. ameharamisha unywaji na utumiaji wa vitu vinavyolewesha na ambavyo vinaathari mbaya sana ya kuharibu akili na bongo, na kwa hakika kuharamishwa huku ni lazima kabisa kwa ajili ya kunusuru maswala hayo.”

Arshe Tung aliuliza tena:

“Unywaji wa kupindukia unaoleta hali ya mtu kuwa amelewa sana ambavyo kwa hakika inadhuru bongo na kuleta madhara yake, lakini wewe unasemaje kuhusu kutumia pombe kwa kiasi kidogo ambacho hakimleweshi mtu ?”

Ayatollah alimjibu:

“Kwa kuwa tumeshakwisha kujua kuwa ubora wa mwanadamu kwa mnyama ni kwa sababu ya akili aliyo nayo yeye, na kwamba ipo dhahiri kuwa wajibu wa mtu ni kujielekeza katika kulinda zawadi kuu za Mwenyezi Mungu kwa hali bora kabisa, kwa hivyo chochote kile kitakacho dhoofisha hivyo haviruhusiwi kamwe. Hivyo ni dhahiri kuwa utumiaji wa pombe, bila kujali kiasi kitakacho nywewa, inaathiri hisia zetu. Zaidi ya hayo, jambo lingine ni kwamba Allah swt anaelewa vyema kabisa maumbile ya mwanandamu na mapenzi ya viumbe vyake vya kupindukia kiasi. Kwa hivyo, kama Yeye angalikuwa ameruhusu kutumia pombe kwa kiasi chochote kile, basi kwa kuwekea kiasi kungezua matatizo makubwa. Kwa hivyo, ili kumwokoa mwanadamu kutokana na maafa na madhara ya pombe ambavyo ni kinyume na kuishi kwake, Allah swt ameharamisha pombe hata kwa chembe kidogo.”

Arshe Tung akasema:

Kwa zaidi ya miaka kumi, uratibu na uendeshaji wa shughuli hizi za vita dhidi ya ulevi humu duniani umekuwa chini ya usimamizi wangu, na katika kipindi hiki mimi nimekuwa na mahojiano mbalimbali marefu pamoja na shakhsiyah maarufu juu ya dini, siasa au masuala ya kijamii. Lakini ni lazima nikiri kuwa hakuna hata mmoja wao ambaye ameweza kutoa hoja zilizo nzuri, nzito na ziendazo sambamba na maisha yetu kama ulivyoweza wewe, na nafikiri kuwa mahojiano nawe ni bora kabisa katika vita dhidi ya ulevi dumu duniani, na kwa kifupi, ili kuweza kufanikiwa katika mapambano haya inatubidi kufuata mafundisho yaliyotolewa na viongozi wa dini ya Islam. Kwa jina langu binafu na kwa majina ya mashirika yote yapiganayo vita dhidi ya ulevi humu duniani, mimi napenda kutoa shukurani kwako wewe ewe mtakatifu, na kwa ushirikiano pamoja na uongozi wako sisi tutafanikiwa katika vita vyetu hivi vitukufu.”

Bentham, Mwingereza, anaandika katika kitabu chake kiitwacho ‘principles of ordinance’ : “Mowapo ya mafanikio makubwa kabisa ya Mtume Muhammad s.a.w.w. katika dini ya Islam ni kule kuharamisha ulevi wa kila aina.”

Mwandishi na msafiri mashuhuri wa Kifaransa, Pierre Loti anaandika : “Mimi niko tayari kabisa kujiunga na sifa za Waislamu kwani mimi kamwe sijawahi kugusa pombe wala ulevi wa aina yoyote ile.”

Kikundi cha Maqureish kilichokuwa kimekaa katika Msikiti wa Makkah, alipoingia al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. basi mmoja alimnyoshea kidole Imam a.s. na kusema : “Mtu huyu ndiye kiongozi wa watu wa Iraq.” Wao wakasema: “Basi aende mmoja wetu akamwulize swali.” Na hapo akainuka kijana mmoja na kwa kumkaribia Imam a.s. alimwuliza : “Je ni dhambi gani lililo kuwa kubwa kuliko madhambi makubwa mengineyo ?”

