Sheria za Kiislamu Katika Dunia ya Kisasa

Mtungaji:Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari

Mfasiri:Muhammad Rida Shushtary

Ndugu Wasomaji:

Sasa tunaingia mwaka wa saba tangu kufani­kiwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba ingawa maadui wa Uislamu wakiongozwa na Shetani Mkubwa (Marekani) wamefanya njama zao zote dhidi ya Mapinduzi haya makubwa lakini hata hivyo yameweza kuimarika na kufikisha sauti yake kwa Waislamu na wanyonge wote duniani na kila siku yanaipa tumaini Ia kuwakomboa.

Hakuna shaka yoyote kwamba siri ya mafanikio ya Mapinduzi haya yanatokana na kuwa na imani juu ya Mwenyezi Mungu, kufuata sheria za Kiislamu na kumfuata kiongozi mkuu wa Mapinduzi, Imam Khomeini.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa tawfiki ya kuchapisha kitabu hiki kwa mnasaba wa kuadhimisha Alfajiri Kumi [siku kumi za kusherehekea Mapinduzi ya Kiislamu na tuna­mwomba atuimarishe kusimama barabara kwenye mstari wa haki wa Kiislamu na atupe uwezo wa kuwa na jitahada za kuendeleza harakati za kuyafikia malengo ya Kiislamu na kuzitekeleza sheria zake katika maisha yetu yote.

Tunategemea uwezo na msaada wa Allah.

Kamati ya Kuadhimisha Mwaka wa Sita wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kijitabu ulichonacho mkononi ni mojawapo kati ya mihadhara yenye thamani na faida ya Ustadh Shahid Murtadha Mutahhari. Mhadhara huu wenye mada: Sheria za Kiislamu katika Dunia ya Kisasa ulirekodiwa kisha ukanukuliwa na kufasiriwa kwa lugha ya Kiswahili.

Idara ya Kimataifa ya Taasisi ya Tablighi ya Kiislamu ambayo mpaka hivi sasa imekwisha­chapisha na kutangaza vitabu kadhaa vya Ustadh Mutahhari katika lugha mbalimbali za dunia, ina furaha pia kukichapisha kijitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili na kukigawa kwa wote wenye kupenda haki.

Ingawa kijitabu hiki ni kidogo kwa ukubwa lakini kimejaa maudhui ya maana. Tunatumai kwamba kijitabu hiki kitaweza kutimiza wadhifa wake wa kufahamisha Uislamu katika zama hizi za maisha mapya ya Uislamu, na kitatoa faida kwa Waislamu wote kwa jumla na hususan kwa vijana.

Idara ya Kimataifa ya Taasisi ya Tablighi ya Kiislamu

Kwa jina la Allah,

Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Maudhui ya mjadala wetu unahusu kanuni (sheria) za Klislamu na namna zinavyoweza kuafikiana na ustawi na mabadiliko ya dunia ya kisasa.

Katika mjadala wetu huu, kuna mambo mawili: Sheria za Kiislamu, na historia hasa ambayo ni ustawi, maendeleo na mabadiliko ya ulimwengu wa kisasa. Bila ya shaka, makusudio yetu kuhusu dunia ya kisasa hayana maana kwamba kuna tukio au jambo la pekee tu linalo­itwa "ustawi na mabadiliko." Ustawi na mabadi­liko ni mambo yaliyo lazima katika maisha ya binadamu. Tangu siku za awali wakati binadamu alipotokeza duniani na kuanzisha maisha ya kijamii, hali yake iliendelea kustawi na kubadilika katika vipindi mbalimbali hadi kufikia katika zama za kisasa. Hakuna shaka kwamba katika zama hizi ambazo ni zama za kisasa kwa dunia ya leo, imepatikana hatua kubwa sana katika maendeleo na ustawi ambayo huenda haikuwahi kupatikana katika zama zilizopita.

Kuna haja ya kuzungumzia mjadala huu, kwani tuna haki ya kupendelea na kutetea mambo hayo mawili: Tuna haki ya kuupenda Uislamu, na tuna haki pia ya kupenda ustawi, mabadiliko na maendeleo ya kistaaarabu. Lakini hapa lazima tuangalie kwamba, tunawezaje kuyapenda mambo hayo mawili kwa wakati mmoja? Yaani, tuwe Waislamu wa kweli na wenye kufuata mafundisho ya kidini na wakati huohuo tuwe tunafuata ustawi na mabadiliko ya dunia kwa kuwa pamoja na maendeleo na ustaarabu.

Tunajua na tunaona kwamba katika jamii yetu kuna matabaka mawili, ingawa tabaka la tatu lipo pia. Kwa ujumla, katika jamii yetu kuna matabaka matatu: Tabaka la kwanza ni la wenye kushika dini. Katika jamii yetu ambayo ni ya Kiislamu, watu wengi ni wenye kushika dini ya Kiislamu na wanafikiri kwamba ni wajibu kwa kila Mwislamu na mwenye kushika dini kuchukia mabadiliko na mambo mapya yanayozuka katika zama hizi. Wao wanadhania kwamba matukio hayo mapya ni mambo ambayo yanapinga dini, hivyo, wanayatazama kwa macho mabaya, wana­rudi nyuma na daima huwa wanafuata jamii. Hii ina maana kusema kwamba wakati tabaka hili linaposhindwa kabisa kukabiliana na matukio mapya ya kijamii, hapo ndipo linaposalimu amri na kufuata jamii. Mfano mmoja mzuri unao­fanana na hali na fikra ya watu kama hao una­elezwa katika ubeti huu:

Alifanyalo jahili, kila jambo kulipinga,

Mwishowe hastahmili, kutokana na ujinga,

Ama mwenye akili, na wenzake hujiunga,

Kizuri kukikubali, kuwa pamoja na mwanga.

Jambo analolifanya jahili na mjinga, mwerevu pia hulifanya; lakini mjinga mwanzo hulipinga jambo hilo mpaka mwisho wake hulikubali baada ya kufedheheka na kushindwa. Lakini mwerevu kwanza hulipima kila jambo. Amirul Muuminiyn 'Ali AS anasema hivi katika Nahjul Balagha kuwalaumu masahaba zake: "Kwa nini kina sisi na nyinyi tuwe na tabia ya kupinga!?"

Hapa "kina sisi" inakusudiwa kuwa ni jamii. Kitu tusichokijua hatukifahamu wala hatukiulizi habari zake mpaka kitokeze na kijulikane kwetu. Hatufikirii kulitatua jambo lolote bali siku zote tunafikiria kulipinga. Huu ndio ubovu wetu. Kwani ni lazima kulifikiria kuhusu jambo moja kabla hata bado halijatukia. Katika mlango wa Akili na Ujahili wa kitabu cha al-Kafi kuna hadithi moja iliyopokewa kutoka kwa Imam Sadiq AS akisema: 'Mwenye kujua zama zake hatofanya makosa."

