rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

NAMNA YA KUZIKA

(1) Ni faradhi kaburi lichimbwe kiasi cha kumfunika huyo maiti asiweze kufukuliwa na wanyama na isiweze kusikilizana harufu yake atakapoharibika.

(2) Ni sunna kuchimba kiasi cha urefu wa binaadamu au uchimbe hadi shingoni.

(3) Alazwe katika ubavu wa kulia iwe sehemu yake yote yote ya uso, kifua, tumbo na miguu (mwili wake mzima umeelekea Qibla).

Na ya Sunna ni haya:

(a) Ardhi ikiwa ngumu inayoweza kujishika, ni lazima ukeketwe ukuta wa Qiblani kiasi cha urefu wake na kwa upana kiasi cha kuweza kukaa huyo maiti, ni lazima aIazwe kwa ubavu wa kulia, hapo kwenye mkeketo huo, unaitwa mwanandani. Na ubao au kitu kingine uwe mgongoni mwake.

(b) Ama ikiwa ardhi laini kama hivi hapa kwetu pwani, na mahala pengine, mwanandani hachimbwi kwenye ukuta; unachimbwa chini upande wa Qibla, achimbwe kiasi cha kuweza kukaa mtu na ubao unamfunika juu: hau mfuniki mgongoni.

(c) Awekewe mawe nyuma ili asipate kupinduka na kulala chali. Ikiwa mtu ametumbukia kisimani na akafa na haikumkinika kumtoa humo, yule maiti basi kizibwe hicho kisima na litakuwa ndilo kaburi lake.

(d) Ni bora wateremke watu wasio jamaa lakini akiwa maiti mwanamke si halali kushuka humo asiyekuwa Mahram (jamaa wa karibu).

(e) Jeneza liwekwe upande utakaokuwa miguu ya maiti anapolazwa kaburini kwani hapo ni mlango wa kaburi.

(f) Jeneza liwekwe kidogo mbali na kaburi kiasi cha mikono miwili au mitatu (3), baadaye iondolewe na ku wekwa mara tatu mpaka kufika kwenye kaburi.

(g) Ni sunna wenye kushuka katika kaburi wawe na (Tahaara) wudhuu, kichwa wazi, miguu wazi na waka wa kutoka watoke upande wa mguu wa maiti.

(h) Atolewe maiti jenezani kwa kichwani, na kuteremshwa kaburini kwa upole bila haraka.

(i) Ikiwa maiti ni mwanamke, jeneza liwekwe upande wa Qibla na maiti atolewe kwa upana, na tangu wakati wa kutolewa maiti (mwanamke) mpaka kwisha funika mwana ndani, kaburi liwe limefunikwa nguo.

(j) Kuna dua wakati wa kuteremsha maiti na kama hawajui basi wataje dhikri yoyote ya Mwenyezi Mungu. Wakati wa kumtoa maiti humo jenezani na kumlaza kaburini ni sunna kusoma hao wanaomtoana kumlaza dua ifuatayo:

BISMILLAHI WA BIL-LAAHI WA 'ALA MILLATI RASULILLAH. ALLAHUMMA ILAA RAHMATIKA LAA ILA 'ADHABIKA. ALLAHUMMA IFTAH LAHU FI QABRIHI WA LAQINHU HUJJATAHU WA THABIT-HU AL-QAWL ATH-THAABIT WA QINA WA IYYAHU 'ADHABAL QABR.

Na wanapoliona kaburi waseme:

ALLAHUMAJ-ALHU RAWDATAN MIN RIYADIL JANNAH WA LA TAJ-ALHU HUFRATAN MIN HUFURIN-NAAR

(k) Afunguliwe vile vitanzi, halafu iregezwe regezwe ile sanda, na kusogeza sanda kwenye shavu la kulia mpaka lilalie mchanga, itakuwa vizuri kama akitengenezewa mto wa mchanga kwenye kichwa chake.