rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

 

UHARAMISHO WA R I B A

Kimekusanywa na kutarjumiwa na : AMIRALY M. H. DATOO

MANENO MAWILI

Kama inavyoonekana katika picha ya ukurasa wa kwanza, utaona kuna kifurushi cha fedha zilizo kidogo yaani mkopaji anapokopa hukopa kidogo na anaporejesha, hurejesha kifurushi kinono, kama kinavyojionehsa. Yaani tusema riba inamnyonya mnyonge anakwisha na kinamnenepesha mtoza riba.

Dhambi la riba ni miongoni mwa Madhambi Makuu. Dhambi hili limeelezwa vyema kabisa katika riwaya na Ahadith za Mtume Muhammad s.a.w.w., Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. , Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. , Al-Imam Musa al-Kadhim a.s. na Al-Imam Muhammad at-Taqi a.s.

Kwa mujibu wa Qur’an tukufu, kuchukua riba ni dhambi ambalo linasababisha adhabu kali kabisa kutoka kwa Allah swt. Adhabu za kuchukua na kutoza riba ni kali kabisa kuliko madhambi mengine. Kama ilivyoelezwa katika Surah Aali Imran, 3, : 130 - 131:

‘Enyi Mlioamini! Msile riba, mkizidisha mara dufu kwa mara dufu; na mcheni Allah ili muweze kuwa na ufanisi’

‘Na ogopeni moto wa Jahannam ambao umetayarishiwa makafiri.’

Inamaanisha kuwa ukali wa moto ambao umetayarishwa kwa ajili ya wale ambao huchukua riba kama vile moto utakavyokuwa mkali kwa ajili ya makafiri.

Allah swt anatuambia katika Surah al Baqarah, 2, Ayah ya 275 :

‘ Wale wanaokula riba, hawasimami ila kama anavyosimama yule ambaye Shaitani kamzuga kwa kumsawaa; na haya ni kwa sababu wamesema, ‘biashara ni kama riba’, Allah ameihalalisha biashara na kaiharamisha riba. N a aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali) aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba) basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.’

Ayah hiyo inatuthibitishia kuwa wale wanaochukua riba watabakia kwa milele katika Jahannam (Motoni) na kamwe hakutakuwa na uwokovu kwa ajili yao. Allamah Muhammad Husain Tabatabai (a.r.) katika Tafsiri ya Al-Mizan , anasema:

“Adhabu aliyoiweka Allah swt kwa ajili ya mla riba ni kali kabisa kwani hakuna mahala pengine palipozungumzwa kwa ajili ya wale wavunjao kutoka Furu-i-Diin. Kosa lingine ni lile la kulea urafiki pamoja na maadui wa Islam. Athari za riba zipodhahiri na bayana kwetu sote. Kukusanya na kuficha mali ndiko kunako ongezea tofauti kati ya tabaka la masikini na tajiri. Umasikini ni ugonjwa ambao unamdhalilisha na kumshusha hadhi mgonjwa wake, unateketeza uthamini wake na kuharibu maadili yake. Na haya yanaelekeza katika mutenda maovu, uizi, ubakaji na mauaji. Walanguzi ndio watu wanaowajibika kwa kuteketea kwa usawa wa kijamii, ambao wamejilimbikizia mali kupita kiasi kwamba haiwafikii wanao hitaji na wenye dharura. Kwa kuvunjika kikamilifu kwa mshikamano wa kijamii unaweza kuzua na kukuza vita vya wenyewe kwa wenyewe au vita vya ndani na kuendelea hadi kuzuka kwa vita vya dunia ambavyo hatima yake itakuwa ni mauaji na maangamizo. Katika ulimwengu wa sasa ikiwa na silaha za kisasa za teknolojia ya hali ya juu na ya maafa makubwa katika nuklia na kemikali, vita vinapozuka si kwamba vinaleta mauaji ya wanaadamu tu bali humgeuza yeye kuwa ni picha tu, mgonjwa na asiye na uwezo wowote na ameharibika kimwili kwa vizazi na vizazi vijavyo.

Athari mbaya kwa jamii ya Waislamu kwa kutokana na urafiki na uhusiano pamoja na maadui wa Islam, yapo dhahiri na bayana.

Wanahistoria wamerekodi kuwa urafiki pamoja na maadui wa Islam unanunuliwa kwa malipo. Na malipo katika swala hili ni kuafikiana. Maafikiano katika misingi hii yanaipeleka nchi katika kupoteza utamaduni na Uislamu vyote kwa pamoja yaani unafika wakati ambapo nchi hiyo haitwi tena nchi au jamii ya Kiislamu.”