Ninalotaka kusema ni kuwa kuna watu wa tabaka moja ambao kwa kutumia jina la dini wanajitenga na ustaarabu, maendeleo na ustawi wa maisha. Vilevile, mkabala wao kuna watu wa tabaka jingine ambao kwa kutumia majina ya ustaarabu, ufanisi wa sayansi, mahitaji ya zama na majina mengine kama haya, wanakata uhusi­ano wao na dini na wanapinga ukweli wa mafundisho ya kidini. Tabaka hili hupinga kila kitu ambacho kinaimarisha dini, na kwa maoni yao, neno "kadimu" au “uzoefu" ambalo maana yake ni "hali ya kuwa na maarifa, ujuzi au mazoea juu ya jambo au kitu kwa muda mrefu" lina maana sawa na "kuukuu", "kongwe" na "zamani." Naam, haya ni maana mawili. "Kadimu" yaani "ya zamani sana", "ya miaka mingi", n.k. Si lazima kwamba kila kitu kilicho kadimu, yaani cha zamani sana, lazima pia kiwe kikuukuu, hakifai na kiharibiwe. Maneno haya hayana faida, lakini watu wanaofikiria hivyo, fikra zao ni kinyume cha fikra za watu wa zamani ambao walikuwa wakikitukuza kila kilicho cha zamani au kadimu. Walikuwa wakisema: "Kitu hiki ni cha zamani, hivyo, ni kizuri zaidi." Sasa maoni ya watu wengine ni kinyume na hayo - kila kitu cha zama, kwao ni kitu kibaya, kikuukuu na hakifai. Maneno kama haya yanatufahamisha kwamba kuna hoja ya kuweko tabaka la watu wa kati (wastani) ambalo linapati­kana katika jamii kwa wachache. Sisi ni katika tabaka la kati. Kwa hivyo, wadhifa na wajibu tulionao ni muhimu na mkubwa. Jukumu letu ni kufanya uchunguzi na udadisi kamili juu ya suala hili. Je, inawezekana au haiwezekani watu wote wakawa Waislamu na washika dini na wakati huo­huo maisha yao yakawa yanaafikiana na kukubaliana na mazingira, mahitaji na maendeleo ya zama zao? Suala hili ni mushkili zaidi kwa dini ya Kiislamu kuliko dini zote nyinginezo kwa sababu Uislamu una sifa ya kuwa ni dini ya daima dawamu, wakati dini nyinginezo zimetangaza umwisho wa utume na kutoendelea wadhifa wa utume. Dini hii ya Kiislamu ndiyo dini itakayoendelea kuwepo siku zote, na hakuna dini nyingine mpya itakayokuja duniani baada yake.

Tatizo jingine ni ustawi wa Uislamu wenyewe. Lau Uislamu ungekuwa kama dini nyinginezo ambazo zimejitosheleza kwa maamrisho machache ya ibada, mafundisho na maadili kadhaa bila ya kuwa na sheria katika vipengee mbalimbali vya maisha ya binadamu, basi usingesumbuka sana kutokana na tatizo hili. Naam, suala la ibada si muhimu sana. Katika kila zama watu wanafanya ibada kwa namna maalum. Hata mawaidha machache si muhimu sana. Lakini Uislamu ni dini ambayo imeweka halali na haramu nyingi sana, na imeweka kanuni maalum katika kila jambo la maisha ya binadamu. Hivyo, kufuatana na mjadala huu, kazi za Uislamu na Waislamu ni mushkili zaidi.

Mjadala huu hautoshi kujadiliwa katika kikao kimoja na kujibu maswali yote kwa ukamilifu. Mahafali haya ni msingi tu kwa ajili ya mtaala na uchunguzi. Kuna miswada ambayo inatayarishwa kuchapishwa katika sura ya kitabu na rafiki yangu mmoja mkazi wa Mashhad. Miswada hiyo ambayo ni mingi niliandika tangu zamani kuhusu Uislamu na Mahitaji ya Zama. Miswada hiyo asili yake ni mihadhara yangu ipatayo 25 ambayo nilitoa kuhusu somo hili [katika msikiti mmoja]. Vilevile kuna maandishi yangu mengine ambayo yamechukuliwa na mtu fulani ili ayasanifu na kuyafanya kuwa kitabu kimoja. Juu ya yote hayo, mimi sichukulii kitabu hicho kuwa kina­tosheleza kujibu maswali yote.

Kwa hivyo, mjadala wetu utakuwa na sura ya faharasa na mwongozo zaidi, na vilevile utakuwa ni ufunguo wa kutatua mushkili huu. Mjadala wetu unahusu masuala mawili: Suala la kwanza linahusu ustawi, maendeleo na mabadi­liko ya historia, na suala la pili linahusu mahitaji ya zama.

Mabadiliko katika Kilichotukia

Ustawi, ufanisi, maendeleo, mabadiliko na mageuzo ya historia ni katika mahitaji ya kimsingi ya maisha ya binadamu. Historia ya binadamu inabadilika lakini hakuna mabadiliko yoyote katika maisha ya mnyama yeyote au viumbe vya kijamii kama vile nyuki. Maisha na tabia ya nyuki haikubadilika. Kwa mfano, maandishi ya miaka elfu kadhaa iliyopita juu ya maisha ya nyuki yanathibitisha kwamba muundo na hali ya maisha ya nyuki ilivyo leo ni kama vile ilivyokuwa zamani. Lakini kinyume chake, miundo na hali ya maisha ya binadamu kila siku inabadilika. Siri ya jambo hili linabainishwa na Qur'ani wakati inaposema kwamba binadamu ni kiumbe wa pekee ambaye yeye mwenyewe tu ndiye mwenye jukumu juu ya maisha yake. Hii ina maana kwamba viumbe vingine hata vile viumbe vyenye kuishi kijamii - maisha yao yana­ongozwa na kusimamiwa na maumbile. Silika ndiyo inayodhibiti maisha yao, wala viumbe havikupewa haki na uwezo wa kuingilia au kugeuza silika yao, wala havikupewa jukumu Ia kustawisha na kuendeleza maisha yao. Maisha yao yanafuata jinsi asili na maumbile yao yalivyokuwa tangu kuumbwa kwao. Lakini bina­damu ni kiumbe anayeanzia katika udhaifu au sifuri na anaendelea katika mwendo wa kujikamilisha. Bila ya shaka mwendo wake hufuata miongozo ya manabii na mitume. Yeye mwe­nyewe ndiye mwenye jukumu la kujikamilisha binafsi. Ni lazima kwa binadamu kutumia akili, uwezo na jukumu lake ili ajikamilishe.

