HOME

(8)

 

BARUA YA WAZI KWA MAWAHABI

 

Baada ya kuona sifa mbaya mbaya za Yazid zilizonukuliwa kwa baadhi ya wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni, hebu sasa tutizame alivyosema Mtume Muhammad s.a.w.w. katika Hadith zake, na jinsi wanazuoni wa Hadith wa Kisunni walivyozieleza.

 

Hadith ambazo nitazitaja humu leo ni zile zilizomo katika Sahih Bukhari peke yake. Kama wengi wetu tunavyojua, kitabu hicho --  kwa masunni na kwa mawahabi pia -- ndicho kitabu kilicho sahihi (kweli) mno baada ya Qur'ani Tukufu. Kwao wao, Hadith iliyotolewa humo huwa haina shaka!

 

Katika Kitaabul Fitan, mlango wa Qawlin Nabiyyi s.a.w.w. Hilaaku Ummatii Alaa Yaday Ughaylimatin Sufahaa, muna Hadith (kwa Kiingereza, ni Hadith Na. 180 iliyomo uk 147 wa Juzuu ya Tisia) isemayo: "Amr bin Yahya bin Said bin Amr bin Said amesema: 'Babu yangu amenipa habari kwa kusema: Nilikuwa nimekaa na Abuu Hurayra msikitini kwa Mtume s.a.w.w. Madina, tukiwa na Marwaan. Abuu Hurayra akasema, 'Nimemsikia mkweli na mwenye kuswadikiwa na Mwenyezi Mungu (yaani Bwana Mtume s.a.w.w.) akisema: Uangamifu wa umma wangu utakuwa mikononi mwa vijana wa Kikureshi. Marwaan akasema: 'Laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie vijana (hao).' Abuu Hurayra aksema: 'Lau ningelitaka kusema ni Banii fulani na Banii fulani ningelisema.' Nikawa ninatoka na babu yangu kwenda kwa Banii Marwaan pale walipoitawala Sham. Walipokuwa wakiwaona ni vijana wadogo, akitwambia: Huenda wale wakawa ni miongoni mwao. (Nasi) tukimwambia: Wewe unajua zaidi."

 

Kabla hatujanukuu ilivyoelezwa Hadith hiyo, ningependa wale wajuwao Kiingereza (wasiojua Kiarabu) wajue kwamba Hadith hiyo haikufasiriwa yote kwa ukamilifu katika hiyo nuskha ya Kiingereza. Kipande kikubwa, ambacho tumekichapisha kwa italiki katika tafsiri yetu ya Kiswahili hapo juu, hakikufasiriwa kwa Kiingereza -- sijui ni kwa mfasiri wake kughafilika au ni kwa kujighafilisha!

 

Hata hivyo, katika kuisherehe (kuifafanua) Hadith hiyo, Imam Ibn Hajar Al Asqalaani, katika uk. 10 wa Juzuu ya Kumi na Tatu ya kitabu chake kiitwacho Fat'hul Baari, ameitaja riwaya ya Ibn Abii Shayba isemayo "kwamba Abuu Hurayra alikuwa akenda sokoni na akisema: 'Ewe Mola! Usinidirikishe na mwaka wa sitini wala utawala wa

vijana.' " Halafu (yeye Ibn Hajar) akasema: "Na katika maneno haya muna ishara kuwa wa kwanza wa vijana hao alikuwa katika mwaka wa 60; na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Maana Yazid bin Muawiya alitawalishwa katika mwaka huo, na akabakia mpaka mwaka wa 64; akafa. Kisha akatawala mtoto wake, Muawiya, aliyekufa baada ya miezi (michache)."

 

Kwa hivyo, kwa mujibu wa Imam Ibn Hajar, miongoni mwa "vijana wa Kikureshi" ambao Bwana Mtume s.a.w.w. alitabiri kuwa umma wake utaangamia mikononi mwao, na ambao Abuu Hurayra alikiomba Mwenyezi Mungu asimkutanishe nao katika huo mwaka wa 60, ni Yazid. Jee, maneno ya Mtume s.a.w.w. yalianguka? Jee, baada ya mauaji aliyoyaamrisha Karbalaa na Madina na Makka, kama tulivyoona katika karatasi zetu mpaka sasa, umma wa Mtume Muhammad s.a.w.w. haukuangamia? Au hao waliouliwa walikuwa ni makafiri, si Waislamu? Hivyo basi, bado Yazid ni Amiirul-mu'minin?

 

Wala si kwamba Abuu Hurayra, pale alipotaja "Banii fulani na Banii fulani" katika Hadith tuliyoitaja hapo juu, alikuwa hawajui ni kina nani; la! Alikuwa akijua, lakini akiogopa kuwataja kwa majina. Na hilo liwazi tunapoiangalia tena Sahih Bukhari. Katika Kitaabul Ilm, Mlango wa Hifdhil Ilm muna Hadith (kwa Kiingereza ni Hadith Na. 121 iliyomo uk. 89 wa Juzuu ya Kwanza) isemayo: "Imepokewa kwa Abuu Hurayra akisema, 'Nimehifadhi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu s.a.w.w. aina mbili za ilimu. Moja ya ilimu hiyo nimeitangaza. Lakini nyengine, lau ningeliitangaza ingelikatwa koo (yangu) hii.' "

 

Katika kuifafanua Hadith hiyo, katika uk. 216 wa Juzuu ya Kwanza ya Fat'hul Baari, Imam Ibn Hajar amesema: "Wanazuoni wamechukulia kuwa ilimu ambayo (Abuu Hurayra) hakuieneza  ni ya zile Hadith ambazo ndani yake mumetajwa majina ya watawala waovu, na hali zao na zama zao. Abuu Hurayra alikuwa akiwataja kikuu tu baadhi yao, wala hakuwa akiwatasua kwa kuiogopea nafsi yake kwao; kama alipokuwa akisema, 'Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na mwaka wa 60 na utawala wa vijana'; alikuwa akiashiria Ukhalifa wa Yazid bin Muawiya kwa sababu ulikuwa katika mwaka wa 60 BH."

 

Wala ufafanuzi huo haukutolewa na Imam Ibn Hajar peke yake. Hata Imam Shihaabuddin Ahmad Al Qastwalaani, katika sherehe yake ya Hadith hizo hizo, ametoa karibu ufafanuzi kama huo. Wale wajuwao Kiarabu, wakitaka kuyaona hayo, nawatizame uk. 374 wa Juzuu ya Kwanza na uk. 11 - 12 wa Juzuu ya Kumi na Tano ya Irshaadus Saari.

 

Kwa hivyo Abuu Hurayra hakumtaja Yazid kwa jina kwa kujiogopea nafsi yake, asije akakatwa koo; si kwamba alikuwa hajui. Kwa lugha nyengine, alifanya taqiyya!

 

Lakini kama Abuu Hurayra alifanya taqiyya, jee wenziwe pia walifanya hivyo? Hilo inshallah tutaliona katika karatasi yetu ijayo.

 

ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

29 Swafar, 1424

  2 Mei, 2003

 

(Inaendelea)