rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

MASHIA NA UANDISHI WA HADITH:

Kwa kuwa riwaya (desturi) ya uandishi wa Hadith ilikuwapo miongoni mwa Shia tangia mwanzoni, wao walikuwa wanaongoza katika uandishi wa Hadith na Fiqh. Dr. Shawqi Dayf anaandika:

"Mwelekeo na umuhimu wa Mashia katika uandishi wa Fiqh umekuja daima ni madhubuti mno. Sababu nyuma yake ilikuwa ni imani yao katika Maimamu wao ambao walikuwa ni kiongozi wao (haad) na wakiwa wameo ngozwa na Allah swt (mahdi) na fatawa zao zimekuwa zimeshikamana. Kwa hivyo, wao walipatiwa uzito na umuhimu katika misemo ya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Na kwa sababu hiyo, mkusanyiko wa kwanza ulifanywa na Mashia, ulifanywa na Sulaym ibn Qays al-Hilali, katika zama za al-Hajjaj."

Al-Allamah al-Sayyid Sharaf al-Din anaandika:

“Imam Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na wafuasi wake walitilia mkazo na kufuatilia swala la uandishi kuanzia mwanzo kabisa. Jambo la kwanza kabisa lililotiliwa mkazo na kufuatiwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s. ilikuwa ni kuiandika Quran nzima, ambayo aliifanya baada ya kifo cha Mtume s.a.w.w. kwa kuiandika kimpangilio wa ufunulio wa Aya za Qurani.Katika Qurani hiyo pia alikuwa ameonyesha ni aya zipi zilizokuwa 'amm au khass, mutlaq au muqayyad, muhkam au mutashabih. Baada ya kukamilisha hayo, aliendelea na kazi ya ukusanyaji wa kitabu kwa ajili ya Fatimah, ambacho kilikuwa kikijulikana kwa vizazi vyao kama Sahifat Fatimah. Baada ya hayo, aliandika kitabu juu ya diyat (fidia) ambacho kilijulikana kama Sahifah. Ibn Sa'id amenakili hivyo katika musnad kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. mwishoni mwa kazi yake mashuhuri al-Jami.' Mtunzi mwingine wa Kishia ni Abu Rafi, ambaye alikusanya maandiko yakiitwa kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya. ”

Marehemu Sayyid Hassan al-Sadr anaandika kuwa Abu Rafi, aliyekuwa mawla wa Mtume s.a.w.w. ndiye aliyekuwa wa kwanza miongoni mwa Mashia kwa kukikusanya kitabu. al-Najashi katika Fihrist ameelezea kuwa Abu Rafi alikuwa ni mtunzi katika kizazi cha kwanza cha Mashia. Mfuasi wa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Abu Rafi alishiriki katika vita vya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na alikuwa ni mwangalizi wa hazina ya Serikali huko Kufah. Kitabu chake kilichokuwa kikiitwa Kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya, ambacho kilikuwa kimeanza kwa sura izungumziayo Salat, kufuatiwa na sura juu ya Saumu, Hajj, Zakat, kutolewa kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib a.s. katika Kufah, Kitabu hiki kilinakiliwa na Zayb ibn Muhammad ibn Ja'afer ibn al-Mubarak katika nyakati za al-Najashi.

Ali ibn Abi Rafi, mwana wa Abu Rafi, aliye tabi't na Mshia khalisi ameweza vile vile kukusanya kitabu kilichokuwa na sura mbali mbali juu ya mambo ya Sheria kama vile wudhuu, Salaat, n.k.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, abu Hanifa alimwita al-Imam al-Sadiq a.s. kutubi (akisema 'innahu kutubi' ) sifa ambayo ilimtambulisha na wengineo. Wakati Imam a.s. aliposikia kuhusu hayo, alicheka na kusema, "...... lakini kila alichokisema kuwa kwangu suhufi ni kweli; mimi nimesoma suhuf (vitabu) vya mababu zangu." Riwaya hii inaonyesha kwa wazi wazi kuwa Imam a.s. alikuwanavyo vitabu fulani ambavyo alipewa na mababu zake, na hiki kilikuwa ni kipindi ambacho Ahl al-Sunnah walikuwa hawakutilia mkazo katika uandishi wa Hadith.

Miongoni mwa mapokezi ambayo inatuonyesha kuwa ma-Imam a.s. walikuwa navyo vitabu kama hivyo, ni mojawapo iliyoripotiwa na Muhammad ibn 'Udhafir al-Sayrafi anasema:

"Mimi nilikuwa pamoja na al-Hakam ibn Utaybah na tulimtembelea al-Imam al-Baquir a.s. Al-Hakam alimwuliza swali Imam a.s. Abu Ja'afer a.s. alikuwa akimstahi sana. Wao walitofautiana juu ya swala fulani na hapo Abu Ja'afer alisema: "Mwanangu (mtoto wake), inuka na ukilete kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Huyo mtoto alimletea kitabu kikubwa, ambacho Imam a.s. alikifungua, na kulipitishia macho hadi kulipata swala walilokuwa wakilizungumzia. Na hapo Abu Ja'afer a.s. alisema: "Haya ni maandishi ya Imam Ali ibn Abi Talib a.s. na yaliyosemwa na Mtume s.a.w.w..........."

Katika riwaya nyingineyo ameripotiwa Imam al-Baquir a.s. akisema: "Katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. nimepaona ambapo Mtume s.a.w.w. akisema: 'Wakati zakat itakapokuwa hailipwi, basi baraka itapotea kutoka ardhi."

