rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

28. MBELE YA ALLAH SWT MIGUU NA MIKONO VITASEMA.

Baadhi ya Mufassirina wanasema kuwa siku ya Kiyama kitakachoweza kusema ni mdomo tu, je viungo kama mikono na miguu vinaweza kusema?Wao wanasema kuwa hali ya udhahiri wa mwanadamu tu ndio utakaodhihirisha hali yake huyo mtu, na wala si mikono au miguu. Basi hao tunamwambia kuwa 'matamshi' si mahitajio ya ulimi bali ni Allah swt anayejaalia uwezo wa mdomo kutamka maneno. Kutamkwa kwa maneno ni Sifa ya Allah swt na wala si kasoro. Iwapo ingalikuwa hivyo, basi ng'ombe na punda pia wanayo midomo na ulimi hata mirefu kuliko wanaadamu. Basi imetuwia dhahiri kuwa mwanadamu amefadhilishwa na Allah swt kwa kumjaalia 'uwezo wa kutamka.' Katika neema kubwa kabisa za Allah swt kwa mwanadamu ni akili, hivyo ulimi ni tafsiri ya akili ili aweze kusema. Wanyama hawajajaaliwa neema hiyo.

Watu wenye akili watambua kuwa 'utamkaji' hauna uhusiano hasa na ulimi, bali ni Allah swt tu aliyezijaalia ndimi za wanaadamu ziweze kutamka maneno. Siku ya kiyama, hata vidoke vyetu vitafanya kazi hiyo hiyo na kusema kuwa huyu mtu alimnyooshea kidole muumin fulani kwa dharau au aliandika kwa kalamu yake mambo dhidi ya muumin. Zipo riwaya zisemazo kuwa hata nywele za mtu pia zitatoa ushahidi wao dhidi ya mtu mwenyewe.

Dalili ya pili ni kule ambapo mtu hatakaporidhika pale viungo vyake na sehemu za mwili wake zitakapotoa ushahidi dhidi yake.Lakini hivyo navyo vitasema kwa kuwa vimejaaliwa Allah swt uwezo huo wa kusema.

Malaika wote wanao uwezo wa kuzungumza na vile vile viumbe vyote tusivyoviona pia vinao uwezo wa kusema:

.Na hakuna chochote ila kinamsabihi yeye (Allah swt ). (17:44)

Baada ya kifo cha mtu, huwa anaelekea katika sehemu za Malaika.

Iwapo ungalikuwa nauwezo wakuyasikia yaliyoghaibu (yasiyoonekana machoni mwetu) Basi hata viungo vyako pia vinamtukuza allah swt, lakini hauyasikii.Mwanadamu hawezi kutambua kwa kuhisi tu kwani sisi tupo humu duniani na wala hatuna uwezo huo wa ziada. (Jikumbushe kisa cha Mtume Suleyman a.s.alipokuwa akipita penye makazi ya mdudu sisimizi).

Kinaadhimisha utukuzo wa Mwenyezi Mungu chochote kile kilicho mbinguni na chochote kile kilicho ardhini. (62:1)

Kesho siku ya Qiyama, Allah swt atakijaalia kila kiungo 'uwezo wa kusema,' na vyote vitasema kama kawaida.Dhambi hata moja halitafichika hata kama kikiwa kidogo kiasi gani, lakini iwapo tutakuwa tumeisha fanya Toba maishani mwetu, basi viungo na sehemu zetu zote za mwili hazitatamka chochote dhidi yetu wala kutushitaki.

Kwa kifupi, itakuwa ni aibu na udhalilisho mkubwa kwetu sisi kushitakiwa na viungo vyetu sisi wenyewe.Hivyo, ili kuepukana na udhalilisho kama huo inatubidi tuwahi kufanya Toba ya madhambi yetu yaliyokwisha tendwa kabla hatujafariki na kukosa fursa hiyo.

