rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

UTAMBULISHO WA MA’SUMIIN A.S. KATIKA AHADITH: KUNIYYAT NA ALQAAB

Mara nyingi tunaposoma vitabu vya riwaya tunapata majina mengine yaliyotofauti na majina ya asili. Hivyo tunaona katika Ahadith kuwa Ma’asumiin a.s. wanatambulishwa kwa majina yanayoitwa Kuniyyat au Iaqab, kwa mfano: Qala Abul Hasan ( yaani amesema Abul Hasan ) au Qala Abu ‘Abdillah (yaani amesema Abu ‘Abdillah) n.k. na hapo ndipo tunakuwa hatuelewi ni Ma’sum a.s. yupi ambaye amesema hayo.

Waarabu wanayo desturi ya kuwaita wazee wao si kwa majina yao bali kwa majina mengineyo yaan Kuniyyat au Alqaab. Hivyo inatubidi tupate ufafanuzi zaidi kuhusu majina hayo yanayotumiwa kwa ajili ya Ma’sumiin a.s zaidi ya mara moja. Na hivyo Maulamaa wetu wametuelewesha ilivyo sahihi kabisa.

Wakati wa kujaribu kufafanua juu ya Laqab au Kuniyyat kunatiliwa maanani kuhusu maneno na maana ya Hadith, zama za kusemwa na habari za wale wanaoziripoti, ndipo hapo panapoweza kutambuliwa kwa Alqaab au Kuniyyat katika Hadith hiyo kunatambulishwa Ma’sumiin a.s. yupi.

Hivyo kuelezea hayo na mengineyo, maelezo yafuatayo yatasaidia kutoa mwanga katika swala hili kwa ujumla:

1. ABUL QASIM Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Mtume Muhammad s.a.w.w. na Imam al-Mahdi a.s. Iwapo kutaripotiwa riwaya kuwa Abul Qasim tu, basi ijulikane kuwa ni Imam al-Mahdi a.f

2. ABU MUHAMMAD Zipo Hadith chache mno zinazojulikana kuwa Imam Hasan a.s. Hata hivyo hiyo ndiyo Kuniyyat yake.

3. ABU ‘ABDILLAH Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Hussein a.s na vile vile inatumika kwa ajili ya Imam Ja’afer as-Sadiq a.s.

4. ABUL HASAN

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. , Imam Musa ibn Ja’afer a.s., Imam Ali ibn Musa al-Ridha a.s. na Imam Ali an-Naqi a.s. Iwapo kutakuwapo na Abul Hasan tu katika riwaya, basi kutatambuliwa Imam Musa ibn Ja’afer a.s. Na iwapo kutaandikwa Abul Hasan Thani (Abul Hasn wa pili) basi kutakuwa kumefanywa ishara ka Imam Ali ar-Ridha a.s. na pale panapoandikwa Abul Hasan Thalith (Abul Hasan wa tatu) basi tujue kuwa kunamaanishwa Imam Ali an-Naqi a.s.

5. ABU MUHAMMAD

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Hasan a.s., Imam Zaynul Aabediin a.s na Imam Hasan al-‘Askari a.s. lakini iwapo kutaandikwa riwaya kwa Abu Muhammad tu tutatambua kuwa riwaya hiyo ni kutoka Imam Hasan al-‘Askari kwa sababu riwaya za Imam Zaynul Aabediin a.s. zinatajwa kwa jina lake tu, bali zipo riwaya chache mno tu kwa Kuniyyat yake.

6. ABU IBRAHIM Katika Hadith Kuniyyat hii inatumika hasa kwa ajili ya Imam Musa ibn Ja’afer a.s.

7. ABU IS-HAQ Kuniyyat hii inatumika kwa kumtambulisha Imam Ja’afer as-Sadiq a.s.

8. ABU JA’AFER

Kuniyyat hii inatumika kwa ajili ya Imam Muhammad al-Baquir a.s. na Imam Muhammad Taqi a.s

Lakini iwapo kutakuwapo na Abu Ja’afer tu au Abu Ja’afer Awwal, (Abu Ja'afer wa kwanza) basi ijulikane kunamaanishwa kwa Imam Muhhammad al-Baquir a.s.

Na iwapo kutaandikwa Abu Ja'afer Thani (Abu Ja'afer wa pili) basi kutambuliwe kuwa ni Imam Jawad a.s.

Kwa mara chache mno Abul Hasan inatumika kwa ajili ya Imam Al Imam 'Ali ibn Abi Talib a.s. lakini mahala pengi mno kunatumika Kuniyyat yake mahsusi ya Abul Hassanain.

ALQAAB.

Wakati pale utakapoona riwaya zinanakiliwa kutoka kwa ‘Aalim, Sheikh Faqih au ‘Abdi Salih, basi mutambue kuwa kunamaanishwa kwa

Al Imam Musa al-Kadhim a.s.

Vile Al Imam Ja'afer as-Sadiq a.s. anajulikana kwa alqaab zifuatazo: Sheikh , Abu ‘Abdillah, Faqih na ‘Aalim.

‘Allamah Majlisi a.r. anasema kuwa mahala pengi mno katika riwaya kunapotajwa Faqih basi kunamaanishwa kwa Imam ‘Ali an-Naqi a.s. na kwa mara chache mno kunatumika Jawallaij kwa ajili ya Imam Hasan al-‘Askari a.s na Al Imam Muhammad Sahibuz-Zamaan a.s.

Naqi, Mazii, Sahibul ‘Askar na Hajul kunamaanisha Imam Hasna al-‘Askari a.s.

