SHAHIDIWA MASH-HAD (IMAMU ALI AL-RIDHA (A.S)

Kimetungwa na Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb

Kimetafsiriwa na Bwana L.W. Hamisi Kitumboy

MWENYEZI MUNGU ANASEMA :

يَوْمَ نَدْعُو كُلَّ أُنَاسٍ بِإِمَامِهِمْ فَمَنْ أُوتِيَ كِتَابَهُ بِيَمِينِهِ فَأُوْلَـئِكَ يَقْرَؤُونَ كِتَابَهُمْ وَلاَ يُظْلَمُونَ فَتِيلاً

 (Ewe mwanadamu! Ikumbuke) siku Tutakapowaita kila watu pamoja na Imamu wao; basi atakayepewa kitabu (chake cha Amali) kwa mkono wa kulia, hao watavisoma vitabu vyao (kwafuraha);..    (Banii Israeil, 17:71)

MTUKUFU MTUME (SA.W.W.) AMESEMA:

من مات ولم يعرف امام زمانه مات ميتة جاهلية

"Ye yote yule afaye pasi na kumjua Imamu wa zama  zake, atakuwa kafa kifo cha ujinga."              —

MTUKUFU MTUME (S.A.W.W.) AMESEMA:

"Hao (Ulul Amr watajwao mwenye Qur-ani 4:59) ni Makhalifa wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa kwanza ni Ali, kisha ni Hassan, kisha ni Husayn, kisha niAli bin Husayn, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Jaafal bin Muhammad, kisha ni Musa bin Jaafar, kisha ni Ali bin Musa, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Ali bin Muhammad, kisha ni Hassan bin Ali, kisha ni Muhammad bin Hassan (Mahd)....."

("Kifayatul Athar" na "Rawdhatul Ahbab", vya Hafidh Jamaluddin Muhaddith).

 رضيت بالله ربا و بمحمد صلی الله عليه و آله نبيا و بالاسلام دينا و بالقرآن کتابا وبالکعبة قبلة وبعلی وليا واماما وبالحسن والحسين وعلی بن الحسين ومحمد بن علی وجعفر بن محمد وموسی بن جعفر وعلی بن موسی ومحمد بن علی وعلی بن محمد والحسن بن علی والحجة بن الحسن صلوات الله عليهم ائمة اللهم انی رضيت بهم ائمة فارضنی لهم انک علی کل شیء قدير

SHUKRANI

Kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Sayyidul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahid wa Chuo Kikuu cha Lucknow, Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kingereza na Sayyid Hashim Raza Rizvi, B.A., B.T., Yadgar-e-Husaini H.S. School, Al-lahabad, Uhindi na kutolewa na Imamia Mission, Lucknow, U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka hiyo tafsiri ya Kiingereza na Marehemu Bwana L.W. Hamisi Kitumboy (aliyekuwa Mubaligh-Mkaguzi, wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo, Edita wa "Sautiya Bilal".

UTANGULIZI

Uislamu ni dini ya matendo. Unatutaka kuifuatia barabara ile njia ya dini wakati tunapoishi katika njia inayohitajiwa na mahitaji ya maisha ya ulimwengu huu. Hilo si jambo rahisi kulifanya. Ni rahisi kuishi maisha ya Kiuchamungu, ukijitenga kabisa na anasa za dunia; lakini kwa uhakika ni vigumu kabisa kupita katika wavu wa maisha ya ulimwengu huu bila ya kupata dosari yo yote.

Ili kuweza kujipatia mwongozo mzuri, tunahitaji kujifunza maisha ya wale waalimu wa kidini waliowajibika kuishi katika hali mbalimbali; ambao wakati mwingine iliwabidi kuishi maisha ya kujitenga na wakati mwingine kufanya mapatano na wenye madaraka ya kidunia (wafalme) na kisha kujisafisha kabisa kutokana na uchafu wa mazingira ya maisha hayo, na ambao kila mara walijali sana kazi yao iliyowabidi kuifanya .(kuutangaza Uislamu). Maisha ya Imamu Ali Ridha yalikuwa ya namna hiyo.

JINA NA NASABA YAKE

Jina lake lilikuwa Ali "Kun'yat" (jina la utoto) wake ni Abul Hassan na jina lake la heshima ni Ar-Ridha.

baba yake ni Imamu Musa Al-Kadhim, na mama yake ni Bibi Umu-ul-BaninTahirah, mwanamke aliyekuwa Mchamungu sana.

KUZALIWA KWAKE        

Imamu Ali Ar-Ridha (a.s.) alizaliwa mnamo tarehe 11 ya mwezi wa Dhul-Qa'adah (Mfunguo Pili) wa mwaka wa 148 Hijiriya, mjini Madina. Wakati huo baba yake Imamu Jaafar As-Sadiq (a.s.) alikuwa keshafariki mwezi mmoja uliopita, kwenye tarehe 15 ya mwezi wa Shawwal (Mfunguo Mosi) na kuzaliwa kwa mtoto huyu kulileta faraja kwa jamii hii iliyoondokewa na baba yao.

