rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

KUHUSU MAMBO YA MAITI

Mwenyezi Mungu katika Qur'ani Tukufu, sura ya 'TABARAKA' Aya ya kwanza na ya pili, Amesema hivi "Ametukuka yule Ambaye Mkononi mwake umo ufalme wote; naye ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu. Ambaye Aliumba kifo na uzima ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye Msamaha. (67:1 na 2).

Kwa kuwa mauti ni haki na lazima, na aendapo huko binadamu atayakuta aliyoyachuma mazuri au mabaya, na kila nafsi ni rehani kwa aliyoyachuma, basi ayatende yale ya kumridhisha Mola kwa kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu, Mtukufu Mtume [s] nauwongozi wa Ahlul Bait [a] watakatifu. Tusiwe miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu Ameeleza katika Qur'ani habari zao. "Ni kipi kilichowapelekeni Motoni? Watasema: Hatukuwa miongoni mwa waliokuwa wakisali, wala hatukukuwa tukilisha Maskini na tulikuwa tukipiga porojo na kuzama katika maasi pamoja na waliokuwa wakizama, na tulikuwa tukikadhibisha Siku ya hukumu (Siku ya Qiyama) Mpaka mauti yakatufika". (74:42 hadi 47) Mwenyezi Mungu Atubarikie "Husnul Khatimah" (Amin).

Kwa vile mauti ni lazima kwa kila kiumbe kilicho hai, kwahiyo imekuwa ni lazima kwa kila kiumbe kufariki na kuacha dunia. Basi ni lazima kwa kila Mwislamu anapoona alama za mauti ausie (afanye wasia) kuhusu mali kama anayo, kuhusu madeni, amana za watu, saumu, Hija (kama hakuhiji na hali ilikuwa fardhi kwake kuhiji) na Sala kama ameacha hakuweza kukidhi. Ni Sunna mtu kuandika wasia wake na akaweka chini ya mito yake.