Tayammum ni kutawadha kwa kutumia mchanga au udongo kutokana na udhuru wa kisheria kama kukosa maji au ugonjwa. Na tayammum huwa badala ya udhu au ghusli na ni wajibu pindi maji yanapo kosekana maji ya kutawadhia, au kama kukiwa na udhuru wa kutumia maji kama kuwa na ogonjwa au kutokana na baridi au kuogopa kuyatumia maji kwa sababu ya kuyahitaji kwa kunywa au kutokuwepo nyenzo ya kutowezesha kuyafikia maji hayo. Na haifai kutumia kitu chochote katika tayammam tafauti na mchanga halisi au udongo.
Kwa ujumla ni nyudhuru ambazo huangusha wajibu wa kutumia maji, na
nyudhuru hizo ni
KWANZA: Kuto patikana maji yatoshayo kutawadhia au kuoga, hata kama yatakayo patikana hayata kuwa na sifa zizingatiwazo katika suala la maji.
MAS’ALA: Haijuzu kwa msafiri kufanya tayammam pale tu atakapo tambua ya kuwa hakuna maji, bali hapana budi kuthibitisha kuto kuwepo kwa maji kwa kuyatafuta, na ikiwa atakuwa na ihtimali juu ya kuwepo maji kati ya watu wale anao safiri nao au katika msafa wake au kwa baadhi ya wapita njia, itakuwa ni wajibu kwake kuyatafuta hadi awe na yakini au uhakika wa kuto kuwepo kwa maji, lakini ikiwa atafahamu ya kuwa maji hayapatikani kabla ya kutafuta na akawa na matarajio ya kupatikana maji hayo, haitawajibika kwake kuyatafuta, na ikiwa atakuwa jangwani na akawa na ihtimali ya kupatikana maji sehemu iliyo karibu nae au njiani, itakuwa ni wajibu kwake kuyatafuta, na kauli iliyo ahwat na ya wajibu ni kuwa inabidi maji hayo ayatafute pande nne.
Sehemu za milimani atatupa mtupo mmoja wa mshale, na sehemu ya tambalale atatumia mitupo miwili ya mishale, na ikiwa anayo ihtimali ya kuto kuwepo maji sehemu hizo, si wajibu kwake kuyatafuta sehemu hizo, na ikiwa atakuwa na ihtimali kati ya sehemu moja wapo kati ya hizo itamuwajibikia kuyatafuta sehemu hiyo, na kuwepo dalili au uthibitisho ni sawa na kuwa na yakini juu ya kuwepo kwake, na ikiwa atashuhudia kutokuwepo maji katika pande fulani haita muwajibikia kuyatafuta sehemu hizo.
MAS’ALA: Ikiwa atayatafuta maji kabla ya kuingia wakati wa sala na hakuweza kuyapata, haitamlazimu kuyatafuta tena baada ya kuingia wakati wa sala, hata kama atakuwa na ihtimali ya kupatikana kwa maji hayo, na ikiwa hakuya tafuta katika baadhi ya sehemu kutokana na kuwa na yakini ya kutokuwepo maji sehemu hiyo, kisha akawa na shaka ya kuwa kuna maji au hakuna, hapana budi kwake kukamilisha utafutaji, vile vile ikiwa atahama kutoka sehmu hiyo itamlazimu kukamilisha utafutaji wake huo.
MAS’ALA: Ikiwa atayatafuta maji kwa ajili ya sala fulani, utafutaji huo utatosheleza kwa ajili ya sala zinginezo, na si wajibu kwake kutafuta tena kila ufikapo wakati wa sala hizo, hata kama atakuwa na matarajio ya kupatikana maji ikiwa atatafuta tena, kwa matarajio ya kuyapata maji hayo.
MAS’ALA: Ulazima wa kutafuta maji huporomoka pindi wakati wa sala unapo kuwa finyu kwa kiasi cha kuweza kusali sala ile, pia huporomoka ikiwa ataogopa kupatwa na madhara juu ya nafsi yake au mali yake kutokana na wezi au wanyama wakali au mfano wa hayo, au akiwa na ihtimali ya kutokea madhara asiyo weza kuyastahamilia.
