rudi maktaba >Fiqh >Yaliyomo >

 

MUT'A NDOA SAHIHI

UTANGULIZI

Alhamdulillahi, kila sifa njema ni ya Mwenyeezi Mngu, Bwana wa walimwengu. Na Rehma na Amani zimshukie Bwana wetu na Muombezi wetu Muhammad S.A.W., na ziwashukie Aali zake watakatifu, na wanaofuata na kuusimamia uongozi wao mpaka siku ya mwisho.

Ndoa ya Mut'a ni katika mas'ala waliyokhitilafiana Shia na Sunni kutoka mwishomwisho wa utawala wa Khalifa wa pili (Umar bunul Khattab) mpaka leo. Tarehe 17/8/1988 kwa tarehe 3 Muharram 1408 katika ukumbi wa Bilal house, Mombasa, nilizungumza juu ya ndoa ya Mut'a.

Tarehe 1/9/1989 katika Msikiti wa Al'azhar Mombasa, Sheikh Muhammad Sharif Famau alinijibu. Sheikh alizungumzia mambo matano:-

Uadilifu wa Masahaba. Tahriful Quran. Wilayatu Ali A.S. Taqiyya. Ndoa ya Mut'a.

Mimi katika kitabu hiki nitashughulika na Mut'a, na haya mengine yameshaanza kujibiwa na Mzee wangu Sheikh Abdilahi Nassir. Kwa hivyo, yeyote anayependa kujua majibu ya vifungu hivyo atasoma vitabu vya Sheikh Abdilahi vya majibu hayo.

Sheikh Muhammad Sharif katika darsa yake alizungumzia kwamba:-

Mut'a ilikuwako wakati wa Mtume. Kisha Mtume aliiondoa kabla ya yeye kufa. Kwa hivyo hivi sasa Mut'a ni haramu yeyote anayeoa hivyo ANAZINI.

Kwa mtazamo wa Sheikh Muhammad Sharif Mut'a ni Zina, na ametoa hoja zake.

Kwa hakika, nachukua nafasi hii kumpa pongezi za kweli kabisa. Ndugu yangu Sheikh Muhammad Sharif Famau kwa hatua aliyochukua ya kusahihisha lile ambalo anaona linapotoshwa nje ya misingi ya Islam. Huu ndio msimamo wa Islam, na mwislamu anapaswa kuwa hivi.

Sisi tuko tayari kujadili Qadhia ya Mut'a kwa ukamilifu, lakini kwa sharti:

Hatutaki matukano wala kejeli. Tuzungumze kielimu.

Kwa hivyo sisi tunaonyesha:-

Mut'a ilikuwako wakati wa Mtume, Mtume S.A.W. hakuiondoa mpaka amekufa. Kwa hivyo ndoa hii si haramu, ni halali mpaka siku ya mwisho.

Kuthibitisha hayo, kutalazimu kuvunja hoja za Sheikh Muhammad Sharif, na kutoa dalili za kuthibitisha kuwa iko, kutokana na vitabu vinavyokubaliwa na Sunni wote.

Mwenyeezi Mngu atupe TAWFIQ, Ee Mola! Tuonyeshe Haki tuifahamu kuwa ni Haki uturuzuku kuifuata. Na tuonyeshe batili tuifahamu kuwa ni batili uturuzuku kuiepuka.

OMAR JUMAA MAYUNGA

24/1/1410

24/10/1989