29. TUSOME TASBIHI KWA VIDOLE KWANI VITATOA USHAHIDI WAKE.

Katika tafsiri 'Ruh al-Bayaan, kwa mukhtasari kuwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. aliwaambia wanawake kuwa wawe wakisema kwa wingi sana tasbili.

Ipo riwaya nyingineyo isemayo kuwa Mtume mtukufu s.a.w.w. anasema:

"Usiku wa Me'raj nilimwona Malaika mmoja akijenga jengo. Alikuwa akiweka tofali la dhahabu na mara tofali la fedha, na mara nyingine alikuwa akingojea. Mimi nilimwuliza 'je kwa nini unangojea?' Alijibu: "Wakati mja wake Allah swt anapoanza Tasbihi, sisi huwa tunaanza kujenga jengo zuri sana, na mara anyamazapo, nasi pia twangoja.

Katika kipindi cha awali cha Islamu, hapakuwapo na tasbihi bali walikuwa wakihisabia kwa vidole vyao. Kuna vifundo vitatu katika kila kidole na hivyo kuna mafundo thelathini kwa jumla ya mikono yetu miwili. Hivyo tutoe tasbihi kwa kutumia vidole vyetu hivi. Amesema Mtume Mtukufu s.a.w.w."Toeni Tasbihi kwa vidole vyenu kwani siku ya Kiyama vitatoa ushahidi kwa kusema:"Ewe Allah swt! huyu mtu alikuwa akitoa tasbihi pamoja nasi."

Tasbihi kwa mara ya kwanza ilifanywa na binti wake Mtume Mtukufu s.a.w.w. Bibi Fatemah Zahra a.s. Yeye alipokuwa amekwenda kuzuru kaburi la Bwana Hamza, alirudi na udongo mchache na ambao aliutumia katika kutengenezaea Tasbihi.Alitumia hiyo tasbihi katika dhikiri ya Allah swt.

Katika kipindi cha Imam Jaafer as-Sadique a.s. alitilizia mkazo wa kutengeneza tasbihi kwa udongo wa Karbala. Iwapo tasbihi iliyotengenezwa kwa udongo wa Karbala ikizungushwa mkononi tu, basi inayo malipo makubwa kwani udongo wenyewe upo unafanya tasbihi.

Allamah Sheikh Shushtary anasema:"Tasbihi iliyotengenezwa kwa udongo wa Karbala, si tasbihi ya kawaida, bali inayo thawabu nyingi kupita kiasi na inazo khususi kwani ardhi ya karbala ni kipande cha peponi (Jannati)."

Imam a.s. alimwambia Sahaba wa Mtume Ja'abir:

"Ewe Ja'abir ! Uwe ukimzuru Hussein huko Karbala kwani Karbala ni kipande miongoni mwa vipande vya peponi (Jannati)."

Msomaji anombwa kurejea maudhui haya ya kusujudia juu ya udongo. "Kwa nini Mashia husujudu juu ya judongo" cha Bilal Muslim Mission of Tanzania P.O.Box 20033 Dar es Salaam Tanzania East Africa na 'Assujuud' ala turbatil Husseyn Inda As-Shiah al-Imaamiyah' (kiarabu) cha Sheikh Abdul Husseyn al-Amiini.Kilichochapwa na Dar az- Zafra, Beirut Lebanon.

30. JE TAWBA IWEJE?

Kufanya TAWBA ya Allah swt ni jambo la daraja la juu, na iwapo jambo hili likiandikewa kitabu kwa ufafanuzi zaidi, basi kitatokezea kitabu kikubwa mno, lakini sisi hapa tutajaribu kuelezea vile TAWBA inavyotakiwa kufanywa. Iwapo mtu atatokezea kusema kuwa ,mimi nimefanya TAWBA, nimehuzunikia na kusikitikia madhambi yangu, na vile vile nimeomba msamaha wake Allah swt lakini moyo wake haukusikitika au haukuhuzunika na wala hakuacha kutenda matendo ya madhambi. Basi watu kama hawa hawatafaidika kamwe na faida za TAWBA zisizo za Nasuha.

