MLANGO 5

MAMBO YA VUNJAYO  SAUMU

Mambo yavunjayo Saumu, ambayo kila mwenye kufunga ni lazima aepukane nayo (asitende) ni kumi:

Jambo la kwanza na la pili: Kula na kunywa makusudi kitu chochote. Hakuna tafauti ikiwa kitu kile kinaliwa kama mkate au maji, au hakiliwi kama udongo au mafuta ya taa; wala hakuna ukomo wa uchache.   Vile vile hakuna tafauti ikiwa unakula na kunywa kwa mdomo kama desturi au kwa pua, au kwa njia ya kupigwa sindano na kikafika tumboni. Lakini kupenyeza dawa kwa njia ya sindano katika mikono au paja au mahala popote pa kiwiliwili haitadhuru saumu.   Kutia dawa machoni au sikioni haibatiliki saumu.

    Ikiwa unapiga mswaki mara ukautoa, basi lazima upanguse mate mswakini ndipo urejeshe mswaki mdomoni, kwani ukirejesha vivyo hivyo bila ya kufuta yale mate kwenye mswaki na ukiyameza hubatilika saumu, kwa vile mate yale yanahesabiwa kitu cha nje; lakini mate yako ya mdomoni humo humo ukimeza haidhuru saumu. Mtu aliyefunga, ikiwa kwa kusahau akila au akinywa kitu chochote haibatiliki saumu yake, lakini akifahamu tu, hapo hapo itamlazimu awache kula na kutema kilicho kinywani; na akila kilicho bakia kinywani, basi saumu hubatilika.

    Kutafuna chakula kwa ajili ya watoto au ndege, na kuonja chakula (kwa wapishi) ambao kwa desturi hakifiki kwenye koo, na hata ikifika si makusudi haitabatilisha saumu; lakini mtu akijua tangu mwanzo kwamba itafika kooni, hapo itabatilika saumu yake, lazima alipe na itampasa atoe kaffara pia.

     Na kama tulivyosema katika 'Kitabu cha Sala' kwamba moja katika suna za kutawadha ni kusukutua mara tatu, basi ' katika hali ya saumu, ikiwa unatawadhia sala ya fardhi, na katika kusukutua maji yakamezeka, haitadhuru saumu, lakini ikiwa unasukutua kusafisha mdomo tu, au kujipoza kwa joto basi yakimezeka maji hubatili saumu, na itakubidi ulipe hiyo saumu.

 Kumeza kohoo (belghamu) inayotoka kifuani ikiwa haikufika kwenye ukingo wa mdomo haitadhuru saumu, lakini kamasi itokayo kichwani (ndani ya pua) ikifika mdomoni usiimeze.

 Jambo la tatu: Kuingiliwa mtu na utupu katika utupu wake saumu ya wote wawili hubatilika, hata kama hawakutoa manii (shahawa). Ikiwa mtu katika hali ya saumu amelala akaota usingizini na ikamtoka shahawa, saumu yake haitavunjika, bali itampasa kuoga janaba anapotaka kusali.

  Jambo la nne: Istimna. Kutoa manii makusudi kwa njia yeyote, hata kama unafanya mahaba na mke wako. Lakini kama ukiwa na hakika kwa kufanya vile haitatoka na ikaja kutoka (si kusudi) saumu haitabatilika.

  Jambo la tano: Kusema uwongo (kuwasingizia) juu ya Mwenyezi Mungu, Mtume (S.A.W.), Maimam kumi na wawili (A.S.) mmoja wapo, Bibi Fatima (A) mitume wa haki wote na Awsiyaa (warithi) wao. Kwa kutoa hadithi hakuna tafauti katika kuwasingizia mambo ya dini au dunia.

  Jambo Ia sita: Al Irtimaas. Kuzamisha kichwa chote katika maji makusudi. Hakuna tafauti ikiwa kiwiliwili kipo ndani au nje ya maji. Muradi wa kichwa ni upande wote wa juu ya shingo. Ikiwa umepiga mbizi kwa kusahau tu, haitabatilika saumu.

Jambo la saba: Kufikisha vumbi au moshi nzito au isio nzito kwenye koo makusudi (kwa kuwacha kinywa au pua wazi pasipo kuzuia kwa kitu kama leso, kiganja au kitu chochote). Ikiwa baada ya kujizuia ikapita vumbi hapo haitabatilika saumu kwani hukufanya makusudi:

Jambo la nane: Kukaa na janaba hadi alfajiri makusudi hukuoga ni haramu, na saumu hubatilika na itakupasa kulipa kadha na pia kaffara. Vile vile mwanamke ikiwa amefunga damu yake ya hedhi au nifasi usiku, na hakuoga kabla ya alfajiri itakuwa hukumu yake kubatilika saumu tu, ijapokuwa bora kaffara vile vile alipe. Haibatiliki saumu yeyote ikiwa mtu kwa kuota usingizini mchana yakamtoka manii.