KULELEWA KWAKE

Alilelewa chini ya ulinzi wa baba yake, Imamu Mussa Al-Kadhim (a.s.) na alipitisha maisha ya miaka thelathini na mitano ya maisha haya chini ya uongozi huu wa kimapenzi na katika mazingira ya kidini hayo hayo. Ingawa katika miaka michache ya maisha yake ya mwishoni ilimbidi kutengana na mpenzi babiye wakati Imamu Musa Al-Kadhim (a.s.) ilipombidi kwenda kupambana na taabu za jela nchini Iraq, Imamu (a.s.) alikuwa tayari keshaishi na baba yake kwa muda wa miaka 28 au 29 hivi.

UIMAMUWAKE

Imamu Musa Al-Kadhim (a.s.) alielewa vizuri kuwa wafalme wa zama hizo hawatamwacha aishi kwa amani, na kuwa muda utafika mwishoni mwa maisha yake ambapo marafiki zake wapenzi hawatapata uhuru wa kuonana naye kila wapendapo kumuona, au kumjua mrithi wake baada ya kufariki kwake. Hivyo alihisi kuwa ipo haja ya kuwafanya wafuasi wa watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) wamfahamu vizuri mrithi wake wakati wakiwa wanaishi kwa amani mjini Madina. Hivyo aliwaita watu kumi na saba wenye cheo kutoka miongoni mwa dhuria wa Hadhrat Ali bin Abi Talib (a.s.) na Bibi Fatimah (a.s.) na 'kutangazia kuwa mrithi wake atakuwa mwanawe, Ali. Vile vile aliandika usia wake kuhusu jambo hilo na ukatiwa saini na watu sitini, wakazi wa mjini Madina.

MUDA WA UIMAMU WAKE

Imamu Ali Ar-Ridha alikuwa na umri wa miaka 35 alipofariki baba yake Imamu, Imamu Musa Kadhimu. Kazi zote na Uimamu zilimuangukia yeye, baada ya kufariki baba yake. Huu ulikuwa ni muda wa utawala wa mfalme Harun-Al-Rashid na makao yake yalikuwa Baghdad (Iraq). Wakati huu ulikuwa mgumu sana kwa dhuria wa Bibi Fatimah (a.s.). Na chini ya hali hizi mbaya, Imamu (a.s.) aliianza kazi yake ya kuitangaza dini ya kweli, na kuudumisha Ujumbe Mtakatifu.

MAISHA YAKE YA UALIMU

Nuru aliyoipewa na Mwenyezi Mungu waliyobarikiwa nayo watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) ilitambuliwa na marafiki zake na maadui pia. Wakati baadhi yao walipokuwa na nafasi kubwa ya kuitawanya mbegu ya elimu ya kweli, wengine walikuwa na nafasi ndogo sana ya kuwaangazia viumbe wa Mwenyezi Mungu. Baada ya Imamu Jaafar (a.s.)Imamu aliyepata nafasi kubwa ya kuutangaza Ujumbe wa Mwenyezi Mungu, alikuwa Imamu Ali Ridha (a.s.). Kabla hajaichukua kazi ya Uimamu, baba yake alikuwa akiwaelezea wanawe na watu wengine wa jamii yake kuhusu Imamu Ali Ridha (a.s.), akisema,

Ndugu yenu Ali Ridha ndiye mlinzi wa Elimu ya Watu wa Nyumba ya Mtume (s.a.w.). Mwendeeni mnapokabiliwa na matatizo ya kidini na kila mara kumbukeni asemavyo". Na baada ya kufariki baba yake, alipokuwa akiishi mjini Madina na alipokuwa na kawaida ya kukaa karibu na kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w.)., wanachuoni wakuu wa Fiqah walikuwa wakimjia wakimletea matatizo yao ayatatue. Bwana Muhammad bin Isa Yaqtini alihadithia kuwa wakati Amamu Ali Ridha (a.s.) alipoyakusanya matatizo yote aliyoletewa na kuyaweka katika hali ya kimaandishi idadi ya matatizo hayo ilifikia elfu kumi na nane.