Riba inapingana na akili na Shariah

Aya za Surah Al-Baqarah zilizoelezwa hapo juu, zinasema kuwa wale watu ambao wanachukua riba (riba katika mikopo) watahesabiwa miongoni mwa vichaa (ambao wameguswa na Shaitani). Siku ya Qiyama, watu watawatambua hawa kuwa ndio waliokuwa wakila riba humu duniani kwamba watakuwa ni vichaa. Utukufu wao utakuwa umeshakwisha teketea, kwa sababu wao humu duniani wamekuwa wakienda kinyume na akili na Shariah. Wao wameshakwisha kusahau tangia zamani matakwa na mahitajio ya binadamu. Wao hawakuwa na uhusiano wa usawa pamoja na wengine na vile vile walikiuka kanuni za ushirikiano. Kwa hakika watu hawa wamekuwa ni wapumbavu humu duniani, kwa sababu wao wamefuata maagizo ya Shaitani na ndivyo maana wamekuwa wakitenda matendo ya kipumbavu.

Je Biashara na Riba ni kitu kimoja ?

Mabishano haya yote kwa pamoja ni upumbavu. Hakuna ulinganisho wowote baina ya biashara na riba. Katika biashara kuna usawa kwa sababu humo kunakuwapo maelewano baina ya mnunuzi na mwenye mali na wote kwa pamoja ama huweza kupata faida au hasara. Katika biashara, muuzaji anauza bidhaa kwa mnunuzi kwa bei wanayoafikiana wote wawili, na swala hili huishia hapo. Lakini kuchukua riba ni swala la mkato la uchafuzi na kuteketeza. Mtu ambaye anayo mali au mapesa ya ziada, ambayo yeye hazihitaji, humwazima au kumkopesha mtu ambaye anakuwa na shida kali. Mtu mwenye shida kali anakubali kulipa riba ambayo kwa hakika hana uwezo nayo ; si kwamba yeye anaikubalia bali anakuwa ameshurutishwa na shida iliyomkaba vibaya sana wakati huo.

Riba na Utofauti wa Tabaka katika Jamii

Haina shaka, kuwa riba ni ubaya ambao hauna haki na inayokandamiza katika jamii. Riba inapingana na maumbile ya kibinadamu na hadhi ya mwanadamu. Hivyo huwaongezea utajiri wa matajiri na kuwaangamiza kabisa walio wanyonge na wale wenye hali ndogo kuingia katika umasikini.

Hakuna shaka, masikini aliyekwisha haribiwa anaanza kuonesha chuki zake dhidi ya matajiri. Kizimba hicho cha uchukivu unajipatia mwanya wa kutokea katika sura ya vurugu, uporaji, machafuko na mapinduzi ya umagikwaji wa damu.

Katika kitabu ‘Islam and World Peace’ imeandikwa:

“Islam inasema kuwa mapato ya mtu yatokane na kiwango cha juhudi na kazi iliyofanyika.” Kwa sababu uwekezaji wenyewe haufanyi kazi wala jitihada ya aina yoyote ile. Hivyo, mali ya matajiri haitakiwi kamwe kuongezeka kwa kutokana na riba.”

Kuiongezea utajiri mali iliyopo kwa kupitia riba ni njia iliyo saheli kabisa ya kujipatia utajiri, lakini imeharamisha kabisa hivyo. Mali haiwezi kuongezwa kwa kumnyonga mnyonge atumbukie katika umasikini zaidi ya hali mbaya aliyonayo; na hicho ndicho kinachofanywa na mtoza riba, husababisha kutokuwa na usawa katika uchumi na kukanyaga haki za binadamu, usawa na haki. Maulana Sayyid Abul ‘Ala Maududi wa Pakistan ameandika kitabu kivutiacho chenye kuieleza na kuipambanua riba na ambacho kinaelezea athari mbaya za riba kwa kutoa hata takwimu mbalimbali.

Mtu mwenye shida si kwamba anarudisha kile alichokuwa amekopa kwa riba bali hulazimika kurudisha zaidi na zaidi ya kiwango alichokuwa amekopa. Ziada hiyo huwa hata inazidi mara dufu na zaidi kuliko kile kiwango alichokuwa amekopa iwapo malipo yatakapotokea kucheleweshwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake. Kwa hakika riba humtumbukiza mtu katika matatizo zaidi ya kifedha juu ya mtu ambaye yupo tayari ameshatumbukia katika shida na hivyo kwa kutambua hayo, bado ikiwa analazimishwa kulipa kile kilicho nje ya uwezo wake ni udhalimu mbaya sana. Kimaadili, mtu mwenye shida asaidiwe kwa kupewa mikopo bila ya kumtoza riba. Na kwa hayo kunaongezea mapenzi ya urafiki, udugu, uhusiano na ushirikiano na ndivyo ni mambo mema.

Riba kwa ajili ya mikopo

Kutoa mikopo kwa kutoza riba si kwamba inateketeza uwiano wa kiuchumi katika jamii, bali inalipua hisia za chuki, uadui na ubinafsi.

