rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

ZAKA NA SADAKA HUONGEZA NEEMA

Faida kuu mojawapo ya kutoa Zaka ni kuongezeka kwa neema na baraka ya mali yetu iwapo itatolewa kwa kuzingatia kanuni na ustaarabu wa kutoa hivyo, na ni kinyume na mawazo na mipango ya ki-Shaytani, kwani mabakhili hufikiria daima kuwa kwa kutoa mali yao kwa ajili ya misaada na Sadaka na Zaka, basi mali yao hupungua na hivyo wanaweza kuwa masikini na kwa hakika hayo ndiyo mawazo na upotofu wa Shaytani.

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Baqarah, Ayah 28 : “Allah swt huongezea katika Sadaka” yaani huongezea baraka humu duniani na vile vile kutakuwapo na malipo mengine huko Aakhera

Na amesema Allah swt katika Quran: Surah al – Saba,34, Ayah 39 :

‘Chochote kile mtakachokitoa (katika njia yake), basi Atawalipeni (humu humu duniani) malipo yake, Naye ni Mbora wa wanao ruzuku.’

Amesema Allah swt katika Quran: Surah al –Rum, 30, Ayah 39 :

‘Na mnachokitoa kwa riba ili kiongezeke katika mali ya watu, basi hakiongezeki mbele ya Allah swt . Lakini mnachokitoa kwa Zaka kwa kutaka radhi ya Allah swt, basi hao ndio watakaozidishiwa.’

Katika Ayah hizo, tumeona kuwa kuongezeka zaidi mno na vile vile Baraka pia itakuwamo, vyote kwa pamoja. Katika kusisitiza hayo, zipo riwayah nyingi mno.

Amesema Bi. Fatimah az-Zahra a.s. bintie Mtume Muhammad Mustafa s.a.w.w. katika hotuba aliyoitoa kuzungumzia Fadakkatika Bihar al-Anwaar, J.8, Uk 109 :

“Kwa ajili ya kujitakasa na dhambi la Shirk, Allah swt ametufaradhishia kuikamilisha imani yetu ( yaani mtu yeyote anayetaka kujitakasisha na unajisi basi inambidi kuleta imani kwa moyo wake kamilifu), na Sala inamwepusha na magonjwa ya kiburi na kujifakharisha, na Zaka inamwepusha mtu kwa magonjwa ya ubahili ili mwanadamu awe mkarimu na mpenda kutoa kwa ajili ya mema ili atakasike) na hii pia ndiyo sababu kuu katika kujiongezea riziki .”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. ameripotiwa akisema katika Al-Kafi:

“Yeyote yule anayetumia kutoka mali yake katika njia ya kheri, basi Allah swt anamlipa mema humu duniani na kumwongezea katika malipo yake.”

Vile vile ameripotiwa akisema Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. katika Wasa’il as-Shiah : Mlango Sadaka, Hadith 19, J.6, Uk. 259 :

“Tafuteni riziki yenu kwa kutoa Sadaka.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameripotiwa katika Kitab ‘Uddatud-Da’i kuwa alimwuliza mtoto wake :”Je nyumbani kuna kiasi gani kwa ajili ya matumizi ?”

Naye alimjibu : “Zipo Dinar arobaini tu.”

Imam a.s. alimwambia “Dinar zote hizo zigawe Sadaka.”

Kwa hayo mtoto wake alimwambia Imam a.s. “Ewe Baba ! Mbali na Dinar hizi arobaini, hatutabakia na akiba yoyote.”

Imam a.s. alimwambia : “Nakuambia kuwa zitoe Dinar zote Sadaka kwani ni Allah swt tu ndiye atakayetuongezea kwa hayo. Je wewe hauelwei kuwa kila kitu kina ufunguo wake ? Na ufunguo wa riziki ni Sadaka ( kutolea mema ).”

Kwa hayo, mtoto wake aliyekuwa akiitwa Muhammad, alizitoa Sadaka Dinar hizo na hazikupita siku kumi, Imam a.s. alitumiwa Dinar elfu nne. Hapo Imam a.s. alimwambia mwanae : “Ewe Mwanangu ! Sisi tulitoa Dinar arobaini tu na Allah swt ametupa Dinar elfu nne badala yake.”

Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Nahjul Balagha kuwa :

“Mtu anapokuwa masikini au mwenye shida basi fanyeni biashara pamoja na Allah swt kwa kutoa Sadaka.”

Al Imam ‘Ali ar Ridha a.s. alimwambia mfanyakazi wake : “Je leo umeshagawa chochote katika njia ya Allah swt .” Mfanyakazi huyo, “La, bado sijagawa.” Kwa kuyasikia hayo Imam a.s. alimjibu, “ Sasa kama haukufanya hivyo, basi Allah swt atatulipa nini badala ya tendo letu ? Hivyo hatutapata baraka wala neema yoyote kutoka kwa Allah swt . Tukitoa chochote ndipo Allah swt atatulipa kwa wingi badala yake.”

Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. ameelezea Hadith katika Al-kafi, Kitab ad-Du’a, J. 2, Uk.595 moja kwa kutokea Ayah Fahuwa Yukhlifuhu (yaani chochote kile kinachotolewa katika njia ya Allah swt , basi hulipa malipo yake kwa haraka sana ). Na Hadith yenyewe ni :

“Je utadhaniaje kuwa Allah swt anakiuka ahadi aliyoitoa ?”

Basi mwandishi akajibu : “La ! Sivyo hivyo.”

Ndipo Imam a.s. alimwuliza : “Sasa je kwanini wewe haupati malipo yako kwa yale unayoyatoa na kugawa ?”

Naye akajibu, “ Kwa hakika mimi sijui sababu zake.”

Imam a.s. alimjibu, “Iwapo miongoni mwenu yeyote atakayekuwa akiipata riziki yake kwa njia zilizo halali, na kama ataitumia hata Dirham moja katika njia zilizo halali, basi lazima mtapata malipo yake na kwa wingi zaidi. Na iwapo mkiona kuwa hamkupata chochote katika malipo yenu basi mutambue kuwa mali hiyo ilichumwa kwa njia zilizo haramu au ilitolewa na kutumiwa katika njia iliyoharamishwa.”

Kuhusiana na swala hili zipo Ayah na riwayah nyingi mno, lakini tunatua hapa. Marehemu Nouri katika kitabu chake Kalimah at-Tayyibah amezungumzia mengi na kwa mapana na undani zaidi kuhusu kutoa Sadaka katika njia ya Allah swt na amedondoa hekaya takriban arobaini ambamo ‘Alim Rabbani Akhwand Mullah Fath ‘Ali amenakili kisa cha jamaa yake ategemewae ambaye amesema,

“Mwaka mmoja ambapo hali ya ughali ilikuwa imekithiri, nilikuwa na kipande kimoja cha ardhi ambapo nilikuwa nimepanda Shayiri na ikatokea kuwa shamba langu hilo likawa na mavuno mengi mno kuliko mashamba mengineyo. Kwa kuwa hali ilikuwa ni mbaya kwa watu wengineo, hivyo tamaa ya kujitafutia faida zaidi katika mazingara hayo niliyatoa kutoka nafsi yangu. Hivyo mimi nilikwenda moja kwa moja Msikitini na kutangaza kuwa mazao yote yaliyo shambani mwangu nimeyaacha kwa masharti kwamba yeyote mwenye shida tu ndiye aende kuchukua na masikini na mafukara waende kuchukua kwa ajili ya chakula cha familia zao. Wote wachukue kiasi wanachokihitaji. Hivyo masikini na mafukara na wenye shida walikuwa wakichukua mavuno kutoka shambani mwangu huku wakisubiri mavuno yao kukomaa. Kwa hakika nafsi yangu ilikuwa imetulia vyema kabisa kwani sikuwa na wasiwasi kwani nilikuwa nimeshajitenga navyo.

Wakulima wadogowadogo wote walipovuna mazao yao, nami nikavuna kutoka mashamba yangu mengineo na nikawaambia wafanyakazi wangu waende katika shamba ambalo nilikuwa nimeligawa kuwasaidia wenye shida wakati huo, wakaangalie kama kumebakia chochote ili waweze kuvuna.