MAS’ALA: Ikiwa ata acha kutafuta maji na badala yake akafanya tayammam na kusali katika wakati mrefu, kwa kutaraji kuwa ametekeleza sheria, tayammam yake na sala yake vitakuwa na ish’kali katika kusihi kwake, hata kama itabainika kuto kuwepo kwa maji.
MAS’ALA: Ikiwa atakuwa na maji na akasahau au akaghafilika ya kuwa alikuwa na maji, na akafanya tayammam na kusali kisha akakumbuka ya kuwa anayo maji kabla ya kumalizika wakati wa sala hiyo, ni juu yake wakati huo kutawadha na kuirudia sala hiyo.
MAS’ALA: Ikiwa atayatafuta maji na hakuweza kuyapata na kukata tamaa ya kupata maji katika wakati wa sala na akafanya tayammam na kusali, kisha ikabainika ya kuwa kuna maji sehemu hiyo aliyo tafutia kwa mtupo mmoja au miwili au katika msafara au kati ya wale alionao safarini, sala yake aliyo Sali ni sahihi na si wajibu kwake kuirudia au kuilipa sala hiyo.
PILI: kuto kuwepo urahisi wa kuyafikia maji yaliyopo, ima kwa kushindwa kuyafikia kutokana na maumbile kama kuwa na umri mkubwa na mfano wa hayo, au kuyafikia kwake kutamlazimu kufanya tendo la haramu kama kutumia chombo cha ghasbi (kilicho nyang’anywa), au kwa kuiogopea nafsi yake au heshima yake au mali yake kutokana na wezi au kupotea na mengineyo.
TATU: Kupatikana madhara kwa kutumia maji, kama kuwa na baridi kali, sawa baridi hiyo iwe ni yenye kuleta madhara au kuzidisha maradhi au yakiwa ni sababu ya kuchelewa kupona, pia kuwa na vipele vinavyo zuwia kutumia maji ikiwa havikusitiriwa, ama ikiwa vime sitiriwa kwa dawa, hapo jukumu litakuwa ni kufanya udhu wa jabira (pio pio) kama tulivyo tangulia kueleza katika udhu, pia ikiwa kuna mikwaruzo ambayo haiwezekani kuivumilia ikiwa itamwagiwa maji (yaani ikiwa atakuwa na ugonjwa wa ukoma) nao ni ugonjwa ambao hupelekea baadhi ya sehemu za ngozi kuchanika chanika, wakati huo si lazima kuwa na yakini au matumaini juu ya kupatikana madhara kwa kutumia maji, bali inatosha kuwa na ihtimali itumikayo kwa watu wenye akili, na ambayo huitwa kwa jina la khofu (woga).
NNE: Taabu na matatizo ambayo ni vigumu kuyastahamili, sawa iwe ni katika kuyafikia maji au kuyanunua kwa thamani ambayo itasababisha madhara katika mali yake, la sivyo itamlazimu kuyanunua hata kama ni kwa kiwango cha juu, au kukawa na madhara katika kuyatumia maji hayo kutokana na baridi kali au kubadilika kwa maji kwa kiwango ambacho kina pingana na maumbile yake, au ikiwa yatasababisha madhara kwa kuyatumia kwake, kama ikiwa anayo maji kidogo ambayo hayatoshi kuweza kutawadhia au kuoga au kuloweshea kichwa kutokana na kuyahitaji wakati wa joto kali, kiasi kwamba akiyakosa maji hayo atajiweka katika taabu kubwa.
TANO: Kukhofia kiu juu yake mwenyewe au mwenziwe kwa wale wenye mahusiano nae na ambao ni wajibu wake kuwalinda na kuwahifadhi na kuyashughulikia mambo yao, hata kama si nafsi zenye kuheshimika sawa awe mwanadamu au mnyama. Na ikiwa ataogopa kiu kwa watu wengine ambao hawahusiani nae au mambo yao haya muhusu, lakini kisheria analazimika kumuhifadhi, au ikiwa hakumuhifadhi na kumuangalia itamlazimu mtu yule kupatwa na madhara au matatizo, khofu kama hiyo itaungana na mambo yale mengine tuliyo yataja yawajibishayo tayammam.
