rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

34. KATIKA TAWBA ULIMI NDIYO MFASIRI WA MOYO.

Katika TAWBA, kama tulivyokwisha elezea hapo awali kuwa kitu cha lazima ni kusikitika na kuhuzunika kwa mtu, vile vile kujuta kwa moyo wake wote pamoja na kunuia kwake kuacha madhambi hayo na yote mengineyo. Na katika hisia hizo nzito atamke maneno mazito ya kuomba msamaha wa Allah swt na kusema: 'Astaghfirullah Rabbi wa atubu Ilayhi.'

TAWBA haiwezi kuwa TAWBA iwapo itatamkwa mdomoni tu bila ya kuwapo kwa hisia za moyoni. Hivyo inatubidi tuuelekeze ulimi wetu katika TAWBA baada ya kujengwa kwa hisia za moyoni kwani ulimi ndio utakao fasiri yaliyo moyoni mwetu. Ndipo hapo TAWBA yetu itakuwa ni sahihi.

Mfano, ninajuta na kusikitika kwa kusema matusi na maneno machafu moyoni mwangu, lakini ulimi wangu bado unaendelea na kuyasema hayo hayo. Basi katika hali kama hii, ulimi haujawa mfasiri wa moyo wangu. Utakuwa mfasiri pale utakapoacha kuyasema maneno hayo na mengineyo pia.

Hivyo tuombe Tawfiki ya kujaaliwa ulimi wetu uwe mfasiri wa moyo wetu ili kutukamilishia TAWBA kimoyo na kimatendo. Vile vile juhudi zetu pia zinahitajika, katika kujielekeza huko.

Ipo hadithi Tukufu isemayo:

"Adda'i bila Aamal kar-raami bila watr" Yaani:

Mwombaji bila matendo ni sawa na upinde bila kamba yake, au mti bila matunda, au mto bila maji.

Sasa tujiulize iwapo tutaomba tu bila kujitahidi wenyewe itakuwaje?

35. KUIACHA TAWBA NA KUENDELEA NA MADHAMBI.

Imam Muhammad al-Baqir a.s. anaielezea 'kugang'ania hivi; katika Usuli Kafi:

"Iwapo mtu mmoja amefanya madhambi na wala yeye hanuii kuyaacha kabisa na wala hafikirii swala la kufanya TAWBA, basi kwa sababu hiyo itakuwa ni mazoea yake ya kutenda madhambu na hakutakuwa dawa nyingineyo yenye kuponya tabia yake hiyo ila TAWBA tu."

Maulamaa wengi wanaafikiana kuwa ni lazima kufanywa TAWBA papo hapo pale mtu anapotenda dhambi. Sheikh Bahi A.R. anasema kuwa mtu anazidi kujitwisha mzigo wa madhambi kila acheleweshavyo TAWBA kwani hiyo ni faradhi mojawapo na anastahiki kupewa adhabu kamili. Iwapo atafanya TAWBA kwa haraka basi atakuwa mustahiki wa rehema za Allah swt.

Ipo riwaya isemayo kuwa wakati mja anapotenda madhambi na kufanya TAWBA na tena akarejea kutenda madhambi na tena kutubu na kwa mara ya tatu tena akarejea kutenda madhambi na kutubu, basi hapo Allah swt anawaambia Malaika: "Enyi Malaika wangu! Angalieni vile mja wangu asivyoiacha nyumba yangu kwani yeye anatambua kuwa hakuna mwingine awezaye kumsaidia ila mimi tu!"

36. TAWBA NDIYO SABABU YA KUSAMEHEWA.

Allah swt anatuambia 'Saabiquu' yaani haraka haraka mtangulie. Je ni wapi huko tena? Basi jibu ni kuelekea kwake Allah swt, hiyo TAWBA inaweza kuwa sababu ya rehema za Allah swt. Faradhi na Sunna zote ni sababu za rehema na Maghfirah za Allah swt. Matendo yote mema ni wasila wa Maghfirah zake Allah swt. Iwapo utauondoa mwiba njiani basi iwe ni kwa ajili ya Allah swt, na ulifanyalo jambo lolote lile, liwe kwa ajili ya Allah swt na yawe yote kwa ajili ya kutaka radhi na maghfirah zake Allah swt.

Katika baadhi ya kazi huwa tunababaika na baadhi huwa tunayo yakini. Lakini TAWBA ni tendo ambalo sisi tunayo yakini ya kutakabaliwa kwake na tukasamehewa madhambi yetu yote papo hapo iwapo tutaifanya kwa masharti na maelezo tuliyoyaelezea hapo awali.

