rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

8. KUFANYA TAWBA PAPO HAPO NI FARADHI

Shaykh Bahai (A.R.) anaandika katika kusherehesha 'Arbain' kuwa: "Madhambi huenea mwilini mwa mtu kama vile sumu kali inavyoenea mwilini mwa mtu, basi juhudi za haraka sana zinavyofanywa kuzuia sumu isienee mwili mzima, ndivyo vivyo hivyo inavyotakiwa kufanya TAWBA ya madhambi yaliyokwisha fanywa ili maovu yake yasienee katika mwili mzima.Kuna hatari mbili ya kutokufanya TAWBA, kwanza iwapo atabakia hai, basi kuna uwezekano mkubwa kwake yeye kurejea katika madhambi aliyokwishayatenda na kuongezea mengine kwani alikuwa hakufanya TAWBA, pili iwapo atafariki (kwani hakuna anayejua wakati wake wa kifo) basi atakuwa amekosa hiyo fursa ya kufanya TAWBA, masikini huyo ataaga duni pamoja na mzigo wake wa madhambi akisubiri adhabu kali ya Allah swt."

Katika hali hii milango ya TAWBA na fursa zake zitakwisha kwa ajili yake. Allah swt anatuambia katika sura Munafiqun, Aya 10-11:

Na toeni katika yale tuliyokupeni, kabla mmoja wenu hayajamjia mauti,kisha akasema:"Mola wangu! Huniahirisha muda kidogo tu nikatoa sadaqa na nikawa miongoni mwa watendao mema?"

Lakini Mwenyezi Mungu hataiahirisha nafsi yoyote inapokuja ajali yake, na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda yote. (63:10-11)

Katika tafsiri ya aya hiyo, tunaambiwa kuwa mwanadamu wakati wa mauti yake huwa anamwambia Malaika wa Mauti kuwa ampatie muhula mdogo wa hata siku moja ili aweze kutubu madhambi aliyoyatenda, na ajiandae kwa ajili ya safari yake ya Akhera. Basi hapo Malaika Izraele atamwambia: "Siku za maisha yako zimeisha."

Hapo basi mwanadamu atasema:"Basi naomba muhula wa hata saa moja."

Atajibiwa:"Saa za maisha yako pia zimekwisha, na hapo pia umefungwa mlango wa TAWBA kwa ajili yako."Na hapo roho yake itatolewa -atakufa.Masikini mwanadamu huyo atafukiwa kaburini mwake akiwa bado amebakiza matumaini na mategemeo mengi, lakini yote hayo humo shimoni yatamsaidia nini? Katika hali kama hii, imani ya mtu ipo hatarini!

Jambo la pili ni kwamba, kwa sababu ya kutofanya TAWBA, kunatanda giza zito moyoni mwa mtu, na huendelea kupakwa giza zito ambayo haiwezi kamwe kutolewa.Kadiri atakavyokuwa akiendelea kutenda madhambi ndivyo utando huo mweusi utakavyoendelea kutanda juu ya moyo wake na hivyo matikeo yake ni kuendelea kutenda madhambi bila hata ya kujuta na kusikitika.Kwa mujibu wa riwaya, moyo kama huo unaitwa 'moyo mweusi.'

Imam Muhammad al-Bakir (a.s.) anasema:"Hakuna kitu chochote chenye kuuleta moyo madhara kuliko madhambi. Kila giza linavyozidi moyoni mwa mtu, hatimaye hulifunika lote kwa giza lake.Hapo ndipo utamwona mtu anatoka kwenye nuru na kuingia katika giza na kupotoka kabisa kwani atakuwa haioni haki."

Katika riwaya nyingine, anasema Imam Muhammad al-Baquir (a.s.) kuwa: "Mfanya madhambi sugu kama huyu hataweza kutenda mema kwani mema yatakuwa yameshamwondokea zamani, na hivyo hadi kufikia mwisho wa maisha yake haweza kufanya TAWBA.Na iwapo atajaribu kufany TAWBA, basi itakuwa ni ya matamshi tu kwani moyo wake hautashiriki naye.Yaani yeye atatamka hivi na hisia zake zitasema vingine.Aina hii ya TAWBA haiwezi kuwa TAWBA halisi na wala haitakuwa na athari zozote.Mfano wake ni ule wa mtu kuzivaa nguo zilizo chafuka na huku akidai kuwa zimefuliwa.Kusema kwake huko hakuwezi kuzifanya nguo chafu zikawa nguo safi. Na mtu kama huyu anaweza kupotoka katika dini yake na wala dini yake haitamwathiri yeye. Mtu yeyote anapoiingiza imani yake katika hali ya hatari kama hii, basi ahera yake pia humharibikia."