MAISHAYAKE

Mfalme Harun Al-Rashid alitawala kwa muda wa miaka kumi baada ya kufariki kwake Imamu Musa Kadhim (a.s.), na kwakweli mfalme huyu wa ukoo wa Bani Abbas hakumpenda mwana huyu Mchamungu (.Imamu Ridha a.s.) zaidi ya alivyompenda yule baba Mchamungu (Imamu Kadhim). Lakini haijulikani kama mfalme huyu aliwapenda hawa Maimamu wawili kwa sababu ya kuogopa

asipoteze mapenzi yake kwa watu au labda inawezekana kwamba ilikuwa ni moyo wake tu uliomtuma kufanya hivyo; hivyo basi, mfalme Harun -Al-Rashid hakuchukua hatua yo yote ile ya kiuadui dhidi ya Imamu Ali Ridha (a.s.). Iko hadithi isemayo kwamba, siku moja mtu mmoja aitwaye Yahya bin Khalid Barmaki, ili kumvika Harun kilemba cha ukoka, alimwambia, "Sasa Ali bin Musa nae anadai kuwayu Imamu kama baba yake". Harun Al-Rashid alimjibu, "Tumemtendea mambo mengi sana baba yake: na sasa unataka niimalizie mbali jamii hiyo".

Lakini, vivyo hisia za Harun Rashid kwa watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) na jinsi walivyotendewa na wafalme kwa ujumla mpaka sasa yalifahamika sana kiasi cha kutomfanya yeyote yule kati ya maofisa kumheshimu Imamu (a.s.), pia wale watu miongoni mwa raia waliotaka majna yao yaandikwe katika vitabu vizuri vya serikali hawakufikiria kufanya hivyo. Watu hawakupata uhuru wa kuja kusomea Fiqah kwa Imamu (a.s) na hakupata nafasi yoyote ya kuutangazaUislamu.

Siku za mwisho za Harun Al-Rashid ziliharibiwa na maasi ya vanawe wawili. Mwanawe aitwaye Amin, aliyezaliwa kutokana la mkewe wa kwanza na aliyekuwa mjukuu wa mfalme Mansur Dawaniqi; hivyo watu wakuu miongom mwa Waarabu walimpendelea sana. Mwanawe mwingine aitwaye Mamun aliyemzaa na mjakazi wake wa Kiirani, hivyo wakuu wa baraza lake wenye asili ya Kiirani walimpendelea mtoto huyu. Maasi ya watoto hao yalimsumbua sana Harun. Alifikiria kuigawa milki yake baina ya hawa watoto wawili, hivyo alimpa Amin sehemu ya Magharibi ya milki hiyo ukiwemo mji mkuu, Baghdad, Shamu, Misr, Hijaz, na yaman. Na sehemu ya Mashariki ikiwemo Iran, Khurasan, na turkistan ilipewa Mamun, lakini kwa kweli hatua hii ingelifaulu tu kama pande zote mbili zingeliuangalia sana msingi wa "Ishi kwa amani na waache wengine waishi kwa amani".

Baada tu ya kufariki Harun hawa watoto wawili walianza kugombana wao kwa wao na baada ya kupigana kwa muda wa

miaka minne, Amin alikatwa kichwa katika mwezi wa Muharram wa mwaka 198 Hijiriya na Mamuun akawa mfalme.

MRITHI WA MAMUN

Ingawa sasa Mamun amekuwa mfalme wa milki nzima, kumwua kwake Amin kulitapakaza fikara za kutoridhika naye miongoni mwa Waarabu wa Iraq na wale wa ukoo wa Bani Abbas waliomuunga mkono Amin.

Kwa sababu Bani Abbas walifaulu kuwapindua Bani Ummayyah kwa msaada wa Mairani na wakapata sababu ya kutawala badala ya Bani Fatimah (watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume s.a.w.), na kwa sababu Mairan wamekwisha ona yalewaliyoyatenda Bani Abbas kwa Bani Fatimah, hivyo Mamun aliona kuwa iko haja ya kuonyesha wazi wazi kuwa yeye hatafuata njia hiyo ya Bani Umayya na wafalme wengine wa Bani Abbas. Hivyo aliuacha utaratibu wote uliokuwa ukifuatiwa na wafalme wa koo zote hizo mbili. Hivyo alitangaza kuwa alipokuwa akipigana na Amin, wakati Sistan na Kirman walipokuwa wakileta vurugu aliapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa kama akishinda dhidi ya maadui wake na akapata amani ataurudisha Ukhalifa kwa Bani Fatimah ambao ndio wenye haki ya kuushika na kuwa baada ya hapo, mambo yake yalianza kumwendea vizuri.

Hivyo alimkaribisha Imamu Ali Ar-Ridha nyumbani kwake. Imamu (a.s.) alipokuwa akiondoka Madina, wale waliomwona akilizuru kaburi la Mtukufu Mtume (s.a.w.) kwa mara yake ya kwanza, waliikumbuka ile ziara ya mwisho ya Imamu Husain (a.s.) kwa Kaburi lile Tukufu. Alimlalamikia Mtukufu Mtume (s.a.w.) kwa yale aliyotendewa na wale wanaojiita Waislamu ambao walidai kuwa wanaiheshimu kumbukumbu ya Mtukufu Mtume (s.a.w.).