Kuhusu suala la mabadiliko ya maisha ya binadamu, kuna mambo kadha wa kadha ambayo kati yao baadhi yake mmeyasikia au mmeyasoma vitabuni. Tunapozungumzia suala hili, wapinzani wanasema: "Uislamu hautoshelezi zama zetu." Wabishi hao hutoa dalili moja ya kifalsafa ambayo inasema kwamba kanuni asilia ya ulimwengu huu hubadilika na iko katika mwendo (harakati). Hakuna hata kitu kimoja duniani ambacho kiko thabiti. Hakuna kitu kimoja katika nyakati mbili kiweze kuwa na hali moja na sawa. Sisi wenyewe ambao tumekaa hapa tukidhania kwamba kama tulivyokuwa jana ndivyo vivyo hivyo tulivyo hivi leo, kwa hakika leo yetu ikilinganishwa na jana yetu imebadilika sana, isipokuwa tu mabadiliko hayo hatuyahisi.

Tunapotazama akrabu inayoonyesha saa tunaona kuwa imesimama, na kila tukitazama zaidi hatuoni mwendo wowote, lakini baada ya saa moja tukitazama tena tutaona kwamba imekwenda 1/12 ya duara la uso wa saa. Kwa hivyo, kutoona kwetu mwendo wa saa hakumaanishi kwamba hakuna mwendo. Maelezo mengi yame­tolewa kuhusu suala hili la asili na namna mwendo (harakati), mabadiliko na mageuko katika ulimwengu yalivyo. Wanafalsafa wa Kiislamu wanaamini kwamba johari (atomi) ina harakati, na kwamba maumbile ni sawa na harakati, hivyo yanabadilika. Ikiwa kitu cha asili kabisa duniani, yaani maumbile, yanabadilika, hivyo hakuna kitu chochote chenye kuishi milele. Naam, dini ni mojawapo wa vitu au matukio ya dunia, hivyo dini haiwezi kubaki daima. Vitu vyote duniani haviwezi kuwepo tangu na tangu. Ikiwa tutaliangalia suala hili kwa mujibu wa nadharia ya kifalsafa tu, basi jibu lake litakuwa rahisi sana, nalo ni kwamba: Kile kinachobadilika na kugeuka ulimwenguni ni matukio ya dunia, yaani matukio au vitu vya kimaada au vya kidunia. Na hapana shaka yoyote kwamba matukio ya ulimwenguni yanageuka na kubadi­lika. Kwa mfano, Mtume Mtukufu Muhammad SAW mwenyewe ambaye ni tukio moja katika matukio ya ulimwenguni, alibadilika katika sura mbalimbali - alizaliwa mtoto mchanga, alikua tangu udogoni na akawa kijana, kisha mzee na hatimaye akafariki dunia. Qur'ani inasema:

"Kwa hakika wewe utakufa na wao (pia) wata­kufa." (39:30)

Mjadala wetu unahusu kanuni za dunia. Je, zinabadilika? Jua na mwezi vinakuwa vikongwe na siku moja vita angamia. Nyota, mimea, wanyama na viumbe vyote vya duniani vinakuwa vikuukuu na mwishowe vitaangamia. Lakini je, huu ni ushahidi wa kwamba kanuni za kifizikia au kimazingira nazo pia zinakuwa kuukuu? Uislamu wenyewe ni kanuni wala si tukio. Kila kinacho­badilika ni tukio, walakini Qur'ani (yenye sheria za Kiislamu) ndiyo itakayobaki na Mtume ata­kufa. Mshairi mmoja amesema:

Mustafa aliahidi

Baada ya kutuahidi

Kwa Molaye atarudi

Kama wote maujudi

Ila tabaki abadi

Qur'ani Yake Mawdudi

Kwa viumbe kustafidi

Sheria ziso na hadi

Kuhusu Mtume Mtukufu, Mwenyezi Mungu anasema: "Kwa hakika wewe utakufa na wao (pia) watakufa.” (39:30) Na kuhusu dini ya Kiislamu, anasema:

"Hakika Sisi tumeteremsha Kumbusho (Qur 'ani), na hakika Sisi ndio tutakayoihifadhi." (15:9)

Qur'ani tunayoikusudia si haya makaratasi ya Msahafu ambayo yanachanika, yanafujika na yanaoza, bali ni ukweli na hakika ya Qur'ani.

Sheria za Kiislamu Zinabadilika?

Mafundisho ya Kiislamu ni mafundisho ya maana wala si ya dhahiri bila kuwa na maana yoyote. Kwa hivyo, mjadala wetu lazima uwe juu ya msingi wa maana na hekima. Ikiwa mafundisho ya Kiislamu yanatambulikana kwa sheria zake, hivyo, lazima tuangalie kwa kiasi gani sheria hizo zina sura ya kimaumbile. Vipi zinatabikiana na kukubaliana na muundo wa maumbile? Uislamu unafahamisha sheria. Sheria za Kiislamu zilizoelezwa, na Mwenyezi Mungu zimezingatia maumbile, binadamu na jamii. Sheria zimezingatia mfumo wa maisha ya binadamu. Kwa hivyo, tukitoa dalili hii yenye kuthibitisha kudumu kwa Uislamu (kama wanavyoandika waandishi wengi katika vitabu vyao kwa kutegemea msingi wa mabadiliko na msingi huo wa kifalsafa) hapana shaka tuta­ambiwa: "Ee Bwana! Maneno hayo si sawa. Kinachobadilika, kinachokuwa kikuukuu, kina­chooza, kinachoharibika na kinachoangamia ni matukio (vitu)."

Sheria haingii katika hoja hii. Sheria lazima ijadiliwe kwa hoja tofauti. Kuna kikundi kingine kilicho afadhali kidogo. Kikundi hicho ingawa kinakubali kwamba sheria za maumbile hazibadiliki, lakini kinasema kwamba sheria zote zinazohusiana na maisha ya binadamu zinabadi­lika kwa kuwa maisha ya binadamu yanabadilika. Kwa dalili gani? Wanasema kwa sababu binadamu ni kiumbe ambaye ana jukumu juu ya nafsi yake mwenyewe, na kwamba kwa kuwa maisha na mahitaji ya binadamu yanabadilika, hivyo, sheria huwekwa ili kukidhi mahitaji yake. Hii ni shabaha ya sheria. Sheria huonyesha njia ya kuti­miza haja za binadamu kiheshima na kiadilifu. Hivyo, msingi wa sheria ni kutosheleza mahitaji ya kijamii.

Sasa tuje kwenye suala la mahitaji. Je, mahi­taji ya binadamu ni ya namna moja daima au yanabadilika? Mahitaji ya binadamu yanabadilika. Mahitaji ya binadamu katika zama za uvuvi yali­kuwa ya namna moja na katika zama za uwindaji yalikuwa ya namna nyingine. Na katika zama zetu za mashine mahitaji ya binadamu ni ya namna nyingine kabisa. Kwa kawaida, ikiwa mahitaji ya kila zama yatabadilika, vivyo hivyo, sheria lazima zibadilike. Hii ina maana kwamba mahitaji ya kila zama yatatofautiana.