SITA: Awe amekalifishwa kufanya wajibu ambao hautimii isipokuwa kwa kutumia maji, kama kuondoa khabathi msikitini. Hakika ni wajibu kwake kutayammam na kuyatumia maji katika kutwahirisha msikiti, hivyo hivyo ikiwa mwili wake au nguo zake zitakuwa zime najisika, na maji yaliyopo hayatoshelezi kutwahirisha hadathi na khabahi kwa pamoja, wakati huo itamlazimu kuyatumia maji hayo kwa kuondoa au kutwahirisha khabathi, japo kuwa ni bora zaidi katika sehemu hiyo kwanza kuyatumia maji kwa kuondoa khabthi kisha baada ya hapo kutayammam.
SABA: Ufinyu wa wakati katika kuyafikia maji au kuyatumia , kiasi kwamba ikiwa atatawadha au kuoga itamlazimu kuisali sala ile au baadhi ya sehemu ya sala hiyo nje ya wakati, wakati huo itafaa kutayammam katika sehemu zote zilizo tajwa.
MAS’ALA: Ikiwa itawajibika kufanya tayammam kutokana na kukosekana baadhi ya masharti ya kutawadha au kuoga, na akatawadha au kuoga kwa kusahau au kwa kughafilika au kwa kuto jua, udhu au ghusli hiyo haito swihi.
Kauli yenye nguvu inasema kuwa inajuzu kutayammam kwa kila kitu kiitwacho kwa jina la Ardhi, sawa uwe mchanga, udongo, changalawe, au mawe, pia matofali na ardhi ya chokaa kabla ya kuchomwa, japo kuwa kauli iliyo ahwat na ya sunna inasema ni bora kutumia udongo tu ikiwa itawezekana, pia kauli iliyo ahwat kama si yenye nguvu zaidi inasema kuwa kitu kitumikacho kutayammam kiwe ni chenye kugandia juu ya mikono, haitoshi kutayammam juu ya kitu kama jiwe mororo lisilo na vumbi juu yake.
MAS’ALA: Haijuzu kutayammam kwa kutumia kitu kisicho faa kuitwa Ardhi, hata kama asili yake ni ardhini, kama majivu, mimea, na baadhi ya madini kama Dhahabu na Fedha, ama jiwe la akiki na Fairuzi na mfano wa hayo kati ya mawe matukufu, kauli yenye nguvu inasema ya kuwa inajuzu kutayammam kwa kutumia vitu hivyo pamoja na kuthibiti ugandiaji, vile vile vyombo vya dongo, chokaa, na matofali baada ya kuyachoma, japo kuwa kauli yenye nguvu inasema kuwa ni bora kuvitanguliza vitu vingine juu ya vitu hivi.
MAS’ALA: Haijuzu kutayammam kwa kitu kilicho najisi, wala kilicho cha ghasbi (kilicho nyang’anywa au kutumika bila ruhusa ya mmiliki wake), wala kilicho changanywa na kitu kingine kiasi kwamba halithibiti juu ya kitu hicho jina la Ardhi, ndio, haitadhuru ikiwa kitu kilicho changanywa hakidhihiri katika udongo au mchanga huo kwa kawaida, na ikiwa mtu atalazimishwa kukaa kwa muda mrefu katika sehemu aliyo nyang’anywa au kudhulumiwa, kauli iliyo wazi inasema kuwa inajuzu kutayammam kwenye ardhi hiyo aliyopo, lakini atatosheka tu na kuweka mikono na wala asipige juu ya Ardhi kwa mikono yake.
MAS’ALA: Ikiwa kutakuwa na shubha kati ya udongo ulio maghsub na ulio halali itawajibika kuto tumia aina zote mbili hizo, na ikiwa kutakuwa na shubha kati ya majivu na mchanga na akatayammam kwa kutumia vitu viwili hivyo tayammam yake itakuwa sahihi, bali ni wajibu kufanya hivyo ikiwa hakuna kitu kingine cha kutumia, na hukumu ni hiyo hiyo ikiwa kutapatikana shubha kati ya mchanga twahara na najisi.