Iwapo ulimdhulumu mtu na unataka msamaha basi lazima kwanza umwombe msamaha huyo mtu na iwapo atakusamehe ndipo hapo ujue kuwa umefaidika kwa kuupata Msamaha wa Allah swt. Allah swt anatuambia katika Qurani Sura al-Baqarah:

Na kuwa nyinyi wenyewe (kwa hiari) musamehe (yote) ni ukaribio kwa ucha Mungu (Taqwa). (2:23)

Msameheni kwa ajili ya Allah swt kwani yeye hupenda sana msamaha!

37. MAZUNGUMZO YA IMAM ZAYNUL AABEDIIN A.S. NA ZAHRA.

Imam Zaynul Aabediin a.s. alikuwa akielekea Makkah na aliliweka hema lake chini ya mlima mmoja ujulikanao kama 'Zahra.' Zahra alikuwa ni hakimu na pia alikuwa mfuasi wa Imam Zaynul Aabediin a.s. na alikuwa akimtembelea mara kwa mara.

Huyo Zahra siku moja alimhukumu mtu mmoja kifungo kwa makosa aliyokuwa ameyatenda, na kwa bahati mbaya huyo mfungwa alifariki akiwa kifungoni. Kutokana na tukio hilo, Zahra alijitoa hapo mjini Madina na kuishi katika mlima huo huu akilia na kujuta mno akiwa amewaacha mke na watoto wake wote.

Imam a.s. aliambiwa, "Zahra amevunjika moyo na kuwehuka na yupo daima akilia tu. Je, utapendelea kuonana naye kwani alikuwa ni miongoni mwa wakupendao wewe? Na Imam a.s. aliwajibu kuwa angelipendelea kumwona na kujua hali yake.

Hapo Imam a.s. alimwendea huyo Zahra mlimani kwa kutaka kumpa mawaidha na hidaya. Zahra alikuwa uchi na katika hali ya kulia tu na alikuwa amedhoofika kabisa.

Riwaya inaendelea kusema kuwa Imam a.s. alimwambia: "Kutotegemea na kutarajia rehema na Maghfrrah za Allah swt kwenyewe ni dhambi mojawapo kuu hata kuliko tendo lako ulilolifanya. Sasa kwa nini hutaki kujitafutia njia ya kupona na hayo."

Hapo Zahra alijikaza na kusema, "Ewe bwana, je kunawezekana kukapatikana njia ya kuniponya na hayo niliyokuwa nimeyatenda kwani mimi nilimwua mtu katika hukumu yangu!"

Hapo Imam a.s. alimwambia: "Nenda kwa jamaa zake uwafidie na kuwaomba msamaha na urejee katika kazi yako hiyo hiyo kwani itakuwa na manufaa kwako humu duniani na akhera pia. Je, humu duniani kuna maumivu yoyote yale yasiyoweza kupatiwa ufumbuzi na matibabu yake? Inambidi kila mtu afanye haraka ya kufanya TAWBA na hii ndiyo njia ya kujipatia msamaha na rehema za Allah swt kwa haraka na urahisi wenye uhakika."

Njooni leo tufanye TAWBA kwa madhambi yote tuliyokwisha tenda na tunuie kutotenda tena madhambi yoyote yale.Tufanye TAWBA leo kwani mauti haina wakati.

38. MADHAMBI NI GIZA WAKATI TAWBA NI NURU.

Allah swt anatuambia katika Qurani:

Mwenyezi Mungu ni mlinzi wa wale walio amini, yeye huwatoa kutoka giza na kuwaingiza katika nuru.....(2:257)

Imam a.s. anasema: "Kuongozwa kunamfanya mtu atolewe kutoka gizani na kuelekezwa penye maghfrah na ambavyo hatimaye TAWBA kamilifu."

Wale ambao wameshapotoka na ambao wanamfuata Taaghuti (sheitani) hutolewa kutoka nuru na kuingizwa katika giza. Hapa muradi (maanisho) ni wale ambao walikuwa katika nuru ya Islam na wakapendana na kiongozi mwovu na mdhalimu (sheitani) basi hao kwa sababu ya mapenzi hayo pamoja na mwovu wametoka kutoka nuru na kuingia katka giza. Basi hapo ndipo Allah swt anawaahidi kuwaingiza katika Jahannam pamoja na makafiri.