Al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. alimjibu : “Utumiaji wa ulevi.” Kwa hayo kijana huyo alirejea na kuwaelezea wenzake kuhusu swali lake na jibu alilopewa. Hao marafiki zake wakamwambia kuwa arudi tena kwa mara ya pili na kurudia swali lake hilo hilo. Naye alifanya vivyo hivyo alivyoelezwa na marafiki zake, na kwa hayo al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. alimjibu : “Kama nilivyokuwa nimekuambia kuwa dhambi kubwa kabisa kati ya madhambi makuu (ghunahan-i-kabira ) ni kunywa kileweshacho.”

Kwa kuyasikia hayo kijana huyo alirudi kwa wenzake, na kuwaelezea kilichotokea. Wao kwa mara nyingine walimsisitiza kuwa arudi kwa al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. kwa mara ya tatu na kulirudia swali hilo hilo. Naye alifanya vivyo hivyo, na kwa mara nyingine tena, Imam a.s. alimjibu kwa furaha : “Ni kunywa pombe na vileweshavyo kwa sababu pombe humburuta mtu kuzini, mauaji na madhambi ya kila aina.”

Mtu mmoja alimwijia al-Imam as- Sadique a.s., Imam wa sita, na kumwuliza : “Je ni kwa nini Allah swt ameharamisha ulevi ambapo ladha na starehe yake inazidi kuliko starehe zote ?”

Imam Ja’afer as- Sadique a.s. alimjibu : “ Allah swt ameharamisha ulevi kwa sababu hiyo ndiyo mama wa maasi na madhambi yote, na ndicho chanzo cha maovu na maasi yote. Mlevi hupoteza fahamu zake zote, huwa hamtambui Allah swt, hutenda kila aina ya dhambi awezalo, huwakashifu watu, huvunja uhusiano wake pamoja na watu, ndugu na jamaa zake na huwa amechafuka na si msafi kiroho wala kimwili. Mlevi huwa yupo chini ya amri za Shaitani, na iwapo Shaitani atamwamrisha kusujudia sanamu, basi huyo bila upingamizi atafanya hivyo na hivyo Shaitani anaweza kumburuta katika upande wowote ule autakao katika maasi.”

Kabla ya kuja kwa Islam na mwanzoni mwa Utume wa Mtume Muhammad s.a.w.w. , uzalishaji na biashara ya ulevi wa kila aina ulikuwa umeshamiri na ndio miongoni mwa biashara muhimu ya Waarabu, hivyo neno biashara lilikuwa likimaanisha biashara ya ulevi wa kila aina na vile vile neno mfanyabiashara lilikuwa likimaanisha muuzaji na msambazaji wa ulevi wa kila aina.

Baada ya kuja kwa Islam na kuenea kwa vuguvugu la ukombozi, watu walielezwa mafundisho moja baada ya nyingine, ama ulevi ambao ulikuwa umeleta madhara na maangamizo makubwa kwa jamii, uliharamishwa moja kwa moja.

Kwa hakika uharamisho huo wa ulevi ulileta matunda mema katika jamii katika kipindi kifupi sana na hatimaye mizizi yake iling’oka kimoja. Islam haikuharamisha tu unywaji wa ulevi, bali uliharamisha uzalishaji na uuzaji kwa ujumla shughuli zote ziliharamishwa zinazohusiana na ulevi kwa njia moja au nyingine.

Mtume Muhammad s.a.w.w. alilaani vikali makundi ya wafanya biashara ya ulevi wa aina yoyote au zinazohusiana nazo vyovyote vile ya kwa kutaja baadhi yao :

Mtu apandaye mti wa kutengenezea ulevi kwa nia ya kutengeneza ulevi wa aina yoyote ile,

Mtu anayesaga zabibu kwa ajili ya kutengeneza pombe,

Muuzaji wa ulevi

Mnunuzi wa ulevi

Mnywaji wa ulevi

Mshikaji wa kikombe cha ulevi.

Mtu yeyote anayefaidika kwa njia yoyote ile kwa kutokana na biashara ya ulevi wa aina yoyote ile.