MAS’ALA: Vumbi lililo kusanyika juu ya nguo au mfano wa nguo ikiwa litahesabika kuwa ni mchanga kiasi kwamba ukawa kama mchanga katika mazowea ya watu, itajuzu kutayammam kwa kutumia vumbi hilo kutokana na kauli iliyo wazi, japokuwa kauli iliyo ahwat inasema ni bora kutumia kitu kinginecho tofauti na vumbi hilo, na ikiwa vumbi ni jingi na lenye kukusanyika juu ya nguo kwa mfano na kukawa na uwezekano wa kulikung’uta na kulikusanya kiasi likionekana itathibitika kuwa ni mchanga itabidi kulitumia vumbi hilo, ikiwa haikuwezekana kutumia kitu kingine.
MAS’ALA: Ikiwa haikuwezekana kutayammam kwa kutumia Ardhi na vitokanavyo na Ardhi kama vumbi, hapo itamlazimu kutayammam kwa udongo, nao ni udongo ulio changanyika na maji mfano wa tope na ambao hugandia juu ya mikono, na haijuzu kuuondoa udongo wote, bali kauli iliyo ahwat inasema kuwa haifai kuondoa kitu kwenye mikono isipo kuwa kile ambacho kukiondoa kwake kutathibitisha kuwa umetumika mkono katika upakaji, na ikiwa itawezekana kuukausha na kuutumia kwa kutayammam itabidi kufanya hivyo, na wakati huo haitajuzu kutayammam kwa udongo. Na ikiwa itashindikana kutumia vitu vilivyo tajwa hapo kabla kutayammam, itabidi kutayammam kwa kutumia kitu chenye vumbi yaani kitu ambacho kina vumbi jingi au chenye mkusanyiko wa vumbi mkusanyiko ambao hukubalika kuwa ni mchanga ulio laini kama tulivyoeleza hapo kabla.
MAS’ALA: Ikiwa atashindwa kuipata Ardhi, vumbi, na udongo au kitu chenye vumbi, hapo atakuwa amekosa twahara, na kauli iliyo adh’har wakati huo ni kuwa sala ita anguka katika wakati wake na itakuwa ni wajibu kuilipa nje ya wakati wake. Na ikiwa mtu ataweza kupata barafu na kaweza kuiyayusha na kuitumi katika udhu, au akaweza kuitumia kupaka uso na mikono kiasi kwamba itathibiti anuani ya kuosha na kupaka kichwa na miguu miwili kwa unyevu nyevu wa mikono itabidi kufanya hivyo na haitafaa kutayammam, ama ikiwa hakuweza kupaka kwa kutumia barafu hiyo kiasi kwamba haitathibiti anuani ya kupaka, kauli iliyo wazi inasema itabidi kutayammam japo kuwa kauli iliyo ahwat na ya sunna inasema, inabidi kukusanya kati ya tayammam na kupaka kwa kutumia barafu hiyo na kuisali sala hiyo ndani ya wakati.
MAS’ALA: kauli iliyo ahwat ni kuwa ni sunna kukung’uta mikono baada ya kupiga juu ya Ardhi, na kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa vitu vitumikavyo kutayammam viwe safi kwa hali ya kawaida, na ni sunna viwe ni katika Ardhi halisi na ziwe ni sehemu za juu, na ni makruhu kuwa ni sehemu ya bondeni, na usiwe ni mchanga wa njiani.
Utaanza kwa kupiga vitanga viwili juu ya Ardhi na inatosha kuweka vitanga hivyo juu yake vile vile- na kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa inabidi kufanya hivyo mara moja-.
Kisha utavitumia vitanga hivyo baada ya kuvipiga juu ya Ardhi vyote kwa pamoja kupaka paji lote la uso kisha pande mbili za uso kulia na kushoto kwa kuanzia kwenye maoteo ya nywele hadi kwenye nyusi na utaendelea hadi kwenye ncha ya juu ya pua iliyo ungana na paji la uso, na kauli iliyo ahwat inasema kuwa ni bora zaidi pia kupaka pande mbili za uso, kisha utapaka sehemu yote ya juu ya kitanga cha mkono wa kulia kwa kuanzia kwenye zand (maungio ya vitanga vya mkono) hadi kwenye ncha za vidole kwa kutumia mkono wa kushoto, kisha utapaka sehemu yote ya juu ya kitanga cha mkono wa kushoto vile vile kwa kutumia kitanga cha mkono wa kulia.