Mtu anapoamua kufanya urafiki wa Mwenyezi Mungu basi utamwona daima akijiweka katika hali ya tahadhari kwani utakachomwambia utaona akikuambia kuwa yeye kwanza atalifikiria na kuona iwapo hakuna uvunjaji wa hukumu za Allah swt na vile vile ataangalia maadili. Kwa hakika katika mambo yako mengi wewe utamwona yeye akikuambia kuwa yeye hataweza kushiriki pamoja nawe katika safari, michezo au hata hafla fulani fulani na hata mikutano kwani sababu atakazokuambia wewe utaona kuwa huyu mtu amezidi mipaka ya ucha Mungu na hapo hautasita kumwambia kuwa 'Bwana, mambo haya unayotaka kufafuata ni ya kale, na dunia siku hizi imeshaendelea, hivyo achana navyo!' Lakini yeye hatatingisika katika uamuzi wake kwani yeye anataka ridhaa ya Allah swt! Na vinginevyo atakushauri wewe uyaache hayo kwani hayana faida kimaadili.

Lakini yule aliyejitakia urafiki wa Sheitani, mambo ni kinyume kabisa na hayo ya juu. Huyu hata bila ya kumwambia chochote utaona akibuni mambo ya kiajabu ajabu, mara hebu twende tukajaribu bangi, pombe, mihadarati, mabibi na maovu ya aina yote. Na wewe iwapo utajaribu kumpinga basi utaona akikulaumu na hatimaye ataweza kukushawishi kwa njia mbalimbali kwani atakuambia,"Basi twende pamoja, lakini wewe usifanye lolote lile" au mara nyingine "Twende lakini utajaribu kidogo tu na iwapo utaona haupendelei kuendelea, basi tutaacha na tutarudi........" Na hapo utaona kweli hebu niende na nitarudi iwapo sitapendezewa, lakini ukifika huko utaona akikugeuka na kukuambia ngojea kidogo tu, sasa hivi tutakwenda hebu jaribu kidogo............

Hii ndiyo tofauti kati ya nuru na giza, urafiki wa Allah swt na sheitani!

39. MADHAMBI YOTE YANAWEZA KUSAMEHEWA.

Katika Qurani Tukufu zipo aya nyingi mno na vile vile zipo hadithi ambazo zinazungumzia ukubaliaji wa TAWBA na vile vile zielezeazo kuwa madhambi yote yanaweza kusamehewa. Katika Qurani Allah swt anajisifu kuwa yeye ndiye Msamehevu na mwenye kuzikubalia TAWBA na vile vile anajiita katika Qurani kwamajina tofauti tofauti: Tawwab, Ghaffar, Ghafirudh-Dhunuub..........

Allah swt anawaita wale wote wafanyao madhambi wajirudi na kufanya TAWBA mara moja kabla hawajakumbana na adhabu zake zilizo kali kabisa. Suluhisho la daima la kuvunjika moyo, katika Sura az-Zumar:

Sema ("Ewe Mtume Muhammad!): "Enyi waja wangu! Ambao mumezibadhirisha nafsi zenu, msikate tamaa ya rehema za Mwenyezi Mungu, kwa hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote kwa pamoja, hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe, mwingi wa Kurehemu. (39:53)

Katika Aya hii Allah swt anawaita waja wake "Enyi waja wangu' na wala hakuwaita 'Enyi mlio asi' au 'Enyi wenye madhambi!' Na vile vile ametuusia sisi tusikate tamaa na kujidhulumu na badala yake anatupatia mawaidha ya kumrejea yeye ili aturehemu na kutusamehea.

Hivyo sisi tushikamane na imani yetu kwa Allah swt kwa maombi yetu na misaada yetu kwani ni yeye pekee awezaye kutusahilishia matatizo yetu. Yeye tu ndiye Tumaini letu.

40. TAWBA YA MAUAJI.

Iwapo mwuaji anataka kufanya TAWBA, basi inambidi kwanza ajisalimishe mbele ya warithi wa marehemu aliyeuawa na hapo ni shauri lao wao iwapo watatekeleza kisasi au watadai fidia au watamsamehe.

Iwapo mtu ataua kwa makosa au kwa kumdhania mtu kimakosa basi ni lazima kwake yeye kulipa fidia kwa familia na warithi wake marehemu. Na iwapo wao watamsamehe, basi ni faradhi juu ya muuaji kumfanya huru mtumwa mmoja, kuwalisha masikini sitini na kufunga saumu kwa siku sitini kwa mfululizo. Kama haweza kumfanya huru mtumwa mmoja, basi avitekeleze vilivyobakia.