Al- Imam ar-Ridhaa a.s. amesema:

"Iwapo mtu atatamka 'Astaghfirullah' ya moyoni, basi atambue kuwa amemfanyia mzaha Allah swt."

31. MAJUTO YA MOYONI YAWE KWA AJILI YA ALLAH SWT TU.

Iwapo mtu atasema kuwa mimi nimekwisha fanya TAWBA na huku moyoni hana majuto yoyote ya madhambi, basi huyo ni MWONGO. Kwani uhakika wa TAWBA ni kujuta kwa madhambi aliyoyatenda mtu. Inawezekana mtu akajuta au kusikitika kwa dhambi alizozitenda na wala majuto yake si kwa ajili ya kutaka kufanya TAWBA na vile vile mtu anaweza kujiepusha na matendo ya madhambi kwa sababu za kidunia tu kama vile anahofia asidhurike kwa hasara za kimwili au heshima yake itapotea kwa kujihusisha navyo au anaogopa asije akafungwa jela. Sasa iwapo yeye atasema 'Astaghfirullah' kwa kutokana na vitisho kama hivyo, basi huyo ni mnaifki na ndiyo maana tunasema kuwa yu-mwongo. Sifa kubwa kabisa ya TAWBA ni kwanza kuacha kutenda madhambi na kufanya majuto na huzuni kwa madhambi yaliyokwisha fanywa hapo awali.

Lakini kwa kuwa kilio chake ni kwa sababu ya khofu ya adhabu au kukosa thawabu za Allah swt basi ni sawa na yule mtu ambaye baada ya kutesa na kudhulumu kupita kiasi na yupo anatafutwa na Serikali kwa kushitakiwa ili akamatwe popote pale alipo na hatimaye kufungwa jela. Sasa anatumia hila kwa kumwendea aliyemdhulumu ili amsamehe huku akilia ili kwamba asije akakamatwa na polisi akahukumiwa. Haya hayakuwa matendo yake yenye nia njema ya kumwomba msamaha wa kweli bali yalikuwa ni baada na kwa khofu ya polisi.

Hivyo huyo mtu akiwa amejaa khofu ya Jahannam anafanya TAWBA - hadaa. Na iwapo angalikuwa na matumaini ya kutoingizwa motoni (Jahannam) basi asingalifanya TAWBA wala asingelisikitika na wala asingejitambua kuwa yeye ni mwenye madhambi. Swala hili lipo wazi na sisi hatuwezi kusema kuwa hiyo ndiyo TAWBA hakiki. TAWBA ya uhakika ni ile ambayo itatoa ushahidi wa nia na matendo yake yaliyo mema na kumfanya mtu akajirekebishe na kufuata njia nyoofu.

Allamah Tusi A.R.na Allamah Hilli A.R. wameelezea katika 'Tajrid al-Kalaam' kwa mukhtasari kuwa, mtu aketi kwa kutulia na kusikitikia madhambi aliyoyatenda dhidi ya hukumu za Allah swt, basi hapo TAWBA yake inaweza kuwa sahihi.Lakini iwapo atafanya TAWBA kwa uoga wa serikali au kwa khofu ya kupoteza heshima yake mbele ya watu, basi TAWBA yake hiyo ni kujihadaa mwenyewe!

Hivyo tumeelewa kuwa TAWBA ni kwa ajili ya Allah swt tu kwani tumemwasi Allah swt na hivyo tunuie kuwa hatutarejea kamwe madhambi na hapo ndipo kweli tutakuwa tumefuata njia ya kufanya TAWBA.

TAWBA inayo mambo mawili, kwanza, kusikitikia na kuhuzunikia matendo maovu tuliyoyatenda, na pili, kunuia na kuazimia kutorejea kutenda madhambi na vile vile kujiepusha nayo.

