rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

HUKUMU ZA KUMWOSHA MAITI

Ni fardhi juu ya kila Mwislamu kumwosha maiti huyo, na kutengeneza mazishi yake yote, lakini wakishajitokeza watu kumshughulikia huyo maiti basi kwa wengine fardhi hiyo huondoka.

  1. Ni haramu mwanamke kuoshwa na mwanamume, au mwanamume kuoshwa na mwanamke, lakini mke ana weza kumwosha mume hata kama wapo wanaume, na mume anaweza kumwosha mke hata ikiwa wapo wanawake wa kumwosha.
  2. Mwanamume anaweza kumwosha mtoto wa kike asiyezidi miaka mitatu, na pia mwanamke anaruhusiwa kumwosha mtoto wa kiume asiyezidi miaka mitatu.
  3. Ikiwa hakuna mwanamume wa kumwosha mwanamume, wanawake walio karibu naye kwa ujamaa na damu wanaweza kumwosha, kama mama, dada, shangazi, mama mdogo (dada wa mama yake). Vivyo hivyo ikiwa maiti mwanamke na hakuna mwanamke wa kumwosha huyo maiti, basi majamaa waliokaribu naye kwa ujamaa na damu wanaweza kumwosha kama baba, ndugu, na mtoto wake na wale ambawo ni haramu kumuoa, kwa kisheria wanaitwa "MAH-RAM".
  4. Mtoto aliyezaliwa kwa kuharibika mimba, ikiwa mimba iko chini ya miezi minne (bado hakukamilishwa umbo lake) huyu hana haja ya kuogeshwa (kumuosha GHUSLI), ni lazima aviringishwe katika kitambaa na akazikwe. Lakini mimba ya miezi minne au zaidi (aliyekamilika umbo lake), lazima aogeshwe na kuvikwa sanda kama desturi.
  5. Mwenye kumwosha maiti lazima awe mwislamu, tena Shia, na awe amebalehe, mwenye akili, na ajue namna ya kumwosha maiti.
  6. Ni fardhi kumwosha Mwislamu hata akiwa wa madhehebu nyingine, lakini utamwosha kwa mujibu ya Madhehebu ya Shia lthnaasharia tu.
  7. Mwosha maiti anapomwosha maiti anuwie kama ninafanya kazi hii Qurbatan llal-Laahi Taala, na vitu vyote avitumiavyo kwa kumwosha maiti viwe vya halali, si vya kunyang'anya au kuiba hata maji na mahala atumiapo wakati wa kumwosha maiti pawe pa halali.