Amesema al-Imam as- Sadique a.s. : “Msijumuike wala kushirikiana pamoja na wazabuni wa ulevi kwani iwapo wataangukiwa na adhabu za Allah swt, wale wote walioko katika jumuiko hilo, watashirikishwa humo.”

Wanasharia wa Islam, ambao walikuwa wakijua madhara maovu yatokanayo na ulevi kwa ajili ya watu, watoto wao na jamii zao, waliharamisha hata kutumiwa kwa kiasi kidodo na uzalishaji wake, usambazaji na biashara yake kwa ajili ya Waislam, kwa sababu unywaji wa ulevi kwa upande wa wazazi unaathiri mfuko wa uzazi na watoto waliokuwamo tumboni na hivyo kuzaa watoto walio dhaifu na wenye kasoro na hatimaye wakawa waovu na wabaya.

Ama swala la kuoa, Amesema al-Imam as- Sadique a.s. :

“Yeyote atakayemwoza binti yake kwa mlevi wa ulevi basi kwa hakika amevunja uhusiano wake pamoja na binti yake.”

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema :

“Baada ya Allah swt kuharamisha ulevi wa kila aina, na iwapo atatokea mtu akanywa, na akileta posa kwa watoto wenu basii musiwaoze binti zenu na iwapo watawatetea watu, basi utetezi wao usikubalike, na iwapo atatoa taarifa yoyote, basi maneno yake yasithibitishwe kuwa ndiyo sahihi. Wala mtu yoyote asiwaheshimu wala kuwa amini na wasipewe kitu chochote kwa misingi ya uaminifu. Iwapo mtu atakuwa akijua kuwa fulani ni mlevi na akampa kitu kwa uaminifu, basi Allah swt hatachukua dhamana la kuhifadhi uaminifu huo na iwapo kitu kilichotolewa katika uaminifu kikaja kupotea, basi Allah swt hatamfidia na hataijali.”

Yapo mapokezi mengi mno kuhusiana na swala hili kutokea kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. na Maimamu a.s. na hasa yanazungumzia kuumbika umbile katika tumbo katika hali ya ulevi kwani ni hatari kabisa.

Amesema al-Imam as- Sadique a.s. :

“Mwanamke anayejisalimisha kwa mume wake aliye mlevi, anatenda madhambi mengi kama zilivyo nyota angani, na vizazi vya wazazi kama hawa huwa ni chafu na maovu. Allah swt kamwe hatakubali tawba au malipo yoyote ya mwanamke huyo hadi hapo mume wake atakapokufa au yeye atakapochukua talaqa na kuivunja ndoa yake.”

Wanazuoni mashuhuri hawaonyeshi shaka ya aina yoyote katika kuelezea madhara ya ulevi katika umbile la mwanadamu humo tumboni mwa mama yake, na utafiti wa kisayansi umethibitisha jambo hili, kwani watoto wanaozaliwa katika mazingira kama haya huwa taathira na walemavu wa matatizo ya kiakili isiyotibika.

Pamoja na nyongeza kwa yale yaliyofanyiwa utafiti na wanasayansi wa Mashariki na Magharibi, uzoefu pia umethibitisha kuwa vizazi vya wazazi walevi huwa na udhaifu na wenye kuathirika vibaya kuliko watoto wa wazazi wasio walevi.

Hakuna shaka, kuzungukwa na ujinga, upumbavu na mnywaji sana wa ulevi kuna kuwa na athari mbaya katika kuumbika kwa watoto, na watoto wanaozaliwa na wazazi wenye kasoro kama hizo basi nao pia huwa wanakasoro na wenye shida kubwa. Kwa misingi hii, Islam ndiyo maana inapiga marufuku kwa wasuasi wake na kuwaonya na kuwatahadharisha dhidi ya maungano yaliyo mabaya na yasiyo tohara, ili kunusuru vizazi vinavyokuja ziwe salama na madhubuti bila kasoro za aina zozote.