Mtu atakapoukaribia wakati wake wa mwisho wa kufariki, na iwapo atafanya TAWBA au asipofanya, lakini ataingizwa kaburini tu.Iwapo atafanya TAWBA basi kuna uwezekano wa kupona adhabu za Jahannam, lakini Maulamaa wanapinga TAWBA ya wakati wa mwisho (sababu zake zitatokezea mbeleni). Firauni alitubu wakati wa mwisho wa maisha yake, lakini ilimfaidia nini? Alizama pamoja na wafuasi wake kwa pamoja.Hivyo nasi tusije tukatubu kumbe kutubu kwetu kusitufaidie chochote.

32. MAPENZI YA AHLI BAYT A.S.. HUELEKEZA KWA TAWBA.

Watu wenye Imani na mapenzi ya Ahli Bayti Toharifu ya Mtume Mtukufu s.a.w.w. wanapotokezewa kufanya dhambi, basi ni rahisi kwao kujaaliwa tawfiki ya TAWBA. Allah swt kwa nuru na baraka za Mtume mtukufu s.a.w.w. na ma-Imam a.s.atawafanyia matokeo yao yawe mazuri.

Iwapo watu waliwafuata viongozi wa sini yetu kwa ukamilifu, wakatekeleza faradhi zao ipasavyo, wakajiepusha na yote yaliyoharamishwa, wakawafuata kikamilifu Ahli Bayt ya Nyumba ya Mtume a.s.na wakawa wakidumisha maulidi ya Husseyn a.s. basi siku ya kiyama Mtume s.a.w.w.atawasaidia wote.Wamebahatika wote wale watakaotetewa na Bibi Fatemah az-Zahra a.s. Wasio na bahati ni wale ambao hawana mapenzi ya Ahli Bayt ya Mtume s.a.w.w..

Pamoja na hayo, faida nyingineyo itokanayo na mapenzi ya Ahli Bayt a.s. ni kuondokana na ubakhili na huingiwa na moyo wa kutoa sadaka na misaada na hiyo ndiyo bakhshishi kubwa (lakini wale wasiotoa khums, zaka au sadaka na ambao hutoa rushwa na kukusanya mali kwa kutumia riba kwa hakika wao si wapenzi wa Ahli Bayt a.s.) Iwapo munataka kufanya mapenzi na Imam Ali a.s. na kumfuata basi muwajue hali mayatima, wajane, wageni na muwasaidie wenye madaris (wingi wa Madrassah au vyuo).

Wale walio wapenzi wa kweli wa Ahli Bayt a.s. kwa hakika hawawezi kufariki bila ya kufanya TAWBA. Tawfiki hiyo Inshaallah watajaaliwa kabla ya mauti kuwafikia, na kuelekea peponi huku wakiwa hawana mzigo wa madhambi yao.

33. TAWBA NI MLANGO WA REHEMA.

TAWBA ni mlango mmoja mtukufu kabisa wa Rehema za Allah swt na TAWBA ni bahati ya watu wenye imani na wapenxi wa Ahli Bayt a.s. Tujue kuwa hakuna dhambi lolote lile lisiloweza kusamehewa, hata TAWBA ya Makafiri au mapagani pia huweza kukubaliwa.

Lakini mapenzi ya Ahli Bayt ya Mtume Mtukufu s.a.w.w. ni sharti mojawapo au sivyo mtu anaweza kukosaukubalio wa TAWBA yake hadi kufari dunia.Kwani mapenzi hayo yapo yameamrishwa na Mwenyezi Mungu katika Qurani Tukufu na vile vile Mtume Mtukufu s.a.w.w. pia ametulazimisha kwa hayo.

