rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

NAMNA YA KUMWOSHA MAITI

Baada ya kusafishwa mwili wote wa yule maiti hapo (yule mwoshaji) atanuia kuwa, namwosha (huyu maiti) ghusli ya kwanza kwa maji yaliyochanganyishwa na majani ya mkunazi kama tulivyoeleza huko nyuma.

(a) Kwanza ataanzia kwa kummwagia maji kichwani (maji yafike hadi utosini kwenye ngozi) masikio, pua, mdomo, macho na shingo pia aoshe. Ahakikishe kilmara anapomwosha, maji yafike sehemu zote za mwili wake.

(b) Tena upande wa mbele wa kulia kutoka begani chini ya shingo na pote kulia hadi kwenye nyayo tena baadaye amlaze ubavu amwoshe sehemu ya nyuma kama alivyomwosha sehemu ya mbele ya kulia.

(c) Baadaye atamwosha upande wa mbele wa kushoto na baadaye upande wa nyuma kama alivyomwosha upande wa kulia.

(d) Utupu wa maiti lazima uoshwe anapokoshwa kila upande (maana yake kwa kila mwosho (ghusli) ataosha utupu mara mbili). Ni haramu kuangalia utupu wa maiti na mwoshaji akiangalia ametenda dhambi, lakini ile ghusli haibatiliki.

(e) Mwoshaji wakati anapoosha utupu wa maiti Iazima aviringe kitambaa au avae mfuko wa kitambaa mkononi, ni haramu kupeleka mkono upekee.

Hii ndio namna ya kumwosha maiti ambayo utaratib huo kwa kisheria unaitwa "ALGHUSL AT-TAR-TIBI" na inambidi kwa kila mwenye Janaba pia akitaka kuondo (kuoga) Janaba au mwanamke mwenye hedhi au nifasi au kuoga ghusli za sunna lazima waoge vivyo hivyo kama tulivyoeleza katika kitabu chetu cha Sala (mlango wa ukurasa wa 33).

Kwa kuoshwa ghusli tatu hizo, tena haina haja kumwogesha, ghusli ya janaba au hedhi au nifas ikiwa maiti alikuwa katika hali ile.

Ikiwa SIDRI (majani ya mkunazi) au KAA-FUR (Kafuri maiti) zote mbili au mojawapo haipatikani, basi maiti ataoshwa kwa maji haya ya kawaida kwa nia ya badala ya Sidri au Kafuri mradi lazima maiti aoshwe Ghusli tatu tu (mara tatu).

(a) Ikiwa maji hayapatikani au maiti ameungua au alikuwa na maradhi fulani na akitiwa maji nyama au ngozi itatoka, basi badala ya maji atafanyiwa Tayamamu mara tatu kwa Ghusli tatu.

(b) Tayamamu ni lazima ifanywe na yule hai, na kumpaka maiti, na kama inamkinika kutayamamu kwa mikono ya maiti pia ifanywe - (Namna ya Tayamamu angalia kitabu chetu cha 'Sala' ukurasa wa 44 Mlango wa 8).