MLANGO 11

ZAKAATUL- FITRI

AL-FITRA

Moja katika maana yake ni kuumba (kuhuluku). Kama ilivyo kuwa kwa kutoa zaka ya mali, huingia baraka na ikazidi mali ya mtoa zaka, basi kwa kutoa zaka ya Al-Fitri husababisha kusafika roho na kukulinda na maut mbaya na humtakasa yule mtu na madhambi.

Imepokewa hadithi inatokana na Al-Imaam As-Sadiq (a.s) kwamba alimwamrisha mjumbe wake: "Nenda toa zaka ya Fitri ya watu wote wa nyumbani, wala usimwache hata mtu mmoja; kwani ukiwacha kutoa zaka ya mmoja katika hao, namwogopea kufa".

Kutoa zaka ya Fitri ndio sababu ya kuifanya saumu yako ikamilike na, ikubaliwe. Basi asiyetoa (mwenye kuweza kutoa) mtu huyo hana saumu, wala haitakubaliwa saumu yake. Katika hadithi iliyotokana na Al-Imaam Jaffar As-Sadiq (a.s) inasema hiyi: "Ukamilifu wa saumu ni kutoa zaka ya Fitri, kama ilivyokuwa Kumsalia Mtume (s.a.w.) na Ahli Baiti wake (a.s.) katika sala ndio ukamilifu wa sala. Basi mtu akifunga na hakutoa zaka makusudi basi hana saumu, na akiwacha kumsalia Mtume (s.a.w.) na Ahli Baiti wake (a.s.) makusudi basi hana sala vile vile.

Mwenyezi Mungu ameanzia kwa hiyo zaka, kabla ya kusali na akasema katika Qur’ani, katika sura ya A’ala (87:14 na 15):

ÞóÏú ÃóÝúáóÍó ãóä ÊóÒóßøóì * æóÐóßóÑó ÇÓúãó ÑóÈøöåö ÝóÕóáøóì

(Hakika amekwisha faulu mwenye kujitakasa (kwa kutoa zaka) na akakumbuka jina la Mola wake akasali).

SHURUTI ZA KUFARADHISHA MTU KUTOA ZAKA

(1)Ubalebe. Awe amebalehe.

(2)Akili. Awe mwenye akili.

(3)Ghumia. Asiwe amezimia. (Aga Khui haafikiani hapa).

(4)Uhuru. Asiwe mtumwa.

(5)Utajiri. Awe mwenye mali.

Shuruti za kusihi Zaka ni mbili:

(1)Uislamu. Asiwe kafiri.

(2)Kutoa Lillahi Taala. Asitoe kwa Riya (kuonesha watu).

Kwa hivyo haitakuwa wajibu kwa mtoto asiyebalehe hata akiwa na pesa; wala mwenda wazimu; wala kwa mtu yule ambaye mwezi wa Shawwal (mfungo mosi) umeandama na yeye hali amezimia; wala kwa mtumwa; wala masikini.

Kwa Sharia Tajiri ni nani?

Muradi na kipimo ni hii: Mtu awe na mali au pesa ya kutosha mwaka mzima matumizi yake na watu wake wote wa nyumbani; haidhuru pesa hizo anazo kwa jumla au anacho kipato kama mshahara, kodi, biashara, ambacho kitatimiza mahitajio yake yote.

Basi kwa hiyo ikiwa katika njia hizo mbili hana hata moja, hapo mtu huyu huitwa masikini, na zaka ya Fitri haimlazimu kutoa, bali ni thawabu tu, na anaweza kufanya namna tutavyoeleza baadaye.

Ni wajibu kutoa zaka ya Fitri kwa kila mtu ambaye zimekamilika shuruti zote za kumfaradhisha. Atoe kwa nafasi yake, na kwa kila aliyekuwa ahali (jamaa) yake, wakati inapoingia usiku wa Idul-Fitri unapoandama mwezi wa mfungo mosi. Wala hakuna tafauti kwa wale wenye kuwatolea wawe katika wale ambao ni wajibu kuwalisha kama mke na watoto, au si fardhi kuwalisha kama ndugu, mgeni, na mtumishi, madamu wamo katika ahali hata kama sio jamaa au sio Mwislamu; hao wote lazima awatolee hata wakiwa mahala pengine. Mtoto aliyopo tumboni mwa mama yake hailazimu kutoa Fitri yake lakini akizaliwa kabla ya magharibi ya usiku wa Idi basi ni wajibu atolewe.

Akifa mtu baada ya magharibi ya usiku wa Idi ni lazima zaka yake pamoja na zaka za watu wa nyumba yake zitolewe katika mali yake. Na ikiwa amekufa kabla ya magharibi si fardhi kutoa zaka yake wala ya watu wake. (Ikiwa hao watu wake (maiti) wanazo shuruti za kufaradhika itawabidi watoe hiyo zaka katika mali zao).