Sahib na Sahibuddaar zinatumika makhsusi kwa ajili ya Imam al-Mahdi a.s. Lakini Sahibun Nahiyah inapokuja, basi kwa mara nyingine hutumika kwa ajili ya Imam ‘Ali an-Naqi a.s. au Imam Hasan al-‘Askari a.s. ‘Allamah Majlisi anasema kuwa mara nyingine katika Ahadith hutumika maneno Ghaib, ‘Alil au Gharim basi inatubidi kuelewa Imam al-Mahdi a.s.

Iwapo kutakuwapo bi ahadihima (kwa mojawapo) basi itatubidi tuelewe kuwa ni ishara kwa Imam Muammad al-Baquir a.s. au Imam Ja'afer as-Sadiq a.s.

Na iwapo tutakuwa bi ‘Askariyyen, tuelewe kuwa ni Imam Ali an-Naqi a.s. na Imam Hasan al-‘Askari a.s.

Vile vile iwapo tutaona bi Kadhimain basi kunamaanishwa Imam Musa al-Kadhim a.s. na Imam Mahammad at-Taqi a.s.

Kwa mukhtasari, zipo alqaab nyingi ambazo zinajulikana kimakhsusi kwa ajili ya Ma’sumiin a.s. kama vile Amir al-Muuminiin, Mujtaba Shahid, Zaynul Aabediin, Baquir, Sadiq, Kadhim, Ridha, Jawad, Hadi, ‘Askari, na Sahib uz Zamaan (salaam ziwe juu yao wote).

MWENYE KURIPOTI AHADITH AWEJE?

Kwa hakika somo hili ni kubwa na lenye kwenda kwa undani zaidi, lakini kwa ajili ya wasomaji, tunawaleteeni habari hizi kwa kifupi ili kuwafaidisha.

Katika lugha ya Kiarabu, mtu anayeripoti riwaya huitwa Rawi na sifa zake zimeelezwa na kubainishwa na Ma’ulamaa walio mabingwa wa ilimu ya Ahadith:

1. Rawi lazima awe mtu mwenye akili na fahamu timamu. Riwaya zozote zitakazotolewa katika hali ya kuwehuka au kurukwa na fahamu, basi hazitathaminika au kukubalika.

2. Ni lazima Rawi awe amebaleghe na Mukallaf, yaani shariah za Dini ziwe zimeshakwisha kuwa faradhi juu yake. Hapa inawajumuisha vijana na watoto na wale wote ambao bado hawajabaleghe lakini wanaweza kutofautisha baina ya wema na ubaya. Aina hii ya vijana hao huitwa Mumayyiz na hivyo riwaya zao zinapotimika masharti mengineyo, huweza kukubalika na kusadikika.

3. Ni lazima Rawi awe Mwislamu. Riwaya za mtu asiye Mwislamu haziwezi kuaminiwa au kusadikiwa.

4. Rawi lazima awe ni Mwislamu mfuasi wa Madhehebu ya Sh’iah Ithna-Asheria. Lakini iwapo kutakuwa na riwaya kutokea Mwislamu mfuasi wa Madhehebu mengine, basi kwa uzito wa dalili zinginezo na kufanya uchunguzi iwapo huyo Rawi ni mtu aaminiwaye katika historia.

5. Uadilifu wa Rawi pia ni sharti mojawapo, yaani asiwe akifanya madhambi makuu (Kabair Dhamb) na wala asiwe akirudiarudia madhambi madogo madogo (Dhamb-i-Saghirah).

Sheikh Tusi a.r. ametilia mkazo swala hili kwa kuelezea kuwa kuna tofauti katika uadilifu wa Rawi na mtoa ushahidi. Iwapo Rawi ni fasiki na iwapo itathibitika kuwa yeye katika riwaya yake na habari zake ni mkweli bila ya udanganyifu, basi riwaya yake inaweza kufuatwa.

6. Rawi asiwe msahaulivu, bali awe ni mtu mwenye kukumbuka vyema na udhibiti wake, (yaani haimaanishi kuwa Rawi asiwe akisahau kama mtu wa kawaida) yaani Rawi anapotaka kuelezea riwaya au Hadith, basi asiwe na mushkeli wa kuikumbuka.

AINA ZA AHADITH

Sayyid Ibn Taus a.r. (amefariki 673 Hijriyyah) na ‘Allamah Hilli a.r. (amefariki 726 Hijriyyah) kwa juhudi zao, wao wamefanikiwa kutuletea kanuni nne kuu zijulikanazo usul-i-‘arbi’ah ambazo ni kama zifuatazo:

1. HADITH SAHIH

Rawi wote lazima wawe waaminifu na Shia Ithna-Asheri na riwaya hizo ziwe zikifika hadi kwa Ma’sumiin a.s.

2. HADITH HASAN

Riwaya ambazo Rawi wake ni Mashiah na ambapo hapakufanywa uchunguzi wowote juu ya uadilifu wao.

Hadith kama hizo zinajulikana kama hasan kwa sababu Rawi amepokelewa kwa misingi ya husn-dhan yaani kwa dhana njema.

3. MUTAWATH-THAQ

Yaani Rawi wote wawe wakiaminiwa lakini miongoni mwao si wote ambao ni Mashiah.

4. DHAIF

Ni riwaya zile ambazo hazina sifa hata mojawapo za hapo juu.

Tanbih lipo jambo moja la kuzingatia, kuwa Ma’ulamaa wanakubaliana na Hadith zilizo Sahih, Hasan na Muwath-thiq. Ama kuhusu Hadith zilizo dhaif ni kwamba iwapo atayamkinika kuwa Rawi hao si watu wa kutegemewa lakini maelezo na maana yake ni sawa na maana ile ya Ma’sumiin a.s. na katika sura hii, itaweza kukubalika, na wakati Ma’ulamaa wanaozisimulia basi nia yao huwa juu ya Hadith, bali huwa ni kutoa ushahidi tu.