rudi maktaba > Fiqh > Yaliyomo >

NASAHA KWA VIJANA

Vijana wa Kiislamu! Mwezi wa Ramadhani umetuwadia, hatuna wakati mwengine tuutarajiao tena na kuutumaini katika kufuzu kwetu usio huu. Balaa zote za kutuletea maafa hapo kesho (Akhera) tuziepuke na tuwe mbali kabisa nazo.

Katika mwezi huu hakuna masingizio yoyote, ambayo tunaweza kujisingizia nayo kama vile kudai kwamba 'O'..... Shetani ametushika sana! Kwani Mtume (s.a.w.) Ametudokezea kwamba, "Mwezi wa Ramadhani unapoingia, milango yote ya rehema huwa wazi (kuwapokea wanaotaka kuingia) milango yote ya Jahannam hufungwa na Mashetani wote hutiwa minyororo ili wasiwahangaishe."

Ajabu kubwa zaidi ni kijana wa Kiislamu kuvaa ushanga, mikufu na bangili namna wafanyavyo wanawake. Ni hadi lini watajisitahi na kuwa na haya juu ya haya wayafanyayo?

Ni aibu kubwa kwa vijana wa Kiislamu kuhalifu sheria za dini yao hasa katika mwezi huu. Kwa kila alye na uchunguzi, atastaajabu sana kumwona mtu aliyekuwa mnyenyekevu mchana kutwa, msalihina, kubadili hali hiyo na kuufanya usiku kuwa sitara ili kumdumishia maasi yake.

Ikiwa hawatajinasihi katika muda huu wa rehma na maghfira wakumbuke kuwa wamo hatarini ya kupoteza imani.

Badala ya kuketi mabarazani kusengenyana na kufitiniana, tunahimizwa kuingia misikitini na kuendesha ibada mbali mbali na tukisome kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa wingi yaani Qur'ani. Kwani pasi na kufanya hivyo, tutakuwa tunaupoteza wakati wetu ambao ni wa thamani sana kama ilivyopokelewa katika kauli za wahenga wa kiarabu kwamba: 'Wakati ni kama upanga, usipouvunja, (mwishowe) utakukata.'