Katika mwaka wa 200 Hrjiriya aliondoka Madina kwenda Merv (Iran), mji mkuu wa siku hizo. Aliiacha jamii yake yote mjini Madina pamoja na mwanawe Imamu Muhammad Taqi (a.s.) aliyekuwa na umri wa miaka mitano wakati huo.

Alipofika Merv, ilifanyika sherehe ya ukarimu kwa muda wa siku chache hivi, na baada ya hapo Mamun alimtaka Imamu Ali Ar-Ridha awe Khalifa. Lmamu (a.s.) alijibu, "Kama unajifikiria kuwa Ukhalifa wa kweli kwa nini unipe Ukhalifa? Na kama unajifikiria kuwa mlinzi wa kweli wa Ukhalifa, basi huna haki ya kumpa yeyote yule umpendaye". Mamum alinyamaza kimya,

lakini mara moja aliendelea kumwomba aurithi Ukhalifa huo kutoka kwake. Imamu (a.s.) alikataa pia kwa sababu kukichukua cheo hicho kutoka kwa mdhalimu ni kinyume na Sheria za Kiislamu. Lakini Mamun hakupenda kuona mpango wake huo ukishindwa. Hivyo alimshikilia akubali na akamtisha kumlazimisha iwapo ataendelea kuukataa na mwishowe alisema kuwa Imamu (a.s.) hataruhusiwa kurudi akiwa hai kama akiukataa Ukhalifa.

Maisha yanaweza kutolewa mhanga kwa ajili ya kuilinda Sheria ya Mwenyezi Mungu kwa njia hii tu, lakini kinyume na hivyo usalama wa maisha ndio msingi wa kwanza wa Uislamu. Hivyo Imamu (a.s.) alisema, "Kama ndio hivyo, ninakubali lakini sitashiriki katika mambo ya serikali. Kwa hakika, kama nikiombwa kutoa ushauri wangu, nitatoa ushauri unaopasika".

Maneno haya yalituliza ghasia zote. Inawezekana kuwa ushauri wa Imamu (a.s.) ungelikuwa na faida kwa Mamun, mwanasiasa, lakini cheo cha Imamu (a.s.) kilikuwa kama kilivyokuwa hapo awali. Imamu (a.s.) hakuwa na madaraka yoyote juu ya yale aliyoyatenda Mamun wala kule kutoa ushauri wake (kwa hakika, kwa mujibu wa Sheria za Dini) hakukuyathibitisha matendo ya Serikali hiyo.

Wafitini wa ukoo wa Bani Abbas hawakupendelea kuchaguliwa kwa Imamu (a.s.) kuwa Mrithi wa Ukhalifa wa Mamun. Lakini Mamun aliwataka wafitina hao wamtaje mtu mwingine afaaye zaidi. Kwa ajili ya jambo hili, yalifanyika majadiliano ya hadhara katika baraza la mfalme Mamun. Imamu (a.s.) kwa kweli ndiye aliyeweza kuwa mlinzi wa kweli wa Sheria za Mwenyezi Mungu. Na hivyo Mamun aliishikilia azma yake hiyo.

Mnamo tarehe mosi ya mwezi wa Ramadhani wa mwaka wa 201 Hijiriya, ilifanyika sherehe kubwa kabisa ya kumrithisha Imamu (a.s.) Ukhalifa. Kwanza kabisa Mamun alimuashiria mwanawe kijana ambaye alikuja na kuweka mkono wake juu ya mkono wa Imamu (a.s.) (Hii ndio jinsi Waarabu walivyokuwa wakionyesha utii) na baada ya mwana huyo kufanya hivyo walifuatia maofisa wa Serikali. Kisha Mamun aliamrisha zifuliwe sarafu zenye jina la Imamu (a.s.). Zilitolewa sadaka za sarafu za

dhababu na fedha na maofisa wa serikali walipewa zawadi. Jina la Imamu (a.s.) liliwekwa katika Hotuba za Sala ya Ijumaa.

