rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

3. MAJUTO NA MASIKITIKO

SABABU YA KUEPUKANA NA MADHAMBI:

Kila itakavyokuwa zaidi imani ya mtu na yakini yake juu ya Allah na Kiyama; Mtume s.a.w.w. na ma - Imam a.s. ndivyo vivyo hivyo itakavyokuwa masikitiko yake kwa madhambi yake, na daima atakuwa akisononeka moyoni mwake kwa kujionea aibu. Kwa hivyo pamoja na majuto, masikitiko na aibu, inambidi mtu afikie uamuzi madhubuti katika kuepukana na madhambi kwani asipojizatiti katika kuepukana na madhambi, basi itamaanisha wazi wazi kuwa yeye hanayo majuto wala masikitiko au aibu kwa madhambi atendayo.

Imam Ali a.s. amesema: "Haiyumkini kwa mtu kusikitika na kujuta huku bado akiendelea kutenda madhambi." Baada ya kusikitika na kujuta kwa madhambi, inambidi mtu atekeleze malipo ya madhambi hayo aliyokuwa akiyatenda. Kama zilikuwa ni haki za Allah swt kama vile sala, saumu, zaka, Hajj n.k. basi baada ya kutubu inamlazimu alipe vyote hivyo.

Iwapo ni haqqun-naas (haki za watu) kama vile amechukua mali ya mtu bila ya ruhusa yake, basi airejeshe hiyo mali haraka sana, na iwapo mwenye mali hiyo amefariki, basi awafikishie warithi wake na iwapo hawafahamu warithi wake, basi atoe sadaka kwa niaba ya mwenye mali. Iwapo alikuwa amemvunjia heshima ya mtu, basi amwombe msamaha yule aliyemvunjia heshima ya mtu, basi na afanye kila jitihada ya kumridhisha. Iwapo ni haki ya kisasi au fidia basi inambidi ajipeleke mbele ya mwenye kisasi au fidia ili itekelezwe au asamehewe. Iwapo ni haki ya adhabu iliyopitishwa, kama vile kumzulia mtu jambo asilolitenda, basi ajipeleke mbele ya huyo mtu ili hiyo hukumu itekelezwe au aweze kusamehewa.

Lakini, iwapo yeye amejitwisha madhambi ambayo hukumu zake zimeshatolewa na Allah swt, kwa mfano wa zinaa, basi haimlazimu mtu kujipeleka mbele ya hakimu wa Kiislamu na kuungama ili atimiziwe adhabu inayomstahiki. Kinachombidi yeye katika hali kama hiyo ni kuacha kutenda madhambi hayo, awe anajuta na kusikitika kwa msimamo imara aombe msamaha kwa Allah swt.Ama kwa madhambi yaliyo Makuu (ghunahi kabirah) na adhabu zao hazikuwekwa waziwazi kama vile kuimba na kusikia muziki, basi kwa mujibu wa Aya za Qurani imedhihirika kuwa mtu huyo awe akisikitika na kujuta na hapo aombe maghfirah, yaani aombe kwa Allah amsamehe madhambi yake na kumbariki.