Anayejitumbukiza katika riba anajikosesha mema

Yapo maovu mengi katika kutoza riba. Mapato yanayotokana na riba huwa yanakosa baraka za Allah swt. Wakati mapato yanyotokana na kuvuja jasho huwa yana baraka kwa wingi.

Mtume Muhammad s.a.w.w. anasema katika Hadith moja, katika Wasa’il al-Shiah :

“Ibada inayo sehemu sabini. Na muhimu kabisa ni mtu kujipatia kipato chake kilicho halali.”

Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Muhajjatul Baidha:

“Mfanyabiashara mwaminifu atahesabiwa pamoja na Mitume a.s. Siku ya Qiyama. Uso wake utakuwa uking’ara kama mbalamwezi.”

Mtoza riba huwa hamwamini Allah swt

Hasara nyingineyo aipatayo mtoza riba ni kule kukosa kumwamini Allah swt. Yeye kamwe huwa haombi kwa Allah swt amwongezee baraka kwani matumaini yake yote kwa pamoja huwa yako katika riba anayoikusanya kutoka wadaiwa wake na hii ndiyo shirk kama vile inavyozungumziwa katika maudhui ya Shirk katika vitabu vya Fiq-hi.

Jambo lingine la kutiwa maanani ni kuwa, katika biashara za kawaida, mfanyabiashara huweza ama kujipatia faida au hasara. Kwa hivyo daima mfanya biashara huyo huwa anajitahidi sana katika biashara yake na humwomba Allah swt ampatie baraka na ufanisi katika biashara yake hiyo ili apate faida. Lakini mtoza riba hana wasiwasi na hasara na hivyo anaona hakuna haja ya kumwomba Allah swt amjaalie riziki. Na hivyo hupoteza fursa hiyo ya kumnyenyekea Allah swt.

Thawabu ya kutoa mkopo ni zaidi ya kutoa sadaqa.

Mtoza riba hujipotezea malipo mema (thawabu) zinazopatikana kwa kutoa mikopo njema. Kama yapo mema kumi katika kutoa sadaqa, basi kutoa mikopo bila riba inayo kumi na nane. Hivyo mikopo bila riba inayo thawabu mara dufu ya kutoa sadaqa katika njia ya Allah swt. Mtu ambaye anawahurumia wadaiwa wake na hawatozi riba basi hupewa thawabu sawa na kiasi hicho kwa kila siku kwa muda atakaouongeza katika kulipwa deni lake. Kwa hakika mtoza riba hastahiki kwa malipo hayo, badala yake yeye anajichumia madhambi. Kwa hakika analaaniwa kwa uchoyo na uroho, ambayo magonjwa hayo huongezeka kila siku. Kwa hakika mwisho wa uchoyo na uroho ni Jahannam (Motoni).

Hatima ya mtoza riba

Kama tulivyokwisha kuona katika Ayah za Qur’an, Ahadith za Mtume Muhammad s.a.w.w. pamoja na Maimau a.s. kuwa adhabu ya mtoza riba ni kali na mbaya kabisa hata kuliko madhambi mengine na tumezungumzia sababu zake pia. Islam imeiweka riba kuwa ni Adh-Dhunubul Kabirah (Madhambi Makuu) na adhabu yake ni kali kabisa kuliko zote. Iwapo mtoza riba hatafanya Tawba kwa matendo yake, hivyo hatima yeke itakuwa pamoja na makafiri ambao hawana mahala pengine isipokuwa ni Jahannam kwa milele. Na mtoza riba kamwe hataachiliwa kutoka humo.

Qur’an Tukufu inarejea kutuambia katika Surah al-Baqarah, 2 Ayah 275 :

‘‘N a aliyefikiwa na mauidha kutoka kwa Mola wake, kishaakajizuia, basi yamekwisha mthibitikia yale (mali) aliyoipata; na hukumu yake iko kwa Allah. Lakini wanaorejea (kula riba) basi hao ndio watu wa Motoni, humo watakaa milele.’

Hata hivyo kuna baadhi ya njia ambazo mtoza riba anaweza kufidia madhambi yake na kuomba Tawba kwa Allah swt. Yapo madhambi ambayo Allah swt huzisamehe kwa kuomba msamaha (Tawba) iliyo sahihi na kweli. Iwapo kafiri akitubu madhambi yake na akawa Mwislamu, basi dhambi kuu kama la shirk linasameheka. Yeye hahitaji kufanya lolote zaidi ya hayo. Lakini zipo baadhi ya madhambi ambayo yanahitaji kulipia fidia sambamba na kufanya Tawba i.e. kama mtu ambaye anayo qadhaa sala na saumu. Yaani pamoja na kufanya Tawba inambidi alipe sala na saumu zote alizoziacha. Vivyo hivyo katika swala la riba, mtoza riba itabidi afanye tawba na wakati huo huo awarudishie mapesa wale wote aliokuwa amewatoza kama riba.