TABIAYAKE

Watu wengi wasiokuwa na uwezo wa kujipatia kitu fulani hujifanya kuwa wametosheka, lakini wale watu wenye utukufu wa kweli na Uchamungu tu, ndio waishio maisha rahisi sana hata wanapokuwa na uwezo wa kuishi kifalme. Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.) ambao hawakuwa na utajiri wala utawala (na hakika wengi wao hawakuwa na vitu hivyo) waliishi maisha rahisi lakini ya kujiheshimu na hawakujali kujipatia mali kwa wingi ili kujiepusha na uchokozi wa maadui zao waliokuwa na kawaida ya kuwatweza kwa kile maadui hao walichokiita kutokuwa na msaada kwao. Lakini kila mara hawa washika Mwenge wa Haki wanaposhikilia madaraka fulani au utajiri fulani, waliishi maisha rahisi sana na ya kimaskini ili kwamba maisha yao yaweze kuwa faraja kwa Waislamu maskini. Maisha ya Hadhrat Ali bin Abi Talib (a.s.) yalikuwa ya namna hiyo. Kwa sababu alikuwa mtawala wa dola ya Kiislamu aliishi kwa uangalifu mkubwa sana katika kutumia fedha kiasi cha kutokuwa na kifani hata kwa warithi wake, Maimamu wengine wa nyumba ya Mtukufu Mtume (s.a.w.). Imamu Ali Ridha (a.s.) nae alikuwa hivyo hivyo. Aliitwa mrithi wa mtawala aliyekuwa na milki kubwa sana hata milki za Kirumi na Ajemi zikasahauliwa kabisa, ambayo kama wingu lingelionekana, Khalifa angeliweza kuliambia, "Nenda kanyeshe mvua popote pale upapendapo, kwa sababu ushuru wa mavuno unaosaidia kukusanya utaletwa kwangu".

Maisha ya Imamu Ali Ridha (a.s.) yalikuwa mfano bora kwa watu wakati mtu anapopewa madaraka yoyote yale kwa Ukarimu wa Mwenyezi Mungu. Maisha ya Imamu Ali wa kwanza (Ali bin Abi Talib a.s.) yalionekana tena (kwa njia ya Imamu Ali Ridha) kuwa kigezo cha kufuatwa na watu wote duniam. Hakuruhusu kutumia mazulia ya Uajemi yaliyokuwa ghali sana nyumbani mwake na badala yake alitumia mazulia ya manyoya wakati wa majira ya kipupwe na wakati wa kiangazi alitumia mikeka. Wakati wa chakula alikuwa akikaa na watumishi na watumwa wake na wakati mtu mmoja wa Balkh aliyekuwa akitayarisha sherehe na tamasha za maafisa wa baraza la mfalme alipopendekeza kuwa matayarisho ya chakula cha watumishi hao yatengwe, Imamu

(a.s.) alijibu akisema, "Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa watu wote; wote ni wana wa Adam na Hawa. Thawabu na Adhabu zao katika Siku ya Kiyama vitategemea matendo yao. Basi kwa nini ziwepo tofauti hapa (duniani)?

Umuhimu wa maisha ya Imamu Ali Ridha (a.s.) unatokana na kuutilia mkazo msingi wa kuwa, kuhusiana (kidamu) na Mtukuf'u Mtume (s.a.w.) hakuna maana yoyote. Aliutilia mkazo msingi huu wakati wa mazingira ambayo wafalme wa ukoo wa Bani Abbas wamewazidi wale wa ukoo wa Bani Umayyah katika udhalimu wao, ufisadi na matendo yaliyo kinyume na Dini na wakati huo huo wakidai kuwa wao ni wana wa ndugu yake Mtukufu. Mtume (s.a.w.).

Maisha haya rahisi ya Imamu Ali Ridha (a.s.) hapo mwanzoni yalionekana kuwa ni jambo la mtu binafsi lakini kwa kweli yalikuwa kuyatangazia maisha ya kweli ya Kiislamu yakiwa kinyume kabisa na desturi zilizojengwa akilini mwa watu katika muda wa karibu karne nzima ya utawala wa Bani Abbas. Maisha yake yalikuwa na sifa sana kwa sababu yalikuwa maisha ya mtu aliyekuwa ameambatana sana na watawala.

Yalikuweko matukio kadhaa ambapo maneno ya Imamu Ridha (a.s.) yalitoa ushahidi ulio wazi kwa kila kilichokuwa wazi kabisa maishani mwake. Siku moja mtu mmoja alimjia Imamu (a.s.) na kumwambia, "Kwa jina la Mwenyezi Mungu hakuna mtu yeyote aliye mbora kuliko wewe, katika ubora wa jamii na wahenga". Imamu (a.s.) alimjibu akisema, "Wahenga wangu wameupata ubora huo kwa ajili ya Uchamungu, utii kwa Mwenyezi Mungu na maisha yao ya kitakatifu". Siku moja Mtu mwingine alimwambia Imamu (a.s.) "Kwa jina la Mwenyezi Mungu wewe u mbora wa wanadamu". Imamu (a.s.) alimjibu akisema, "Usiape. Mtu ambaye Uchamungu wake unauzidi wangu yu mbora kuliko mimi".

Bwana Ibrahim bin Abbas amehadithia kuwa Imamu AIi Ridlha (a.s.) alisema; Watumwa wangu wote wanaweza kutoka katika milki yangu ikiwa ninajifikiria vingine kuliko kutojifikiria kuwa ni hora kuliko huyu mtumwa wangu mweusi kwa sababu tu ya kuwa kwangu kizazi' cha Mtume (s.a.w.). Kwa hakika. kama nikifanya matendo    na ninaweza kuwa hora mhele ya

Mwenyezi Mungu kuliko yeye".