Ni lazima vile vile tutambue kuwa TAWBA itakayofanywa katika uhai wa mtu kabla ya kifo chake, ndiyo itakayomfaidi kwani atanuia kuacha maovu kuanzia hapo anapotubu lakini yule mtu anayefanya TAWBA wakati wa mwisho wa pumzi yake hutambua kuwa sasa hanao muda mwingine wa kutubu, hivyo anajaribu kufanya TAWBA ili anusurike, lakini hivyo haitamsaidia kwani anatambua kuwa hana njia nyingine ila ni TAWBA tu na hivyo hana wakati wa kujirekebisha na kuacha maovu kwani mauti imeshaanza kumtoa jasho utosini. Je, mtu kama huyo anaweza kudai kuwa hatarudia kutenda maovu tena? Ambapo katika TAWBA tunanuia kutotenda tena madhambi. Huyo amejihadaa kabisa. Watu kama hawa wapo wanzungumzwa katika Qurani Tukufu:

Na TAWBA (yenye faida) kwa ajili ya wale watendao maovu hadi mauti inapowahudhuria mmoja wao. (4:18)

TAWBA si jina la kulazimishwa, bali ni kutekelezwa kwa ibada zote zilizo za faradhi tulizoziacha, iwapo tunadaiwa fidia, basi tuzilipe na tuache kabisa mambo yote yaliyoharamishwa katika Islam.

Kwa kifupi ni kwamba, iwapo mtu ataathirika kwa masikitiko ya madhambi yake wakati wa kufa, basi haitambuliwi kuwa ni TAWBA. Kwani TAWBA ni kusikitika na kujutia kwa yale mambo yaliyo kinyume na maamrisho ya Allah swt na wala si kusikitika baada ya kuona na kuhisi adhabu.

Imam Zaynul Aabediin a.s. anasema katika Sahifa-i-Sajjadiyyah, kuhusu TAWBA:

"Mlango wa Rehema ulioufungua wewe (Allah swt) kwa ajili ya waja wako unaitwa TAWBA, mlango huo huwa daima upo wazi, sasa hakutakuwapo yeyote na kisingizio mbele yako...."

Allah swt anatuambia katika Qurani:

Basi hoja yaMwenyezi Mungu (pekee) ndiyo amri (6:149)

Kwa yakini kuna ushahidi kamili mbele ya Allah swt, hivyo iwapo mtu atajaribu kujitetea visivyo kwa kusingizia kuwa alipotoshwa na matamanio nafsi yake, basi hapo atajibiwa:"Je, hatukuwawekeeni wazi mlango wa TAWBA? Sasa kwa nini haukufanya TAWBA na kuomba msamaha na rehema za Allah swt.

Bila shaka Rehema na Maghfirah za Mwenyezi Mungu zipo kwa wingi, hivyo inatubidi sisi tufanye TAWBA kamilifu ili maovu yetu yabadilishwe kuwa mema, kama vile Qurani isemavyo:

..Hao (waliotubu) ndio Mwenyezi Mungu atawabadilishia maovu yao kuwa mema. (25:70)

Kwa mujibu wa Aya hiyo juu ya sura al-Furqaan, si kwamba ni madhambi yetu tu ndiyo yatakayo futika bali hata matendo yetu maovu pia yatabadilishwa kuwa mema. Hivyo tujihadhari na jitihada za sheitani ambaye daima huwa akibuni kila aina ya mbinu za kuwapotosha wale walio katika Siraat-i-Mustaqiim.

Katika Sura an-Nahl twaambiwa:

Kisha hakika Mola wako kwa wale wanaotenda ovu (tendo) katika hali ya ujahili (ujinga) na hugeuka (kwa kutubu) baada yake na hujirekebisha, kwa hakika Mola wako ni mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu. (16:119)

Katika tafsiri 'Majmaul Bayaan' na 'Al-Miizan fi Tafsiril Quran' Juzuu ya nne na Juzuu ya ishirini uk. 398 ya Allamah Syad Muhammad Husseyn Tabatabai. Chapa ya pili 1974 Beirut. Ipo riwaya ifuatayo juu ya Istighfaar:

'Baada ya kuteremka kwa Aya 3:135, Sheitani alikuja Makkah na kupiga sauti kubwa mno juu ya mlima Thuwayr, ambayo iliwafanya mashabiki wake wote wakusanyike, nao walipokuja walimwona bwana huyo amezongwa na mushkeli mkubwa sana na hapo hawakusita kumwuliza: "Je umekuwaje na hoja gani ya kutukusanya hapa?"