Hakuna Baraka katika riba

Ayah ya hapo juu ya Qur’an inaendelea Surah al-Baqarah, 2 Ayah 276 :

‘ Allah huyafutia (baraka mali ya ) riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa . Na Allah hampendi kila kafiri (na) afanyaye dhambi.’

Sadaqa inaeneza amani, inaongeza ukarimu, uwema na mapenzi katika jamii, ambapo riba inaangamiza amani na kuzifanya nyoyo za watu ziwe ngumu.

Wakati riba inapotanda mizizi yake katika jamii, basi watu katika jamii hawatasita kudhulumiana haki zao miongoni mwao. Wao watakuwa wameghalibiwa na hisia za chuki, uadui na uchu wa kulipiza kisasi. Jamii ambayo imeondokewa na ushwari, upendo na ushirikiano basi kamwe haiwezi kujipatia maendeleo, kwa hakika inajiangamiza kwa maovu yake yenyewe. Misaada na sadaqa kwa upande mwingine, huongeza hisia na moyo wa urafiki, mapenzi na udugu. Hali ya amani na baraka hutanda kote ambavyo ni changamoto kwa watu kundeleza matendo mema.

Vita dhidi ya Allah swt na Mtume Muhammad s.a.w.w.

Qur’an Takatifu inatuambia Surah al-Baqarah, 2, Ayah 278 :

‘ Enyi Mlioamini ! Mcheni Allah, na acheni yaliyobakia katika riba, ikiwa mmeamini.’

Ushahidi wa imani ya mtu katika utiifu wa Hukumu za Allah swt, ayah hiyo hiyo inaendelea :Al-Baqarah, 2, Ayah 279

‘Na kama hamtafanya hivyo, basi fahamuni mtakuwa na vita na Allah na Mtume Wake….’

‘Na mkiwa mmetubu, basi matapata rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiane.’

Yeyote yule asiyeitii amri hii basi ajitayarishe kwa vita dhidi ya Allah swt pamoja na Mtume Muhammad s.a.w.w. .

Twapatiwa ufafanuzi wa Ayah hii katika Tafsir Minhajus-Sadiqiin . Inaweza kumaanisha kuwa dhambi la riba ni mbaya na ovu kabisa hadi kwamba iwapo Mtume Muhammad s.a.w.w. angelikutana na mtoza riba humu duniani basi Mtume Muhammad s.a.w.w. asingalisita kuutoa upanga wake na kupigana vita na huyu mtu punde wangalikuwa wameonana uso kwa uso. Na huko Aakhera, Moto mkali wa Jahannam utamweka katika adhabu kali yenye mateso kwa amri ya Allah swt. Mtoza riba lazima apigwe vita vikali hadi hapo aache kutoza na kupokea riba. Riwaya zinatuelezea kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. baada ya kuteremka kwa Ayah hiyo, alimjulisha Gavana wa Makkah kuwa iwapo kabila la Bani Mughaira hawataacha kutoza na kupokea riba, basi lazima vita vitakatifu vitangazwe dhidi yao.

Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amezungumzi katika hotuba yake huko Makkah :

“Muelewe kuwa riba iliyokuwa imekusanywa katika zama za ujahiliyya sasa imesamehewa kabisa. Kwanza kabisa mimi binafsi nina wasameheni ile riba ( iliyopo shingoni mwenu) ya (mjombangu) '‘Abbas ibn Abdul Muttalib."

Ahadith zinazokana riba

Imeripotiwa kutoka Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. kuwa, katika Al-Kafi :

“Kuchukua Dirham (au pesa moja) kama riba ni vibaya sana machoni mwa Allah swt kuliko kuingiliana na mwanamke aliyeharamishwa kwako.”

Al-Imam ‘Ali ibn Abi Talib a.s. amesema katika Wasa’il al-Shiah :

“Mtume Muhammad s.a.w.w. amemlaani vikali yule ambaye anayekubali riba, anayelipa riba, aneyeinunua riba, anayeiuza riba, yule anayeandika mikataba ya riba na yule anayekuwa shahidi wa mikataba hiyo.”

Ibn Baqir anaripoti kuwa Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. alijulishwa kuhusu mtu mmoja aliyekuwa akitoza na kupokea riba kama ndiyo halali kama vile ilivyo halali maziwa ya mama. Kwa hayo, alisema Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. katika Al-Kafi :

“Iwapo Allah swt atanipa uwezo mimi juu ya mtu huyu, basi nitamkata kichwa.”

Hivyo imetuwia dhahiri kuwa riba ni haraam kabisa na hii ndiyo imani ya Mwislamu kukiri na kuamini na kuifuata kuwa riba ni haraam. Iwapo mtu yeyote ataipuuza hivyo na akasema kuwa riba si haraam, basi huyo atakuwa ni kafiri papo hapo. Na hivyo Imam a.s. anaweza kumwua.