Labda watu wengine huyahusisha yote haya na upole, lakini mtawala wa ukoo wa Bani Abbas hakuwa mpumbavu kiasi cha kutohisi kuwa matendo na hadithi zote hizo za Imamu (a.s.) vilikuwa vikiziondoa zile fikara zilizokuwa misingi ya milki yake. Mara moja aliona kuwa kama Imamu Ali Ridha (a.s.) ataendelea kuishi basi mara moja atasababisha mabadiliko katika fikara za watu ambayo yatakuwa hatari kwa milki yake.

KUMUOMBOLEZEA IMAMU HUSAIN (A.S.)

Imamu Ali Ridha (a.s.) alikuwa na nafasi ya kutosha kuyafanya maombolezo ya msiba wa Imamu Husain (a.s.) kuwa jambo maarufu sana, kuliko waliyo ipata Imamu Muhammad Baqir (a.s.) na Imamu Jaafar As-Sadiq (a.s.). Kwa maana, zaidi ya cheo chake cha ualimu wa dini sasa amekuwa na cheo kingine cha kuwa mrithi wa mfalme. Alikuwa akiishi mjini Merv, karibuni katikati ya nchi ya Iran na watu wa aina mbalimbali walimtembelea. Watu waliona kuwa mwezi wa Muharram unapoingia machozi yalimtiririka Imamu (a.s.) bila ya kukoma. Wengine nao walianza kufanya vivyo hivyo. Kila mara Imamu (a.s.) alikuwa akisema, "Ye yote yule akaaye katika Majlis (Mkutano) ambayo hadithi zetu zinasimuliwa hatauona moyo wake ukizama katika siku ambayo roho nyingine zitazama. Neno "Majlis" linalotumika katika maombolezo ya msiba wa Imamu HUSAIN" limechukuliwa kutokana na hadithi hii ya Imamu Ali Ridha (a.s.). Yeye mwenyewe aliitayarisha mikutano hiyo ambayo wakati mwingine yeye mwenyewe alilielezea tukio la Karbala na wakati mwingine washairi kama vile Bwana Abdallah bin Sabit au Bwana Di'bal Khuza'i walisoma mashairi yao ya kuomboleza. Imamu (a.s.) alimpa Bwana Di'bal Khuza'i joho la thamani kubwa. Wakati mshairi huyu aliposita kulichukua na kuomba apewe jingine lililokwishatumiwa na Imamu (a.s.), Imamu (a.s.) alimpa majoho yote mawili.

KUFARIKI KWAKE

Mfalme Mamun, kama tulivyoelezea hapo juu, alihisi kuwa kuendelea kuishi kwa Imamu (a.s.) kulikuwa hatari kwake hivyo uliitumia silaha ile ile ili kuyaondoshea mbali maisha ya Imamu (a..s.) kama walivyofanya wafalme wa kabla yake kwa Maimamu

wengine. Mamun alimpelekea Imamu (a.s.) zawadi ya zabibu zenye sumu ambazo Imamu (a.s.) alizila na kafariki mnamo tarehe 17 Safar (Mfunguo Tano) wa mwaka 203 Hijiriya. Mamun alijionyesha sana kuwa yu mwenye huzuni na akatayarisha maziko ya Imamu (a.s.) karibu na kaburi la baba yake mfalme Harun Al-Rashid, ambaye kaburi lake halifahamiwi na wale wanaolitembelea kaburi hili tukufu la Shahidi wa Mash-had (Imamu Ali Ridha a.s.) ambalo huwavutia na litaendelea kuwavutia mahujaji wengi mno wanaokwenda kutoa heshima zao kwenye hii Nuru isiyozimika".

NYONGEZA

 Kuba la Imamu  Ali Ridhaa (a.s.)

Mji wa Tus (Mash-had) lilimo Kuba la Imamu Ridha (a.s.) wakati huo, kama anavyotuelezea mwanahistoria Bwana Yaqub katika kitabu chake kiitwacho "Kitabul Buldan" ulikuwa wilaya badala ya kuwa mji maalum tu. Miji yake miwili iliyokuwa muhimu sana ni Naugawn na Tabaran na katika hiyo miji miwili, Naugawn ndio uliokuwa mkubwa na ndio uliokuwa mara kwa mara ukiitwa Tus. Waarabu waliokuwa wakiishi katika wilaya hii walikuwa wa kabila la Tayy. Lakini watu wengi walikuwa ni Waajemi. Ni katika mji huu wa Naugawn alimofia mfalme Harun Al-Rashid na Imamu Ali Ridha (a.s.), ingawa baadaye mji wa Tabaran ndio uliokuwa mji mkuu wa wilaya ya Tus.