MAS'ALA: Si wajibu kupaka kwa kutumia vitanga vyote vya mikono, bali inatosha kupaka kwa kutumia baadhi ya sehemu ya vitanga hivyo kiasi ambacho kita enea kwenye paji lote la uso na pande mbili za uso pia kama ilivyo tangulia.
MAS’ALA: Kauli iliyo dhahiri (iliyo wazi) ni kuwa, inatosha kupiga mara moja juu ya Ardhi wakati wa kutayammam badala ya ghusli ( kuoga) au kutawadha, japokuwa kauli iliyo ahwat na ya sunna inasema ni bora kupiga mara mbili, pigo la kwanza kwa ajili ya uso, na pigo la pili kwa ajili ya vitanga au mikono miwili, na inatosha katika kufanya ihtiyaat kupaka mikono na uso katika pigo la kwanza, kisha utapiga pigo la pili na uta paka mikono yako, na utafanya hivyo hivyo iwapo utaweka mikono juu ya Ardhi.
MAS’ALA: Ikiwa itashindikana kupiga na kuweka, pia kupaka kwa kutumia sehemu ya ndani ya vitanga vya mikono, utatumia sehemu ya juu ya vitang hivyo, vilevile ikiwa vime tapakawa na najisi sehemu zote hadi kwenye kitu kitumikacho kutayammam, na hukuweza kuiondoa najisi hiyo, ama ikiwa najisi si yenye kutapakaa sehemu zote, utaitumia sehemu ile isiyo na najisi kwa kupiga juu ya Ardhi au kuweka juu yake kisha utapaka kwa kutumia sehemu hiyo, bali kauli iliyo dhahiri ni kuwa si lazima kiungo chenye kupaka na chenye kupakwa viwe twahara. Na ikiwa juu ya kiungo kinacho pakwa kuna kizuwizi kama bandeji au pio pio na hakuna uwezekano wa kulitoa, itamlazimu kupaka juu yake, ama pio pio au bendeji likiwa sehemu ya kupakia, ikiwa halikufunika sehemu yote, utapaka kwa kutumia sehemu iliyo bakia, ama ikiwa hakuna sehemu iliyo wazi kauli ya ahwat na ya wajibu inasema itakuwa ni wajibu kukusanya kati ya kupaka kwa kutumia mkono wenye pio pio na kupaka kwa kutumia sehemu ya juu ya mkono baada ya kupiga juu ya Ardhi au kuweka.
MAS’ALA: Mwenye hadathi ndogoatafanya tayammam badala ya udhu. Na mwenye janaba atafanya tayammam badala ya ghusli ( kuoga), na mwenye hadathi kubwa tofauti na janaba atafanya tayammam badala ya ghusli, na ikiwa atakuwa na hadathi ndogo, kauli ya ahwat na ya sunna inasema, ni sunna pia kutawadha, na ikiwa hakuweza kutawadha atafanya tayammam badala ya udhu, na ikiwa ataweza kuoga itamlazimu kuoga, na ikiwa ataoga haita hitaji kutawadha kwani josho hilo linatosheleza kutawadha, isipokuwa katika istihadha mutawassit (istihadha ya kati) katika hali hiyo itamlazimu kutawadha, na ikiwa hakuweza kutawadha atafanya tayammam badala ya udhu, vilevile ikiwa hakuweza kuoga, kuli iliyo dhahiri ni kuwa atafanya tayammam moja na itakuwa imetosheleza kwa ghusli na udhu.
Ni sharti katika tayammam kutia Nia (kunuwia) kama ilivyo tangulia kwenye udhu, na Nia hiyo inabidi iambatane na tendo la kupiga juu ya Ardhi au kuweka mikono juu ya Ardhi kwa kauli iliyo ahwat.
