HOME

(10)

 

BARUA YA WAZI  KWA  MAWAHABI

 

Katika makala yao ambayo tumekuwa tukiyajadili katika mfululizo huu, mawahabi waliwalaumu maimamu wa kisunni wa Mombasa kwa kufanya mihadhara yao katika Msikiti wa Konzi katika siku kumi za kwanza za mwezi wa Muharram! Kwa nini? Kwa sababu, kwa mantiki ya kiwahabi, kwa kufanya hivyo maimamu wa kisunni wanawapoteza "wafuasi wa Sunna kwa kuwaiga hao hao MaShia"!

 

Kabla ya kulijibu neno lao hilo, ningependa wasomaji wetu waelewe mambo mawili muhimu. La kwanza ni kwamba, katika mihadhara yao hiyo, maimamu hao kwa kawaida hawazungumzii yanayozungumzwa na mashia katika majlisi zao za Muharram, bali ni kinyume chake kamwe! Kwa hivyo wanawapoteza vipi masunni, na wanawaiga vipi mashia?

 

La pili ni kwamba, kwa maneno hayo, masunni wasihadaike wakadhania kwamba mawahabi ni wenzao. Maana, kwa maneno yao na imani yao, masunni wasiozikubali itikadi za kiwahabi, na mashia, ni gora (doti) moja. Wote si waumini bali ni mushrikina ambao "ni halali (kuimwaga) damu yao na (kuwanyang'anya) mali yao hata kama wasema laa ilaaha illallaah, waswali, wafunga na wadai kuwa ni Waislamu"! Kwa lugha nyengine, sote (masunni na mashia), kwa mawahabi, tu makafiri! Hayo siwazulii bali yameelezwa wazi katika uk. 179 wa kitabu cha maisha ya Imam wao kiitwacho Muhammad bin Abdilwahhaab: Muswlihun Madhluum wa Muftaraa Alayh cha Ustadh Mas'ud An-Nadawii.

 

Sasa tuangalie ya "kuwaiga hao hao MaShia". Ni mwanzo leo mawahabi kufanya hivyo? Jawabu ni: La! Sio mwanzo, japokuwa hawa wetu wa Mombasa wamekuja na kisingizio cha kwamba mihadhara hiyo inayofanywa na maimamu wa kisunni, mbali na kuiga mashia, haikufanywa na Bwana Mtume s.a.w.w. Kwa hivyo, maadamu halikufanywa na Bwana Mtume s.a.w.w., halifai kufanywa!

 

Unapoyazingatia maneno yao hayo, kwa dhahiri, utadhania kwamba mawahabi wana ghera sana ya kulifuata kila lililofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w., na kulipinga kila ambalo hakulifanya. Lakini kwa wale ambao wameusoma Uwahabi na kuujua, wanajua kwamba ukweli si hivyo bali ni kinyume chake! Wao hutumia ghera zao hizo kuficha chuki zao tu walizonazo dhidi ya waumini hata kama waumini hao watayafanya yaliyofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w.!

 

Tuchukue mfano mmoja tu wa yaliyosemwa na Ibn Taymiyya. Huyu ni mwanachuoni wao aliyefariki dunia katika mwaka wa 728 BH, baada ya kuishi miaka 67. Mawazo yake yalimuathiri sana Muhammad bin Abdilwahhab ambaye, kwa kusaidiwa na ufalme na mali ya Mfalme Saud, ameweza zaidi kuyaeneza madhihabi yake kuliko Ibn Taymiyya mwenyewe. Yeye, Ibn Taymiyya, katika zama zake, hakufaulu kufanya hivyo kwa sababu alipingwa vikali na mashekhe wenzake waliofikia hadi hata ya kumkufarisha!

 

Katika uk. 143 wa Juzuu ya Pili ya kitabu chake kiitwacho Minhaajus Sunnah amesema kuwa inafaa "kuacha baadhi ya mambo ya sunna (mustahabbaat) yawapo ni alama yao (mashia)"! Moja kati ya sunna, ambazo wasio mashia huhimizwa waziache, ni kuvaa pete mkono wa kulia japokuwa hivyo ndivyo alivyokuwa akivaa Bwana Mtume s.a.w.w.! Kwa nini? Kwa sababu sunna hiyo inafuatwa sana na mashia!

 

Ewe ndugu yangu! Kama mawahabi wawaita ahlul bid'a wale watu wanaofanya ambayo hayakufanywa na Mtume s.a.w.w., sisi tuwaiteje wao wanaozuiya watu kuyafanya yaliyofanywa na Bwana Mtume s.a.w.w. kwa sababu tu yanafanywa na wasiowapenda (yaani mashia)? Baina ya mashia (wanaoifanya sunna ya Bwana Mtume s.a.w.w.) na mawahabi (wanaoizuiya) ni nani ahlus sunnah, na ni nani ahlul bid'a? Uamuzi ninakuachia wewe.

 

Kwa hivyo mawahabi wanapowazuia maimamu wa masunni wasiwaige mashia, mambo ni hayo. Pengine, hapa, tumalizie mfululizo wa makaratasi yetu haya kwa suali hii: Kama mashia, wanapomaliza haja zao, hujitwahirisha (huchamba) kwa mkono wa kushoto, ndio masunni wachambe kwa mkono wa kulia ili wasiwaige mashia? Jamani! Hawa mawahabi wanahukumu vipi mambo?

 

 

ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

14 Rabiiul Awwal, 1424

16 Mei, 2003

 

(Mwisho)