Leo hii wanazuoni wengi wanatilia mkazo swala hili na kusisitiza kuepukana na ndoa kama hizi. Katika baadhi ya nchi za Marekani, kumewekwa hata baadhi za sheria za kuziweka vizazi hivi vya sasa katika hali safi, na kwa mujibu wa sheria hizi, wale wavulana na wasichana wanaotumbukia katika magonjwa yanayotokana na ulevi wa kupindukia, huondolewa uwezo wa kuzaa.

Hatari nyingine inayowakumba hawa walevi ni kule akili na seli za fahamu zao huharibiwa vibaya kabisa na huweza kupatwa magonjwa ya kila aina.

Profesa mmoja kutoka Chuo kikuu cha Teheran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anasema : “Ulevi ni aina mojawapo na mihadarati ambayo inayodhuru mishipa ya fahamu. Inadhuru seli za bongo na kusababisha ukichaa na kuwehuka kwa mtu.”

Katika kutoa maelezo ya Ayah ya Quran isemayo; Ewe Muhammad, wanakuuliza juu ya ulevi …, basi ieripotiwa kutoka kwa daktari mmoja wa Kijerumani akiiambia serikali yake na watu wake kuwa : “fungeni nusu ya milango ya madanguro ya pombe na ulevi na hapo ninachukulia dhamana kuwa nchi yetu haitazihitaji nusu ya mahospitali na magereza yatafungwa.”

Katika mapokezi ya Kiislamu, sababu kuu ya kuharamishwa kwa unywaji wa ulevi wa kila aina ni kwa sababu ya athari zake mbaya mno katika ubongo na maisha ya mwanadamu kwa ujumla.

Amesema al-Imam ‘Ali ar-Ridha a.s. “Allah swt ameharamisha ulevi wa kila aina kwa sababu ya maovu yasababishwayo nayo na kwa sababu huharibu ufahamu na busara za mwanadamu na huondoa uwema na heshima.”

Amesema al-Imam Zayn-al-‘Aabediin a.s.: “Madhambi yanayoteketeza uwezo wa mtu kujizuia kutenda madhambi (yaani uwezo wa fahamu na utukufu) na huvunja mishikamano inayohifadhi hayo, yanatokana na unywaji wa ulevi na uchezaji wa kamari.

Mwanasaikolojia mashuhuri anasema: “Ulevi unatokomeza uwema na utukufu, unachana chana pazia la utukufu, unamtoa mtu kutoka mishikamano ya kijamii, kidini na kimaadili na mipaka ya wema wa kila aina. Hatua ya kwanza iliyochukuliwa zaidi ya utukufu ni hasa wakati wa ulevi, kwani kwa kunywea, fahamu na uwezo wa mwanadamu kujitambua huondoka na katika hali kama hiyo ya ukosenaji wa hivyo basi utukufu hupoteza maana yake. Vijana wa kiume na kike wanapokuwa wamepotoka, basi ndio huwa watu wa kwanza kuingia katika mtego wa utumiaji ulevi na vyote vinavyolewesha, hupotea katika maisha yao na kuangukia katika jangwa la upotofu. Na huwa ndiyo kumaanisha kuwa maisha yao yameharibika na kupotea na kudhalilika.”

Tolstoi anasema: “Watu wanaelewa vyema mambo ya ulevi na hunyonga miito ya fahamu zao, na hii ndiyo maana wao hutumia ulevi.”

Mtu awapo katika fahamu zake timamu huwa hayupo tayari kutenda matendo yanayoaibisha na kufedhehesha au kutamka matusi na kutenda kinyama lakini anapokuwa amelewa basi huweza kutenda tendo la aina yoyote ile au makosa ya aina yoyote yale. Hata anaweza kuzini pamoja na mama au mtoto wake ! Loh hii ndiyo laana kubwa ya kunywa mkojo wa firauni kama unavyojulikana.

Dr. Alexis Karl anasema : “ Kumomonyoka kwa ufahamu na uwezo wa akili ya kawaida unatokana na utumiaji wa ulevi na tabia za kupindukia na kuharibika kwa tabia. Bila shaka, kuna mshikamano baina ya kiwango cha utumiaji wa ulevi na kuharibika kwa akili za jamii.

Miongoni mwa nchi ambazo zinazokaribisha kazi za kisayansi, Wafaransa ndio watumiaji wakubwa wa ulevi, na hivyo hushinda kidogo tuzo za Nobeli.”