MAS’ALA: Si wajibu katika tayammam kunuwia badala ya udhu au ghusli, bali inatosha tu kutia Nia ya kujikaribisha kwa Allah, ndio, ikiwa atafanya tayammam mbili, moja badala ya ghusli na nyingine badala ya udhu, kwa ihtiyat ni lazima kuzitofautisha tayammam hizo kwa aina fulani, na inatosha kuzitofautisha kwa kutia Nia ya ubadala.
MAS’ALA: Kauli yenye nguvu ni kuwa tayammam ni yenye kuondoa hadathi ikiwa haikutokea moja wapo kati ya vitu vitenguavyo twahara, na wala si wajibu kutia Nia ya kuondoa hadathi au ya sunna, au kwa ajili ya sala kwa mfano.
MAS’ALA: Ni sharti tayammam ifanywe na mtu mwenyewe bila kusaidiwa na mtu, vile vile ni sharti kufuatanisha, hata katika tayammam ambayo ni badala ya ghusli, vile vile ni sharti kufuatanisha au kufuata mpangilio kama ilivyo tangulia, na kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa, ni lazima katika kupaka kuanzia juu kuelekea chini.
MAS’ALA: Mtu ambae moja wapo kati ya kitanga chake kimekatika au vyote viwili, atafanya tayammam kwa kutumia muundi wa mkono, na mtu ambae moja wapo kati ya mikono yake umekatika kuanzia kiwikoni, atafanya tayammam kwa kutumia mkono ulio bakia, ima kwa kupiga juu ya Ardhi au kwa kuweka juu yake, na atapaka juu ya paji la uso kwa kutumia mkono huo, kisha atapaka juu ya mkono huo kwa kutumia Ardhi, ama alie katika mikono yote miwili kuanzia kwenye viwiko, itatosha kupaka uso wake kwa kutumia Ardhi, na mtu mwenye pio pio au mwenye kizuwizi kwenye mkono wake hukumu yake ime elezwa hapo kabla, na hapa zitatumika hukumu zilizo tangulia zihusianazo na pande la nyama lililo zidi au mkono ulio zidi.
MAS’ALA: Ikiwa hakuweza kufanya tayammam yeye mwenyewe isipokuwa kwa kupata usaidizi kutoka kwa mtu mwingine kiasi kwamba inambidi amsaidie au ashirikiane nae katika kupiga juu ya Ardhi au kuweka mikono juu ya Ardhi au juu ya kitu akitumiacho kutayammam kisha kuiweka juu ya paji la uso na juu ya mikono yake pamoja na kuwa yeye mwenyewe ndie afanyae tendo la kupaka kwa mikono yake, itambidi kufanya hivyo na yeye mwenyewe ndie atakae tia Nia kwa wakati huo, na ikiwa haikuwezekana kufanya tayammam au kupaka yeye mwenyewe hata kama ni kwa kusaidiwa, itambidi amuombe mtu amtayamamishe, na atapiga juu ya Ardhi kwa kutumia mikono ya mgonjwa na kupaka uso kwa kutumia mikono hiyohiyo, na ikiwa itashindikana, itatumika mikono ya yule mwenye kutoa usaidizi yeye mwenyewe na atapaka kwa kutumia mikono yake, na kauli iliyo ahwat katika hali mbili hizo ni kuwa kila mmoja inambidi kuti nia.
MAS’ALA: Nywele zilizo funika au kuangukia usoni ni wajibu kuziinua na kupaka juu ya ngozi iliyo chini ya nywele hizo, ama nywele zilizo ota kwenye uso, kauli iliyo dhahiri ni kuwa itatosha kupaka juu ya nywele hizo.
MAS’ALA: Ikiwa mtu atakhalifu utaratibu pamoja na kuto fatanisha, tayammam itabatilika, hata kama ikiwa ni kutokana na kuto jua au kwa kusahau, ama ikiwa utaratibu na kufuatanisha havi kukosekana baada ya kuirudia, tayammam itakuwa sahihi.
MAS’LA: Pete izuwiayo mchanga kufika kwenye vitanga, ni wajibu kuivua wakati wa kupaka.
MAS’ALA: Ni sharti mchanga utumikao kutayammam uwe mubaha (halali), kama ilivyo elezwa hapo kabla, na kauli iliyo ahwat inasema sehemu na chombo chenye mchanga wa kufanyia tayammam visiwe ni vya ghasbi (kunyang’anya) au vya dhuluma.
