rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

1. TAWBA

Allah swt katika sura Tahrim Aya ya 8 anatuambia:

"Enyi mlioamini! tubuni kwa Mwenyezi Mungu TAWBA

iliyo ya kweli.........." ( 66 : 8 )

Kwa watu wenye kuona na kufikiri, haikufichika kwao kuwa TAWBA ni fungu mojawapo la ukarimu na rehema za Allah swt na kwamba TAWBA ni mlango mmojawapo mzuri kabisa ambao Allah swt ametufungulia ukawa wazi daima kwa ajili ya sisi waja wake. Iwapo mlango huu wa TAWBA ungalikuwa umefungwa, basi hakuna mtu ambaye angeweza kuokoka na kufanikiwa mbele ya Allah swt, kwani maisha na matendo yake mwanadamu yamejaa makosa, madhambi na maasi.

Ndiyo hivyo ilivyo kuwa kila mtu amekuwa akijitumbukiza katika shughuli fulani fulani ambapo ni Allah tu ndiye aliyekuwa akimhifadhi na kumsitiria hayo maovu yake. Kwa kifupi ni kwamba mwanadamu anaweza kujizuia asitende madhambi, lakini hakuna mtu anayeweza kudai kuwa yeye hakutenda madhambi tangu alipopata akili, isipokuwa Mitume a.s. na ma-Imamu a.s. ambao hatuna shaka na utoharifu wao.

Ni kwa sababu hiyo Allah ametuwekea dawa ya kutuponyeshea magonjwa yetu na maradhi ya kiroho na ni njia ya kuyasafisha matendo yetu maovu, ili kwa baraka za TAWBA, madhambi ya mwanadamu yaishe na aweze kujipatia uokovu wa milele.

Amebahatika mtu ambaye ameweza kuuthamini huu mlango wa rehema na kuweza kufaidika nao akawa mpenzi wa allah swt na ameweza kuwa mja mwenye kushukuru neema zake. Lakini hakubahatika yule ambaye hakuweza kufaidika kwa mlango huo ambapo milango na njia zote za TAWBA zimekuwapo wazi mbele yake!

Siku ya Kiyama wakati wa kutoa hisabu, mtu atakapokuwa akijitafutia visingizio na sababu katika kujibu maswali atasema: Ewe Mwenyezi Mungu! Mimi nilikuwa mjinga na wala sikuwa na habari, matamanio na ghadhabu zangu zilinifunga kwa minyororo na wala sikuweza kamwe kumudu msimamo wangu dhidi ya wasiwasi na upotofu wa Sheitani." Hapo atajibiwa pamoja na masingizio na sababu zake "Je, sikukuwekea wazi njia zote za TAWBA? Ulielezwa kazi zote zilizo ngumu, na je alitokea yoyote mwenye kuzidi uwezo wako? Je, masharti ya TAWBA yalikuwa hayakushughulishi wewe?"

Hapa ninaonelea vyema kuelezea machache juu ya TAWBA.