Tuchukulie mfano mmoja. Je, katika miaka mia moja iliyopita, binadamu alihitajia sheria za trafiki? Kwa mfano, sheria za barabarani za kuendesha upande wa mkono wa kulia au kushoto; kupiga faini kwa kosa Ia kitrafiki, n.k. Hapakuwepo haja ya kuwepo sheria za trafiki katika zama za punda kwa sababu hapakuwepo tatizo la trafiki katika mawasiliano ya watu. Suala la trafiki limezushwa na magari.

Sheria nyingi za kimataifa hazikuhitajiwa zamani, k.v. sheria za kimataifa za vyombo vya baharini. Haya ni mahitaji mapya na sheria mpya. Sheria zinazohusu mawasiliano ya angani ni sheria zinazohusu mataifa yote na zinakubaliwa na watu wote. "Kwa kuwa mahitaji yanabadilika hivyo sheria lazima zibadilike pia."

Hapana shaka kwamba maneno haya haya­husiani na hoja yetu. Hata hivyo, ni lazima tuzungumzie juu ya suala hili. Ingawa ni kweli kwamba wakati mazingira ya binadamu yanapo­badilika mahitaji yake hubadilika pia, lakini suala lenyewe si rahisi kama linavyoelezwa kwa maneno hayo. Kwa nini? Kwa sababu binadamu ana mahitaji yaliyo thabiti na ya siku zote, na mahitaji yanayobadilika na ya muda maalum tu. Si mahitaji yote ya binadamu yanayobadilika. Mahitaji yanayohusiana na maana na shabaha ya maisha ya binadamu ni mahitaji yaliyo thabiti, na mahitaji yanayohusiana na muundo (sura au mazingira) wa maisha ya binadamu ni mahitaji yanayobadilika na kugeuka. Huwezi kuchukulia kubadilika daima kwa muundo wa maisha ya binadamu kuwa ni dalili ya kubadilika kwa maana na roho ya maisha ya binadamu. Mambo ya kidini yanahusiana na roho na msingi wa maisha wala hayahusiani na muundo wa maisha. Ukichungua mafundisho ya Kiislamu hutaona kwamba yanatilia mkazo muundo wa maisha. Huwezi kusema kwamba muundo wa maisha ubaki thabiti bila ya kubadilika. Uislamu unaupa uzito maana na roho ya maisha. Nimetoa mfano wa binadamu kuhusu suala hili. Ulimwengu pia uko katika hali kama hii.

Suala la Uthabiti na Ubadilikaji

Kusema kwamba kila kitu ulimwenguni kina­badilika si sawa. Maumbile ni sura ibadilikayo ya ulimwengu. Lau ulimwengu haungekuwa na sura iliyo thabiti basi kusingewezekana kuwepo sura ibadilikayo. Ikiwa kila kitu kitabadilika kama alivyoitakidi Heraclitus hapo zamani na itikadi yake ikafuatwa na watu wengi - basi hakutabaki kitu chochote kuwa sawa katika nyakati mbili wala hapatakuwepo uhusiano wowote kati ya zamani na sasa; hivyo, hapatawezekana kuwepo kanuni yoyote ulimwenguni. Ukweli ni kuwa ulimwengu huu una maumbile yanayobadilika na kwa wakati huohuo pia una hali iliyo thabiti ambayo ndiyo inayohifadhi hali ibadilikayo ya ulimwengu huu. Lau isingekuwepo hali igeukayo, hali thabiti isingekuwepo pia.

Wanafalsafa wa Kiisiamu ambao walizungu­mzia suala Ia mwendo wa atomi (harakati za johari) wakati huohuo walizingatia pia sura thabiti ya ulimwengu. Walisema kwamba ingawa maumbile yanabadilika lakini yana roho ambayo daima ni thabiti.

Kwa ufupi, katika ulimwengu mzima kuna mambo yaliyo thabiti katika sura na hali ibadili­kayo. Tuangalie viwiliwili vyetu vyenyewe - lau tusingekuwa na roho au maisha isiyotetereka au miliki maalum, basi viwiliwili navyo pia visinge­badilika. Sisi ndisi; ndio wanadamu wenyewe tuliokuwepo miaka arobaini, hamsini, sitini au sabini iliyopita ingawa viwiliwili vyetu vilibadilika mara nyingi sana. Baadhi ya viwiliwili vyetu vili­kauka na kutoka. Kwa mfano, sehemu moja ya viwiliwili vyetu iligeuka kuwa kucha; kucha tukazikata na kuzitupa katika madebe ya taka. Na sehemu nyingine ya viwiliwili vyetu ilikuwa katika umbo jingine kama seli za ngozi zetu, zikakauka na zinatoka. Mwenyezi Mungu anajua hivi viwiliwili vyetu miaka kumi iliyopita vili­tupwa katika madebe ya taka gani, au katika vyoo gani; au mahali gani? Lakini tuishio ndio sisi, kwa kuwa roho zetu zimebaki.

Maisha ya kijamii ya banadamu yamefanana sawasawa na viungo vya binadamu. Vivyo hivyo kwa ulimwengu – vyote vina roho thabiti (isiyobadilika) na maumbo yabadilikayo.

Binadamu tangu zama za zamani amekuwa na haja ya kuyawekea maumbile yake nidhamu na utaratibu. binadamu alikuwa na maumbile ya kuashiki, kupenda cheo na maumbile mengine mbalimbali. (Ni suala jingine ikiwa vyanzo vyake ni vimoja au tofauti). Alikuwa nayo maumbile ya kijinsia, ya kutafuta elimu na kuchunguza; maumbile ya uzuri, wema ihsani, maadili na maumbile ya kuabudu. Lakini binadamu alihitaji maumbile yote hayo yawe na nidhamu na utaratibu mmoja. Na nidhamu hiyo inaitwa maadili (akhlaq). Maadili ni tofauti na adabu. Kile kinachohusu utoaji wa mpango mzuri wa kutenda jambo, yaani nidhamu haibadiliki. kwa mfano, miongoni mwa misingi ya ulezi katika binadamu ni kuifanya akili ndiyo yenye kutawala matamanio na matakwa ya binadamu. Wahenga wamesema kwamba “Akili itawale nafsi.” Hii ni kanuni moja kwamba kiwiliwili kinazeeka na maumbile ya ulimwengu yanakuwa makuukuu pia. Kanuni hii au msingi huu hauwi mkuukuu.

Kwa mfano, unaweza kusema kwamba: “Ni jambo zuri kwa binadamu kujitetea.” Haya ni maadili ambayo hayawezi kuwa makuukuu hata ikipita miaka elfu moja. huwezi kusema kwamba: “Zamani lilikuwa jambo zuri mtu kujitetea na kuvumilia lakini sasa si jambo zuri mtu kujiamini mwenyewe au kujitegemea mwenyewe.” Mambo haya hayawezi kubadilika. Mambo mengine yote ya kijamii, k.v. kusema kweli na kutosema uwongo, kuwa mwaminifu na kutofanya hiana, uadilifu, uhuru, usawa na kadha wa kadha, yote haya yanahusiana na roho au uhai wa maisha, hivyo hayawezi kubadilika.