Ikiwa umemkaribisha (alika) mtu usiku wa Idi kuja kufuturu kwako na baada ya magharibi kaja kufuturu kwako haitakulazimu (wajibu) kutoa Fitri ya huyo uliemwalika ijapokuwa ulimwalika tangu mchana. Lakini akifika kabla ya maghribi na ikiingia magharibi kwako hapo itakubidi utoe zaka yake.

Ikiwa mtu wakati wa magharibi wa usiku wa Idi, akiingiliwa na wazimu, kutoa zaka kwao si fardhi, lakini ikiwa kabla ya kuingia magharibi au wakati ule ule wa kuingia magharibi mwenda wazimu kapata akili, mtoto kabalehe au maskini kapata mali na akawa tajiri, na ikiwa shuruti zingine pia zimetimia, basi itawapasa watoe zaka.

Ni suna kwa masikini asiyemiliki chakula kwa mwaka mmojo kutoa zaka ya Fitri hivi: Atoe sehemu iliyowekwa kwa nia ya zaka kisha ampitishie mkewe tena mtoto mmoja baada ya mwingine kwa nia hiyo hiyo hadi kwa kila mmoja wa nyumba yake. Hatimaye atoe sehemu ile kwa masikini. Kwa kufanya hivyo Mwenyezi Mungu atawakubalia wote wa nyumba hiyo kwamba wamelipa zaka zao.

Aina ya vitu vya kutolea zaka ya Fitri

Chakula kinacholiwa sana katika nchi, kwa mfano, ngano, mchele, shayiri, tende, zabibu, mahindi, unga na maziwa. Ni thawabu na ina fadhila sana kutoa zaka kwa tende. Ukitoa bei ya mojawapo ya vitu hivyo itajuzu; si lazima kutoa hasa ile kitu, bali wakati mwingine ni bora sana kutoa pesa kupewa yule maskini ili aweze kununua nguo yake au ya watu wake.

Kadri na kiasi cha Fitri

Kwa kipimo kilicho tajwa katika vitabu vya sharia ni 'SAA’ moja ambayo ni sawa na kilo tatu na gram mia mbili (3 1/5 kilo) ambazo ni ratili sita na nusu kiasi.

Wakati wa kutoa zaka ya Fitri

Wakati wa kutoa zaka ya Fitri huanzia panapo zama jua siku ya mwisho wa Ramadhani. Wale wanaosali sala ya Idi inawapasa wasicheleweshe kutoa hiyo zaka mpaka wakati wa sala ya Idi, bali kabla yake iwe wameshatoa; na wasio sali sala ya Idi hawaruhusiwi kuahirisha kutoa hadi sala ya adhuhuri, bali  waitoe kabla ya kuingia wakati huo.

   Ikiwa mtu katenga zaka ya Fitri, basi haijuzu kubadilisha kile kitu au pesa. Na akichelewesha kumpa masikini, kwa hali aliweza kumfikishia masikini, na ikaja potea, basi itamlazimu kulipa.

   Na ikiwa hadi wakati huo hakutoa au hakutenga kiasi kinachombidi kutoa, basi sasa akitoa asinuwie kwa nia ya “adaa” au “qadhaa” bali atoe qurbatan illa-llah. Mtu akitenga (pesa au kitu) zaka huo wakati ulioainishwa na akazuwia kutoa kumungojea huyo masikini mahsusi aliemkusudia kumpa anaruhusiwa hivyo. Haruhusiwi kutoa zaka ya Fitri kabla ya mwezi wa Ramadhani; na hata katika mwezi wa Ramadhani huwezi kumpa masikini zaka hiyo ila kama unamkopa na baadae utapoingia usiku wa Idi, ile pesa uliomkopesha huyo masikini ukalipia hivi leo; ni bora zaidi ukimpa hiyo zaka mkononi mwake, na baadae huyo masikini akurejeshee kama analipa deni.

Matumizi ya zaka ya Fitri

Zaka ya Fitri wapewe masikini “MU-MIN” na bora kabisa jamaa zako masikini walio karibu na wewe sana, majirani Muumin, na wanafunzi wanaochukua elimu ya dini na sharia ya Kiislaam. Usimpe masikini chini ya kadri ya zaka ya mtu mmoja hata wakiwa wanaostahiki ni wengi au watakosa vilevile unaruhusiwa kumpa masikini zaidi ya zaka ya mtu mmoja. Huwezi kuwapa zaka ya Fitri wale ambao ni jamaa zako (wenye kukupasa kuwalisha) na umewatolea wewe Fitri zao. Unaweza kumpelekea Mujtahidi wako (ambae unamfuata) hizo pesa zako za Zaka ya Fitri ikiwa hakuna masikini katika mji ukaao.