Vile vile ipo imeripotiwa kuwa Imam al-Sadiq a.s. amesema:

Baba yangu alisema:

"Mimi nimesoma katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa Mtume s.a.w.w. ameandika mkataba baina ya Muhajirun na Ansar na watu wengineo wa Yathrib ambao waliungana naye, ikisemwa humo hivi: "Jirani ni sawa na mtu mwenyewe; asitendewe visivyo haki au kutendewa madhambi. Utukufu wa jirani wa mtu ni sawa na ule utukufu wa mama yake."

Katika riwaya nyingine al-Imam al-Sadiq a.s. amesema:

Imeelezwa katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s.

"Mfano wa dunia ni sawa na mfano wa nyoka: ngozi yake nyororo mno, lakini ndani yake ni sumu kali mno. Mtu aliye mwenye busara hujiweka naye mbali, lakini jahili anafanya kila aina ya jitihada ya kutaka kuikaribia."

Kwa mujibu wa riwaya nyingineyo, habari ifuatayo imetoka katika kitab adab Amir al-Muminiin:

Mtu yeyote asijaribu kurejea katika mithali katika masuala ya Din, kwani amri ya Allah swt haiwezi kutambuliwa kwa mithali. Watatokezea watu ambao watakuwa wakirejea katika mithali, na hao watakuwa na uadui pamoja na Din.

Zurarah anaripoti:

Nilimwuliza al-Imam al-Baquir a.s. kuhusu hisa ya babu katika urithi. Imam a.s. alijibu: "Sijawahi kumwona mtu yeyote yule akilisemea swali hili bila ya kuongezea mawazo yake ya kibinafsi, isipokuwa Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s.." Mimi nilimwuliza: "Na jee alisema nini?" Imam a.s. alinijibu: "Njoo kesho, mimi nitakusomea kutoka kitabuni." Mimi nilisema, "Mimi niwe fidia juu yako, naomba uiseme katika mtungo wa Hadith kwani Hadith zako ni afadhali kwangu kuliko kukisoma kitabu." Imam a.s. alisema: "Tafadhali usikilize kile nilichokuambia. Njoo kesho na mimi nitakusomea kutoka kitabu hicho." Siku ya pili mimi nilimwendea Imam a.s. wakati wa adhuhuri. Jaafer ibn Muhammad mwanae Imam a.s. alinikaribia na Imam a.s. alimwambia kunisomea kitabu hicho........

Katika riwaya nyingine, Imam al-Sadiq a.s. anasema:

"Ipo imeelezwa katika Kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib a.s. kuwa mtu anywaye pombe na mwenye kumsaidia aliyelewa (muskir) basi wote wanastahili kuadhibiwa, ambavyo ni sawa katika sura zote mbili."

Muhammad ibn Muslim, Sahaba wa Imam al-Baquir a.s. asema:

"Abu Jaafer alinisomea kitabu kitab al-faraidh, ambacho yalikuwemo yaliyosemwa na mtume s.a.w.w. na kuandikwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s.."

Habari zote zilizotajwa hapo juu, ambazo ni chache sana kutokea riwaya nyingi mno kama hizo, zinatudalilisha kuwa desturi ya Mashia ya kuandika Hadith imetangulia mawaidha ya ma-Imam a.s. kwa sahaba wao kuhusu uandishi wa Hadith. Ilikuwa ni desturi ambayo ilianzia katika zama za Mtume Mtukufu s.a.w.w. na ilikuwa imeanzishwa na Imam Ali ibn Abi Talib a.s. Zipo Hadith, nyingi katika desturi ya Mashia ambazo zimetimiza kanuni za tawatur, na vile vile yapo marejeo katika Sunni ambazo zinathibitisha na kushuhudia Hadith kama hizo.

Mambo yote hayo yanakuelekeza katika uimara na uhakikisho wa usahihi wa Hadith zilizonakiliwa na Mashia. Hii ni kwa sababu pamoja na kuendelea na maongozo ya Maimamu a.s. hadi kufikia katikati ya karne 3 A.H./9 A.D., Hadith za Mashia zilitoa watunzi wengi mno na ambao maandishi yao kuanzia kipindi cha al-Imam al-Sadiq a.s. yamekuwa kwa hakika ni katika idadi kubwa sana. Iwapo mtu ataweza kutupia macho Rijal al-Najashi, basi huyo ataweza kuona kuwa wafuasi wa Imam a.s. wametupatia kazi kubwa ambazo zimetumika kama misingi ya Fiqh katika Ushia.

Ukweli ni kwamba, Mashia idadi yao ndogo kwa upande mmoja na maisha ya hatari waliyokuwa wakiishi kwa upande wa pili ambayo iliwazuia watu waovu na wenye kuvizia majukumu kuingia katika Ushia pamoja na umuhimu uliosisitizwa na Maimamu a.s. na wafuasi wao katika uandishi, ndivyo vilivyoleta matokeo ya utajiri na usahihi wa Fiqh ya Kishia. Haya ndiyo faida ambazo hazikupatikana kwa Ahl al-Sunnah kwani, kwanza, wingi wa idadi yao, pili, kwa kuwa madhehebu ya Sunni ndiyo iliyokuwa Dini ya utawala wa Dola, na tatu, kwa sababu ya ukosefu wa Hadith zilizoandikwa kwa Waislam kwa ujumla kuyafuatilia yale yanayotokana na ukweli wa misingi ya kihistoria.