SALA YA AYAAT

Sala ya ayaat ina rakaa mbili, na kila rakaa ina  rukuu tano, na namna yake ni kama ifuatavyo:

 Kwanza utanuwia na kutoa takbira na kusoma suratul faatiha –yaani- al hamdu na sura nyingineyo kamili, kisha  utarukuu na utakapo inuka kutoka kwenye rukuu  utasoma suratul faatiha na sura nyingine kamili, kisha utarukuu  na utainuka kutoka kwenye rukuu  na utasoma tena al hamdu na sura nyingine na utafanya hivyo hadi zifike rukuu tano, na utakapo maliza rakaa ya tano na kuinuka, utasujudu mara mbili kama ufanyavyo katika sala za faradhi za kila siku, kisha utasimama kwa ajili ya rakaa ya pili.na utafanya kama ulivyo fanya katika rakaa ya kwanza, na ukimaliza utasoma tashahhudi  kamaufanyavyo katika sala zingine.

Na inajuzu kusoma tu suratul faatiha mara moja na kusoma baada ya suratul fatiha aya kadhaa katika sura nyingine kwa sharti kwamba isiwe chini ya aya moja ikiwa si jumla iliyo kamili kwa kauli ya ahwat, kisha utarukuu  naukiinuka kutoka kwenye rukuu  utasoma kipande kingine cha sura hiyo kwa kuanzia sehemu ulipo ishia kisha utarukuu, na utafanya hivyo na kuikamilisha surahiyo katika rakaa ya nne kisha utarukuu, na utafanya hivyo hivyo katika rakaa ya pili.                              

Na inajuzu  kutenganisha kwa kusali rakaa ya kwanza kwa utaratibu huu ulio tangulia, na katika rakaa ya pili kutumia utaratibu huu au kinyume chake, na kuna namna nyingine ya kuisali sala hii  lakini hakuna haja ya kuielezea.

Mas’ala: Ni sunna kusoma kunuut katika sala ya ayaat kabla ya rukuu ya pili,  rukuu ya nne,  rukuu ya sita, rukuu ya nane na rukuu ya kumi, na inajuzu kutosheka kwa kunuut moja kabla ya rukuu ya kumi.

Mas’ala: kauli ya ahwat inasema kuwa haitoshelezi kusoma bismillahi baada ya al hamdu katika sala ya ayaat kama tulivyo eleza hapo kabla.

Mas’ala: Ina juzu kuisali sala ya ayaat kwa sura ya jamaa, kama ambavyo inajuzu kuisali mtu mmoja mmoja, lakini ikiwa  hakuweza kumdiriki imam katika rukuu ya kwanza katika rakaa ya mwanzo  au rakaa ya pili  ataisali peke yake.

Mas’ala: Mambo yote tuliyo yataja katika sala za kila siku  kama masharti ya sala na mambo yabatilishayo  sala na hukumu za shaka  na sahau hutumika katika sala ya ayaat.

Mas’ala: Ikiwa  mtu atatia shaka kuhusiana na idadi ya rakaa katika sala ya ayaat na hakuweza kuipa uzito idadi fulani kati ya pande mbili hizo  sala yake itabatilika, na ikiwa atatia shaka katika idadi ya rakaa,  hata zitilia maanani ikiwa ni baada ya kuvuka sehemu hiyo ama ikiwa bado hajavuka sehemu hiyo  atajengee katika idadi ndogo na ataitekeleza sehemu aliyo itilia shaka.

Mas’a’la: Ikiwa mtu atafahamu ya kuwa jua au mwezi vimepatwa,  na hakusali sala ya ayaat  kwa kuasi au kwa kusahau hadi kupatwa huko kuka ondoka, ni wajibu wake kulipa sala hiyo, na  hakuna tofauti kati ya kupatwa jua lote au nusu yake, na kauli ya ahwat ya wajibu ni kuwa inabidi  kuoga  kabla ya kuilipa ikiwa lilipatwa lote, na ikiwa hakuisali kwa kuasi,   na ikiwa hakufahamu ya  kuwa jua au mwezi ulipatwa hadi kupatwa huko kukatoweka , ikiwa kupatwa  huko kwa jua au kupatwa kwa mwezi ilikuwa ni lote kiasi kwamba  jua lote au mwezi wote ulipatwa,  hapo itawajibika kuilipa la sivyo haitakuwa wajibu, na kauli ya ahwatul awlaa inasema kuwa inabidi  kuilipa sala ya ayaat  hata katika matukio mengine tofauti na kupatwa kwa jua au mwezi na sawa awe amefahamu kutokea kwa tukio hilo wakati lilipo tokea au hakufahamu.

Mas’ala: Haijuzu kwa mwenye hedhi  na mwenye nifasi kusali sala ya ayaat na kauli ya ahwatul awlaa ni kuwa atailipa baada ya kuwa twahara.

Mas’ala: Ikiwa mukallaf anajukumu la kusali sala ya ayaat na  faradhi ya kila siku, anahiyari ya kuitanguliza  yoyote ile aitakayo, ikiwa wakati utakuwa ni mpana wa kuweza kuzitekeleza sala hizo, ama ikiwa wakati uliopo unatosha kwa sala moja wapo na usitoshe kwa nyingine  ataitanguliza ile ambayo wakati wake umekuwa finyu zaidi.

Kisha ataitekeleza ile ambayo wakati wake ni mpana, na ikiwa wakati wa sala zote mbili umekuwa finyu  ataitanguliza sala ya kila  siku, na ikiwa ataitakidi ya kuwa wakati wa sala ya ayaat ni mpana  na akaanza kusali sala za kila siku, kisha ikabainika kuwa wakati  was ala hiyo ni finyu, ataikata sala hiyo ya kila siku na atasali sala ya ayaat, ama ikiwa ataitakidi ya kuwa wakati wa sala ya kila siku ni mpana na akaanza kuisali sala ya ayaat kisha ikabainika ya kuwa wakati wa sala ya kila siku ni finyu, ataikata na kusali sala ya kila siku, na atarudi kuisali sala ya ayaat kwa kuanzia sehemu alipo ikatia  ikiwa halikutokea tendo libatilishalo sala na ambalo haliitenganishi na sala ya kila siku.