Je, unaweza kusema kwamba ilivyokuwa dunia ya leo ni dunia ya kisasa, hivyo haiwezi kukubali maneno hayo? kwa hivyo, uadilifu, usawa na kupendana kumekuwa kuukuu? Tunaona leo kwamba kila taifa lina historia yake ambayo alikuwepo mtu miongoni mwao aliyesimama kupigania uadilifu, usawa na uhuru miaka elfu kadhaa iliyopita. Je, tunaweza kusema kwamba kupigania kwake kulikuwa bure? Hapana shaka hakukuwa bure kwani aliyoyapigania yalikuwa no mambo yaliyohusu roho ya maisha wala hayakuwa umbo au sura ya maisha.

Binadamu na Mahitaji ya Zama

Suala hili tunalizungumzia hapa kwa kugusia tu. Kwa hivyo, ikiwa mtu atataka kutuambia kuhusu suala hili kwamba mahitaji ya binadamu yanabadilika, sisi tutamjibu kwamba: "Ndiyo, lakini si kama unavyosema wewe. Binadamu ana mahitaji ya aina mbili. Mahitaji yaliyo thabiti na ya daima, na mahitaji yanayobadilika. Kwa hivyo, si sawa kwa jumla kuwa mahitaji yana­badilika."

Uislamu unasemaje kuhusu mahitaji yaliyo thabiti na yanayobadilika? Nitalizungumzia suala hili katika sehemu nyingine ya mjadala wangu. Sasa tunataka kulizungumzia suala jingine, nalo linahusu mifano michache ya falsafa ya Ulaya na hasa falsafa ya [mwanafalsafa George Wilhelm Friedrich] Hegel [1770-1831] ambayo inalipa umuhimu mkubwa suala Ia utaifa na ukabila. Hegel ameliita suala hilo "Utovu wa Kukosea Zama" - yaani zama ina hali ambayo haikosei. Hegel anaitakidi kwamba utaifa au roho ya taifa moja daima huenda mbele na huongozwa na akili kamilifu. Kwa hivyo, roho ya taifa haiwezi kukosea. Mtu anaweza kukosea lakini roho ya taifa haiwezi kukosea. Kwa maana nyingine, roho ya zama haiwezi kukosea. Baadhi ya wana­falsafa licha ya roho ya zama wanaitakidi kwamba hata roho ya jamii ya kibinadamu haikosei pia! Mambo haya vipi?

Ni lazima hapa niseme kidogo kuwajibu mabwana hao kwamba suala hasa si hilo wanalo­lizungumzia wao, bali suala lenyewe ni hili, kwamba: Zama si kitu ambacho tunaweza kusema kwamba chenyewe kinakosea au haki­kosei. Kinachotolewa na binadamu katika jamii kinatofautiana. Baadhi ya wakati maua huchanua kwenye akili, elimu, utafiti na uchunguzi wa binadamu. Hayo ni mambo ambayo ingawa huenda binadamu kwayo akakosea lakini kwa wastani tukiyatilia maanani tutaona kwamba kila binadamu anavyozidi kuendelea mbele basi makosa yake hupungua na huelekea kwenye kutafuta uhakika. Matukio ya kila zama ambayo ni matokeo kamili na halisi ya elimu, utafiti na akili ya binadamu ni lazima yatabikiane (yalin­gane) na ulimwengu. Ni muhali katika baadhi ya sehemu binadamu asijisawazishe na dunia, kwani hawezi kushindana nayo.

Chombo kipya kinapoundwa lazima kiwe rahisi, kiwe na nguvu zaidi na kudumu zaidi. Katika ulimwengu wa uchumi; yule mtu anaye­tumia gharama kubwa kutengeneza vitu kwa kutumia chombo cha kizamani kisha ikambidi aviuze kwa bei ghali, hawezi kabisa kushindana na yule mtu anayeuza vitu kwa bei rahisi. Kwa hakika, haya ndiyo mambo yanayohusiana na ulazima wa kihistoria (historical determinism). Na hakuwezekani kukabiliana na kushindana na ulazima wa kihistoria.

Kwa mfano, ikiwa katika dunia hii ya kisasa iliyojaa zana na silaha za kivita itatokea nchi ambayo itaonyesha ukaidi wake kwa kutaka kutumia silaha za kivita za zamani, k.v. panga na mikuki, ili kuilinda nchi yake, hapana shaka yoyote kwamba kitendo hicho hakitachukuliwa kuwa ni ulinzi wa nchi, bali ni kusalimu amri. Haiwezekani kabisa silaha za kizamani ziweze kushindana na silaha za kisasa ambazo kila siku hubadilika.

Lakini pana jambo moja hapa ambalo ni lazima tulielewe. Nalo ni kuwa binadamu si kiumbe cha pekee katika ulimwengu huu, wala si kweli kwamba vitendo vyake vyote vinatokana na maumbile yake ya kielimu. Binadamu ni kiumbe mwenye hawaa, matamanio na tamaa pia. Vitu vingi sana vimetokeza katika dunia na vingi vyao ni vipya. Lakini ikiwa tutavichunguza kuona kama vitu hivyo vimetokana na akili na elimu ya binadamu au tamaa, uroho na hawaa yake, tutaona kwamba vitu hivyo havikutokana na elimu yake bali vilitokana na tamaa, uroho na hawaa ya binadamu, kwani hata kile kitu kilicho­tokana na elimu na sayansi kimo mikononi mwa watu wenye tamaa na hawaa.

Nakutoleeni mfano mmoja. Heroini (kasumba) ni tukio jipya au kitu kipya kabisa kilichotokeza na kuenea duniani. Heroini ni matokeo ya elimu, lakini si elimu huru. Heroini si matokeo ya elimu au akili bali ni matokeo ya elimu iliyotiwa mikononi mwa nafsi zenye hawaa na tamaa. Je, haya mabomu ya atomiki na silaha haribifu si matunda ya dunia ya kisasa? Basi kwa nini hata madola makubwa yenyewe yanafanya mikutano kushauriana jinsi ya kupata utatuzi wa kuzuia utengenezaji wa silaha hizo? Viongozi wa madola makubwa wanakaa pamoja ili kufikia mwafaka wa kuziangamiza silaha kali zinazoleta hasara na maafa makubwa. Hawasililizani kuwa wengine watengeneze silaha kali na wengine wasitenge­neze. Mikutano hiyo ya kuzuia silaha ina maana gani? Ina maana kwamba wao wenyewe wana­hakikisha kuwa wameiendesha kombo na wame­ipotoa elimu (sayansi).

