rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

NDOA KATIKA ISLAM

Kimekusanywa na kutarjumiwa na: AMIRALY M. H. DATOO

1. MANENO MAWILI

Namshukuru Allah swt,Mtume Mtukufu s.a.w.w. pamoja na Ahli Bayt Tukufu a.s. kwa kunijaalia niweze kufanikisha juhudi zangu hizi katika kukitayarisha kitabu hiki juu ya maudhui haya ya ndoa katika Islam.

Mnamo mwezi April 1994 nilifanywa operesheni ya appendix huko Dar Es Salaam,na wakati bado nikiwa ninauguliwa, nilikianza kitabu hiki. Na baada ya kukusanya yakutosha nilikiacha, na kuendelea na maudhui nyinginezo katika kufanyia utafiti.

Na takriban tarehe 28 mwezi Julai 1995 nilibahatika kumtembelea Chief Missionary wa Bilal Muslim Mission of Tanzania, Hujjatul-Islam Sayyid Saeed Akhtar Rizvi,na katika mazungumzo yetu kulitokezea mazungumzo juu ya kitabu cha ndoa katika Islam. Na nilimwambia kuwa nilikuwa nimekifanyia kazi kiasi fulani.

Kwa hakika yeye alivutiwa mno, na kuniomba nikikamilishe haraka iwezekanavyo kwani alikuwa akihitaji kuchapa kitabu juu ya maudhui hayo. Nami baada ya kurejea kwangu Bukoba,2.8.95 nilikalia kitabu hiki na kuweza kukikamilisha vyema kwa uwezo wangu mdogo hadi leo tarehe 28.8.95.

Hivyo ni matumaini yangu kuwa,utafiti nilioufanya kwa kiasi hicho kidogo,kitasaidia katika ndoa na masuala yanayohusiana nayo na wengi tutaweza kujirekebisha ili kuweza kujipatia matunda bora kabisa katika maisha ya ndoa.

Hata hivyo nitapenda kupokea maoni na ushauri na masahihisho kuhusu maudhui na kitabu hiki kwa ujumla ili n iweze kuendeleza sura zinginezo ambazo sikuzigusia,ingawaje ni nyingi.