HOME

(6)

 

BARUA YA WAZI  KWA  MAWAHABI

 

Katika karatasi yetu ya tano tuliona, katika mkutano wake wa hadhara aliouita, jinsi Muawiya alivyombandika Yazid kutawala baada yake. Vile vile tulianza kuyadondoa mambo mabaya aliyoyafanya Yazid mara tu baada ya kukikalia kiti cha ufalme wake. Leo tutaendelea na yaliyobakia, japokuwa kwa ufupi, ili tusiyarefushe mambo.

 

6. Baada ya kumuuwa Imam Husein a.s. na aliokuwa nao katika mwaka wa 61 BH, Yazid  aliiingilia Madina. Sheikh Abdalla Saleh Farsy anatwambia (uk. 41): "Wakauawa Masahaba wengi hapo Madina na wasiokuwa Masahaba. Na wakafanya fisadi kubwa sana hapo Madina muda wa siku tatu mfululizo. Ikawa hakuna kisichoharibiwa; si roho wala mali wala hishima. Aliwaamrisha Yazid wafanye hivyo. Na masahaba wasiokufa

aliwaamrisha wapigwe chapa za mgongo za kuonyesha kuwa wao ni watumwa wa Yazid." Subhaanallah! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi wetu!

 

Katika dondoo hilo hapo juu, hata hivyo, Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; hakulifunua. Lakini wanazuoni wenziwe wamelifunua. Kati ya hao ni Ibn Kathir ambaye, kwa mawahabi wa ulimwengu, ni kama Sheikh Abdalla Saleh Farsy kwa mawahabi wa Afrika ya Mashariki; wanamuenzi sana. Yeye, katika uk 220 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, amesema kuwa idadi ya hao "masahaba wengi" waliouwawa ilikuwa " mia sabaa: vigogo vya muhaajiriin na answaar"; na "wasiokuwa masahaba" walikuwa " elfu kumi". Kuhusu " fisadi kubwa sana", alizosema Sheikh Abdalla S. Farsy, Ibn Kathir anasema ( uk. 222) kuwa "hazisemeki hazielezeki; hakuna anayezijua ila Mwenyezi Mungu" japokuwa, kabla ya hapo katika uk. 220, alikuwa ameshatasua kuwa " wanawake walihashiriwa  mpaka ikasemwa kuwa 1000 ( elfu moja ) walishika mimba na kuzaa bila kuwa na waume"!

 

Baada ya Ibn Kathir kuyaeleza hayo, na kama kwamba anataka kuzindua tumfahamu Yazid ni nani, anatutajia (uk 223) Hadith tatu za Bwana Mtume s.a.w.w. Ya kwanza, iliyopokewa na Bukhari, inasema: "Hakuna yoyote atakayewafanyia vitimbi watu wa Madina ila atayayuka kama inavyoyayuka chumvi katika maji." Ya pili, iliyopokewa na Muslim, inasema: " Haikusudii Madina yoyote kwa uovu ila Mwenyezi Mungu atamyayusha katika moto myayusho wa risasi, au myayusho wa chumvi katika maji." Ya tatu, iliyopokewa na Imam Ahmad bin Hambal, inasema: "Anayewatakia khofu watu wa Madina kwa dhulma, Mwenyezi Mungu naye atamtia khofu na ashukiwe na laana ya Mwenyezi Mungu na malaika na watu wote. Wala Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, hatamkubalia toba wala fidia."

 

Haya! Kama hayo yaliyofanywa Madina yalifanywa kwa amri ya Yazid, kama asemavyo Ibn Kathir (uk. 220 ) na Sheikh Abdalla S. Farsy (uk. 41), mtu huyo -- kwa Hadith zilizotajwa hapo juu -- bado yu salama? Ni Amiirul-mu'minin gani huyo anayeshukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu, malaika Wake na watu wote?

 

7. Mwaka mmoja baada ya kuiingilia Madina, aliiingilia Makka (katika mwaka wa 64 BH)! Huko, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk.41): "Majeshi ya Yazid yaliuwa watu wengi na kuivunja Al Kaaba."

 

Hapo pia Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; lakini wenziwe wamelifunua. Kwa mfano, huyo huyo Ibn Kathir ameandika (uk. 225) kuwa majeshi hayo "yaliipiga mawe Al Kaaba kwa teo (manjaniiq) na kuishambulia hata kwa moto mpaka ukuta wake ukaungua"! Na katika uk. 72 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab, Ibnul Imaad al Hambalii anasema: "mpaka likaanguka jengo lake"!

 

Haya! Hiyo ni "Nyumba ya Mwenyezi Mungu" ambayo Qur'ani Tukufu inatwambia (Sura 3:97) kwamba aliyeko nje akakimbilia huko, huwa katika amani; leo Yazid anaiondolea amani hivyo! Na huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi ambaye wanataka Waislamu wamtambue hivyo! Subhaanallah!

 

Hayo basi, kwa mukhtasari, ndiyo yaliyofanywa na Yazid. Jee, acha ya Amiirul-mu'minin, Mwislamu wa kawaida tu anaweza kuyafanya kama hayo? Bila shaka hawezi. Ikiwa ni hivyo basi, vipi Yazid aliweza?

 

Kuijibu suali hiyo, itabidi tujue Yazid alikuwa ni mtu wa aina gani. Hilo inshallah tutalitizama katika karatasi ijayo kwa kunukuu maneno yaliyomo katika vitabu vilivyotungwa na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni (si wa Kishia).

 

 

 

 ABDILAHI NASSIR

S.L.P. 84603

MOMBASA

 

   15 Swafar, 1424

   18 Aprili, 2003

 

(Inaendelea)