Vitu vingi vimevumbuliwa, k.v. atomi, umeme, jenereta, baruti, n.k. Wavumbuzi wa asili wa vitu hivi wamevivumbua vitu hivyo kwa lengo kwamba vitoe huduma na manufaa kwa wanadamu. Mmesoma kwamba yule mvumbuzi wa baruti (Alfred Bernhard Nobel (1833-96)] alipoona kwamba baruti inatumiliwa vibaya alihuzunishwa sana kwa kadiri kwamba akaanzisha taasisi moja kwa ajili ya kutoa zawadi za Nobel kwa watu watakaotoa huduma zenye faida ili kufidia kitendo chake. Je, hamjasikia mara kwa mara habari za mwanasayansi mkubwa katika ulimwengu huu, Albert Einstein [1879-1955] ambaye amefariki katika zama zetu? Einstein alikuwa daima akisikitika kuona kwamba uvumbuzi wake katika mambo ya atomi uli­tumiliwa vibaya hata kabla ya watu kunufaika nao. Alikuwa akisema: "Afadhali kama nisinge­kivumbua kuliko sasa kutumiwa na watu wenye tamaa na matamanio."

Kwa hivyo, kuna uwezekano wa kuendelea au kupotea binadamu katika zama hizi. Sisi hatuwezi kukubali maneno haya kwamba ni lazima tujitabiki na kujirekebisha na mahitaji ya zama. Lazima hapa tufafanue kwamba mahi­taji ya zama maana yake ni mahitaji na maisha ya binadamu. Je, mahitaji yepi tunayoyakusudia? Je, kila kitu kipya au kilichovumbuliwa katika karne hii ni kizuri? Au kila kitu cha zamani hakipendezi na hakifai tena? Haya si maneno sawa kusema kwamba katika dunia ya leo kitu hiki kinafaa na kupendwa au kitu kile hakifai au hakipendwi. Kupendwa au kutopendwa kitu kipimo chake si dunia hii. Dunia ya leo maana yake ni watu walio wengi. Watu walio wengi hawawezi kuwa mizani. Lazima tuvipambanue vitu vipya vya zama hizi. Sisi tu huru.

Aya ya Qur'ani inasema:

"Kwa hakika sisi tulivipa amana mbingu na ardhi na milima, lakini vikakataa kuichukua na vika­iogopa; lakini mwanadamu akaichukua. Hakika ni dhalimu mkubwa, mjinga sana." (33:72)

Binadamu amechukua amana hiyo ambayo ni dhima na jukumu kubwa linalomtaka afuate mkondo wa zama na asipinge maendeleo ya zama. Asiwe mwenye kupendelea mambo ya kizamani kama walivyo baadhi ya watu. Lakini wakati huohuo ana jukumu jingine kubwa, nalo ni kupambana na upotofu wa zama.

Hapa panajitokeza jukumu Ia tatu, nalo ni kutambua na kupambanua baina ya maendeleo ya zama na upotovu wa zama. Tusiwe mfano wetu kama wale watu ambao wanapinga maende­leo ya zama eti ni upotovu, au wale wanaounga mkono upotovu wa zama eti ni maendeleo. Ikiwa sisi tunajihesabu kuwa ni walinzi wa mafundisho ya Kiislamu, basi ni wajibu wetu kupambanua njia ongofu katika jamii kwa kuielewa vizuri misingi ya kisayansi na kifalsafa ya jamii na kwa kusoma sana historia. Kwa kufanya hivyo ndipo tutakapoweza kupambanua baina ya kikundi kiaminifu na kikundi kiharibifu. Tutaweza kupambana na kile kikundi kinachopinga kila kitu kipya au jambo jipya.

Wako baadhi ya watu ambao wameng'ang'a­nia kwa kusifu kila kitu cha kizamani. Kwa mfano, wako baadhi ya watu wanapendelea kutumia kalamu ya zamani yenye umbo maalum pamoja na dawati lake, kila wanapoandika wawe wakichovya wino. Huko ni kuchukua taabu na kupoteza wakati. Inatosha mtu atumie kalamu ya wino ya kawaida ambayo atajaza wino mara moja kisha ataandikia kwa saa kadhaa. Hatokuwa na haja tena ya kufikiria wino uko wapi na kila mara awe akichovyachovya. Kidau (kidawati) kilikuwa cha zama za mababu zetu. Kwa hivyo, haielekei tuache kutumia hii kalamu ya kisasa na tushikilie kalamu ya kizamani. Jamaa mmoja aliyekuwa akiwakejeli watu wenye kutumia vitu vya kisasa na kuviacha vya kizamani, alikuwa akisema: "Wanaacha kupanda punda wa Mungu wanapanda motokaa ya shetani!"

Wakati taa za umeme zilipoanza kutumiwa, watu wengi ambao hawakuona kwa mara ya kwanza walipinga. Mimi mwenyewe sikumbuki, lakini nimehadithiwa kwamba wakati taa za umeme zilipowashwa mjini Mash'had, mtu mmoja alianza kufanya ghasia kupinga na watu wakaja na wakazizima. Kwa nini? Kwa sababu gani? Kwani miongoni mwa aya za Qur'ani kuna aya inayosema: "Enyi mlioamini! Nakuusieni kiba­tari. Msije mkaacha kutumia kibatari cha mafuta ya taa mkafikwa na balaa!!"? Ama kuna aya nyingine inayosema: "Enyi mlioamini! Naku­usieni daima pandeni punda wala msipande kitu kingine!!??"

Hii ni desturi iliyozoewa na watu kisha ika­pewa sura ya kidini. Kuna kisa kingine ninacho­kikumbuka cha bwana mmoja wakati shule zilipokuwa zikifunguliwa mikoani. Bwana huyo alikuwa akifikiri kwamba kama hutosoma chuoni (madrasani) hutoweza kuwa shekhe (mulla). Alikuwa akisema: "Mambo gani haya? Kwani watoto wasomapo chuoni hawawi mashekhe? Kwani Sheikh Murtadha Ansari kwa kusoma alif be chuoni hajawa shekhe mkubwa? Kwa hivyo, watoto wetu wakisoma vyuoni na madrasani watakuwa wanavyuoni lakini hawato­kuwa hivyo wakisoma shuleni." Bwana huyo alikuwa akifikiri kwamba Sheikh Murtadha Ansari amekuwa mwanachuoni mkubwa kwa sababu ya kusoma chuoni peke yake. Ingawa chuo hakikuwa kizuizi kikubwa kwake lakini lau masomo yake angefundishwa kwa mpango bora zaidi basi hapana shaka angekuwa mwana­chuoni mkubwa zaidi.

Haya si miongoni mwa mafundisho ya Kiislamu kwamba tukitaka kuwafunza watoto wetu ni lazima tuwafunze kwa utaratibu wa alif be, n.k. Uislamu haukutilia mkazo mbinu hizi.

Sheria za Kilslamu katika Zama Hizi

Katika sehemu nyingine ya mjadala wangu, kuna masuala mengine mengi ya kujadiliwa lakini hapa nitayataja kwa muhtasari tu. Uislamu una mfumo mahsusi wa utungaji wa sheria. Ajabu ya mfumo huo ni kuwa sheria zake zinaweza kwenda sambamba na maendeleo ya zama, na hata zina­weza kuwa ni mwongozo kwa maendeleo na wakati huohuo zikaweza kupambana na upotovu na ufisadi.