Riba imekanwa katika Qur’an

Samaa anasema kuwa yeye alimwuliza Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. je ni kwa nini Allah swt ametaja kuharamishwa kwa riba mahala pengi katika Qur’an. Al-Imam Ja’afer as-Sadiq a.s. alimjibu, katika Wasa’il al-Shiah :

‘Ili kwamba watu wasiache tendo la kutoa misaada (kama vile kutoa mikopo bila ya riba).”

Amesema al-Imam Muhammad al-Baqir a.s. katika Wasa’il al-Shiah :

“Shughuli mbaya kabisa ni ile ambayo inahusisha riba.”

Mhalifu anakosa Imani ya Dini

Zurarah anasema kuwa yeye alimwuliza Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. kuhusu Ayah ya Qur’an isemayo katika Surah Al-Baqarah,2, Ayah 276:

‘‘ Allah huyafutia (baraka mali ya ) riba: na huyatia baraka (mali yanayotolewa) sadaqa .’

Na akaongezea kusema :

“Lakini mimi ninaona kuwa mali na utajiri wa watoza riba inaendelea kuongezeka tu kila siku.”

Amesema Al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa’il al-Shiah :

“Loh ! hasara inawezekana kuwa kubwa sana ? Kwa merejeo ya Dirham moja yeye anaipoteza Dini yake. Na iwapo yeye atafanya Tawba humu duniani basi kutafikia mwisho kwa mali aliyoichuma humu duniani kwa njia iliyo haramu na hivyo kuwa fukara.”

Matumbo ya watoza riba zitajazwa kwa moto

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il :

“Yule anayechukua riba basi Allah swt atalijazatumbo tumbo lake kwa moto kiasi hicho hicho. Iwapo yeye amechuma zaidi kwa kutokana na mapato ya riba, basi Allah swt hatakubalia matendo yake mema. Hadi kwamba kiasi cha punje moja kama kitabakia ambacho kimepatikana kwa njia ya riba. Allah swt pamoja na Malaika Wake wataendelea kumlaani huyu mtu.”

Adhabu za mpokea riba katika ‘Barzakh’

Vile vile Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema :

“Usiku wa Me’raj Mimi niliwaona baadhi ya watu waliokuwa wakijaribu kusimama lakini hawakuweza kufanikiwa kwa sababu ya matumbo yao makubwa, niliuliza, ‘Ewe Jibraili ! Je ni watu gani hawa ?’

Jibraili alijibu : “Hawa ndio wale waliokuwa wakichukua riba. Sasa wao wanaweza kusimama tu kama wale waliokamatwa na Mashetani.”

Mtume Muhammad s.a.w.w. aliendelea,

“Na hapo nikawaona wao wakikusanywa katika njia za wafuasi wa Firauni. Kwa kuona uchungu wa joto la Moto mkali, wao walipiga kelele : ‘Ewe Allah swt ! Je Qiyama itakuwa lini ?’

(Hivyo imekuwa dhahiri kuwa Moto unaozungumziwa katika riwaya hii ni adhabu katika Barzakh ).

Watoza riba kukanyagwa na miguu ya Firauni

Katika riwaya nyingine imeelezwa kuwa watu hawa walipowaona watu wa Firauni, basi walijaribu kuinuka na kutaka kukimbia, lakini kwa kutokana na matumbo yao kuwa makubwa kupita kiasi, hivyo hawakuweza kuinuka na hatimaye wafuasi wa Firauni walipita na kuwakanyagakanyaga kwa miguu yao, na wakaendelea mbele na safari yao.

Imepokelewa kutoka kwa Mtume Muhammad s.a.w.w. akisema, katika Mustadrakul Wasa'il :

“Wakati zinaa na riba vitakapokuwa ni vitu vya kawaida katika mji wowote basi Allah swt huwapa ruhusa Malaika kuwaangamiza wakazi wake.”

Ipo riwaya nyingine isemayo kuwa Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, katika Mustadrakul Wasa'il kuwa :

“Utakapofika wakati Ummah wangu utaanza kutoza na kupokea riba, basi mitikisiko na mitetemeko ya ardhi yatakuwa yakitokea mara kwa mara.”

Riba ni mbaya kabisa kuliko hata Zinaa

Mtume Muhammad s.a.w.w. amesema, Wasa’il al-Shiah :

“Iwapo mtu atazini pamoja na mama yake katika Al-Ka’aba tukufu, basi dhambi hili litakuwa hafifu mara sabini kuliko tendo la kutoza na kupokea riba.”

Amesema al-Imam Ja'afar as- Sadique a.s. katika Wasa’il al-Shiah :

“Katika macho ya Allah swt, kuchukua Dirham moja ya riba ni mbaya kabisa hata kuliko matendo thelathini ya kuzini pamoja na maharimu wake yaani baba kuzini pamoja na binti yake.”

