MLANGO 9

MATOKEO MUHIMU KATIKA MWEZI WA RAMADHANI

Mwezi wa Ramadhani umejaa kwa matukio adhimu ya historia ya Uislaam na isiokuwa ya Uislaam. Mwezi huu mtukufu ni mwezi ambao viliteremshwa vitabu juu ya Mitume na Marasuuli. Inatosha katika utukufu wa mwezi huu na kuwa ni bora kuliko miezi mingine kwa kuterenishwa vitabu vitakatifu, ijapokuwa kuna mambo mengi yanayozidisha pia utukufu wa mwezi huu.

Huenda kwa ajili ya matukio muhimu, yaliyotokea katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. ndio ikafaradhishwa kufunga. Na sasa hapa tunakuleteeni baadhi ya matukio adhimu kwa mpango wa siku za Ramadhani.

Siku ya kwanza

Siku hiyo vilikuwa vita vya Tabuuk kama  ilivyo tajwa katika kitabu cha Waqai-ush-shuhuur-e-wa-ay-yaam. Navyo ni vita alivyo pigana Mtume (s.a.w) kwenye tabuuk, mahala ambapo walikusanyika jeshi la warumi kuushinda Uislaam na Waislaam. Tabuuk ni mji kati ya Madina na Damascus.

Siku ya pili

Siku hiyo ameteremshiwa Mtume Ibrahim (a.s) Sura tukufu  za hukumu za Mwenyezi Mungu.

Siku ya sita

Siku hiyo katika mwaka 201 A.H., watu walimbaayi Imam  wetu wa nane, Al-imam Ali bin Mussa Ar-ridhaa (a.s).

Siku ya kumi na tano

Siku hiyo ambapo alizaliwa Imam wetu wa pili Al-Imam Al-Hassan bin Ali bin Abi Twalib (a.s) katika mwaka wa nne.

Siku ya kumi na saba

Usiku wa siku hiyo, mwaka wa pili, yamekutana majeshi ya Mtume (s.a.w) na majeshi ya makafiri kwenye ardhi inayoitwa Badri, na mchana wake ikapiganwa vita kubwa vya Badri ambavyo Mwenyezi Mungu aliwapa ushindi masahaba wa Mtume (s.a.w) juu ya mushrikiin. Na vile vile usiku wake (kama inavyo semekana) Mtume akaenda Miiraji kutoka nyumba ya Ummu Haani, dada yake Amiirul muuminiin Ali (a.s) katika makka; ambapo akapanda Buraq na kuruka kwenda juu mbinguni, na Mwenyezi Mungu matukio hayo ameyataja mwanzoni mwa sura ya Is-raa katika Qur’ani. (juzu 15:s 17(.

Siku ya kumi na tisa

Siku adhimu kwa Waislamu, siku ambayo imebomoka nguzo ya Kuongokea (Hidi) na asubuhi ya siku hiyo ikakatika kamba ya Urwatil Wuth-qa (kishiko chenye nguvu) na umoja wa Waislamu ukatawanyika. Hii ni siku ambayo Ameeral-Mu-mineen (a.s) amepigwa kwa upanga katika Mihrabu ya Masjidul-Kufa (Iraq) alipokuwa akisali, pigo ambalo ndio sababu ya kufariki dunia. Amempiga mtu duni na mbaya kabisa, jina lake Abdur-rehman bin Muljam Al-Murady (Mwenyezi Mungu amlaani).

Siku ya Ishirini

Katika siku hiyo, mwaka wa nane wa al-Hijra, Mtume (s.a.w) akauteka mji wa Maka bila ya vita. Na Al-Imaam Ameerul-Mu-muteen Ali (a.s) alipanda juu ya mabega ya mtume kuvunja masanamu yale yaliyokuwa yametundikwa kwenye Kaaba tukufu, akayavunja na akayatupa yote, kama alivyo yavunja baba yake Mtume Ibrahim (a.s) masanamu zama za kale.

Siku ya Ishirini na moja

Siku ya msiba na hasara kubwa; siku ya huzuni kubwa kwa Waislamu wote; kwani siku hiyo amefariki dunia Al-Imaam Ameerul Mu-mineen Ali (a.s) hakika ni siku ya kusikitika na kulia.

Siku ya Ishirini na tatu

Usiku wake ambao ni Lay-Latul-Qadri, iliyo mashuhuri imeteremshwa Al-Qur-anul-Hakeem, kitabu kitukufu cha jamii ya wanadamu wote, na Kanuni za Mwenyezi Mungu hapa Ulimwenguni.

Imeelezwa katika kitabu mashuhuri Majmaul Bayaan kwamba Ibnu Abbas amesema, "Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’ani kwa jumla kutoka AlLaw-hul-Mah- fuudh kuletwa mpaka mbingu ya kwanza ya dunia katika usiku wa Lay-latul-Qadri, baadaye Jibrilu (a.s) kwa amri ya Mwenyezi Mungu aliteremsha juu ya Mtume Muhammad (s.a.w.) katika wakati makhsusi kidogo kidogo na ikachukua muda wa miaka ishirini na tatu, kuanza mpaka kwisha

Siku ya Ishirini na nane

Siku ambayo Mtume (S.A.W.) alitengeneza jeshi la Waislamu kwenda kupigana na makafiri katika vita vya Hunain, mwaka wa nane wa al-Hijra.

Siku ya thdathini

Siku ambayo Mtume (S.A.W.) alitoka Maka, baada ya kuiteka, kwenda kwenye vita vya Hunain na majeshi elfu kumi na mbili (elfu mbili watu wa Maka waliobaki watu wa Madina).

Vile vile yapo matukio mengi ya mambo muhimu yaliyofanyika zaidi kuliko tuliyo yataja katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, na anayetaka kujua yote hayo, avipitie vitabu vya tarikhe na historia. Sisi hapa tumetaka kuandika kwa ufupi basi tukayawacha yote hayo