Msingi wa hoja yangu ni aya moja ya Qur'ani inayosema kwamba dini ya Kiislamu si dini iliyo mbali na maumbile na sheria (kanuni) za maum­bile. Kwa sababu Mtungaji wa sheria hizo Ndiye Huyo Huyo Muumba wa maumbile. Na sheria Zake amezitunga kuambatana, kukubaliana na kwenda sambamba na alivyoviumba. Aya yenyewe inasema:

"Basi uelekeze uso wako kwenye dini iliyo sawa­sawa, ndilo umbile (mahsusi) Allah alilowaumbia watu." (30:30)

Mwenyezi Mungu anasema kwamba dini ikiwa kama ni umbile moja inaafikiana na maumbile mengine ya Mwenyezi Mungu.

Aya nyingine inasema:

"Na vile vinavyowanufaisha watu vinakaa katika ardhi." (13:17)

Kwa kuwa dini ni umbile la aina ya pekee alilowaumbia kwa faida na manufaa ya watu, hivyo, ni lazima (dini) ibaki na iendelee duniani. Hii ni kanuni ya kimsingi. Kuna vitu gani katika dini ya Kiislamu ambavyo vinaafikiana na kuku­baliana na maumbile na kanuni ya kimaumbile ambavyo kuwepo kwavyo ni miongoni mwa misingi ya maendeleo na ukamilifu katika maumbile? Miongoni mwa siri za misingi hiyo ni kuthaminiwa akili katika Uislamu. Wewe huto­weza kuona dini yoyote au kitabu kitakatifu chochote ambacho kimeipa umuhimu na thamani akili kama dini ya Kiislamu. Kwa bahati mbaya, sisi hatuwezi kuwa watangazaji wazuri kwa ajili ya dini yetu. Hakuna mzaha! Lakini wewe ukivi­rejea vitabu vya kifiqihi (sheria za Kiisiamu) na ukitaka kutumia ijtihadi (mbinu ya kutoa fatwa)

ili utatue masiala ya kidini, misingi ipi utaitumia? Bila ya shaka utaitumia misingi minne - Kitabu (Qur'ani), Sunna, ijmaa (mwafaka wa wanazuoni) na akili. Akili ni msingi mmoja kati ya Kitabu, Sunna na ijmaa. Ijmaa pia ina nafasi yake mah-susi. Hii haina maana kwamba akili na ijmaa viko mbali na Kitabu na Sunna. Hii ni fahari kubwa sana kuona kwamba tangu mwanzoni mwa Uislamu wanavyuoni wa Kitslamu wamesema kwamba kuna itifaki na makubaliano baina ya akili na sheria. Wameweka kanuni isemayo:

"Kila linalohukumiwa na akili linahukumiwa na sheria pia, na kila linalohukumiwa na sheria lina­hukumiwa na akili pia." Makusudio yao ni kuwa ikiwa akili imehukumu kitu ambacho hatuna ushahidi wake ulioandikwa, basi uamuzi huo wa kiakili unatosha kutufahamisha kwamba kitu hicho kinakubaliana na Uislamu. Kwa hivyo, hata kama hatuna ushahidi ulioandikwa, akili inatosha kuhukumu, kwa sababu kile kinacho­hukumiwa na sheria kinahukumiwa na akili vivyo hivyo. Hii ina maana kwamba sheria za Kiislamu hazikutungwa kwa mujibu wa mambo yasiyoeleweka au yasiyo na maana bali zime­tungwa kufuatana na hekima, busara na akili; na vilevile zimewekwa kwa ajili ya maslahi na faida kwa maisha ya binadamu. Sheria za Kiisiamu zinaafikiana na akili.

Uisiamu ni dini ya kimantiki. Tuchukulie kwa mfano katika falsafa kuna suala moja ambalo hukumu yake haikuwa wazi kwa akili, lakini si jambo lililofichika au lisilo na maana au lisilo­kubaliana na akili, kama yale maneno ya Wakristo wanaosema kwamba akili na imani ni mbalimbali. Uislamu unasema kwamba akili na imani ni vitu vimoja na lazima viende sambamba na viafikiane. Hivi ni mizani katika fiqihi ya Kiislamu. Katika mafundisho ya misingi ya Kiislamu, akili ni kitu muhimu sana. Katika Uislamu akili ni kipimo cha msingi katika kuamini, lakini kinyume chake katika Ukristo kutumia akili katika kuamini ni marufuku. Jambo hili limewafanya wanavyuoni wa Kiislamu wapate uwanja wa kutumia akili katika masiala ya kidini. Na hii ndiyo sababu ya kufanikiwa fiqihi ya Kiislamu tangu zamani. Mmewahi kusikia kwamba wakati fiqihi ya Kiislamu inapojadiliwa katika mikutano mingi ya kimataifa, inasifiwa sana kutokana na wepesi na ukunjufu wa sheria zake. Jambo jingine ambalo ni sababu ya kusifiwa dini ya Kiislamu (kama nilivyokwishaeleza) ni kule kutojali hail na sura ya dhahiri ya maisha na badala yake kuitilia maanani roho ya maisha. Hii ndiyo sababu iliyoifanya dini ya Kiislamu ijiepushe kugongana na maendeleo ya kimaisha, kwa sababu yale maendeleo ya kimaisha yanayo­tegemea sayansi na teknolojia ambavyo vimeyapa maisha, sura, umbo na muundo, yananitaka mimi nitoe pesa kununua kitu ambacho kwa kweli hakina faida wala manufaa yoyote. Uislamu unasema kwamba muamala huu ni haramu. Biashara hiyo inakutaka wewe ununue mali ambayo haitakuletea faida yoyote, na kama una­dhani kuna faida, basi faida hiyo haitambuliwi katika Uislamu.

Mafaqihi (wataalam wa sheria za Kiislamu) wamesema kwamba vitu ambavyo asili yake ni najisi vimeharamishwa kutumiwa katika Uislamu. Kwa hivyo, hakuruhusiwi kuuza au kununua vitu ambavyo ni najisi asilia, k.m. damu. Katika zama zile watu walikuwa wakinywa damu, hivyo, Uislamu uliharamisha. Sasa ikiwa zama zime­geuka na damu inatumiwa kwa faida nyingine kinyume na matumizi yale ya zamani wakati ilipoharamishwa, hapo Uislamu unaruhusu matumizi haya mapya ya damu ya mtu mmoja kumtia mtu mwingine, kwa mfano, mtu aliye­jeruhiwa na akapoteza damu nyingi. Uislamu umesema kunywa damu ni haramu lakini haukukataza mtu mmoja kumpa damu mtu mwingme. Zamani matumizi ya damu yalikuwa ni kula mali kwa batili lakini muamala wa sasa si batili. Kwa hivyo, ile sheria thabiti haitobadilika abadan. Sheria inasema:

"WVala msiliane mali zenu kwa batili" (2:188)

Hakuna mtu yeyote anayeweza kukataa sheria hii. Ikiwa kitu kimoja siku moja kilikuwa kikitumiwa kwa njia ambayo ilikuwa sawa na kula mail kwa batili, na siku nyingine kikatumiwa kwa njia iliyodhibitiwa ghairi ya hiyo, hapo pata­tokea badiliko la maudhui au hali. Maudhui ikibadilika hukumu yake hubadilika pia. Lakini hii haina maana ya kufutwa kwa sheria asilia na thabiti, kwani katika Uislamu sheria haifutiki bali maudhui tu ndiyo inayobadilika.

