rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

MAANA YA 'SAUMU'

Neno 'Saumu' ki lugha ya Kiarabu lina maana ya kujizuia. Pia ni neno ambalo lilitumika kabla ya zama za Uislamu. Baadaye Uislamu ulipokuja ukalijaalia neno hili kuwa ni moja kati ya maneno yatumikayo kiibada.

Ama maana ya neno hili Kisheria, ni kujizuia kutokana na mambo yanayobatilisha Saumu yaitwayo 'al-Muftiraat'.

Kinyume cha watu wengi wanavyodhani kwamba Saumu hasa ni kujizuia kula na kunywa tu. La Hasha! Bali Saumu ni kukihifadhi kila kiungo chako kutokana na mambo yasiyotakikana.

Amesema Imam Ja'far Assadiq, "Kufunga siko kujilinda na kula na kunywa tu, bali utakapofunga hifadhi (chunga) macho yako, ulimi wako, tumbo lako, masikio yako na uchi wako. Vile vile ilinde mikono yako, pendelea sana kunyamaza ila katika heri (tu kama kusoma Qur'ani n.k.) na umhurumie mtumishi wako."

Naye Mtume (s.a.w.) amesema: "Mambo matano hutengua Saumu ya mtu: Uongo, kuseng'enya, kufitinisha, kula viapo vya uongo na (mwanamke) ku mkazia macho mwanamume asiye maharimu wake au (mwanamume) kumkazia macho mwanamke asiye maharimu wake kimatamanio.

Kuseng'enya kumekatazwa katika kauli hii ya Mtume (s.a.w.) na badala yake tunahimizwa na hadithi nyingi tujiepushe na lolote la kutuharibia Saumu zetu.

Mtume (s.a.w.) anasema: "Mwenye kufunga huwa ibadani wakati wowote hata kama analala madamu hajaitengua Saumu yake kwa usengenya. Kwa hapa utaona kwamba, kule kutokula na mfano wake kama tulivyo yabaini hapo mbeleni siko kufunga hasa kunakotakikana, bali kufunga ni kujizuia na makatazo yote na mabaya.

NYAMA MDOMONI

Siku moja Mtume (s.a.w.) alimsikia mwanamke mmoja akisengenya na hali amefunga. Mtume (s.a.w.) akamwitishia chakula ili ale, yule mwanamke akasema: "Mimi nimefunga". Mtume akaendelea kuhimiza chakula iletwe mara moja ili yule bibi ale naye, yule bibi azidi kukariri kuwa angali anafunga. Hapo Mtume akamwambia: "Unafungaje na hali menoni mwako mna kipande cha nyama? Yule mwanamke akazidi kubishana na huku Mtume amwambia "Hebu tia mkono wako kinywani mwako" na kweli alipouingiza mkono wake menoni, alitoa kipande cha nyama. Hapo Mtume (s.a.w.) akamwambia "Waona? Wataka kula nyama ya nduguyo aliyekufa? Yaani kusengenya ni sawa na kula nyama ya mfu tena nduguyo.

Hapo waona ndugu? Kwa hakika kile kipande cha nyama mdomoni mwa yule bibi kilipatikana kwa kule kusengenya, na yeyote asengenyaye huwa Saumu yake si sawa na huwa amekula nyama ya mfu tena nduguye.

PIA KUTUKANANA

Siku moja Mtume (s.a.w.) alimsikia mwanamke mmoja akimtusi msichana wake - mfanya kazi - na yule bibi alikuwa amefunga, Mtume,(s.a.w.) akaitisha maji ampe yule bibi afuturu (na ilikuwa ungali mchana). Yule bibi akasema "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika mimi nimefunga" Mtume (s.a.w.) akajibu, "Unawezaje kuzitusi mtu au kuteta naye na hali umefunga? Wewe tayari Saumu yako ni batili, yaani si makbuli.

Viungo vyako ni hadiya ya Mwenyezi Mungu kwako, kwa hivyo haifai kuvifaniya hiana.

Katika masiku haya ya Saumu, na mengine pia ambayo ni heshima kuu na utukufu kwa Waislamu, ni lazima kujilinda.

MIGUU: Isielekee kulikokatazwa ambako kunajulikana kama Makadara, kwenda disco, kwenda sinema na kadhalika, na badali yake ni muhimu lau tutakwenda misikitini, kutembeleana kwa heri kama alivyotuhimiza Mola wetu kwa kutuambia: "Saidianeni katika mema na kwa kumcha Mwenyezi Mungu, lakini msisaidiane katika kumwasi Mola na kufanyiana uadui. Na kujilinda huku kuendelee hata baada ya Ramadhani.

MIKONO: Izuie kuwadhuru watu kwa kuwaibia, kuua, kupiga na kadhalika, na badala yake ishikishe Qur'ani, iamkize jamaa na kadhalika.

MACHO: Usiyatizamishe ulichokatazwa. Kuwaangalia watu wasio wa maharimu yako, kutamani kisicho chako na kadhalika bali fungua Msahafu usome.

MASIKIO: Usisikilize upuzi uliokatazwa kama nyimbo, kusengenya, udaku n.k.badala yake nenda ukasikilize mawaidha na kama hayo ambayo ndani yake mna radhi ya Allah.