MAS’ALA: Ikiwa mtu atatia shaka kati ya sehemu moja wapo za kufanyia tayammam ya kuwa ameifanyia tayammam au la, na shaka hiyo imekuja baada ya kumaliza au kuvuka sehemu hiyo, shaka hiyo hataitilia maanani, ama shaka ikihusika na sehemu ya mwisho na wakati huo hali ya kufuatanisha bado haija toweka na kabla ya kufanya kitendo kingine kama sala na mfano wake, kauli iliyo ahwat na ya wajibu ni kuwa shaka hiyo itatiliwa maanani, na ikiwa atatia shaka kuhusu sehemu Fulani baada ya kuvuka sehemu hiyo na kuingia sehemu nyingine, hapo shaka hiyo haitatiliwa maanani, japo kuwa kauli aliyo ahwat na ya sunna ni kuwa atairudia sehemu hiyo.
Haijuzu kutayammam kwa ajili ya sala ambayo wakati wake umefika ikiwa utafahamu ya kuwa udhuru utatoweka na kuna uwezekano wa kujitwaharisha kwa maji kabla ya kumalizika wakati wake, bali haijuzu kutayammam ikiwa huja kata tamaa ya kukosekana kwa maji au kuondoka kwa udhuru pia, ama ikiwa uta kata tamaa ya kuwa udhuru hauta ondoka, wakati huo hakuta kuwa na tatizo ikiwa utafanya haraka kufanya tayammam, na ikiwa utasali kwa kufanya tayammam, kauli iliyo adhahiri ni kuwa si wajibu kuirudia sala hiyo hata kama udhuru huo utatoweka kabla ya wakati wa sala hiyo kumalizika.
MAS’ALA: Ikiwa mtu atafanya tayammam kwa ajili ya sala ya faradhi au sunna, kutokana na udhuru na akaisali sala hiyo, kisha ukaingia wakati wa sala nyingine, ikiwa hatakuwa na matarajio ya kutoweka kwa udhuru huo na kuweza kujitwaharisha kwa maji, itajuzu kwake kufanya haraka kuisali sala hiyo katika wakati ulio mpana, na si wajibu kwake kuirudia ikiwa udhuru utatoweka baada ya hapo, ama ikiwa kuna matarajio ya kuondoka kwa udhuru, kauli iliyo ahwat ni kuwa ni lazima kuchelewa kufanya hivyo.
MAS’ALA: Ikiwa yatapatikana maji katikati ya sala ya faradhi au ya sunna, ataendelea na sala yake, na kauli yenye nguvu inasema kuwa sala yake itakuwa sahihi, japo kuwa kauli ya ahwat inasema ni bora zaidi kuirudia sala hiyo baada ya kujitwaharisha kwa maji ikiwa maji hayo yamepatikana kabla ya rukuu, bali hata baada yake maadamu rakaa ya pili haijamalizikia.
MS’ALA: Ikiwa mtu mwenye hadathi kubwa atafanya tayammam, kama mtu mwenye janaba hedhi na mengineyo kutokana na udhuru, kisha akatokwa na hadathi ndogo, tayammam yake haitabatilika, ikiwa itawezekana atafanya tayammam, la sivyo atafanya tayammam badala ya udhu, na kauli iliyo ahwat ni kukusanya kati ya kutaymmam badala ya ghusli na kutawadha ikiwa itawezekana, na atafanya tayammam kwa makusudio ya kuodoa dhimma ikiwa haikuwezekana kutawadha.