Takwimu zifuatazo zitatushtusha kuona na kupima uharibifu wa ulevi : Andre Minu, katibu wa kongamano la kimataifa la Kupigana Vita dhidi ya Ulevi, anaelezea : “ Asilimia themanini ya wenda wazimu na asilimia arobaini ya wenye kuathirika magonjwa ya zinaa, yanatokana na utumiaji wa ulevi. Miongoni mwa watoto, asilimia sitini ya wapumbavu na asilimia arobaini ya wenye hatia wametokana na familia zinazotumia ulevi.

Maafa yaliyoathiri jamii za kibinadamu kwa kutokana na utumiaji wa ulevi ni mkubwa kuliko hata majeraha na upoteaji kwa kutokana na magonjwa hatari.

Kwa mujibu wa wanasayansi waliobobea, utumiaji wa ulevi huleta magonjwa mabaya kabisa ya kansa ya matumbo na maini, magonjwa ya matumbo, neumonia, kifua kikuu, magonjwa ya akili kama vile kichaa n.k., na kuharibu vizazi kwa kuathiri maumbo kuanzia tumboni na mamilioni ya maovu yanayotokana na ulevi.

Maafa mengine yanayoyakumba jamii za watu kwa kutumiwa ulevi ni ajali za magari yanayosababishwa na madereva walevi ambao pamoja na maisha yao hupoteza maisha ya watu wengi. Utasikia deveva mmoja mlevi husababisha ajali hata ya kufikia abiria kumi, au ishirini au mamia. Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, imeonyesha kuwa mlevi hupoteza fahamu na uwezo wake wa kuona hudhoofika, na uwezo wa kuwa makini na hisia za kuhisi hatari yanakuwa yemerejea nyuma na hivyo hawezi kudhibiti hali inayotokea ya hatari. Hivyo mtu awapo katika hali kama hiyo, hutawaliwa na majivuno na hupenda kujiona kuwa yeye ndiye sawasawa kuliko watu wengine na hivyo huzua vurugu na mara nyingi huishia katika maafa makubwa kama vile kupiga au kupigwa, kuua au kuuawa, kuharibu mali zake au za wengine na hivyo kutumbukia katika makesi na chuki zisizoisha. Na wengine utawasikia kuwa akiwa katika ulevi, alikula hata mavi na alilalapo mitaroni, n.k. na vituko kama hivyo tunavisikia, tunavisoma na kujionea macho katika magazeti, radion na hata katika televisheni au kwa macho yetu. Ulevi unapokuwa umeteremka, utamwona huyo huyo mtu anajuta kwa kile kilichokuwa kimetokea wakati akiwa amelewa.

Kama vile serikali ya Baraza la Usalama la Marekani ilivyokubali kuwa robo ya vifo vya ajali za barabarani zitokeazo ni kwa uendeshaji wa magari, hutokana na madereva kuwa walevi.

Leograin asema : “Kati ya kesi 761 za watumiaji wa ulevi, 322 wamezaliwa wakiwa na kasoro, 155 vichaa na 131 wanauwezo wa kupatwa na kasoro nyingi za aina mbalimbali.” Asilimia zipatazo thelathini hadi arobaini za kesi za wenye kasoro za akili ni wale walevi kupindukia. Wale waliokunywa sumu kwa kutokana na ulevi huko Iran katika mwaka 1965 ( kabla ya mapinduzi ya Kiislamu ! ) ilikuwa 1875. Ulevi ndio sababu kuu za madhambi. Zinasababisha asilimia 75 za mauaji, kesi asilimia 38 za vurugu na madhambi na asilimia 82 za utumiaji wa silaha na mauaji. Na yote hayo yanatokana na utumiaji wa ulevi.

