rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

TAWBA

Kimeandikwa na: SHAHID-I-MIHRAB SYED DASTAGHIB SHIRAZI

Kimetarjumiwa na kuhaririwa na : AMIRALY M. H. DATOO

KUTOKA KALAMU YA MTAYARISHAJI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, mwenye kurehemu.

Sifa zote ni za Allah swt Mola wa dunia zote na salaam zimfikie Mtume wake Muhammad s.a.w.w. pamoja na ahali yake Tahirifu a.s.na Sahaba Muttaqiina.

Vijana wetu katika zama hizi wapo wanasikitikia na kujutia juu ya yale waliyoyatenda, lakini kwa kuwa hawana mategemeo, basi wapo wanaendelea na matendo yao maovu.Wanafikiri kuwa sasa wameshatenda madhambi na hawajui kama watasamehewa au la, na hivyo utawaona wakiupoteza ujana wao katika maasi mbele ya Allah swt. Hivyo nimeonelea afadhali niketi na kukitayarisha kitabu hiki cha TAWBA pamoja na kutarjumu mengi ya makala ya Shahid Mihrab Muallim Akhlaq Ayatullah Shahid-i-Dastaghib Shirazi juu ya TAWBA katika lugha ya Kiswahili ili kuwanufaisha vijana na wazee.

Iwapo kazi hii ndogo itaweza kuiathiri roho ya mtu au nafsi yake, ingawaje mmoja tu, basi itakuwa ni furaha yangu.Ingawaje matamanio ya mwanadamu ni mengi mno kupita kiasi, lakini umri wake upo unamnyima nafasi hiyo. Kila usiku na mchana kunapozunguka kunampunguzia umri wa mwanadamu huyo, wala mwanadamu kutoka dunia hii na kama vile tujuavyo kuwa mauti itatujia siku moja na kutuchukua kutoka humu duniani. Iwapo mwanadamu amekwisha tenda madhambi katika maisha yake huku duniani, basi asikate tamm bali inmbidi ajitokeze mbele ya Allah swt kwa taadhima na heshima kwa kuomba TAWBA na MSAMAHA, na kwa hakika Allah swt lazima atatusamehe. Allah swt yupo kila wakati akisema: 'Ewe Mja wangu! na kamwe hujatuita;Ewe mwovu, muasi au jina lingine lolote lililo ovu, Ilhali unazijua aibu zetu, lakini kazificha. Sisi tunapojua aibu za mtu miongoni mwetu, basi huwa tunamwona kwa mtazamo wa dharau, lakini Allah swt amezificha aibu zote.

Mtu anapokuwa akilaumiwa na dhamira yake, akili yake na nafsi yake kumfanya au kumshurutisha afanyeTAWBA, basi asiwe na wasiwasi, ila ajielekeze katika kufanya TAWBA YA ALLAH swt na hivyo atoe ahadi yake thabiti ya kutotenda madhambi tena. Hapo ndipo Allah swt anaposema kuwa kilio cha mwenye madhambi ni afadhali kuliko tasbihi za Malaika.

Kwa mujibu wa Ahadith na riwaya mbalimbali, madhambi ya mfanya TAWBA hudondoka kama vile yanavyodondoka majani katika mti au mfano wa mtoto mchanga anapozaliwa huwa hana madhambi. Hivyo inambidi mtu asiendelee kufanya madhambi baada ya kufanya TAWBA wala tusisite kuomba TAWBA kwa ajili ya madhambi tuliyokwisha tenda hapo kabla.

Ayatullah Dastaghib Shirazi, alikuwa ni shakhsiyyah mashuhuri sana huko katika Jamhuri ya Kiislamu Iran. Nchi hiyo haitaweza kamwe kusahau mchango wake katika nyanja nyingi za : elimu, dini n.k. Alipokuwa akitoa hotuba zake, basi nywele za wasikilizaji ziliweza kusimama na kujawa kwa hofu ya Allah swt, miili yao ilikuwa ikitetemeka. Maneno yake yalikuwa ni kama jawhari zenye thamani kubwa mno.

Laana ziwe juu ya maadui wa Islam ambao hawakupendezewa kuishi kwake humu duniani na maluuni mmoja asiye na huruma alimwua akiwa katika Mihrabu kwa mlipuko wa bomu. Shahidi Mahrabu (alijulikana tangia hapo) alipokufa shahidi kama Babu yake al-Imam Ali a.s. ambaye pia aliuawa kwa upanga wa ibn Muljim akiwa katika

Mihrab.Tunamwomba Allah swt amweke mahala pema na kumrehemu, pamoja na Mitume a.s. na ma-Imamu a.s.

Katika utafiti wangu nilioufanya, nimejaribu kwa uwezo wangu kuongezea pale nilipohisi palihitajika na vile vile hapo mwishoni nimeongezea aya za Quran zizungumziazo TAWBA, pamoja na Hotuba ya Imam Ali (a.s.) kutoka Nahjul Balagha na Doa Na. 31 kutoka Sahifa-i-Sajjadiyyah juu ya TAWBA.

Ni matumaini yangu kuwa kazi hii ndogo itatusaidia sote na tuombe kwa Allah swt aikubalie na kutujaalia tawfiqi ya kutenda matendo mema na tukifariki tuwe miongoni mwa wale waliokwisha fanya TAWBA.