Hadith iliyopita inaelezea dhambi hili kuwa ni mara sabini ya kuzidi dhambi la zinaa. Ipo riwaya nyingine inayosema kuwa kuchukua Dirham moja ni sawa na matendo sabini kama hayo. (Wasa’il al-Shiah )

Hata katika dunia ya leo, mabaya ya riba yametapakaa kwa kiasi cha kutisha cha kwamba uchumi upo unaangamia. Baadhi ya wanauchumi wanasema kuwa riba ni muhimu kwa maendeleo. Kama hivi ndivyo ingalikuwa kweli, basi Dini ya Islam kamwe isingalikuwa imeharamisha. Kwa sasa hivi zipo fikra mbili za kiuchumi ambazo fikra zao haziendeshwi na riba. Moja ni Ukomunisti na nyingine ni Islam. Wakati ambapo misingi ya mabepari ni riba. Hata hivyo kuna tofauti kubwa baina ya Wakomunisti na Uchumi wa Kiislam.

Uislamu kamwe haujaona dharura ya kupokea riba kama ndio uhai wake katika uchumi, ambapo ukomunisti unapokea riba. Na hivyo haijawahi kusikika kuwa uchumi wa Kiislam umedhoofika kwa kutokushirikisha riba.

Hivyo, tutakubaliana kuwa hivyo ni lazima kwa wachache fulani walio na uroho wa kulimbikiza mali zaidi ya kile walichonacho kwa kuwanyonya na kuwakandamiza wanyonge na wenye shida. Madhumuni yao ni kuwafanya watumwa wao. Na sisi sote tunajua habari zao.

Mikopo yenye kutoza riba

Mikopo inayotoza riba ni ile ambayo mtu anapopewa mkopo anapewa masharti ya kuirudisha kwa wakati maalumu ikiwa pamoja na nyongeza ya mapesa, sharti la lazima. Mkopo uliotolewa unaweza kuwa wa mapesa au vitu vinginevyo, mfano, mtu anaweza kukopa vibaba vitano za mchele na kutegemea kurudishiwa vibaba sita. Nyongeza iliyoshurutishwa inaweza kuwa katika sura ya fedha au kitu kingine, utumishi au upendeleo.

Mfano, mtu anaweza kutoa mkopo kwa masharti kuwa mtu aliyekopa atazirudisha fedha hizo na atamfanyia kazi mbalimbali nyumbani mwa mkopeshaji. Au mkopeshaji anaweza kumkopa mtu kiasi fulani cha fedha kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa masharti kuwa ataishi katika nyumba ya mwenye kukopa kwa mwaka mzima bila ya kulipa kodi ya nyumba hiyo. Au mtu anaweza kutoa dhahabu kama mkopo na akimtaka mtu aliyekopa amtengenezee vito bila ya kumtoza gharama. Yaani chochote kile kitakachotakiwa kwa kuzidi kiasi cha kile kilichotolewa, bila ya kujali aina ya kitu, ni riba ambavyo ndivyo Haraam katika Dini ya Islam. Haidhuru kama masharti kama hayo yalikuwa yamewekwa kuanzia mwanzoni au baadaye. Katika sura zote ni Haraam.

Mambo muhimu ya kuzingatia

Mapatano ya aina yoyote yale yanayohusisha riba ni haraam. Kutoza riba pia ni haraam na kulipa riba pia ni haraam vile vile. Iwapo mtu atakopa na atachukua fedha kwa riba na akazitumia na kupata faida, basi atambue kuwa mwenye faida si yeye bali ni mwenye kumkopesha. Kwa mfano iwapo yeye atakopa ngano na kuzipanda shambani, basi mazao yanayoota kutokana na hayo, kwa hakika ni mali ya mkopeshaji. Hata hivyo, iwapo mkopeshaji atakuwa amekubali kuwa mkopo wake utumike hivyo, basi faida itakayopatikana itakuwa ni mali ya mtu aliyekopa.

Iwapo mtu atampa mfanyabiashara kiasi fulani cha fedha kwa maelewano kuwa yeye atamrudishia kasoro ya kiasi hicho, inakubalika. Kwa mfano, yeye atampatia mfanyabiashara wa Bukoba Shillingi elfu moja na akakubaliana kurudishiwa shilingi mia tisa na tisini tu katika mji wa Mwanza, hivyo anaruhusiwa kufanya hivyo. Aina hii ya mapatano inajulikana kama sarf-i-baraat, kwani humu riba haikuhusishwa.