Kwa kuyaona maafa kama haya yakiangamiza wanaadamu na kuwatumbukiza katika maangamizo, Dini tukufu ya Islam imezuia chanzo hicho cha maangamizo, na kwa kuchukua hatua ya tahadhari kwa kuwadhibiti. Islam inasema : “Msikae katika meza moja ambapo ulevi unatumiwa na wengineo. Wala msihudhurie hafla ambapo hata kama wewe haunywi. Wala musifanye uhusiano pamoja na walevi, isije ikatokea kuwa nyinyi mukaambukizwa na tabia hiyo. “

Ofisa mmoja katika jeshi la Mansur, Khalifa wa ‘Abbasi, alipanga hafla ya kusherehekea kuwekwa sunna mtoto wake huko Heyra ambamo aliwaalika watu mbalimbali waliokuwa wakiheshimika akiwemo Imam as- Sadique a.s. , Imam wa sita. Wakati waalikwa walipokuwa mashughuli katika kula juu ya meza, mmoja wao aliomba apatiwe maji ya kunywa. Hapo mhudumu alimkaribisha kikombe cha pombe badala ya maji. Punde pombe ilipoletwa tu juu ya meza, Imam as- Sadique a.s. aliinuka na kuondoka hapo. Mwenye hafla alipomwona Imam a.s. akiondoka alimwuliza sababu, na Imam a.s. alimjibu :

“Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. : ‘Yeyote yule atakaye keti juu ya meza ambapo wengine wanalewa, basi amelaaniwa.”

Ndugu msomaji, je umeona tofauti ya Makhalifa waliojipachika kwa kimabavu na wale waliochaguliwa na Allah swt kuwa Makhalifa halisi ? Huyu Khalifa Mansur ambaye alekalia kiti cha Ukhalifa anafanya hafla ambamo pombe inatumika. Je Huyu alikuwa khalifa wa Ummah wa Mtume Muhammad s.a.w.w. au kiongozi wa kisiasa na utawala ?

Imam as- Sadique a.s. ambaye kwa hakika ndiye Khalifa halisi aliyechaguliwa na Allah swyt kwa kupitia Mtume Muhammad s.a.w.w. ameonyesha wazi vile anavyoijali dini ya Islam na kuifuata vile ipasavyo kwani hakuvumilia hata kukaa na kuangalia uvunjwaji wa Shariah za Dini zikitendeka.

Kwa ziada ya yale yaliyosemwa, historia kwa mukhtasari imetuonyesha kuwa ulevi umeangamiza mataifa na kuteketeza tawala. Historia inaendelea kutuambia kuhusu familia ya Barmak, pamoja na utajiri na kuwa katika utawala, umekumbwa na makucha ya ulevi na vileweshavyo. Iwapo Ja’afar Barmaki hakuwa amelewa, na iwapo angalikuwa hakupoteza fahamu zake kwa kutokana na kulewa , basi tukio la Abbasa, bintiye Rashid, bila shaka kusingalitokea, na hivyo Barmaki wasingaliuawa. Ingawaje Barmaki wamekumbana na hali hiyo iliyo mbaya sana ni kwa sababu zilizochangia kwani yeye alikuwa mshiriki katika mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad s.a.w.w. aliyeitwa Al-Imam Musa al-Kadhim a.s. na hasa wakati Ja’afar alipoanza kuwa mlevi.

Historia inatuambia kuwa utawala wa Jalal-i-Din Kharazmshah ulifikia ukingoni kwa kuanguka kwa kutokana ulevi na maovu ya kijamii na yeye alikipoteza kichwa na kiti cha ufalme wake kwa ajili ya ulevi. Kwa hakika huyo alikuwa ni mfalme hodari ambaye aliwashinda Wamongoli, kwa miaka mingi na kumtesa Chengiz na jeshi lake la kivita, lakini hatima yake imekuwa mfungwa wa ulevi uliomwangamiza. Katika siku zile alizokuwa mfalme mashughuli sana katika kunywa ulevi na maovu, alitumia masaa mengi mno katika kunywa na na kusahau yote, katibu wake makhsusi , Nurdin Zaydari alikuwa akisoma mashairi yafuatayo: “Ewe Mfalme ! Je pombe iliyo kali itakuzalishia nini ? Mfalme amelewa chakachaka, uhakika umetokomezwa, na maadui wapo wametapakaa kila mahala.”

