NYONGEZA YA PILl

Siku moja Mutawakkil alimwomba Bwana Ibn Sukait (Soma maandishi ya kitabu hicho jina hili limeandikwa kitabuni humo lbn-Al-Sakit) kumwuliza Imamu [a] maswali magumu sana ambayo yangemshinda kuyajibu. Hivyo alimwuliza maswali yafuatayo:

Ibn Sukait: Mungu alimpa Mussa Muujiza wa fimbo na Issa alipewa Muujiza wa kuwaponya wakoma na kuwafufua wafu na Muhammad Mtume wetu alipewa Qur'ani na upanga: Kwa nini hakuwapa mitume hawa wote muujiza wa aina moja?

Imamu [a]: Kila muujiza unafaa kwa wakati wake ulipotolewa. Wakati wa Mussa wachawi walikuwa mashuhuri sana, hivyo alipewa muujiza huo wa Fimbo na Taa ya mkono. Wakati wa Issa, sayansi ya utabibu ilikuwa imefikia kilele chake, hivyo alipewa muujiza wa kuponya magonjwa na kufufua wafu Na wakati wa Mtakatifu Mtume, ufasaha wa kusema, elimu ya usemaji na ushujaa vilikuwa na sifa zaidi, hivyo alipewa Kitabu (Qur'ani) na Upanga, ili kupambana navyo.

lbn Sukait: Sasa siku hizi wakati ambapo hakuna mwenye muujiza, nini "Hujjah" (Kipomo cha tabia ya watu)?

Imamu [a] "Ni akili yao ya kuweza kujua mema na mabaya.

Ibn Sukait: Lakini akili ilikuwepo katika miili tangu awali?

Imamu: Lakini milango ya kupambanua ilikuwa bado haijafunguliwa. Milango hiyo imefunguliwa na Mitume.

Ibn Sukait: Ni nani huyu anayetajwa katika Qur'ani, kwani "... yule aliyekuwa na elimu ya Kitabu..." (Qur'ani, 27:40).

Imamu [a]: Asif bin Barkhiya.

Ibn Sukait: Lakini wakati Mtume Suleiman alipowauliza wafuasi wake ni nani kati yao awezaye kumleta Malkia Bilqis (wa Sheba) pamoja na kiti chake cha enzi, haujua kwamba Asif anaweza kufanya hivyo?

Imamu [a]: AIijua, lakini alitaka kuhakikisha ubora wa Asif kwao na kuwaambia kuwa atakuwa Mrithi (Khalifa) wake.

Ibn Sukait: Kwa nini Yaaqub alimsujudia Yusufu? Je, ni haki baba kumsujudia mwanawe? Je, mwanadamu anaweza kufanya hivyo kwa mwanadamu mwenzie?

Imamu [a]: Kusujudu kule kulikuwa ni utii kwa Mwenyezi Mungu na kumtakia heri Yusuf. Kusujudu huku kulikuwa sawa na kule malaika walikokufanya kwa Adamu. Kusujudu kwa Yaaqub na wanawe kulikuwa ni shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwamba aliwakutanisha tena wakawa pamoja tena baada ya kutengana kwa muda mrefu.

Ibn Sukait: Ni mti gani ule Adamu alioamriwa asiukaribie wala kula matunda yake?

Imamu [a]: Ulikuwa ni mti wa Wivu. Mwenyezi Mungu alitaka kawaokoa wana wa Adamu kutokana na wivu.