Iwapo wakati wa kutoa mkopo hakukuzungumzwa riba na mtu aliyekopa anataka kurudisha mkopo huo ikiwa pamoja na nyongeza kidogo kwa furaha yake mwenyewe bila ya kushurutishwa, basi inakubalika na si haraam. Kwa hakika hivyo ndivyo Sunnah. Vile vile ni Sunnah kulipa mkopo kabla ya wakati wake au kabla aliyekopa hajazidai. Vile vile ni Sunnah kwa mtu aliyekopa kuongezea chochote kidogo kama kazawadi wakati anapomlipa yule aliyemkopa. Lakini ni lazima kuwa nyongeza hiyo iwe imenuiwa kuwa ni zawadi na kamwe si riba. Hata isidhaniwe kuwa ni riba. Vile vile ni Sunnah kwa wakopeshaji kupokea chochote kile cha ziada wanachopewa kama zawadi, wala wasidhani kuwa ni riba, na hivyo wakubali ni kama ishara ya ukarimu.

Mapatano yanayohusiana na riba

Iwapo kutakuwapo na masharti yoyote yale katika mapatano , basi hayo mapatano yenye riba yatakuwa haraam :

Chochote kile kilichochukuliwa na kilichorudishwa ni vya aina moja lakini idadi, uzani au ujazo wake si sawa au iwapo idadi au uzani wake ni sawa, kunatofauti katika ubora wake, n.k.

Iwapo kutakuwa na aina moja ya uzani na uzito, kiasi kilichochukuliwa na kurudishwa vitakuwa vya uzito na uzani tofauti. Hata hivyo, iwapo wakati wa kukopesha uzani ulikuwa katika kilogramu na wakati wa kurudisha uzani ukawa katika ratili au seer, hivyo pia inaruhusiwa. Vivyo hivyo iwapo vitu vilichukuliwa katika vipimo vya mita na wakati wa kurudishia vikawa katika futi au yadi, vyote vinaruhusiwa.

Vile vile ni haraam kwa mtu kumkopa mtu mmoja kibaba kimoja cha ngano kwa mwezi mmoja na baadaye yeye mwenyewe akakopa kibaba kwa miezi miwili kutoka kwa mtu huyo huyo. Ingawaje kiasi kwa kipimo ni kile kile, mapatano hayo ni haraam kwa sababu swala la muda nalo ni nyeti humo.

Mambo matatu yakuzingatia

Katika swala la riba, ngano na shayiri ni vitu mamoja. Iwapo mtu atatoa chungu kimoja cha ngano na kupokea chungu kimoja na nusu cha shayiri, basi hiyo ni riba na hivyo ni haraam.

Vivyo hivyo, chochote kile kinachofanya kitu chenyewe inajulikana kama ni sawa kwa sawa. Kwa mfano, maziwa na maziwa mgando, vyote ni sawa, siki ya zabibu na zabibu viko sawa, sukari na miwa ni sawa vile vile. Vyote hivi kama vitakopeshwa basi lazima virudishwe kwa vipimo hivyo hivyo ama sivyo vitahesabika katika riba na hivyo kuwa haraam.

Iwapo mtu atatoa mkopo wa kibaba kimoja cha ngano na kitambaa cha leso na kuchukua kibaba kimoja na nusu cha chungu cha ngano, basi hii haisemwi kuwa ni riba na hivyo haiwi haraam.. Katika mapatano haya, chungu kimoja kitakuwa ni badala ya chungu kimoja cha ngano na nusu chungu itakuwa ni badala ya kitambaa cha leso. Vile vile inawezekana kuwa mtu akatoa kibaba kimoja cha ngano pamoja na kitambaa cha leso na badala yake akapokea kibaba kimoja cha ngano na kitu kingine badala ya kitambaa cha leso, kama vile sabuni. Katika hali hii riba haikuhusishwa.

Iwapo mtu mwanzoni atauza kibaba kimoja cha ngano kwa Shilingi mbili na baadaye akanunua kibaba kimoja na nusu kwa shilingi mbili, inaruhusiwa. Kwa kuwa mapatano yote hayo ni mbalimbali na yanajitegemea. Hivyo havihusishi riba.

Inawzekana vile vile kuwa Zaid anamwuzia Khalid kibaba kimoja cha ngano na Khalid anampa kibaba kimoja na nusu cha ngano Zaid kama zawadi. Haya pia yanaruhusiwa.

Wakati ambapo kuchukua riba inaruhusiwa

Kuna aina tatu za watu ambapo kuchukua na kulipa riba inakubaliwa:

Baba na mtoto Baba na mtoto wanaweza kuingia katika mapatano ya riba. Lakini mapatano baina ya mama na mtoto yanayohusisha riba ni haraam.

Mume na mke : Mume na mke wanaweza kutozana riba. Kwa mfano iwapo mmoja atatoa Shilingi mia moja na badala yake akadai Shilingi mia moja na hamsini. Inaruhusiwa.

Kafiri ambaye haishi katika nchi ya Kiislamu. Kwa Mwislamu anaweza kuchukua zaidi lakini ni haraam kwake Mwislamu huyo kutoa zaidi. Hadi hapo Kafir Dhimmi (ambaye anaishi katika nchi ya Kiislamu) anahusika, ni hraam kuingia naye katika mapatano yoyote yanayohusisha riba. Kulipa na kuchukua iba, vyote ni haramu katika sura hii.