MAS’ALA: Haijuzu kumwaga maji yatoshayo kwa udhu, au ghusli baada ya kuingia wakati wa sala, bali kutokana na kauli iliyo ahwat ni kuwa haijuzu kumwaga maji kabla ya kuingia wakati wa sala ikiwa utafahamu ya kuwa hayatapatikana baada ya kuingia wakati wa sala, na ikiwa utakusudia kuyamwaga maji hayo itawajibika kufanya tayammam ikiwa pia hakuna matarajio ya kuyapata maji hayo na utasali kwa kutayammam,na ikiwa utaweza kuyapata maji baada ya kusali sala hiyo kwa tayammam haitawajibika kuirudia wala kuilipa sala hiyo kutokana na kauli iliyo adh’har (iliyo dhahiri), na ikiwa utakuwa na udhu haitajuzu kuutengua au kuubatilisha udhu huo kutokana na kauli iliyo ahwat ikiwa utafahamu ya kuwa hakuna maji au ikiwa utakata tama juu ya kupatikana maji, na ikiwa uta ubatilisha udhu katika hali kama hii itakubidi kufanya tayammam na kusali na haita kulazimu kuirudia kama tulivyo tangulia kusema.
MAS’ALA: Ni sheria kutumia tayammam kwa kila jambo ambalo ni sharti kuwa na twahara katika kutekelezwa kwake, kama sala ya faradhi na sunna, vile vile kila jambo ambalo halitimii isipokuwa kwa kuwa na twahara ikiwa jambo hilo limeamrishwa na hupelekea kwenye ukamilifu, kama kusoma qur’ani, na kukaa msikitini na mfano wa hayo, na kutayammam kwa ajili ya kuwa na twahara tu kuna ish’kaal, na kauli iliyo dhahiri ni kuwa inajuzu kutayammam kwa ajili ya kutenda mambo yaliyo haramishwa kwa mwenye hadathi hata kama hakuamriswa kufanya hivyo, (kama kugusa qur’ani na kugusa jina la Mwenyezi Miungu mtukufu) kama tulivyo elezea katika malengo ya udhu.
MAS’ALA: Ikiwa mtu mwenye hadathi atafanya tayammam kwa jili ya lengo fulani, itajuzi kuitumia tayammam hiyo kwa lengo lingine lolote na jambo hilo litasihi, kwa mfano ikiwa atafanya tayammam kwa ajili ya sala itajuzu kuingia msikitini kwa tayammam hiyo na sehemu za kufanyia ziara kama kwenye makaburi ya maimam na mengineyo kati ya mambo ambayo ukamilifu wake au kusihi kwake au kujuzu kwake ni sharti kujitwahirisha kwa maji. Na ikiwa atafanya tayammam kutokana na ufinyu wa wakati, itajuzu kusali kwa tayammam hiyo na itajuzu kuitumia tayammam hiyo kwa lengo lingine kama kugusa qur’ani na kusoma suratul azaaim na mfano wa hayo.
MAS’ALA: Tayammam hutenguka na kubatilika pale tu kunapo kuwa na ewezekano wa kutumia maji hata kama kutapatikana udhuru baada ya hapo, isipokuwa ikiwa uwezekano huo utamkuta katikati ya sala wakati huo tayammam yake haitabatilika kama ilivyo tangulia. Na mtualie fanya tayammam mbili –kwa ihtiyaat- moja badala ya udhu na nyingine badala ya ghusli ikiwa atapata maji yamtoshayo kwa kutawadhia, tayammam yake iliyo kuwa badala ya udhu itabatilika, na ikiwa atapata maji yamtoshayo kwa ajili ya ghusli, tayammam zote mbili zitabatilika sawa maji hayo yaweyatatosha kwa udhu na ghusli kwa pamoja au laa, na wakati huo atafanya ghusli tu. Na hali hii itatumika kwa mtu asie na istihadha mutawassit, ama mwenye istihadha mutawassit yeye katika hali ya kwanza na katika sura ya mwisho atafanya ihtiyaat kwa kufanya ghusli na kutawadha, na katika hali ya pili ata tawadha na kufanya tayammam badala ya ghusli kutokana na kauli ya ahwat, kutokana na hayo inadhihiri hukumu wakati atakapo kosa maji yatoshayo kwa ghusli kabla ya kuyatumia na kwamba hukumu yake ni sawa na hukumu ya kabla ya kutayammam.
MAS’ALA: Ikiwa mtu atatia shaka ya kuwa kuna kizuwizi katika baadhi ya viungo vya kufanyia tayammam au laa, hali yake ni sawa na hali ya udhu na ghusli, kwani ni wajibu kufanya uchunguzi hadi kupata yakini au matumaini ya kuto kuwepo kizuwizi.