rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

UTARATIBU WA KUMWOSHA MAlTI

(a) Baada ya kusafishwa mwili wake wote kwa sabuni (au kitu kingine) na kuondoshwa uchafu wa aina yo yote kama (madawa, marhamu au mafuta) ndipo huyo mwoshaji Mwislamu atamwosha ghusli tatu (mara tatu kuoshwa). Ni sunna kabla ya kuanza kumwogesha maiti ghusli tatu, atamwosha mikono yake mara tatu, kwa kila ghusli.

(b) Kwa mara ya kwanza, atachanganya katika maji ya kumwoshea maiti kidogo SIDRI (majani ya mkunazi) kwa kutia katika pipa la maji anachochotea maji ya kumwoshea huyo maiti (atayafikicha yale majani yapate kutoa harufu), wala asitie majani mengi hata maji yawe mudhafu. Baada ya kumaliza ghusli ya kwanza atakisuza kile chombo (pipa) kuondoa harufu ya Sidri.

(c) Na kwa mara ya pili atamwosha kwa maji yaliyochanganishwa na 'Kaafuri' (Karafu maiti) kidogo tu, wala asitie nyingi hata maji yakawa mudhafu. Tena atasuza pipa baada ya kumaliza ghusli ya pili ili kuondoa harufu ya Kaafuri.

(d) Na kwa mara ya tatu atamwosha (ghusli) kwa maji haya ya kawaida yaliyo safi bila ya kuchanganywa na cho chote, na hii ndio mara ya mwisho. Ni sunna mwoshaji katika muda anapomwosha maiti awe anasoma, "AFWAN AFWAN".

HADHARI: Taratibu zote za kuosha ni lazima zifuatwe na kama si hivyo GHUSLI ya maiti hubatilika na ni lazima uanze upya kwa utaratibu ule ule tuliyoueleza.

Kwa hivyo huyo maiti wa Ki-Islamu baada ya kuoshwa ghusli tatu hizo kama tulivyoeleza, sasa atakuwa ametaharika, Mwislamu yo yote akimgusa wakati huu, hakuna haja ya kuoga kwa yule mwenye kumgusa, lakini ikiwa baada ya kutoka roho na kupoa mwili, na kabla hajapewa (maiti) hizo ghusli tatu, akimgusa tu kwa mwili (si juu ya nguo) basi kwa kila mwenye kumgusa ni fardhi juu yake aoge "ghusli massul Mayyit", (ghusli ya kumgusa maiti). Na ghusli (kuoga) hiyo ni faradhi kwa mujibu wa Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.) tu.