Ni dhahiri kile kitakachozaliwa katika sura kama hii kwani Mfalme pamoja wanabaraza wake wote hawakuyajali maneno aliyokuwa akiyasema huyo ya kuwaonya na kuwatahadharisha, kwa sababu wote walikuwa walevi wa kupindukia. Usiku wa manane ulipowadia, Wamongoli walifanya hujuma za ghafla kama vile ilikuwa ni adhabu kali kutokea mbingunu na walifanikiwa kumzingira mfalme na mahema yaliokuwamo ndani. Mmoja wa washiriki wake aliyekuwa amepata habari za hujuma hiyo alikimbia hadi katika baraza la kifalme na kwa jitihada kubwa sana alifanikiwa kumwamsha kutoka usingizi wa ulevi wake na kumjulisha juu ya kile kilichokuwa kikitokea. Mfalme alijisikia mdhaifu kiasi kwamba hata hakuweza kumpanda farasi wake kutokana na kulewa kwake topu. Ili kutaka kumzindua, huyo bwana alimrushia maji baridi usoni mwake, lakini nayo hayakufua dafu kwani kulikuwa kumeshacheleweshwa isipokuwa yeye mwenyewe alikimbia kuinusuru nafsi yake. Yeye aliwakimbia Wamongoli akini mbeleni aliuawa na nani haijulikani na akauchukua mkoba na farasi wake hadi milima ya Kurdistan.

Historia inatuambia kuwa utawala wa Kisafawi uliteketea kwa sababu ya Shah Tahmaseb alikuwa na tabia ya kulewa.

Hayo yote yaliyozungumzwa hadi hapa yanazungumzia maovu yatokanayo na ulevi ikiwemo hasara kubwa ya kimaumbile na kiakili ya watu binafsi au jamii nzima, hatari za kimapato na hasara zake n.k. katika dunia hii tunamoishi.

Ama wale ambao wana imani juu ya Tawhidi na wanaamini katika maisha ya awali na ya Aakherah, swala zima la ulevi una sura nyingine pia, yaani athari za ulevi katika Aakherah.

Ni lazima tuweke mikakati madhubuti swala hili la ulevi kwani mtu anaweza kujitumbukiza katika unywaji na utumiaji wa ulevi kwa ajili ya raha inayodumu kwa muda mfupi huku akijiangamiza na kujiteketeza mwenyewe bila ya yeye kuyajua hayo yote. Lakini Islam haitaki kamwe Muislamu akumbwe na balaa na laana hii ya maangamizo kwa mikono yake mwenyewe. Bali inamtaka atende mema na kuyatengeneza maisha yake ya Aakherah yawe mema.

Al-Imam Muhammad al-Baquir a.s. amesema : “Mnywaji na mtumiaji wa ulevi ni kama kafiri anayeabudu sanamu, kamwe hataruhusiwa kutokezea mbele ya uadilifu wa Allah swt.”

Vile vile Amesema al-Imam as- Sadique a.s. : “Allah swt amewaharamishia Peponi watu wa aina tatu : wa kwanza, wanywaji na watumiaaji wa ulevi…”

MASUALA MCHANGANYIKO

Serikali nyingi hujipatia mapato makubwa sana kutokana na makampuni yanayoendesha biashara za kutengeneza pombe na ulevi kwa ujumla. Na hivyyo huridhika kushamiri kwa biashara hii, lakini hawajiulizi kuwa ummah wao unatokomea na kuangamia katika ulevi huu. Utawasikia wakipiga makelele kuwa watu wanalewa sana na hivyo hawafanyi kazi iwapasavyo huko mashambani na maofisini, sasa jee ulevi unaotengenezwa ni kwa ajili ya raia gani si hawa hawa ambao sasa wanakuwa na tabia ya kulewa kwa kupindukia.

Nchi inaendelea kuwa masikini kwa sababu hakuna uzalishaji mashambani wala viwandani kwa sababu wote wameingia katika ulevi. Akili zao hazifanyi kazi sawasawa.

Hata katika hafla zao za kiserikali utawaona wakinywa ulevi wa kila aina, sasa jee hawa watu na viongozi wakubwa wa idara mbalimbali za Serikali na taasisi wamekutana kuongea kama watu wenye fahamu kamili au wakishapiga chupa moja mbili ndipo wanaweza kuzungumza ?