Maelezo zaidi juu ya maswala kama hayo yanaweza kupatikana katika vitabu vya Fiqhi na Mafuqahaa wanaweza kutoa maelezo zaidi.

Tahadhari: Ni haramu kabisa kujitolea majibu ya maswala katika fiqhi tukisema: 'Kwa kuwa swala hili liko hivi, basi labda au bila shaka jibu lake litakuwa hivi na hivi.....' Hiyo ni Qiyaas, na qiyaas katika fiqhi ni haramu kwani itakuwa ni uamuzi usiofanyiwa utafiti.

41. TAWBA HUTUEPUSHA NA MOTO WA JAHANNAM.

Imam Jaafer as-Sadique a.s. amenakiliwa riwaya moja katika Usuli Kaafi:

Siku moja Imam Ali ibn Abi Talib a.s. alimtembelea Sahaba mmoja na hapo alitokezea mtu mmoja akisema: "Ya Ali! Mimi nimetenda tendo la aibu pamoja na kijana mmoja (ulawiti), hivyo naomba nitakasike kwa mujibu wa Shariah za Allah swt."

Imam Ali a.s. alimwambia:"Kwa hivi sasa naomba uende zako kwani inawezekana ulitenda tendo hilo kwa ushawishi uliokuwa umekughalibuNa hivyo inawezekana kuwa akili zako hazikuwa timamu na maneno yako yasiwe yenye fahamu au maana yoyote."

Huyo mtu alirijea siku ya pili na kuyasema yale yale tena ya kutaka aadhibiwe.

Kwa mara ya pili, Imam Ali a.s. "alimwambia kuwa labda ulitenda katika hali ya ghadhabu ambayo ilikughlibu."

Aliporudia mara ya nne, Imam Ali a.s. alimwambia: "Mtume Mtukufu s.a.w.w. alitoa hukumu tatu katika sura kama hii, hivyo uchague mojawapo unayoipenda: (1) mikono na miguu yako ifungwe kwa pamoja na wewe utupwe chini kutoka mlimani, (2) Kichwa chako kikatwe kwa upanga na (3) Uchomwe mzima mzima kwa moto."

Hapo huyo mtu akamwuliza Imam Ali a.s..,"Je, ni adhabu ipi iliyo ngumu kati ya hizo tatu?" Na Imam Ali a.s. alimjibu, "Adhabu ya kuchomwa kwa moto." Na hapo huyo mtu alichagua kuchomwa kwa moto. Na alisema kuwa yu tayari kwa hayo.

Baada ya hapo aliondika, akaenda kusali rakaa mbili na akaanza kusema: "Ewe Allah swt! Mimi nilishawishiwa na hisia zangu za kinyama na dhamira yangu ipo ikinilaumu, nami ninaogopa madhambi na hivyo nimejileta mbele ya Mpenzi wa Mtume wako Muhammad s.a.w.w. ili yeye aniadhibu vilivyo kwa makosa yangu. Yeye amenielezea kuwa kuna adhabu tatu, nami, Ewe Allah swt! nimechagua ile ambayo ni ngumu kuliko zinginezo na ni matumaini yangu kuwa wewe U mkarimu na mrehemavu basi utanisamehe madhambi yangu kwa adhabu yangu hiyo ikiwa ni kaffar na utaniepusha na Moto wa Jahannam na ghadhabu zako."

Baada ya hapo alilia mno na kujielekeza katika moto. Miale ya moto yaliongezeka. Hapo Imam Ali a.s. pamoja na Sahaba wake walipoona hali hiyo, walilia mno. Na Imam Ali a.s. alisema: "Ewe mtu! Inuka, wewe umewaliza hata Malaika wa ardhini na mbinguni,yakini TAWBA yako imekubaliwa mbele ya Allah swt!"

Imam Jaafer as-Sadique a.s. amenakiliwa katika Bihar al-Anwaar cha Allamah Majlisi A.R. hivi:

Zipo mashua mbili zikielea majini mojawapo ipo imepakia shehena ya bidhaa na nyingine ipo tupu. Zinakaribia bandari ya nchi fulani na huko wanawakuta Maofisa forodha na kodi wakiwasubiri kupakua na kukisia kodi ya kuwatoza.