Wakati Harun Al-Rashid alipokuja mjini Tus, alilala nyumbani mwa mtu mmoja aitwaye Hamid, aliyekuwa Gavana wa wilaya hiyo na aliyekuwa na nyumba na shamba mahali paitwapo Sanabad, yapata maili moja kutoka Naugawn. Kufuatana na ombi lake, Harun alizikwa katika chumba Kimojawapo cha nyumba hii, na mwanawe Mamun aliamrisha lijengwe Kuba katika kaburi hili. Hivyo Imamu Ali Ridha (a.s.) alipofariki katika mji huo huo wa Naugawn na kazikwa katika Kuba hilo hilo, aliambiwa, "Aliingia nyumba ya Hamid ibn Ghutbah At-Ta'i. Na aliliingia Kuba la Harun Al-Rashid". (Habari hizi zimechukuliwa kutoka kitabu cha mwana historia Bwana Ibn Baba waihi).

 MAOFISA NA WATUMISHI WA KUBA

Inapoanguka theluji nzuri ya kwanza, kila mara huwa kuna shangwe mjini Mash-had, kwa maana ndio zinamalizikia mvua za

kipupwe na barafu ambayo husababisha maisha magumu na njaa. Kwa sababu hiyo, kila inapoanguka theluji ya kwanza, huwa ni kawaida kwa maofisa wakuu wa Kuba kwenda wao wenyewe na chepe na kuiondoa katika paa lililo chini ya Kuba la dhahabu. Hili ni onyesho la kihadhara la shukrani yao kwa Imamu (a.s.) wakati watu wanapouona kwa furaha kuu mwaka mpya mwingne wenye chakula tele.

Ofisa wa cheo cha juu zaidi ni "Mutawalli Bashi" (Mwangalizi Mkuu) ambaye huteuliwa na Shah (mfalme wa Uajemi) kuongoza mambo ya Kuba hilo. Anayemfuatia ni "Na'ib At-Tauliyah" (Naibu wa Mwangalizi Mkuu) ambaye ni lazima atokane na dhuria wa Imamu Ridha (a.s.). Madaraka yake ni ya kurithi kama yale ya "Qaim Maqam" ambaye yu rais wa halmashauri ya wadhamini.               

Zaidi ya hapo wako maofisa wengine sita au nane wa kazi za kiutawala au kikatibu ambao hupata ada na mishahara itegemeayo na mapatano. Baadhi ya maofisa hawa wametajirika kutokana na marupurupu ya mara kwa mara ya kuimiliki hazina itokanayo na mali ya Kuba hilo.

Walakini, upotevu mkubwa wa fedha kwa upande wa mapato ya Kuba hilo umetokea kutokana na idadi kubwa ya watumishi na wahudumu. Hadi mnamo miaka ya karibuni (yapata miaka ishirini na mitano iliyopita) walikuweko mabawabu mia saba walioandikishwa kafika orodha ya mishahara. Hawa mabawabu waligawanyika katika shifti, kila shifti ikiwa na zamu ya masaa ishinni na nane katika kila siku ya tano tangu shifti yao kupita. Kazi zao zilikuwa ni zile za ubawabu na ulinzi. Zaidi ya hapo walikuwepo wahudumu elfu moja ambao kila mmoja alikuwa akipata mshahara maradufu ya ule wa mabawabu ambao nao vile vile waligawanywa katika shifti tano zilizo sawa sawa. Katika usiku wa siku ile ambayo hiyo shifti iko katika zamu, walipata chakula cha jioni cha pilau. Kazi ya hawa wahudumu ni kuhakikisha kuwa kama sehemu fulani katika uwanja au katika ukumhi wa Kuba inanajisika, inatoharishwa mara moja, pia na kuwasha mishumaa, kusaidia kufagia n.k. Na hao mabawabu (darban) au mhudumu (khadim), kila mmoja wa hawa watumishi mia saba vile vile alikuwa na haki ya kuzika ndugu zake wasiozidi watano katika uwanja wa makaburi wa Kuba hilo.

     Lakini zaidi ya hawa watumishi wa kudumu ipo idadi kadhaa ya watu walitumialo eneo la Kuba hilo kuwa ni sehemu za shughuli zao. Yapo madrasa ya kila siku ya wahubiri (Wu'adh) waendao kukaa katika mimbari nyingi zilizoko kila mahali katika uwanja na kumbi za Kuba hilo na kuhubiria. Kishawapo wasomaji wa Our'ani walioihifadhi Qur'ani yote kwa kichwa (hufadh), na kuigawanya katika juzuu thelathini na kusoma juzuu moja kila siku wakati mwingine wao wenyewe lakini mara kwa mara kwa kondorati ya watu fulani wachache hivi. Pia wako wasomaji arobaini au hamsini wa dua maalum isomwayo na mahujaji wa Kuba hiyo, ambao hufuatana na kundi la mahujaji wasiojua kusoma wakati wanapoomba ruhusa ya kuingia katika Kuba na wanaposoma "Salaam" kwa Imamu (a.s.) katika sehemu maalum wanapolizunguka hilo kaburi. Hawa watu wanaosoma vitabu vya dua hupewa Bahashishi.