Ukiwa mahakamani katika kesi au unapotakiwa kufanywa operesheni au unapotakiwa kuendesha gari au ndege na iwapo utagundulikana kuwa umelewa basi kesi yako itaahirishwa kwani watasema ‘amelewa’ kesi yake itasikilizwa pale atakapokuwa na fahamu kamili, na vivyo hivyo ndivyo kwa masuala mengine. Sasa jee itawezekanaje watu wakalewa hata kwa kiasi kidogo na ndipo waweze kuzungumza ya maana ?

Na mapesa mengi yanayopatikana kwa kufanywa biashara ya kutengeneza na kuuza na kusambaza ulevi nchini kote, hebu wataalamu wakae na kupiga mahisabu kuhusu kipato kinachopatikana na kiwango kinachotumika katika kukabiliana na waovu na maovu ya ulevi : watu wanaangamia kwa kasi, ajali za barabarani n.k., uzembe kazini na mashambani. Watu wanakuwa wamedhoofika kiakili na kimwili.

Pombe ni sumu na hivyo hakuna mtu yeyote atakayesema kuwa sumu kwa kiwango kidogo hakidhuru.

Kwa kutumia Whisky kama ndicho kizuiacho unywaji ni sawa na kutaka kuuzima moto kwa mafuta ya taa.

Serikali zote duniani zinatakiwa kupiga vita na kulaani ulevi kwani ndiyo hatua ya kwanza katika kuingia katika mihadarati, uasherati na zinaa.

Serikali zote duniani zinaposikia kuwa kumezuka ugonjwa mbaya unaoangamiza maisha wa raia wake, basi hutangaza vita dhidi ya ugonjwa huo lakini jambo la kusikitisha tunaona kuwa serikali hizo zimekaa kimya na havitangazi vita dhidi ya kamari na ulevi. Na badala yake zinafurahishwa na mapato yatokanayo na viwanda hivyo. Kila mapato yanvyozidi ndivyo waelewe kuwa raia wao wanaangamia na kuteketea kwa baraka za serikali zao.

Iwapo serikali za humu duniani zitapiga marufuku ulevi basi wataweza kubakiza mapesa yao ambayo yanatumika kupita kiasi katika mahospitali, magereza na nyumba za kulea vichaa.

Imeripotiwa na Al-Kulaini kwa mamlaka ya Ja’abir kuwa siku moja katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, mshairi Najjashi aliletwa mbele ya Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. kwa mashitaka ya kuwa mlevi na baada ya uchunguzi ilithibitika kuwa yeye kwa kweli alikuwa amelewa. Hapo Imam a.s. alitoa hukumu kuwa achapwe viboko themanini. Na adhabu hiyo ilitekelezwa.

Siku ya pili, Najjashi alichapwa viboko vingine ishirini. Na alipouliza iwapo Qur’an inaamrisha viboko themanini tu sasa hizo ishirini za nyongeza zilikuwa za nini. Alijibiwa kuwa hizo zilikuwa ni kwa sababu ya kutouheshimu utukufu wa Mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. : “Chochote kile kileweshacho kinaingia katika jina la khamr na hivyo ni haramu kukitumia.”

“Ulevi ni mama wa maasi yote”

ENYI WAISLAMU NI WAJIBU WETU KUJIEPUSHA KILA KITU KILICHO KIBAYA NA MADHARA KWA MIILI NA AKILI NA AFYA YETU. TUSIJIHARIBU KWANI TUNAWAJIBU WA KULEA VIZAZI VYETU VIWE WEMA NA VYENYE KULETA SIFA NA HESHIMA KWA MAJINA YETU NA WALA WASITUAIBISHE.

HIVYO TUWE WAISLAMU WA KWELI NA SAFI.

TUPIGE VITA MAOVU YOTE NA WALA TUSISHIRIKI KWANI TUTAHARIBU AAKHERA YETU AMBAYO NDIYO MAISHA YETU YA KUISHI MILELE.

KAMA TULIKUWA TUKITENDA MAOVU BASI TUFANYE TAWBA NA TUSIRUDIE KUTENDA TENA….