rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

KWA AKINA DADA

Dada wapendwa wa Kiislamu, mwezi mtukufu wa Ramadhani hutujia mara moja tu kwa mwaka. Tunapokaribia kuumaliza mwezi wa Shabani, huwa na furaha tele nyoyoni mwetu ya kuukaribisha mwezi wa Ramadhani. Na kwa wakati huu hatunalo ila kumshukuru Mwumba wetu aliyetuongoza kwenye njia yake nyofu (ya Kusilimu), maana lau si Yeye kamwe hatungeongoka.

Dada wapendwa, tunapaswa kukumbuka kwamba, kufunga siyo kutozingatia kula na kunywa tu na hatimaye kutayarisha futari, bali kufunga kunakotakikana ni kuzingatia maamrisho yake Sub'haanuhu Wataala na Mtumewe (s.a.w.).

Miongoni mwa maamrisho yake kwetu ni kuwatii waume zetu kwani Mwenyezi Mungu Hako tayari kuzipokea Saumu zetu tukiwa na ufidhuli kwa waume zetu kwani Mola wetu Anatuambia katika Qur'aan: "Waume ndio wasimamizi wa wanawake."

Naye Mtume (s.a.w.) anasema kutufunza namna ya kutunza nyumba zetu kwamba "Mwanamke aki funga Saumu yake ya wajibu, asali sala zake fardhi na amtii mumewe, bila shaka ataingia peponi."

Huo ndio wajibu wetu. Ama mtindo wa kuwasengenya wenzetu, majirani zetu, waume zetu, au waume wa wenzetu ni kinyume cha dini ya Islam, na wakati wowote ule haitakikani kuendesha mikutano ya namna hii, na hasa katika Ramadhani, maana yanaweza kukuharibia Saumu yako.

Pia kujifahiri kubughudhiana, kukaripiana, kunyimana vifaa vya nyumbani kama shoka, chumvi, mwiko n.k. na kujiunga katika makundi ya karata hasa na waume ni dhambi isiyosameheka ila kwa kutubia hasa wakati kama huu wa Ramadhani.