NYONGEZA YA KWANZA

Mwanahistoria Bwana Mas'ud ananakili tukio ambalo habari zake amezichukua kutoka katika kitabu kiitwacho 'Al-Mubarrad' na ambalo mwanahistoria mwingine Bwana Ibn Khallikan ameliweka katika maelezo (katika Juzuu ya Pili, uk. 214 wa tafsiri ya Kifaransa ya "Tarikh" ya Bwana Ibn Khallikan iliyofanywa na Bwana de Slane) ya Imamu Ali Naqi (Abul Hasan Askari [a] lisemalo kuwa, "Habari ya siri alipelekewa Al-Mutawakkil kuwa lmamu alikuwa na zana za vita, vitabu na vitu vingine ambavyo ilikuwa vitumiwe na wafuasi wake waliyojificha nyumbani mwake, na kushawishiwa kwa taarifa mbaya ili waamini kuwa alikuwa akijitahidi kuipata dola ile. Usiku mmoja Muttawakil alipeleka askari wa Kituruki kuingia nyumbani humo wakati asiotegemea hivyo. Walimkuta akiwa peke yake na akajifungia chumbani mwake akiwa amevaa shati la manyoya na kichwani kwake akiwa amejitanda shuka ya sufi na akielekeza uso wake mjini Makka, akisoma aya za Qur'ani zenye kuonyesha ahadi na vitisho vya Mwenyezi Mungu akiwa hana hata zulia lolote ila kokoto na mchanga tu.

Alichukuliwa hivyo hivyo na kutolewa nje gizani mpaka kwa Al-Mutawakkil ambaye wakati huo alikuwa anakunywa mvinyo. Alipomwona Imamu [a] alimpokea kwa heshima na alipoambiwa kuwa hakuna kilichoonekana nyumbani mwa Imamu [a] kiwezacho kuthibitisha yale mambo yaliyodhaniwa, alimwambia aketi karibu naye na akampa kikombe cha mvinyo alichokuwa nacho mikononi mwake. Abul Hasan (Imamu [a]) akasema, "Ewe Amirul-Muuminin", kufuatana na imani ya wanahistoria waandishi wala sio kwa mujibu wa aaminivyo Imamu [a]; pombe kama hii haijachanganywa na mwili na damu yangu, hivyo nisamehe nisiinywe." Mfalme alimkubalia ombi lake lakini alimwomba Imamu [a] amsomee beti fulani fulani za Mashairi ambazo zingelimfurahisha. Imamu Abul Hasan [a] alimjibu kuwa alikuwa amekariri mashairi machache sana lakini Al-Mutawakkil aliposisitiza kuwa aimbe, aliimba mashairi haya yafuatayo:

"Usiku kucha walikesha katika vilele vya milima,

Wakilindwa na askari shujaa,

Lakini hata hivyo maficho yao hayakufaa kitu.

Baada ya fahari na madaraka yote waliyonayo,

Iliwalazimu wateremke kutoka kwenye ngome zao,

ndefu na kuingia mwenye kifungo cha kaburi,

O! Mabadiliko hayo ni yenye kuogofya kiasi gani?

Makaburi yao yalikwisha wapokea wakati sauti iliposikika ikisema:

Ziko wapi falme zenu na mataji na kanzu zenu za heshima?

Sasa ziko wapi nyuso za hao wazuri, zilizofunikwa na maovu na kulindwa na mapazia ya kumbi za wasikilizaji?

Kwa ombi hili kaburi lilitoa jibu kamili.

Likasema, sasa mafunza wanazifurahia nyuso hizi (kwa kuzila).

Watu hawa walikuwa wakila na kunywa kwa muda mrefu lakini sasa badala yake wanaliwa.

Kila mtu aliyekuwepo pale alihofia usalama wa Abul Hasan [a]. Waliogopa kuwa Mutawakkil katika hasira yake ya kwanza tu angeweza kuimalizia hasira yake kwake. Lakini badala yake walimwona Mfalme huyo akilia kwa uchungu mwingi sana, machozi yakatiririka kutoka ndevuni mwake hivyo wote waliokuwa pale walianza kulia nao. AI-Mutawakkil aliamuru mvinyo huo utolewe na badala ya hayo alisema: "Niambie Abul Hasan una deni lolote udaiwalo. "Ndiyo", alijibu Imamu [a] "Nilikopa dinari mia nne. Mfalme aliagiza Imamu [a] apewe fedha hiyo na apalekwe kwake kwa heshima zote."