JINSI KABURI HILO LILIVYO

Lango la kawaida la kuingilia katika kaburi hilo liko upande wa Mashariki, lakini kipo kilango au sebule katika kila upande wa dira wa Kuba hiyo ambako mahujaji wanaweza kusimama na kusoma dua maalum za Kuba hiyo, na katika kuta za sebule hizi yako maandishi mengi yanayoelezea umaarufu wa Kuba hiyo.

Kaburi limehifadhiwa kwa fito tatu za chuma mmoja ndani ya mwingine. Lipo .sanduku kubwa la mbao lililonakishiwa kwa dhahabu lenye jina la Shah (mfalme) Abbas Safavi. Sanduku hilo limezungukwa na ufito wa kwanza wa chuma ambao umewekewa kisetiri cha waya wa shaba ili kuwekea zawadi ziwekwazo humo na mahujaji, zawadi ambazo kwakawaida huondolewa na maofisa wa Kuba hiyo siku chache kabla ya Sikukuu ya Naumz (tarehe 21 au 22 Machi siku ambayo jua humalizia mzunguko wake na kuanza mwaka mpya) na kuziuza kwa mnada. Ufito wa pili wa chuma umenakshiwa kwa dhahabu na johari na una maandishi yaonyeshayo kuwa ulitolewa zawadi na Shah Husain Safavi; na ufito wa tatu au ufito wa nje pia ni wa chuma, na umenakishiwa kwa maandishi ya kupendeza ya sura nzima ya "Al-Insaan" (sura ya 76). Ufito wa pili na wa tatu kila mmoja una matufe ya dhahabu katika pembe na juu ya kaburi liko paa la ubao lililofunikwa kwa bamba la dhahahu na mvunguni mwake yako mapambo ya dhahahu yanayoning'inia ambayo pia yametarizwa kwa johari.

MAJENGO YA NJE

Nyuma ya jengo la Kuba upo Msikiti wa Gauhar Shad ambao eneo lake lote lina urefu wa futi 181 na upana wa futi 164. Msikiti huo una Kuba kubwa lenye rangi ya samawati na mbavuni mwake ipo minara miwili yote iliyojengwa kwa matofali ya rangi ya samawati na yote ikiwa ina urefu wa futi 140. Msikiti wenyewe kwa ndani una urefu wa futi 116 na upana wa futi 41 na kuta zenye urefu wa kwenda juu wa futi 87 na katika kila upande wa ukumbi huu mkubwa vipo vyumba viitwavyo "sehemu za usiku". Na katika hilo Kuba kubwa la matofali ya rangi ya samawati ambalo huonekana kama kwamba linabadilika rangi zake katika mabadiliko ya nuru ya anga, inaonekana ile "Shahada ya Kiislamu" inayoshuhudia "Umoja wa Mwenyezi Mungu" na kutangazia kuwa "Mtume Muhammad (s.a.w.) ni Mtume wa Mwenyezi Mungu". Na chini ya hilo Kuba kubwa zimeandikwa aya 39 za kwanza za Sura ya "Yaasin" (Sura ya 36).

Katikati ya uwanja wa msikiti upo ulingo wa mawe ulio inukia, wenye urefu na upana wa futi 37 na wenye hodhi katika kila upande. Msikiti huu unaitwa "Msikiti wa Bibi Kizee" kwa ajili ya kumbukumbu ya bi kizee mmoja anayefikiriwa kuwa zamani sana alikataa kuiuza ardhi hii. 

Mashariki mwa jengo kubwa la Kuba hilo upo Uwanja Mpya, uliojengwa katika zama za mfalme Fath Ali Shah. Uwanja huu pia una tangi la maji katikati kwa ajili ya mahujaji na kuwawezesha kutawadha katika uwanja wowote ule kati ya viwanja hivyo vitatu vikubwa. Katika mwezi mzima wa Ramadhani na wakati wa mausiku ya kuchea siku za sikukuu viwanja vyote vya Kuba hilo huangazwa kwa taa ziwakazo sana. Siku hizi ziko taa za umeme katika Makuba na minara ili kwamba maumbo yao, ming'ao yao na rangi zao ziweze kuonekana katika usiku wowote ule, sio tu karibuni kutoka kila mahali katika mji huo, bali vile vile viweze kuonwa na mahujaji na wasafiri walioko milimani wakija, katika umbali wa maili kumi na tano. (Maelezo haya yamechukuliwa kutoka katika kitabu kiitwacho The  Shi'ite Religion" cha Bwana O.M. Donuldson).

MWISHO