Nyongeza ya madondoo kutoka hapa na pale

MADHAMBI NA ATHARI ZAKE

1. Amesema Mtume Muhammad s.a.w.w. , Bihar al- Anwar ,j.77,uk.79 na

Mustadrak Al-Wasail ,j.11, uk. 330 :

“Msitazame udogo wa dhambi, lakini muangalie muliyemuasi (Allah swt).”

2. Amesema Al-Imam Amir-ul-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s., Bihar al- Anwar ,j. 70, uk.18

“Iwapo mtu anapenda kujiona vile alivyo mbele ya Allah swt, basi ajitathmini kwa madhambi na maasi yake mbele ya Allah swt; basi kwa kipimo hicho ndivyo alivyo huyo mtu mbele ya Allah swt.”

3. Al-Imam as- Sadique a.s. aliwauliza watu ni kwa nini wanamwudhi Mtume s.a.w.w. Basi mmoja wa watu alimwuliza Imam a.s. vipi, naye Imam a.s. aliwaambia, Usul-i-Kafi , j.1, uk.219 :

“ Je hamujui kuwa matendo yenu yapoyanajulishwa kwa Mtume Mtukufu s.a.w.w. na pale aanapoona madhambi dhidi ya Allah swt miongoni mwao, basi husikitishwa mno. Kwa hivyo musimuudhi Mtume wa Allah swt na badala yake munatakiwa kumfurahisha (kwa kutenda mema).”

4. Amesema Ali ibn Abi Talib a.s. , Ghurur al-Hikam, uk. 235

“Kukosa kusamehe ni kasoro moja kubwa kabisa na kuwa mwepesi katika kulipiza kisasi ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa.”

5. Kutokea Asbaghi bin Nabatah kutokea kwa Ali ibn Abi Talib a.s. amesema, Al-Khisal,cha as-Sadduq, j.2, uk. 360

“Amesema Mtume s.a.w.w. kuwa Allah swt anapoikasirikia Ummah na kama hakuiadhibu basi bei za vitu vitapanda juu sana yaani maisha yatakuwa ghali, maisha yao yatakuwa mafupi, biashara zao hazitaingiza faida, mazao yao hayatukuwa mengi, mito yao haitakuwa imejaa maji, watanyimwa mvua (itapungua), na watatawaliwa na waovu miongoni mwao.”

(Yaani Hadith hiyo juu inatubainishia kuwa iwapo kutakuwa na jumuiya ambayo imejitumbukiza katika madhambi basi wanabashiriwa kupatwa na mambo saba hayo yaliyotajwa. )

6. Al-Imam al-Baqir a.s. amesema kuwa amekuta katika kitabu cha Al-Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib a.s. akisema kuwa Mtume s.a.w.w. amesema: Safinat –ul-Bihar, j.2, uk.630

“Wakati zinaa itakapokithiri katika jumuiya basi idadi za mauti za ghafla zitakithiri; na patakapokuwa na uovu basi Allah swt atawatumbukiza katika maisha ya ghali na hasara. Wakati watu watakapoacha kulipa zaka , basi ardhi itazinyakua baraka zake kutokea mazao, matunda, madini na vitu vyote kama hivyo. Wakati watakapotenda bila haki kwa mujibu wa Shariah, basi itakuwa sawa na kumsaidia dhalimu na ugaidi. Na watakapozikiuka ahadi zao, basi Allah swt Allah swt atawafanya maadui wao kuwasaliti na kuwakandamiza. Wakati watakapoacha uhusiano pamoja na ndugu na jamaa zao, basi yote yale wayamilikiayo yatakwenda mikononi mwa waovu. Na wakati watakapojiepusha na kutoa nasiha ya mambo mema na kuyakataza maovu na kama hawatawafuata waliochaguliwa Ahl-ul-Bayt a.s., basi Allah swt atawasalitisha kwa walio wenye shari miongoni mwao na katika hali hii, wataomba duaa lakini hazitakubalika.”

7. Amesema Al-Imam Ali ibn Abi Talib a.s. , Bihar al- Anwar , j.70,uk.55

“Machozi hayaishi illa kwa nyoyo kuwa ngumu, na nyoyo haziwi ngumu illa kukithiri kwa madhambi.”

8. Allah swt alimwambia Mtume Dawud a.s.: Ithna-Ashariyyah, uk.59

“Ewe Dawud ! Wabashirie habari njema wale watendao madhambi kuhusu msamaha wangu, ambayo inajumuisha kila kitu kilichopo humu duniani, ili wasikate tamaa ya msamaha wangu; na waonye wale watendao mema kwa adhabu zangu ili wasije wakajifanyia ufakhari kwa utii wao, kwani ufakhari ni dhambi mbaya kabisa.”

T A M A T I ALHAMDU LILLAAH