Akajibu: Imeteremka Aya isemayo kuwa Ummah wa Muhammad utasamehewa kabisa madhambi yake na masharti ya TAWBA yaliyokuwa yamewekewa Ummah yaliyotangulia, yameondolewa kwao. Na iwapo sisi hatukubuni mbinu dhidi yake, basi juhudi zetu zote za kuwapotosha hazitakuwa na athari yoyote kwani wao watakapofanya TAWBA,madhambi yao yatasamehewa yote kwa pamoja na hata kubadilishwa kuwa matendo mema."

Kwa hivyo nimekuiteni hapa ili tutafute mbinu za kukabiliana na swala hili ama sivyo sisi hatutakuwa na kazi yoyote ile."

Kila mmoja wao alitoa mpango wake aliinuka mmoja wa Masheitani, akasema: "Nitafanya hivi na vile......." Lakini hawakukubaliana naye, nao wengine pia walisema walivyokuwa wakiona, nao wote walikwenda wakipingwa mmoja baada ya mwingine.

Na hapo akainuka Waswas - Khannas, naye akasema: "Nitawatia watu katika hatia (madhambi) na papo hapo nitawasahaulisha Istighfaar (TAWBA) na nitawaambia kuwa "Ewe bado unao muda mwingi wa kufanya TAWBA, haraka ya nini? Huu ndio muda wako wa kustarehe na kufaidi umri wako! Siha yako na vile nguvu zako zinakuruhusu ufanye hivyo, hivyo starehe hadi utakapokuwa mzee, utafanya TAWBA kiasi utakacho!"

Kwa hayo, Masheitani wote walifurahi mno na yeye Khannas alikabidhiwa kazi hiyo hadi kufika siku ya Kiyama.

(Tafakari Sura an-Naas, Nambari 114)

Hizi ndizo wasiwasi za Sheitani ambazo huwapotosha watu wengi hasa vijana ambao hudhani kuwa wao bado wanao umri mrefu wakufanyw TAWBA hapo mbeleni. Sisi twachukulia uzee ndio wakati wa kufanya TAWBA, lakini nani anayejua kuwa uzee huo ataufikia au atakufa kabla yake. Je siku hizi hatuoni kuwa wazee ndio waliobakia hai ambapo vijana wamekufa kwa magonjwa kama UKIMWI? Na magonjwa mengine ambayo hayana hata muda wa kuyashughukikia vyema kama homa ya uti wa mgongo, (seven days) n.k. Kwa hivyo fanya lile uliwezalo leo badala ya kungojea kesho, kwani unaweza kuugua vibaya sana na hata kufa! Jambo linlotubidi kujiambia ni : "Sielewi ni lini mauti yangu itanifikia na kunichukua, labda hata sasa hivi ipo mgongoni mwangu ikinichukua, hivyo ni aibu kufika mbele ya Mwenyezi Mungu huku nimejitwisha mzigo mzito wa madhambi bila ya kufaidi fursa ya TAWBA!"

Je, ndugu zangu, Imani yetu haipo hatarini? Labda tukafa mauti isiyo ya Islam na ambapo Allah swt anatuambia tusife ile tukiwa Waislamu!

Quran Tukufu inatuambia katika Sura ar-Ruum:

"Kisha ubaya ndio ulikuwa mwisho wa wale waliotenda uovu, kwa kukadhibisha Aya za Mwenyezi Mungu, na kwa haya walizoea kudhihaki. (30:10)

Vile vile twaambiwa katika Sura Aali Imraan:

Na harakisheni kwa (njia ya kujipatia) Maghfirah kutoka Mola wenu! (3:132)