Katika zama zetu alikuwepo aalimu (mwana­chuoni) mashuhuri sana ambaye alikuwa mtu mcha-Mungu sana, zahidi (walii) na faqihi, aki­itwa Agha Sheikh Ali Zahidi Qummi. Haikosi mmewahi kusikia habari zake. Alikuwa na taasubu sana hivi kwamba alijiharamishia vitu vyote vya kigeni. Hakuwa akitumia kitu chochote cha kigeni. Kama kitambaa cha kienyeji kilikuwa kikipatikana alikuwa hanunui kitambaa cha kigeni. Alikuwa akisema kwamba maadamu vitu vinavyotengenezwa na Waislamu vinapatikana hakuna haja ya kutumia vitu vya kigeni. Alikuwa hanywi chai ya kigeni ila akinywa chai ya nchini tu. Hata sukari ya kigeni alikuwa hatumii na alikuwa akitumia zabibu badala ya sukari.

Walikuwepo Wazungu wawili, mama na binti yake ambao wote wawili walisilimu. Baadaye wawili hao wakakaa mjini Karbala (Iraq) na jirani yao alikuwa shekhe huyo. Watu kadhaa walishu­hudia kwamba binti Mzungu alikuwa Mwislamu msalihina sana na alishika dini mpaka mwisho wa umri wake. Baada ya kufariki kwa mke wa Agha Sheikh Ali Zahidi, msichana huyo wa Kizungu mwenyewe akataka aolewe na Agha Sheikh Ali Zahidi. Agha Sheikh Ali akamwoa na akaishi maisha mazuri sana na mke huyo wa Kizungu. Inasemekana kwamba alipofariki mwanamke huyo hali ya Sheikh Ali iliharibika. Mtu mmoja alimwendea Sheikh 'Ali na akam­wambia: "Shekhe, wewe ulikuwa ukituambia kuwa hutumii vitu vya kigeni, basi ilikuwaje ukamwoa mwanamke wa kigeni?" Sheikh Ali akajibu: "Mwanangu! Maudhui imebadilika. Mgeni huyo amekuwa Mwislamu."

Kwa hivyo, suala la kubadilika na kugeuza maudhui au hali ni suala jingine. Hebu nikutole­eni mfano mwingine.

Katika vitabu vya kifiqihi kuna mlango mmoja unaoitwa Mashindano na Kutunga Shabaha. Ni sunna (mustahabu) kwa kila Mwislamu, kujifunza mashindani ya mbio za farasi ili kuweza kuwalea farasi wa mbio (resi). Inaruhusiwa kutumia pesa katika kuwafunza farasi wa mbio lakini hairuhusiwi katika kazi nyingine.

Kutunga shabaha kwa mshale ni sunna pia. Huenda mtu akahoji kwamba katika zama hizi hakuna haja kubwa ya kuwepo mada ya mashin­dano ya farasi na kutunga shabaha kwa mshale, hivyo ifutwe kabisa. Lakini mtu akiangalia ataona kwamba mada hiyo imeandikwa kwa mujibu wa kanuni thabiti. Na kanuni yenyewe ni aya hii ya Qur'ani:

"Na waandalieni nguvu mwezavyo, na kwa farasi waliofungwa [tayari kwa vita], ili mwatishe maadui wa Allah na maadui wenu na wengineo ghairi ya wao msiowajua nyinyi, (lakini) Allah anawajua." (8:60)

Uislamu ni dini ya kijamii inayoutaka umma wa Kiislamu ujiandae na ujizatiti barabara kwa ajili ya kujihami. Nguvu za Waislamu zinatakiwa ziwe za kiwango cha juu kabisa. Sababu ya kuwekwa mashindano ya farasi na kutunga shabaha kwa mshale ni kuwafanya wapiganaji wa Kiislamu wawe mashujaa na simba katika medani za mapambano. Maneno haya yanawapa moyo wapiganaji. Mashindano ya farasi na

kutunga shabaha ni kielelezo cha hiyo sheria thabiti na ya daima dawamu. Sheria hiyo haiwezi kufutwa.

Kwa maana nyingine farasi na mshale ni sura moja ya utekelezaji wa aya: "Na waandalieni nguvu mwezavyo, na kwa farasi waliofungwa [tayari kwa vita]." Wakati mashindano ya farasi na utungaji wa shabaha kwa mshale unapokuwa sunna katika jamii, hutumiwa kazi zake, lakini wakati vitu vingine huvumbuliwa badala yake, msingi wa "kuwaandalia" hubaki vivyo hivyo katika utekelezaji. Hii haina maana kusema kwamba katika utekelezaji wa amri hiyo kinacho­andaliwa kiwe kitu cha aina moja daima. Kwa hivyo, kama nilivyokwishaeleza, Uislamu ume­weka sheria thabiti na zisizobadilika kukidhi haja zilizo thabiti, lakini wakati huohuo ume­zingatia sheria nyinginezo kwa ajili ya haja zinazobadilika ambazo huambatana na sheria zilizo thabiti.

Inatosha kwa mwanachuoni wa Kiislamu mwenye kufahamu kusema kwamba katika kutekeleza sheria hii haina maana kwamba ni lazima ufanye mashindano ya farasi na kutunga shabaha kwa mshale. Sasa maudhui imebadilika, hivyo sheria hii inaweza kutekelezwa vizuri kwa kufanya mashindano ya silaha na zana za kivita, k.v. bunduki, ndege za kivita za phantom, MiG, n.k. badala ya farasi na mshale.

Ni wazi kabisa kuwa kitu kinachopendelea Uislamu si mishale na pinde bali ni nguvu na ushujaa. Farasi na mishale vimetajwa kama mfano wa msingi huo wa kujizatiti.

Katika mfumo wa utungaji wa sheria za Kiislamu kuna vipengee kadhaa vinavyozipa uhai na nishati sheria za Kiislamu. Mojawapo kati ya wajibu wetu mkubwa sana ni kuivumbua hiyo nishati ya sheria za Kiislamu.

AS: kufupisho cha alayhis/alayhas/alayhimus salaam, m.y. amani iwe juu yake/yao.

SAW: kifupisho cha sallallaahu alayhi wa-'Ali, m.y. baraka za Mwenyezi Mungu ziwe kwake na kwa ali (wazaa) wake.