MLANGO 8

MAELEZO YA KULIPA SAUMU NA KAFFARA

Mahala ambapo ni wajibu kulipa Saumu tu:

(1) Kujitapisha  makusudi mwezi  wa Ramadhani (si kwa dawa). Ni bora hata kulipa kaffara.

(2) Kulala makusudi na janaba (baada ya kujua unayo janaba) na bila ya kuwa na nia ya kuoga na usizindukane mpaka ikiingia asubuhi.

(3) Mtu ijapokuwa hakutenda linalo vunja saumu, lakini nia ya saumu hakuweka, au alifanya Riya (kujipendekeza)  au amenuia  asifunge, au amenuia atende moja lenye kuvunja saumu.

(4) Katika mwezi wa Ramadhani kasahau kuoga janaba na katika hali ya janaba amefunga siku moja au zaidi, basi azilipe zote.

(5) Bila ya kuhakikisha kwamba asubuhi imeingia au bado, na akafanya moja katika yanayovunja saumu, baadaye akatambua kwamba ilikuwa asubuhi. Vile vile baada ya kuhakikisha kwa hali anadhani asubuhi imeingia na akatenda yavunjayo saumu, baadaye ikajulikana kwamba ilikuwa asubuhi; bali hata baada ya kuhakikisha akitia shaka kwamba asubuhi imeshakuwa au bado na akafanya yavunjayo saumu, baadaye akajua ilikuwa asubuhi, lazima alipe siku hiyo.

(6) Mtu aseme kwamba asubuhi bado, na kwa usemo wa huyo, mtu atende yavunjayo saumu, na baadaye akajua ilikuwa asubuhi.

(7) Mtu aseme  kuwa sasa  ni asubuhi,  lakini wewe usemi wake hukuwa na yakini nao, au ufikirie kwamba alikwambia hivyo kwa mzaha tu, ukitenda yavunjayo saumu, na baadaye ikajulikana kuwa ni asubuhi.

(8) Kipofu, na mtu kama huyo, kwa kumsikia mtu akisema magharibi imekuwa na akafuturu, baadaye akajua kwamba haikuwa magharibi.

(9) Ikiwa hali ya hewa safi, lakini kwa kuona kiza imjie yakini kwamba magharibi imeshaingia na akafuturu, baadaye  ikajulikana haikuwa  magharibi.  Lakini ikiwa hali ya hewa ni mawingu mawingu, na akafuturu, baadaye ikajulikana   haikuwa magharibi,   haimpasi kulipa (lakini  hali kama hiyo inambidi ahakikishe kwanza).

(10) Kwa ajili ya kujipoza, au bila ya haja yoyote mtu akisukutuwa,  na maji  ikawa amemeza lazima alipe hiyo  saumu. Lakini kwa kusahau kwamba yeye amefunga akameza maji, au alisukutuwa kwa ajili ya kutawadha na maji yakamezeka   ikiwa ni   ya sala   ya fardhi haidhuru   neon kama tulivyoeleza nyuma, lakini ikiwa sala ya sunna ni mushkili (ina matatizo) na bora alipe ile saumu.

MAELEZO YA KAFFARA

Kaffara za Mwezi wa Ramadhani:

Kama   tulivyoeleza   mwanzo   kwamba   mtu yeyote atakayetenda makusudi katika mwezi wa Ramadhani mambo kumi yanayovunja saumu basi itamlazimu kulipa ile saumu, au kaffara pia, nazo ni hizi itampasa kufanya mojawapo:-

(a) Awache huru mtumwa mmoja.

)b) Afunge miezi miwili (siku sitini).

(c) Awalishe masikini sitini, au awape kila masikini hao sitini mud (kibaba) kimoja cha ngano au shayiri na kadhalika.

Mwenye kutaka kufunga siku sitini, lazima siku thelathini na moja (31) afunge mfululizo na zilizobaki anaruhusiwa kuzigawa.

Ikiwa mtu anataka kufunga hizo sitini za kaffara, basi asianze kufunga wakati ambapo itaingia katika hizo siku thelathini na moja, siku ambayo kufunga kwake ni haramu, kwa mfano, siku kuu kubwa (Idi ya kuchinja nyama). Ikiwa mtu ambaye inampasa kufunga mfululizo siku thelathini na moja, akiacha kufunga siku moja kati ya siku hizo, bila ya udhuru, hapo itambidi kuanza upya hizo siku thelathini na moja, lakini ikiwa umetokea udhuru (ambao kwa sharia unakubaliwa) kama mwanamke kumjia hedhi, au nifasi, au mtu akapata ugonjwa (na kufunga kutamdhuru) au imembidi kusafiri, hawa wote baada ya kuondoka udhuru wao, haitawalazimu kuanzia mwanzo, bali watamaliza, siku zao zilizobaki.

Ikiwa mtu katika hizo kaffara tatu hawezi kutimiza hata moja, basi lazima afunge mfululizo siku kumi na nane (18). Na ikiwa hawezi hata hiyo, basi atoe sadaka kwa kuwapa masikini awezayo mud (kibaba) kila mmoja, na ikiwa kufunga na kutoa chakula mud vile vile hawezi, basi atoe Istighfari kwa kusema AS-TAGH-FIRUL-LAAH, na itamlazimu akipata uwezo baadaye alipe hiyo kaffara.

Ikiwa katika hali ya saumu mtu katenda moja katika vitu vinavyovunja saumu mara nyingi katika siku moja hiyo basi kaffara yake kwa yote aliyoyatenda kwa siku hiyo ni moja katika tatu, isipokuwa kumwingilia mke wa halali na kutoa manii (shahawa) Istimna itarejea kaffara kwa kila uingiliaji.

           Ikiwa kwa kitu cha haramu kavunja saumu yake basi ni wajibu azilipe zote kaffara tatu tulizozitaja hapo mwanzo. Hakuna tafauti kitu kile kiwe tangu asili ni haramu, kama, mvinyo, au kuzini, au kwa sababu fulani fulani kikawa haramu, kama kumwingilia mke wake wa halali katika hali ya hedhi au chakula cha halali ambacho akila kitamdhuru.

(2)Ikiwa mtu anafunga (analipa) kadha, basi haruhusiwi kuvunja hiyo saumu baada ya adhuhuri, na akifuturu basi itambidi kutoa kaffara kwa kuwalisha masikini kumi (10), kila maskini "Mud" moja, na kama hana uwezo huo basi afunge siku tatu mfululizo.

(3) Ikiwa mtu kaweka nadhiri au ahadi au kaapa kufunga siku maalum, na siku hiyo makusudi kabatilisha saumu yake, hapo ni wajibu atoe kaffara, kwa kumwacha huru mtumwa mmoja, au kuwalisha masikini kumi au kuwavisha; na ikiwa hawezi hayo, basi afunge siku tatu mfululizo.

Katika kaffara yoyote haijuzu kulipa pesa badala ya kitu kinachotakiwa utoe.