Je, mashua ipi itakayopita upesi bila ya kuulizwa maswali mengi na kufanyiwa upekuzi mkali? Bila shaka ni ile mashua isiyo na shehena ya bidhaa.

Mashua yenye shehena ya bidhaa itapekuliwa na kuhojiwa maswali mengi ya kila aina na bila shaka itachukua muda mrefu sana kabla haijaruhusiwa kuendelea na shughuli yake na kufika katika manxili yake. Na hapo watalipizwa kodi kubwa bila shaka na labda kupewa adhabu kali iwapo kutatokea hali isiyo halali.

Vivyo hivyo iwapo mtu atakufa huku akiwa ameshajitakasisha kwa kutimiza wajibu wake TAWBA basi siku ya Kiyama hatakuwa na muda mrefu wa kuhojiwa kwani atakuwa ametimiza wajibu wake humu duniani sala, zaka, khusi, saumu n.k. na vile vile amekuwa akiwatunza ahali yake, hakuwadhulumu wala kuwaonea watu, wazazi wake wamekuwa daima wakiangaliwa naye na kutimiza haki zao vile vile majirani wake na majamaa wake pia wamekuwa wakiangaliwa naye. Yaani kwa ufupi, amekuwa ni mwislamu mwenye kuzingatia maamrisho ya Allah swt wakati akiwa yu hai humu duniani. Basi mtu kama huyo hatakuwa na mengi ya kuulizwa wala shida yoyote katika safari yake hiyo.

Vile vile ipo riwaya nyingineyo isemayo mtu kama huyo atakapoteremshwa kaburini kutakuwa kumejawa na nuru na atakuta kuna msafirishaji wake hapo na katika punde atajikuta yupo Jannati (peponi). Hapo wakazi wa Paradiso watamwuliza "Je, vipi mambo yako ya maswali na majibu yamekwendaje?" Na jee usafiri huu vipi? Basi hapo huyo atajibu: "Huu usafiri ni msikiti ambao nilikuwa nikiupenda mno nilipokuwa duniani na sasa umenifikisha hadi hapa Peponi."

Tuelewe wazi wazi kuwa Maasumiin-min -Allah ni shakhsiyyah wasiyo kuwa na madhambi na vile vile wale ambao watatenda mema na kufanya TAWBA ni sawa na watu wasiopata kutenda madhambi kamwe, hivyo ndivyo isemavyo Quran Tukufu na riwaya mbali mbali.

Na Allah swt amewaahidi watu kama hao: Sura al-Furqaan:

...Hao (waliotubia) ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema.........(25:70)

Kwa kifupi ni kwamba iwapo mtu atafariki dunia akiwa hana dhambi basi hatakuwa na maswali mengi ya kuulizwa na wala hatasumbuliwa popote pale katika safari yake hiyo. Iwapo mtu atakuwa amejitwisha mzigo mzito wa madhambi, basi atakuta maswali na mahojiano mengi yakimsubiri kwa muda mrefu katika Barzakh hadi hapo atakapotakasika kabisa na kuingia katika siku ya Kiyama.

Al-Imam as-Sadique a.s. amenakiliwa riwaya: "Mtu yeyote ampendaye Ali a.s. na kuwachukia maadui wake, na iwapo atakuwa amejitwisha mzigo wa madhambi bila TAWBA, basi huyo atabakia muda mrefu katika Barzakh akiadhibiwa hadi kutakasika kabisa. Atakapotokea siku ya malipo atakuwa hana la kujibu kwani atakuwa ametakasika."

(Tafsir Nuru Thaqalain, Kitabu cha tano, Uk. 165: Tafsir Majmaul Bayaan).

Imam a.s. alisema vile vile: "Mimi ninawakhofia mno adhabu za Barzakh (kizuizi) na siku ya kiyama tutawatetea waumini."

Hivyo inatubidi sisi tufanye TAWBA sahihi na kamilifu kabla ya kifo chetu ili tukifa tuwe ni waumini wa kweli ndipo tutakapopatiwa Shifaa ya Mtume s.a.w.w. na Maimamu a.s. kwani sisi tulivyo dhaifu hatutaweza kustahimili adhabu za mwenyezi Mungu na moto wa Jahannam. Tuelewe vyema kuwa huwa daima mauti inatufuata kama vile kilivyo kivuli chetu na labda muda huu tulio nao ndio wa mwisho, hivyo TAWBA ndiyo suluhisho letu la kuokoka humu duniani na vile vile Aakhera.