Ikiwa mtu ameshajiona kwamba anayo janaba usiku, na akalala pasipokuwa na dhamiri ya kuoga na hakuzindukana mpaka asubuhi, basi hukumu yake sawa na kukaa na janaba hadi alfajiri. Lakini ikiwa amelala kwa dhamiri ya kuoga kabla ya alfajiri na usingizi ukamchukua mpaka asubuhi mtu huyu saumu yake haibatiliki. Ikiwa mtu amelala akazindukana na akaona anayo janaba, kwa kuwa upo wakati mwingi hadi alfajiri, akalala tena kwa nia ya kuamka na kuoga kabla ya alfajiri, alipoamuka safari hii akaona bado upo wakati, akalala tena asiamke mpaka asubuhi, basi mtu huyo saumu yake hubatilika na lazima baadae alipe. Na ikiwa mtu huyo aliamka mara ya tatu na kwa kuona bado upo wakati akalala tena na hakuzindukana mpaka asubuhi, saumu itabatilika alipe kadha na juu ya hayo alipe kaffara.

Ikiwa mtu amesahau kuoga janaba usiku, hadi ikapita siku moja au zaidi katika mwezi w a Ramadhani, basi saumu za siku zote hizi hubatilika na itampasa kuzilipa ikiisha Ramadhani. Ikiwa mtu usiku anajua akijitia janaba (akimwingilia mkewe) hana wakati wa kuoga au kutayammamu na akafanya, basi itakuwa hukumu yake sawa na yule aliyekaa makusudi na janab hadi alfajiri.   Lakini ikiwa ameweza (amewahi) kutayammamu hapo saumu yake itasihi ijapokuwa amefanya dhambi, na ikiwa hakuifanya hiyo tayammamu, saumu yake itabatilika na itamlazimu alipe baadaye.

Ikiwa kabla ya adhana ya sala ya asubuhi mwanamke imefunga damu yake ya hedhi au nifasi, na wakati wa kuoga hana, na anataka kufunga fardhi au kulipa kadha, basi hapo hapo lazima atayammamu, na lazima akae macho mpaka adhana ya asubuhi.

   Jambo la tisa: Kupiga bomba nyuma kwa kutilia dawa ya maji maji kwa mgonjwa (kwa ajili ya kujitibu) saumu hubatilika, itampasa kulipa. Lakini ikiwa anatia kitu kikavu kwa dawa basi haibatiliki saumu.

Jambo la kumi: Kujitapisha makusudi, hata ikiwa kwa dawa kwa ajili ya kujitibu vile vile saumu hubatilika. Lakini mtu akitapika bila ya kusudi basi hapo haitadhuru saumu.

Mtu akila usiku kitu chochote ambacho anahakika kwa kula kitu hicho, mchana atatapika bila kutaka, basi saumu ya siku hiyo itambidi baadaye ailipe.

    Mambo yote haya kumi yanavunja saumu kama tulivyo taja ikiwa mtu anafanya kwa makusudi basi bila shaka hubatilika saumu yake. na alipe kaffara pia, wala hakuna tafauti kwa wale wenye kuzijua hukumu hizo, au kwa wasio jua.

Mambo yenye karaha katika hali ya saumu

Ni karaha mchana: (1) Kucheza mtu na mke wake wa halali, au kumbusu ikiwa hakukusudia kumwaga shahawa, au sitabia yake kwa kufanya hayo kumtoka. Lakini ikiwa anajua au ni tabia yake akifanya humtoka basi ni haramu kwake hata kama haikumtoka, kwani amekusudia kuvunja saumu; (2) Kutia machoni wanja ikiwa ladha au harufu ya wanja inafika kwenye koo; (3) Kujitoa damu au kufanya jambo tolote lenye kumdhoofisha; (4) Kunusa kila aina ya maua yenye harufu kali nzuri, (S) Kuvaa nguo majimaji au Kujilowesha nguo; (6) Kukaa mwanamke ndani ya maji; (7) Kung'oa jino; (8) Kusukutua bure; (9) Kusoma mashairi yeyote isipokua mashairi ya sifa, au masaibu juu ya Mtume (S.A.W) na Ahlibayti wake (A.S.)