Kwa hakika hao walipokwenda shambani humo walikuta shamba zima limejaa Shayiri kupita kiasi na baada ya kuvuna na kusafisha nilikuta kuwa nimepata mavuno mara dufu kuliko mashamba yangu mengineyo. Ingawaje humo watu wote walikuwa wakivuna kwa ajili ya chakula chao na familia zao, ilitakiwa kuwa tupu kumbe Allah swt amerudishia mavuno tena mara dufu.

Vile vile sisi tulikuwa tukipanda mwaka mmoja na kuipumzisha ardhi mwaka mmoja, lakini shamba hilo halikuhitaji kupumzishwa wala kuwekewa mbolea na badala yake nimekuwa nikilima na kupanda nafaka kila mwaka na nilikuwa nikipata mavuno mara dufu kila msimu.

Mimi kwa hakika nilistaajabishwa mno kuona hayo na nikajiuliza isije hiki kipande cha ardhi kikawa ni kitu kingine na mavuno yanapokuwa tayari, hupata mavuno mengi kabisa kuliko mashamba mengine yangu na ya watu wengineo.

Mbali na hayo, Merehemu amenakiliwa kuwa :

‘Yeye alikuwa na shamba moja la mizabibu kandoni mwa barabara na kwa mara ya kwanza kulipozaa zabibu katika matawi yake, alimwammuru mtunza shamba wake kuwa zabibu zote zilizopo kando ya barabara aziache kwa ajili wapitao njia. Hivyo kila mpita njia alichuma na kula zabibu zilizokuwa hapo na wengine hata walichukua pamoja nao. Msimu ulipokwa ukiisha aliwaamuru wafanyakazi wake waende kuangalia kama kulibakia zabibu zilizokuwa zimefichika nyuma ya majani au pembeni. Lakini jambo la kustaajabisha ni kwamba, wafanyakazi waliporudi, walikuwa wamevuna zabibu mara dufu ya mashamba yake mengineyo pamoja na kwamba kila mpita njia alikuwa akichuma zabibu hapo.’

Vile vile imenakiliwa kuwa :

‘Kila msimu alipokuwa akivuna ngano na kuzisafisha, alikuwa akizileta nyumbani kwake na hapo ndipo alipokuwa akitoa Zaka yake. Lakini safari moja alipovuna na kusafisha, akiwa akielekea nyumbani kwake aliwaza kuwa inambidi alipe Zaka haraka iwezekanavyo, kwani si vyema kuchelewesha ulipaji wa Zaka. Ni ukweli kwamba ngano ipo tayari na mafukaraa na masikini pia wapo. Hivyo aliwajulisha mara moja mafukaraa na masikini waje kuchukua ngano, na hivyo akapiga mahisabu yake na kuwagawia sehemu yao na hivyo sehemu iliyobakia aliileta nyumbani kwake na kujaza madebe makubwa makubwa na alikuwa akijua ujazo wao. Lakini alikuja kuangalia hapo baadaye akakuta kuwa idadi ya ngano imeongezeka mara dufu pamoja na kwamba alikuwa amepunguza kwa ajili ya kuwagawia mafukaraa na masikini.Na hivyo alikuta idadi ya ngano ipo pale pale kabla ya kutoa Zaka.’

Katika kitabu kilichotajwa, Alhaj Mahdi Sultan Abadi amenakili kuwa :

‘Mwaka mmoja mimi nilipovuna mavuno, nilipima uzito wa ngano na nikatoa na kuigawa Zaka yake. Na nafaka hizo zilibakia mahala hapo hapo kwa muda wa mwezi mmoja ambapo wanyama pamoja na mapanya walikuwa wakila humo. Na nilipokuja kurudia kupima uzito wake nikakuta kuwa uzito wa ngano ulikuwa vile vile kama siku ya kwanza yaani kiasi nilichokitoa Zaka na kilicholiwa na wanyama na mapanya hakikupungua hata chembe kidogo.’