rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

BAADA YA KILA SALA

Dua hizi mbili husomwa baada ya kila sala ya Fardhi, na ni vyema sana kuzihifadhi ili kuzisoma kila wakati na kila mahali katika mwezi wote wa Ramadhani.

Ama hiyo dua ya pili, inafaa kuiendeleza, yaani kuisoma masiku yote hata yasiyo ya Ramadhani.

"Ee Mwenyezi Mungu Mtukufu! Msameheve, Mrehemevu, Wewe tu ndiwe Mola Mlezi Asiyefanana na chochote Aonaye Asikiyaye. Huu ni mwezi ambao Umeuadhimisha, Ukautukuza, Ukaupa hesima ya Ukaufadhilisha kuliko miezi yote. Na ndio mwezi ambao Umenifaradhia kuufunga, nao ni mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa mwongozo wa watu, na ishara ziliso wazi za mwongozo na kipambanuzi. Na ukaujaalia usiku wa Laylatul Qadri kuwa katika mwezi huu na Ukaujaalia usiku huo (wa Laylatul Qadri) kuwa bora kuliko miezi elfu. Ewe Mwenye Kuneemesha Asiyeneemeshwa nineemeshe kwa kuniachilia huru kutoka katika adhabu ya moto pamoja na Utakaowaachilia, na Uniingize peponi wa rehema zako Ewe Mrehemevu wa Wanaorehemu.

Ee Mwenyezi Mungu! Waingizie furaha waliomo makaburini (yaani wafurahishe). Ee Mwenyezi Mungu! Mtajirishe kila aliye maskini. Ee Mwenyezi Mungu! Mshibishe kila aliye na njaa. Ee Mwenyezi Mungu! Mviahe kila aliye uchi. Ee Mwenyezi Mungu! Mkidhie deni kila mdaiwae. Ee Mwenyezi Mungu! Mfariji kila aliye na dhiki. Ee Mwenyezi Mungu! Mrudishe (uwenyejini salama usalimini) kila aliye ugenini. Ee Mwenyezi Mungu! Mwachilie huru kila mateka. Ee Mwenyezi Mungu! Yasuluhishe yote yaliyo kombo miongoni mwa mambo ya Waislamu. Ee Mwenyezi Mungu! Mponye kila mgonjwa. Ee Mola wetu! Ibadilishe hali yetu mbovu kwa hali yako njema. Ee Mola wetu! Tukidhie madeni (yetu) na Ututajirishe tuondoke umaskinini kwani hakika Wewe ndiwe Mweza juu ya kila kitu.